MANARA ANATANGAZA KUMUOA WEMA SEPETU KWA KUWA ANAJUA TFF NI DHAIFU
Na Saleh Ally
MKUU
wa Kitengo cha Habari cha Klabu ya Simba, Haji Sunday Manara juzi
ameandika waraka wake akielezea namna ambavyo anaamini Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) limekuwa si makini katika suala la ratiba.
Moja ya sehemu ya alichoandika Manara katika makala yake hiyo ni hiki hapa;
“Wakati
wenzetu wanazungumzia changamoto nzito na kubwa katika maendeleo yao
ya mchezo murua zaidi duniani wa soka. Watanzania tunahangaika namna ya
kupanga ratiba ya mechi zetu za ligi yetu na Kombe la Shirikisho, ratiba
inayobadilishwa Kama nguo, tena mvaaji mwenyewe ni mbunifu wa mavazi au
mwanamitindo, ambae huvaa nguo tano Kwa siku.”
Mwishoni
alimalizia hivi: “Nimalizie Kwa kuwapa mtihani mwingine TFF na bodi ya
Ligi, iwapo kama ratiba yao ya ligi kuu na Kombe la Shirikisho
haitabadilishwa kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu, ntamposa mlimbwende
Wema Sepetu, na akikubali ntamuoa. Akikataa ntatembea na boxer (nguo ya
ndani) tokea nyumbani kwangu hadi TFF.”
Umbali
wa kutoka nyumbani kwa Manara, Magomeni Mikumi hadi TFF si mbali sana,
takribani kilomita tatu au nne. Kweli si mbali lakini kwa kutembea na
nguo ya ndani, hata hatua nne ukiwa hadharani, ni mbali sana.
Jiulize
kwa nini Manara anaweza kutoa kauli tata kama hiyo ya kumposa au kumuoa
Wema Sepetu au kutembea na nguo ya ndani huku akijiamini haiwezi
kutokea.
Haiwezi
kutokea na ana uhakika kwa kuwa anaijua TFF kwamba si ya uhakika na
mambo yao mengi ni ya kubahatisha. Kwa hiyo uhakika unapozungumzia mambo
yasiyo na uhakikia, kwa TFF ni uhakika.
Lakini
unapozungumzia yale ya uhakika kwa TFF si uhakika. Ndiyo maana Manara
anaweza kutoa ahadi ambayo anajua ni ngumu kwake lakini ana uhakika
hawezi kuifanya kwa kuwa TFF haitaweza kwenda mwendo sahihi.
Kweli,
kama watu wanazungumzia mambo ya maendeleo mengi, vipi sisi hadi leo
eti ratiba haiwezi kupangwa bila ya kuwa na mabadiliko?
TFF
inawezaje kuzungumzia program bora ya vijana kwa muda mfupi na mrefu au
ya soka la wanawake kwa muda mfupi na mrefu wakati ratiba ya msimu
mmoja tu haina uhakika wa kuipanga ikiwa na uhakika?
Kumekuwa
na mawazo ya kuongeza watu uwanjani baada ya mapato kuathirika kwa
kiasi kikubwa na suala la mechi kuanza kuonyeshwa mujarabu na runinga ya
Azam TV.
Moja
ya mikakati ilikuwa ni kuzungumzia uuzaji wa tiketi kwa msimu au nusu
msimu. Lakini unawezaje kufanya hivyo wakati hakuna uhakika wa ratiba?
TFF
hiyohiyo, ilifanya madudu msimu uliopita kwa kuiruhusu Azam FC iondoke
kwenda kucheza mechi za tamasha nchini Zambia na kusababisha kuwe na
viporo kwenye ligi kuu.
Baada
ya presha kubwa ya vyombo vya habari, nayo ikaweka presha kwa Azam FC
kuhakikisha inamaliza viporo vyote baada ya kurejea kwenye ligi kuu.
Ukiangalia hapa, hakukuwa na sababu za msingi na TFF yenyewe ilionyesha
haiheshimu ratiba ya ligi ambayo imepangwa na wanaoitwa wataalamu.
Ligi
inakwenda na malalamiko makubwa ya viwango duni vya waamuzi, viwango
duni vya upangaji ratiba lakini hata viwanja vibovu ambalo liko nje ya
TFF. Kwa nini TFF isiwe mstari wa mbele kuondoa mapungufu hayo laini ya
upande wake ambayo yanawezekana?
Binafsi
siamini kama kuna kiongozi hata mmoja wa shirikisho hilo anataka
maendeleo ya soka nchini. Ninaamini hivi; viongozi wanataka maendeleo
yao, ya familia zao, ya ndugu zao na ikiwezekana ya washikaji wao tena
si kwenye mpira.
Umesikia
siku nne tu zimepita, eti waliopanga ratiba ya Kombe la Shirikisho
ambalo TFF wanadhaminiwa na Azam Sports HD kwa mamilioni ya fedha.
Lakini eti wapanga ratiba waliisahau timu.
Kwangu
niliona kama miujiza, lakini miujiza ya TFF haijawahi kupungua kwa kuwa
kila mwaka inaongezeka. Hivyo kushangaa ni kujishangaza tu maana pale
ndiyo jumba la miujiza.
SOURCE: CHAMPIONI
Post a Comment