Kubenea Afutiwa Mashitaka ya Uchochezi Mahakamani Kisutu
MAHAKAMA ya
Hakimu Mkazi Kisutu imemuondolea mashtaka ya uchochezi Mbunge wa Ubungo, Saed
Kubenea, kutokana na upungufu katika hati ya mashtaka.
Hata hivyo,
mara baada ya kuondolewa kwa hati hiyo ya mashtaka, Kubenea alichukuliwa na
maofisa wa polisi hadi Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa mahojiano
ambapo inadaiwa baada ya mahojiano aliachiliwa.
Uamuzi huo
umetolewa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, baada ya
Wakili wa Serikali, Derrick Mkabatunzi, kueleza kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili
ya uamuzi.
Katika
uamuzi huo, Hakimu Mashauri alisema anakubaliana na pingamizi zilizowasilishwa
na upande wa utetezi kupitia Wakili Jeremiah Mtobesya kuwa hati ya mashtaka ina
mapungufu na ilikuwa na utata kiasi kwamba haiendani na kosa analoshitakiwa mshtakiwa.
Kubenea
anatuhumiwa kuandika kichwa cha habari ambacho kinadaiwa kilikuwa na uchochezi, kilichosema: ‘Yuko wapi atakayeiokoa Zanzibar?’ ambacho kwa
mujibu wa hakimu alidai kichwa hicho hakina kosa lolote na upande wa mashtaka ulipaswa kuandika
maneno yanayodhaniwa kuwa ni ya uchochezi.
Hakimu
alifafanua kuwa hati hiyo ina mapungufu
kwa sababu haielezi ni namna gani mshtakiwa ametenda kosa na hivyo ingesababisha mshtakiwa ashindwe
kujitetea.
Aliendelea
kueleza kuwa hati ya mashtaka
imeondolewa mahakamani, isipokuwa jamhuri bado wanayo nafasi ya kufungua kesi
nyingine kwa mujibu wa sheria ya magazeti na ya makosa ya jinai.
Awali katika
kesi hiyo wakili Mtobesya alidai kuwa hati hiyo ya mashtaka ina mapungufu na inakinzana na matakwa ya
sheria ya magazeti na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, hivyo akiomba
mahakama iifutilie mbali na kumuachia huru Kubenea.
Wakati
huohuo, Wakili Mkabatunzi alidai kuwa hati ya mashtaka inayomkabili Kubenea ipo
sahihi na kwamba imekidhi matakwa ya kisheria
na akaongeza kuiomba mahakama itupilie mbali pingamizi lao.
Katika kesi
hiyo, Kubenea anadaiwa kuwa alifanya
kosa hilo Julai 25, 2016 ambapo alichapisha habari ama makala ambayo ingeweza
kusababisha hofu kwa jamii ama kuharibu hali ya amani. Chapisho hilo lilitolewa kwenye gazeti la Mwanahalisi la Julai 25-31, 2016.
Post a Comment