Taarifa kutoka Ikulu: Rais Magufuli amtumia salamu za rambirambi kufutia kifo cha SACP Peter Kakamba
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu
kufuatia kifo cha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi (SACP) Peter Kakamba kilichotokea tarehe 30
Novemba, 2016 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam
alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika
salamu hizo Rais Magufuli amesema anaungana na askari wote wa Jeshi la
Polisi, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na
kifo cha SACP Peter Kakamba katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
“Natambua
mchango mkubwa alioutoa Marehemu (SACP) Peter Kakamba katika Jeshi la
Polisi na katika jukumu kuu la ulinzi wa raia na mali zao, kwa hakika
tumempoteza kiongozi aliyekuwa akifanya kazi zake vizuri” amesema Rais Magufuli.
“Nakuomba
IGP Ernest Mangu unifikishie salamu nyingi za pole kwa familia ya
marehemu, askari na wote walioguswa na msiba huu na sote tumuombee
Marehemu (SACP) Peter Kakamba apumzishwe mahali pema peponi, Amina” Amemalizia Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Post a Comment