ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-08



NYEMO CHILONGANI
“Nipo Australia!”
“Mbona ghafla na hukuniaga?”
“Kwa sababu sipendi kuaga watu! Una shida yoyote?” aliuliza Nicolaus swali ambalo liliendana na emoji ya kucheka katika mtandao huo.
Melania hakutegemea kama angepewa jibu kama hilo. Moyo wake ulimuuma sana kwani aliambiwa hivyo na mtu aliyekuwa akimpenda mno moyoni mwake. Baada ya kusema hivyo, Nicolaus hakutaka kuzungumza na Melania, alichokifanya ni kukata simu.
Hayo ndiyo maisha aliyoamua kuishi. Baada ya kukaa kwa wiki mbili, akazichukua picha zote kwenye simu yake na kuzihamishia kwenye barua pepe zake, hakutaka zionekane na mtu yeyote yule, alitaka kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ili kila mtu auone utupu wa msichana huyo aliyekuwa na urembo wa ajabu.
“Nicolaus...” aliita Melania kwenye simu kwa njia ya meseji.
“Unasemaje?”
“Ulitaka picha, nimekutumia, sasa tatizo nini? Mbona umebadilika hivyo?” aliuliza msichana huyo.
“Nimebadilika nimekuwaje? Wa kijani au mwekundu?”
“Nico, mbona unanifanyia hivi?”
“Nimekufanyaje? Mbona kawaida tu!”
“Naomba uzifute picha zangu basi.”
“Ili?”
“Naomba tu uzifute,” alisema msichana huyo huku akianza kutoa kilio cha kwikwi.
Nicolaus hakutaka kuandika ujumbe wowote ule alichokifanya ni kupuuzia. Nchini Tanzania, Melania alikuwa na mawazo tele, hakujua lengo la mwanaume huyo lilikuwa ni nini juu ya picha zile.
Baada ya siku mbili, picha zake, baadhi ambazo hazikuwa za utupu moja kwa moja zikaanza kuonekana kwenye mitandao ya kijamii huku kukiwa na neno yaliyosomeka ‘Slut’ likiwa na maana ya mwanamke mchafu.
Uso haukuonekana lakini Melania alijua kwamba zile zilikuwa picha zake na mtumaji alisema kwamba baada ya siku kadhaa angetuma picha zote huku msichana huyo akionekana kwani alikuwa mmoja wa mabinti ambao wazazi wao walikuwa maarufu sana.
Melania akachanganyikiwa, hakuamini kama kweli Nicolaus aliamua kufanya jambo kama hilo. Alimtumia meseji na kumpigia lakini meseji hazikuwa zikijibiwa japokuwa zilionekana kusomwa na simu wala haikupokelewa.
Melania hakutulia, mbele yake aliiona aibu kubwa, moyo wake ulimuuma mno na muda mwingi alikuwa akijuta sababu zilizomfanya kumtumia mwanaume huyo picha zile. Alichanganyikiwa na hakutaka kubaki nchini Tanzania, alichokifanya ni kuwaaga wazazi wake kwamba alitaka kuelekea nchini Australia.
“Kuna nini?” aliuliza baba yake, Mzee Edward.
“Nakwenda kutembea tu!”
“Ndiyo uende Australia!”
“Baba! Naomba nikapumzike. Sipo sawa.”
Hawakuwa na jinsi, hawakutaka kumzuia binti yao kwani walimpenda sana hivyo kumruhusu kwenda huko. Aliondoka baada ya siku mbili, alichanganyikiwa, ndani ya ndege alikuwa na mawazo tele, alitaka kumuona Nicolaus na kuzungumza naye juu ya picha hizo.
Ndege ilichukua saa kumi na nane mpaka kufika huko. Ikatua katika uwanja wa ndege hapo Melbourne na kisha siku hiyohiyo kuondoka kuelekea katika Chuo cha Monarch kwa ajili ya kuonana na Nicolaus.
“He left to Perth,” (aliondoka kwenda Perth)
“Oh my God! I just want to see him,” (Oh Mungu wangu! Ninataka kumuona) alisema msichana huyo huku akionekana kuwa na uhitaji wa kuonana na Nicolaus.
“Who are you?” (wewe ni nani?)
“His sister,” (dada yake)
“Where are you from? Manhattan, Brooklyn or DC?” (umetoka wapi? Manhattan, Brooklyn au DC?) aliuliza jamaa aliyekuwa akizungumza naye chuoni.
“Tanzania!”
“Tanzania! What the hell is that?” (Tanzania! Ndiyo nini?) aliuliza jamaa huyo. Hakukumbuka kama Marekani kulikuwa na sehemu iliyoitwa Tanzania.
Ikambidi Melania aanze kumwambia jamaa huyo kuhusu Tanzania. Hawakuamini walipogundua kwamba Nicolaus alitoka Tanzania na si Marekani kama alivyokuwa akijulikana mahali hapo.
Wengi walishangaa, Melania hakujua sababu ya watu hao kushangaa namna hiyo, hakujua kwamba Nicolaus alijitambulisha kama mtu aliyetoka Marekani huku hata lafudhi yake ikionyesha kweli alitoka nchini humo.
“Sasa hujawasiliana na ndugu yako wakati unakuja?” aliuliza jamaa mmoja.
“Sikuwasiliana naye kwani nimetoka Uingereza mara moja na kupitia hapa. Huko Perth ni mbali sana?” aliuliza Melania.
“Si mbali sana. Ila msubiri kwani amekwenda mara moja na msichana wake, Kattie, nafikiri mpaka kesho wanaweza kuwa hapa,” alisema jamaa huyo.
Maneno hayo yalimchoma mno Melania, hakuamini kile alichokisikia kwamba kila siku aliweka tumaini kwa mwanaume huyo na wakati huko nchini Australia alikuwa na msichana mwingine.
Nguvu za miguu yake zikamuisha, akashindwa kuvumilia kusimama, akachuchumaa na kukiinamisha kichwa chake, macho yakajaa machoni mwake na baada ya sekunde kadhaa machozi hayo yakaanza kutiririka mashavuni mwake.
Aliumia mno, mbele yake aliona giza zito. Wakati mwingine alikuwa akimlaumu Mungu kwa kile kilichotokea, kumruhusu mwanaume huyo kuingia moyoni mwake. Alijua kwamba alifanya makosa kwa sababu hakumtaka Nicolaus kuzivua nguo zake mpaka siku ambayo wangeoana na kuwa mume na mke.
Alitulia hapohapo huku akiwa amechuchumaa. Aliendelea kulia kiasi kwamba wanaume aliokuwa nao mahali hapo wakaamua kuondoka zao na kumuacha. Alikaa hapo kwa dakika kadhaa, akainuka, akalishika begi lake na kwenda hotelini.
Siku hiyo ilikuwa kama msiba, ilikuwa ni kama amefiwa na mzazi wake, hakuwa na furaha hapo Melbourne, muda wote alikuwa ni mtu wa kulia na hata kitandani alipokuwa amelala, shuka lililowanishwa na machozi yake.
Akajuta kwa uamuzi wa kujipiga picha za utupu na kumtumia mwanaume huyo. Alijua kwamba kwenye maisha yake aliwahi kufanya makosa mengi aliyojutia lakini hilo la kujipiga picha za utupu na kumtumia Nicolaus hakika lilikuwa kosa kubwa sana kulifanya katika maisha yake.
Wakati yeye akilia na kuhuzunika, upande wa pili Nicolaus alikuwa akiyafurahia maisha yake na msichana wake mpya, Kattie. Moyo wake ulikuwa kwenye furaha kubwa, huko Perth walipokuwa wamekwenda ilikuwa ni kwa ajili ya kuyafurahia maisha na kulinogesha penzi lao.
Hakumfikiria Melania kichwani mwake, aliamua kumsahau msichana huyo kwani kitu alichokigundua wakati huo ni kwamba Wazungu walijua kupenda kuliko hata ngozi nyeusi. Alikuwa kwenye uhusiano na msichana huyo kwa wiki chache lakini tayari walilala sana kitandani, walifanya sana ngono tofauti na jinsi alivyokuwa na msichana Melania ambaye kila siku alimwambia asubiri na hivyo kuwa mpenzi mtazamaji tu.
Walikaa huko kwa siku mbili ndipo wakarudi jijini Melbourne. Alipofika tu chuoni akaambiwa kwamba kulikuwa na msichana aliyekuwa amefika chuoni hapo kumuona, alipouliza kuhusu msichana huyo, akaambiwa kwamba alitoka Tanzania.
“Ndiyo wapi huko?” aliuliza huku akijifanya kushangaa.
“Anasema Afrika!”
“Sipajui na sina ndugu huko Afrika.”
“Au ni tapeli?”
“Inawezekana!”
Baada ya kukaa kwa saa chache chuoni hapo, Melania akarudi na kumuulizia tena. Akaambiwa kwamba mwanaume huyo alirudi na alikuwa katika chumba chake hapohapo chuoni, hivyo akapelekwa.
Alipofika huko, kitu cha kwanza alifurahi kumuona mpenzi wake huyo, moyo wake uliokuwa na hasira naye ukapoa, akahisi nguvu kubwa ya mapenzi ikirudi moyoni mwake hali iliyoufanya uso wake kuwa na tabasamu pana. Akaanza kumsogelea kwa ajili ya kumkumbatia.
“Who the hell are you?” (wewe ni nani?) aliuliza Nicolaus, alijifanya kutokumjua msichana huyo kwani aliamini angeunguza picha kwani chuo kizima kilijua kwamba alitoka Marekani na ndiyo sababu iliyomfanya kupendwa.
“Nicolaus...what the hell wrong with you?” (Nicolaus...una nini?) aliuliza Melania huku akimshangaa mpenzi wake huyo.
Alichokifanya Nicolaus ni kumchukua Melania na kuondoka naye mahali hapo huku akiwa amemshika mkono. Safari yao hiyo ikaishia chini ya mti mmoja mkubwa, wakatulia hapo.
“Umefuata nini hapa?” aliuliza Nicolaus kwa ukali.
“Nimekuja kuzungumza na wewe.”
“Kuzungumza na mimi! Kuhusu nini?”
“Kuhusu picha, ila pia kuhusu uhusiano wetu,” alisema Melania.
“Kuhusu uhusiano wetu? Kwani hukujua kwamba sikutaki tena?” aliuliza Nicolaus huku akimwangalia msichana huyo ambaye uso wake ulionyesha kuumizwa zaidi juu ya kile alichoambiwa.
“Nicol....”
“Melania! Nina mpenzi, ninampenda, sitaki kuwa na wewe. Halafu wewe ni mtu mzima, wakati mwingine lazima uusome mchezo, siku hizi tunaacha kidigitali, unaachwa kimyakimya. Hupigiwi simu, hutumiwi meseji, sasa mpaka hapo hujashtukia kama umeachwa?” aliuliza Nicolaus huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu, hakuyajali maumivu aliyokuwa nayo msichana huyo moyoni mwake.
“Basi naomba uzifute picha zangu!”
“Picha zipi?”
“Zile nilizokutumia. Nimeona umeanza kuziweka kwenye mitandao,” alisema Melania huku akilia.
“Kwani picha ni zako au zangu? Si ulinitumia, kwa maana hiyo ni kama uliniuzia, sasa kwa nini nizifute picha zangu? Haiwezekani,” alisema Nicolaus, hakutaka kuzungumza sana, akaondoka mahali hapo na kumuacha msichana huyo akilia kama mtoto.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku mbaya maishani mwake, alijiona kuuza utu wake, aliumia na kitu kilichomuumiza zaidi ni kuhusu wazazi wake. Walikuwa watu walioheshimika sana, aliamini kwamba kama kweli picha zake zitawekwa mitandaoni na sura yake kuonekana basi ingekuwa aibu kubwa mno.
Hakutaka jambo hilo litokee na ndiyo maana aliamua kuondoka na kwenda Australia ili kuzungumza na Nicolaus lakini matokeo yake, hakueleweka na kwa jinsi mwanaume huyo alivyoonekana, ilionyesha kabisa kwamba angekwenda kuziweka picha hizo mitandaoni huku sura yake ikionekana.
Akarudi nchini Tanzania huku akiwa hakijielewi kabisa. Safari ilikuwa ni ya huzuni na kulia sana. Alijua kwamba angeweza kumshtaki lakini hiyo isingesaidia kwa sababu kama angezitoa picha zake na kuwekwa mitandaoni na sura kuonekana basi watu wangezipakua na kuwa nazo kwenye kompyuta zao.
Alipofika Tanzania, hakutaka kuchelewa, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwatafuta wataalamu wa IT, alitaka kuzungumza nao ili ikiwezekana waingie katika barua pepe ya Nicolaus na kuzifuta picha hizo.
“Nitafanya kazi hiyo,” alisema jamaa mmoja, alikuwa mtaalamu wa kompyuta kutoka katika chuo cha kompyuta cha UCC (University Computing Centre) kilichokuwa ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Kwa hiyo utaweza?”
“Kazi nyepesi sana. Sisi ndiyo hackers wenyewe,” alijigamba jamaa huyo.
“Sawa. Kwa hiyo itakuwa kiasi gani?”
“Milioni tano!”
“Haina shida. Ukifanikiwa hata kumi nitakupa,” alisema Melania hali iliyoonyesha ni kwa jinsi gani alitamani picha hizo zifutwe.
Kijana huyo wa IT aliyeitwa Ibrahim Musa akaondoka na kwenda kufanya kazi yake. Alikuwa mtaalamu mkubwa wa kuchezea kompyuta zaidi ya wanafunzi wote chuoni hapo. Aliijua kompyuta na kuifanya alivyotaka.
Aliamini kwamba angefanikiwa kutokana na utaalamu wake mkubwa aliokuwa nao. Kama alikuwa na uwezo wa kuingia kwenye akaunti za watu Facebook, WhatsApp na Instagram, ingeshindikana vipi kuingia kwenye barua pepe kama Yahoo?
Alijiamini, akaanza kuifanya kazi hiyo kwa nguvu kubwa. Haikuwa kazi nyepesi hata kidogo, ilikuwa ni kazi kubwa ambayo hakuwahi kukutana nayo kabla. Akaunti ya Nicolaus ilikuwa na ulinzi mkubwa, ilikuwa vigumu sana kuingia na kuichezea.
Ibrahim alitumia muda wa wiki nzima, hakufanikiwa, alitamani kuzipata fedha za Melania lakini kazi aliyopewa ilikuwa kubwa mno hivyo kunyoosha mikono juu na kumtafuta msichana huyo.
“Vipi?”
“Daah!”
“Imekuwaje? Umefanikiwa?”
“Hapana! Huyu jamaa kaifunga sana akaunti yake.”
“Kwa hiyo imeshindikana?”
“Ndiyo! Nimeshindwa labda unipe siku zaidi,” alijibu Ibrahim, alizitamani fedha lakini kazi ya kuifanya mpaka hizo fedha zipatikane haikuwa kazi nyepesi.
Melania akachoka, akanyong’onyea na kuhisi kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yake, alitamani kuchimba shimo na kujifukia kwani hakuona kama angehimili kupigana na aibu kubwa ambayo angeipata hapo baadaye baada ya picha zake kusambazwa katika mitandao ya kijamii na kuonekana hadharani.
Kila siku alilia kwa uchungu, alipambana, aliwasiliana na watu wengine na kuwaambia kuhusu suala lake, alipelekewa wataalamu wengi wa IT lakini hawakufanikiwa kulimaliza tatizo lake hivyo kukata tamaa kabisa.
Alivumilia, alilifanya jambo hilo kuwa siri lakini mwisho wa siku akaamua kumshirikisha rafiki yake aliyeitwa Michael Msofe ambaye aliwahi kusoma naye shule. Alipomwambia, Michael akamlaumu kwa kuchukua uamuzi wa kumtumia mtu huyo picha hizo.
“Sawa. Umeshanilaumu, nimekubali, kwa hiyo nifanye nini?” aliuliza Melania aliyeonekana kukata tamaa.
“Kuna mtu anaweza kuifanya kazi hiyo!”
“Nani?”
“Anaitwa William!”
“Amesoma kompyuta? Ni mkali?”
“Huyo hajawahi kusoma kompyuta hata siku moja.”
“Sasa atawezaje kuifanya kazi hii? Nimewapelekea waliosomea na wenye digrii zao wote wameshindwa. Michael, atawezaje?” aliuliza Melania, hakutaka kuamini kama katika dunia hii kuna mtu angeweza kuingia katika akaunti ya Nicolaus.
“Ataweza tu!”
“Naomba nionane naye. Anaishi wapi?”
“Anaishi Tabata.”
“Naomba twende huko.”
“Sawa.”

Je, nini kitaendelea?
Je, William ataweza kuifanya kazi hiyo?
Kwa watakaopenda, ningeomba wanisaidie kuSHARE hadithi hii!
Tukutane Alhamisi hapahapa.

No comments

Powered by Blogger.