ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-03



NYEMO CHILONGANI
ILIPOISHIA JUMANNE
“Pole sana mshikaji wangu,” alisema Pamela, jina hilo likamfurahisha mzee huyo, akaachia tabasamu pana.
“Nashukuru sana! Naomba nikuone leo,” alisema mzee huyo.
“Leo?”
“Ndiyo!”
“Mmh!”
“Kuna nini? Mbona unaguna jamani?
“Nitakwambia! Ngoja nicheki ratiba yangu,” alisema Pamela.
“Sawa. Nakupenda Pamela!”
“Ahsante!”
SONGA NAYO...

Moyo wake uliumizwa vya kutosha, ulijeruhiwa mno, ulikosa amani na kila siku ulikuwa ukipitia katika maumivu makali. Alichoka, alilia usiku na mchana na ndiyo maana mzee Edward alipomwambia kwamba alikuwa tayari kumpa furaha akahisi kitu cha tofauti ndani ya moyo wake.
Hakuhitaji mapenzi, kitu alichokihitaji ni furaha tu, hakutaka fedha, hakutaka mali, kitu ambacho alikihitaji kuliko kitu chochote ni furaha ambayo Dickson alishindwa kumpatia kwa kipindi kirefu.
Baada ya kujifikiria kwa saa kadhaa, akamwambia mzee huyo kwamba alikuwa tayari kwenda naye sehemu kama alivyoomba kitu kilichomfurahisha mzee huyo na hivyo baada ya saa mbili, wakaonana.
Pamela akakutana na mzee huyo katika mgahawa wa Jumanji uliokuwa Msasani, hapo walizungumza sana, kwa jinsi alivyoonekana Pamela hakuwa na furaha, hilo lilimfanya mzee Edward kukosa amani na hivyo kumuuliza sababu ya kuwa hivyo.
Pamela hakuficha, alimwambia ukweli kile kilichokuwa kimetokea, alimwambia jinsi moyo wake ulivyokuwa na majeraha kutokana na yale aliyokuwa akifanyiwa na mpenzi wake. Maneno hayo yalimpa uhakika mzee huyo kwamba angemchukua Pamela kwani alimuahidi kitu ambacho alikihitaji kila siku katika maisha yake, FURAHA.
“Unampenda?” aliuliza mzee huyo.
“Ukweli wa moyo wangu unampenda ila sihitaji kuwa naye na sijui nitamtoa vipi moyoni mwangu,” alisema Pamela huku akionekana kuwa na huzuni mno.
“Huwezi kumtoa kama hutomuingiza mtu mwingine. Ili huyo atoke, ni lazima mwingine aingie kwani ndani ya moyo hakuwezi kukaa watu wawili,” alisema mzee huyo.
“Najua hilo!”
“Naomba niwe nawe. Nakuahidi huyo kiumbe atatoka na tutakuwa mimi na wewe, wewe na mimi,” alisema mzee huyo.
Walizungumza mambo mengi, kwa sababu msichana huyo alihitaji sana furaha katika kipindi hicho, akakubali kuwa na Mzee Edward na hivyo uhusiano mpya kuanza. Kama alivyosema mzee huyo ndivyo alivyofanya, alimpenda sana Pamela na kila wakati alikuwa akiwasiliana naye na kutaka kujua anaendeleaje.
Kitendo cha mzee huyo kuwa karibu naye kila wakati kikamfanya kuanza kumuingiza taratibu na kumuondoa Dickson ambaye kila alipokuwa akipiga simu kazi yake ilikuwa ni kulalamika tu na kumpa vitisho vya kumuacha kwa mara nyingine.
Pamela hakujali, hakutaka kusikia kitu chochote kile, vile vidonda vilivyokuwa moyoni mwake vikaanza kupona na ile furaha ambayo ilikuwa imepotea kwa kipindi kirefu ikaanza kurudi moyoni mwake.
Akabadilika, mama yake akamshangaa, haikuwa kawaida kuliona tabasamu la binti yake lakini kipindi hicho, kila wakati msichana huyo alikuwa akitabasamu tu. Mama yake hakutaka kukaa kimya, akamuuliza, alitaka kujua siri kubwa ya tabasamu lile.
“Nina furaha tu mama,” alisema Pamela.
“Sawa. Najua una furaha! Ila furaha ya nini?” aliuliza mama yake.
“Nitakwambia mama!”
“Kwa nini usiniambie sasa hivi?”
“Na kwa nini nikwambie sasa hivi? Mambo mazuri hayataki haraka mama,” alijibu Pamela huku akiwa na tabasamu pana.
Ndani ya miezi mitatu ya mahusiano ya kimapenzi, mzee huyo hakumwambia Pamela kuhusu kufanya mapenzi, kwake, kuwa karibu na msichana huyo ilikuwa ni furaha tele. Wakati mwingine alikuwa akimuita hotelini, huko walikaa na kuzungumza huku msichana huyo akiwa amekiegemea kifua chake, hakumvua nguo zake zaidi ya kuendelea kupiga stori mpaka walipoondoka.
Pamela akajihisi vibaya, akahisi kwamba mzee huyo alikuwa na matatizo mwilini mwake, haikuwa kawaida kuwa na mwanaume na kukaa naye kwa kipindi kirefu bila kufanya mapenzi na wakati alikuwa akimgharamia kwa kila kitu.
“Hakuna tatizo! Ila kufanya mapenzi ni maamuzi, kupanga wote wawili,” alisema mzee Edward.
“Ila tatizo nini mpenzi?”
“Pamela! Tatizo kubwa ni mke wangu! Ananifanya nijisikie vibaya sana. Nilikwambia kwamba ninampenda, kufanya mapenzi na wewe nahisi kama nitamsaliti,” alisema mzee huyo ambaye hakutaka kabisa kuficha juu ya penzi alilokuwa nalo kwa mkewe.
“Pole jamani! Mungu atamponya tu!”
Siku zikaendelea kukatika huku akiishi nyumbani kwao Manzese. Baada ya miezi mitano ya mahusiano ya kimapenzi na mzee huyo, Pamela akapangiwa jumba kubwa maeneo ya Kijitonyama na kutakiwa kukaa huko.
Hakuamini siku ambayo alichukuliwa na mzee huyo na kuonyeshewa jumba hilo, alimkumbatia mzee huyo na kulia kifuani mwake. Kutoka Manzese, kwenye nyuma ya kimasikini mpaka katika jumba hilo kwake ilionekana kuwa ndoto kubwa.
Mbali na jumba hilo, akanunuliwa gari, akafunguliwa biashara mbili ambazo alitakiwa kuziendesha yeye mwenyewe. Mpaka kufikia kipindi hicho hakutaka kumficha mama yake, akamwambia ukweli kuhusu mzee Edward.
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo mama! Ananipenda, nipo naye kwa miezi sita,” alijibu Pamela.
“Huyo anataka kukuchezea tu halafu akuache,” alisema mama yake ambaye alionekana kuwa na hofu kubwa.
“Mama! Tupo kwenye uhusiano kwa miezi sita, hakuwahi kuniomba penzi! Tunakaa wote hotelini, chumbani lakini hataki kufanya mapenzi,” alisema Pamela, mama yake hakuamini, akauliza mara mbilimbili na jibu likawa hilohilo.
Mwanamke huyo akataka kuonana na mzee Edward, hilo halikuwa tatizo, mzee huyo alipopewa taarifa hiyo akaonana na mwanamke huyo. Alimchangamkia, akamwambia kabisa mama Pamela kwamba alimpenda mno binti yake, hakujali umri wake, alitamani sana kuwa naye ila kuna baadhi ya vitu hakuwa akivifanya kwa sababu ya mke wake aliyekuwa hoi kitandani.
“Bora umekuwa mkweli! Kwa hiyo una malengo gani na Pamela?” aliuliza mama yake.
“Ninataka kuishi naye! Ninataka kumpa furaha maishani mwake, najua moyo wake umekata tamaa ya kuishi, najua ameumizwa sana, huu ni wakati wa kubadilisha kila kitu, ninahitaji kumpa furaha moyoni mwake,” alijibu mzee huyo.
Mama Pamela akaridhika na mzee huyo, hakuwa na jinsi zaidi ya kutoa ruhusa. Kwa kitendo cha kuwa karibu na Mzee Edward, akaamua kabisa kumuacha Dickson, alijua namna ambavyo mwanaume huyo angemtafuta sana, alichokifanya ni kubadilisha namba ya simu kitu kilichomaanisha kwamba hakutaka kuwasiliana naye tena katika maisha yake.
Mapenzi yakanoga, Mzee Edward hakutaka kumficha mkewe, alijua kwamba alikuwa mgonjwa kitandani, alimjali lakini aliamua kumpa ukweli kuhusu msichana aliyekuwa amempata.
Hilo halikumuumiza mwanamke huyo, alimpenda sana mume wake, kwa miaka yote hiyo ya kuishi pamoja, hawakuwa wamepata mtoto japokuwa walikuwa matajiri wakubwa, Mzee Edward hakuwa na tatizo bali tatizo kubwa lilikuwa kwa mkewe aliyekuwa ameharibika mfuko wa uzazi.
Kwa kipindi chote hicho, mzee huyo hakutaka kumsaliti mkewe, alijua kwamba hakuweza kushika mimba lakini hilo halikumfanya kutembea nje ya ndoa yao, aliendelea kumjali na kumpenda kila siku.
Kitendo cha kumwambia kwamba alipata msichana ambaye aliamini kwamba angempa furaha, mwanamke huyo akafurahia, hakuumia, akamuita mumewe na kumkumbatia kisha kumbusu mdomoni.
“Sina muda mwingi wa kuishi mume wangu! Nahisi huu ndiyo mwisho wa safari yangu, nitakufa siku yoyote ile, ila naomba kabla sijafa nifanyie kitu kimoja,” alisema mwanamke huyo kwa sauti ndogo.
“Bila shaka mke wangu!”
“Naomba nimuone mwanamke uliyeamua kumchukua na kumsaidia,” alisema mwanamke huyo kitandani pale.
Mzee Edward hakuwa na jinsi, alitaka kumfurahisha mke wake katika siku za mwisho za uhai wake, alichokifanya ni kuondoka na aliporudi, alikuwa pamoja na Pamela, alimtambulisha kwa mke wake kwamba ndiye msichana aliyeamua kuwa naye kwa ajili ya kumpa furaha.
Mwanamke huyo alifurahi, alimshukuru Mungu kuonana na Pamela na baada ya siku tatu, akafariki dunia kitandani hapo kitu kilichomfanya Mzee Edward kuwa na maumivu makali moyoni mwake.
Msiba ukafanyika, mzee huyo alihuzunika na kulia, katika kipindi chote alichoishi na mke wake, waliishi kwa upendo mkubwa, alimpenda na kumthamini na kwake alikuwa kila kitu katika maisha yake. Wakamzika katika makaburi ya Kinondoni na baadaye kuamua kuishi na Pamela kitu kilichompa amani na furaha msichana huyo.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi mahali hapahapa.
Share kwa ajili ya marafiki zako.

No comments

Powered by Blogger.