KIFO CHA MTU ASIYE NA HATIA - 10 (MWISHO)

Prosper alitetemeshwa na swali la Alicia, alishindwa kuelewa ni jibu gani angempa mtoto wake, ingawa alielewa wazi ni kitu gani mtoto wake alitaka kufahamu! Ni yeye ndiye alikuwa na wajibu wa matatizo yote ndani ya familia yake na ni yeye ndiye aliyeuingiza Ukimwi ndani ya nyumba yake kwa sababu ya tabia ya kishoga aliyojifunza gerezani.
“Mwanangu Alicia!”
“Naam baba!”
“Ni mimi mwanangu ni mimi ninayekutesa!”
“Kwani ulifanya nini baba?”
“Ni mimi ninayekuua mwanangu!” Alisema Prosper na baadaye kuangua kilio.
“Ninahitaji kusamehewa sana Alicia na si wewe tu bali hata mke wangu anisamehe ninajua sote tutakufa kwa sababu ya uzembe wangu mimi!”
“Kwanini unasema hivyo baba?”
“Sikiliza Alicia, nilikutana na mama yako miaka mingi iliyopita tukiwa shuleni na tukapendana,lakini nilipata bahati mbaya ya kufungwa kwa kosa ambako sikulifanya, muda wote uliokuja kule nilikokuwa nikiishi nilikuwa gerezani lakini hatukukuambia ukweli ni huko gerezani ndiko nilikoambukizwa Ukimwi ambao mimi niliupitisha hadi kwa mama yako na kutoka kwa mama yako ndiyo ulifika kwako nisamahe mwanangu!”
“Kwa hiyo mimi naumwa Ukimwi baba?Kwahiyo nitakufa?” Aliuliza Alicia huku akilia machozi.
“Huo ndio ukweli mwanangu si wewe tu utakayekufa bali mimi pia na tutakufa sababu ya baba yako lakini hakuna sababu ya kumlaumu tumekwishachelewa hivyo ni vyema kumsamehe kwani maji yakimwagika hayawezi kuzoleka, sawa mwanangu Alicia?” Aliuliza Belinda akitegemea mtoto wake angetoa msamaha lakini alishangaa kuona Alicia akiendelea kulia kwa uchungu na kuwalaumu wazazi wake kwa kila kitu.
“Siwezi kuwasamahe kwani sikustahili kufa kwa sababu ya makosa yenu! Ee Mungu kwanini uliruhusu jambo hili linitokee mimi?” Alicia aliendelea kulia machozi! Maneno mengi aliyoyasema hayakuwa ya mtoto wa umri wake!
“Nisamehe mwanangu!” Alisema Prosper huku akimbeba Alicia na kumweka miguuni pake.
“Kwanini nikusamehe baba?”
“Nisamehe ni makosa yangu ndiyo yanayokutesa!” Aliendelea kusema Prosper.
Alicia aliendelea kulia na kuongea maneno ya kuwalaumu wazazi wake kwa kitendo walichokifanya kusababisha yeye asiifaidi dunia na kuyafupisha maisha yake, aliwalaumu zaidi kwa kitendo cha kutomwambia ukweli kwa kipindi kirefu na kutojali afya ake ili aishi maisha marefu zaidi.
“kwanini kama mlijua nilikuwa na Ukimwi hamkunifanyia kama daktari alivyoeleza, yaani kujali afya yangu ili niishi maisha marefu zaidi?”
“Tusamehe sana Alicia ni kwa sababu hatukutaka uujue ukweli huu!”
“Sasa imewasaidia kitu gani kunificha si ndio mneniua mapema zaidi wazazi wangu?” Alisema Alicia huku akijifuta machozi machoni pake.
Prosper na mke wake waliyajua makosa yao na hapakuwa na njia nyingine yoyote zaidi ya kumwomba msamaha mtoto wao, waliendelea kumwomba awasamahe kwa masaa matatu zaidi lakini Alicia hakujibu kitu zaidi ya kuendelea kulia, kila alipouangalia mwili wake ulivyokonda na kujaa vidonda alizidi kulia kwa uchungu na kuwatupia wazazi wake lawama.
“Basi nimewasamahe wazazi wangu ila yote namwachia Mungu aliyeruhusu jambo hilo litokee yeye ndiye anayejua mwisho wangu!”
“Ahsante Alicia!” Prosper na mke wake walijikuta wakiitikia kwa pamoja na kumkumbatia mtoto wao, waliyajua makosa yao.
***************
Hali ya Alicia iliendelea kuwa mbaya kadri siku zilivyozidi kwenda, jambo hilo liliwaumiza sana mioyo wazazi wake! Jamii ya wanafunzi katika shule aliyosoma walimtenga hawakutaka kucheza naye wala kusoma pamoja naye, alikaa peke yake katika dawati mambo hayo yalimkosesha raha kabisa na kusababisha achukie shule na kusimama masomo!
Wazazi wake walitumia karibu kila kitu walichopata kumtibia mtoto wao lakini haikusaidia kitu hali yake ilizidi kuwa mbaya hatimaye Alicia alikufa kwa kifua kikuu alichoogua siku za mwisho kabisa za uhai wake, lilikuwa pigo kubwa mno kwa Prosper na mkewe Belinda! Kilikuwa kilio kikubwa mno kilichowatia simanzi na moyo wa Prosper uliumiza zaidi sababu siku zot alijiona yeye ndiye alikuwa muuaji wa familia yake.
************
Baada ya kifo cha Alicia maisha ya Belinda na Prosper yalikuwa ni huzuni tupu, hawakuwa na kimbilio jingine zaidi ya kumwamini Kristo! Walijiunga na kanisa la Full Salvation Bible fellowship lililoko Mikocheni jijini Dar es Salaam, ambako waliamini wangepata faraja.
Wakiwa ndani ya kanisa hilo matumaini yao yaliyokwishapotea yalirejea! Walikutana na waathirika wengine ndani ya kanisa na kwa pamoja waliamua kuanzisha chama cha waathirika wakristo kilichoitwa Christians affected with HIV&AIDS Solidarity (CAHAS).
Chama hiki kiliwakutanisha waathirika wote Wakristo hata kutoka madhehebu mengine na kuwafanya wawe wamoja, Prosper ndiye alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho kilichojishughulisha na Elimu na ushauri nasaha kwa wagonjwa na waathirika wa Ukimwi! Kilifanya mikutano ya Dini iliyofundisha watu juu ya gonjwa hilo hatari.
Pamoja na faraja na matumaini kurejea, siku zote Prosper na mkewe hawakumsahau mtoto wao Alicia, karibu kila kitu walichokiona ndani ya nyumba yao na hata barabarani kiliwakumbusha mtoto wao,iliwatia uchungu sana kumpoteza mtoto wao mzuri! Kila siku iliyokwenda kwa Mungu hawakuacha kumwombea Alicia kwa Mungu ili apumzike kwa amani!
Mei 23 kila mwaka waliazimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Alicia, kama kumbukumbu ya mtoto wao. Maisha yao yaliendelea vizuri na walizidi kunawiri haikuwa rahisi kuamini kuwa wote wawili walikuwa waathirika na Ukimwi kwa jinsi walivyoonekana wanene wenye afya na siha njema! Lakini huo ndio ulikuwa ukweli wa mambo.
****************
Miaka mitano baadaye:
Mama wa kambo wa Belinda alikuwa katika hali mbaya kwa ugonjwa wa homa ya matumbo, homa hiyo iliutoboa kabisa utumbo wake sababu ya kuchelewa kupata matibabu, hali ambayo madaktari waliita Intestinal Perforation, madaktari walisema kwa hali ilivyokuwa ilikuwa si rahisi kuokoa maisha yake labda kubadilisha utumbo na kuweka mwingine jambo ambalo ilikuwa si rahisi kuwezekana.
Pamoja na mabaya yote ambayo mama yake alimfanyia ni Belinda aliyeshughulikia matibabu ya mama huyo, hakuwa na mtu mwingine wa kumsaidia zaidi ya Belinda.
“There is nothing we can do! Your mom’s intestines are badly perforated! Unless intestinal transplant is done! Which is not easy here!”(Hakuna kinachoweza kufanyika kwa sababu utumbo wa mama yako umetobolewa vibaya sana labda kuubadilisha kabisa jambo lisilowezekana kufanyika hapa) Daktari alimwambia Belinda.
“Where do you think that procedure can done, all we need is to save my mom’s life!”( Wapi unafikiri hilo linaweza kufanyika! Tunachohitaji ni kuokoa maisha ya mama tu) Aliuliza Belinda.
“There is no place in Africa, but why do you want to spend your money for an impossible mission?”(Hakuna mahali hapa Afrika lakini kwanini unataka kutumia pesa yako kwa kufanya jambo lisilowezekana?) Daktari alimuuliza Belinda ni hapo ndipo alipogundua haikuwa rahisi kuokoa maisha ya mama yake wa kambo.
Mama yake alifariki siku tatu tu baadaye na kabla ya kifo chake mama huyo alimrithisha Belinda kisheria mali zote alizoachiwa na mume wake akazikwa na idadi kubwa ya watu wa jiji la Dar es Salaam.
****************
Kufuatia kurithishwa mali za mamilioni Belinda na Prosper wakawa miongoni mwa watu matajiri katika jiji la Dar es Salaam! Magari yote yaliyoendeshwa na marehemu mama wa kambo wa Belinda yakawa mali yao! Majumba yote ya kifahari yakawa mali yao, watu wengi waliwaona wana maisha mazuri lakini kwa Belinda na Prosper mali haikuwa na maana tena kwa sababu maisha yao yalikuwa ukingoni.
Walichofanya na kilichowashangaza wengi ni uamuzi wao wa kuanza kuuza mali zote walizoachiwa na kugawa pesa iliyopatikana kwa vituo vya watoto yatima nchini, waliendesha mnada kila sehemu kulikokuwa na nyumba au mali za marehemu baba yao na pesa iliingizwa katika akaunti maalum ya kusaidia watoto yatima wa Ukimwi iliyofunguliwa katika benki ya CRDB!
Sifa zao zilienea nchi nzima na hata kuvuka mipaka ya Tanzania, walialikwa kuhudhuria mikutano mbalimbali ya Ukimwi duniani! Uamuzi wao wa kutumia walichokuwa nacho kusaidia mayatima wa Ukimwi ulikuwa ni wa kishujaa!
Wafadhili wa shirika la umoja wa Kimataifa linalojishughulisha na Ukimwi, UNAIDS waliposikia habari juu ya juhudi zao walisafiri hadi Tanzania na kufanya nao maongezi juu ya namna gani wangeweza kuwasaidia, baada ya makubaliano walilazimika kuanzisha mfuko maalum waliouita PROBE FUNDS! Yaani mfuko wa Prosper na Belinda, Pro ikisimama badala ya Prosper na Be ikisimama badala ya Belinda pesa yote waliyokuwa nayo waliingiza katika mfuko huo.
UNAIDS ilingiza kiasi cha dola za Kimarekani milioni tano katika mfuko huo na kuufanya mfuko huo kuwa na kiasi cha dola za Kimarekani milioni tano na nusu ambazo zilikuwa ni sawa na shilingi za Kitanzania bilioni nne na nusu!Pesa hizo zote zilitumika kusaidia mayatima wa Ukimwi, vituo zaidi ya mia vya kulea watoto yatima vilijengwa nchini Tanzania kwa kutumia pesa ya mfuko huo.
Prosper na mkewe hawakutumia hata senti tano kutoka katika mfuko huo, waliishi maisha ya kawaida hadi walipoanza kuugua na baadaye kufa wakiwa wamepishana miezi mitatu tu kati yao !Majina yao hadi leo hii yanaheshimika nchini Tanzania na mfuko wa Probe bado unaendelea kusaidia waathirika na mayatima wa Ukimwi!
MWISHO.
Post a Comment