KIFO CHA MTU ASIYE NA HATIA - 09

Mzee Nyonganyonga akawa amekufa tena kifo cha kujichoma mwenyewe kwa sindano ya sumu iliyomaanishwa kumuua Prosper kama hukumu ya mauaji aliyoyafanya! Kushuhudia kwa maiti yake ikitolewa katika chumba cha mauaji kulimfanya Belinda aamini kuwa aliyekufa ni mumewe Prosper, alilia na kuanguka chini akawa amepoteza fahamu!
Belinda alibaki katika hali hiyo kwa kipindi kirefu bila kujitingisha mtoto wake Alicia akiwa mgongoni kwake, Maaskari Magereza waliokuwa karibu walimfungua nguo aliyombebea mtoto na kumtoa mgongoni! Belinda aliendelea kulala chini bila kufahamu yoyote, maaskari walianza kufikiri alikuwa amepoteza uhai.
Kila mtu alishtuka na hapakuwa na njia nyingine ya kufanya zaidi ya kumkimbiza hospitali, maaskari wawili wenye nguvu walimbeba Belinda mikononi mwao na kuanza kumpeleka kwenye zahanati ya gereza ingawa hakuwa mfungwa.
“Kawaje huyu?” Daktari aliuliza baada tu ya Belinda kuingizwa hospitali.
“Ameanguka ghafla na kupoteza fahamu baada ya kumwona mume wake akitolewa chumba cha mauaji baada ya kunyongwa!”
“Mume wake kanyongwa?”
“Ndiyo!”
“Ni yupi huyo?”
“Ni mfungwa mmoja aliletwa hapa kutoka Tabora!”
“Aliitwa nani?”
“Prosper!”
“He! Yule kijana mpole mrefu?”
“Ndiyo!”
“Kanyongwa yule?”
“Kweli kabisa! Na huyu ndiye mke wake alipouona tu mwili wa mume wake ukitolewa chumba cha mauaji akapoteza fahamu!”
Daktari alisikitishwa sana na habari hizo lakini wakati maongezi hayo bado aliendelea kumpa Belinda matibabu! Dripu za maji ziliwekwa katika mishipa yake na kitanda kilinyanyuliwa miguuni ili damu nyingi zaidi itiririke kwenda kwenye ubongo, hatua ambazo daktari aliamini zingemrejeshea Belinda fahamu zake.
Dakika kama kumi hivi baadaye daktari akiwa bado katika masikitiko juu ya habari aliyopewa, mlango wa wodi ulifunguliwa na kijana mmoja mrefu akaingia akiongozana na maaskari magereza wawili, daktari alipomwona kijana huyo aliguna na kumwangalia askari magereza waliyekuwa naye.
“Mh! Si ulisema kijana huyu ndiye amekufa?” Daktari aliuliza na askari magereza aliyekuwa ameinama alinyanyua uso wake kuangalia mlangoni, hakuamini macho yake yalipokutana na sura ya Prosper.
“Hata mimi nashangaa sasa ni nani aliyekufa maana nilishuhudia mwili wa mtu ukitolea chumba cha mauaji na mtu aliyetakiwa kufa leo ni huyu au kimetokea nini maafande wenzangu?”Aliuliza askari huyo akiwaangalia maaskari wenzake waliosimama pembeni mwa kitanda alicholala Belinda.
“Ni habari ya kusikitisha sana!”
“Habari gani hiyo?”
“Mzee Nyonganyonga ndiye kafa!”
“Kafa? Kafa vipi?”
“Yeye ndiye kajichoma na sindano ya sumu badala ya kumchoma huyu kijana!”
“Mungu wangu kwanini?”
“Eti amechoka kuua watu wasio na hatia!”
“Nyie nani kawaeleza?”
“Katueleza huyuhuyu kijana!”
“Kwahiyo?”
“Maiti yake iko chumba cha maiti!”
“Na huyu Prosper itakuwaje sasa?”
“Ana bahati sana kwani kuna barua kutoka kwa Mwanasheria mkuu wa serikali adhabu yake imesitishwa mpaka uchunguzi wa kina ufanyike, kuna habari kuwa hakuyafanya mauaji!”
“Mkuu wa gereza ana taarifa hizo?”
“Ndiyo na tumetoka ofisini kwake sasa hivi tumemwacha anashughulikia barua ya kumwachia huru kijana huyu!”
Wakati maongezi hayo yakiendelea Prosper akiwa amembeba mtoto wake Alicia mikononi alikaa pembeni mwa kitanda alicholala Belinda akimwangalia kwa macho ya huruma hasa aliposikia habari kuwa alianguka na kupoteza fahamu baada ya kuona maiti aliyodhani ni yake ikitolewa chumba cha mauaji.
“Daktari mke wangu atapona kweli?”
“Atapona tu wala usiwe na wasiwasi!”
Baadaye daktari ambaye pia alikuwa askari magereza pamoja na maaskari wengine waliondoka na kumwacha Prosper peke yake pamoja na mtoto wake Alicia aliyeonekana kuwa na furaha kupita kiasi kuwa na baba yake.
“Dady wake mom up! We have to go home for Christimas, why has she slept all that time?”(Baba mwamshe mama, twende nyumbani kusherehekea Krisimasi kwanini amelala muda wote huo?) Alicia aliuliza akiwa amemkumbatia baba yake.
Prosper alielewa ni kiasi gani mtoto wake hakuuelewa ukweli juu ya mambo yaliyokuwa yakitokea, hakutaka kumweleza ukweli aliendelea kumbembeleza atulie mpaka mama yake akiamka ndio waondoke kwenda nyumbani.
Kama dakika arobaini na tano hivi baada ya daktari kuondoka, Belinda alijitingisha na kugeukia upande wa pili kisha akayafungua macho yake na kuanza kuangaza huku na kule chumbani, macho yake yalitua moja kwa moja usoni kwa Prosper!Hakuamini kama alichokuwa akikiona kilikuwa ni kweli, ilikuwa ni kama ndoto.
“Prosper!Prosper ni wewe au ni mzimu wako?”
“Ni mimi darling!”
“Lakini umekufa?”
“Sijafa bado niko hai!”
“Aliyekufa ni nani?”
“Ni aliyetaka kuniua badala ya kuniua mimi alijiua yeye!”
“Kweli au naota ndoto?”
“Huoti ndoto ni kweli kabisa Belinda bado niko hai ingawa natamani kufa!”
“Kwanini unasema hivyo Prosper?”
“Nakiogopa kifo kilichoko mbele yangu! Kifo cha Ukimwi ni kifo cha mateso mno ni heri ningechomwa sindano ya sumu nikafa!”
“Prosper kwanini unasema maneno mabaya kiasi hicho? Wala hunifikiri mimi na mwanao wakati hata sisi tutakufa kifo cha aina hiyohiyo? Kwanini sasa tusiishi pamoja mpaka Mungu atakapochukua maisha yetu ikiwezekana siku moja?”
“Sawa Belinda lakini....!”
“Lakini nini Prosper hutupendi mimi na mtoto wako?”
“Nawapenda Belinda na sitatamani kufa tena nimebadilisha msimamo wangu nashukuru kwa kuokoa maisha yangu Belinda!”
Dripu aliyokuwa nayo mkononi ilishachomoka, maji yote yalikuwa yakimwagika chini! Haikuwa rahisi kwa Belinda kuamini alikuwa pamoja na Prosper na wangeendelea kuishi maisha yao yote wakisubiri kifo! Yeye pia alikiogopa kifo cha Ukimwi lakini kufa pamoja na Prosper haikuwa huzuni kubwa, alijua wazi ni yeye na mchezo wake wa kishoga ndiye aliuleta ugonjwa huo katika familia yao lakini alishamsamehe na hakutaka kukumbuka tena.
*******************
Saa kumi ya jioni siku hiyohiyo waliruhusiwa kuondoka gerezani na kwenda nyumbani kwa Belinda, Prosper hakuamini alipoiona nyumba ambayo Belinda aliishi, ilipambwa na ilikuwa na kila kitu ndani! Maisha ya mke wake yalionekana kuwa mazuri.
“Belinda nyumba yako ni nzuri sana!”
“Sio yangu!”
“Ni ya nani sasa?”
“Sema nyumba yetu sio nyumba yangu!”
“Ok! Nyumba yetu!”
“Tutaishi hapa sote watatu mpaka mwisho wa uhai wetu, baba alinipa nyumba mbili lakini moja ilibidi niiuze ili kupata pesa za kumlipa huyu wakili wetu!” Belinda alisema akimuonyesha wakili wao aliyekuwa amesimama pembeni.
“Ahsante mke wangu kweli penzi lako ni la dhati ni hakika nimechangia sana kuyaharibu maisha yako nafikiri utanisamehe!”
“Usijali Prosper Mungu alipanga tuwe wawili maishani mwetu!”
Wakili wao hakukaa sana kitu kama masaa mawili baada ya chakula cha usiku aliondoka akiahidi kuonana nao kama wangemhitaji ni usiku wa siku hiyo ndiyo Prosper alilala usingizi mororo katika miaka karibu kumi iliyopita kabla.
“Prosper ni miaka mingi imepita nakumbuka mara ya mwisho ni wakati mtoto huyu anapatikana! Ninakuhitaji mume wangu!” Alisema Belinda kwa sauti ya mahaba.
“Hapana Belinda haiwezekani hata kidogo siwezi kuua mtoto mwingine asiye na hatia! Makosa makubwa niliyafanya kwa Alicia na sasa atakufa bila hatia kwa makosa yangu mimi”
“Lakini tunaweza kutumia kinga!”
“Kama ni hivyo sawa lakini sipo tayari upate mimba na kuzaa mtoto mwingine tutakuwa tunaua damu isiyo na hatia!”
“Sawa!”
Baada ya kukubaliana walifurahi kama mke na mume baada ya miaka mingi ya kuishi mbali na kila mmoja wao, ulikuwa ni usiku wa raha mno kwa Belinda pamoja na Prosper kujaa upele na ukurutu mwili mzima bado Belinda alifaidi kila alichofanyiwa.
Siku iliyofuata Belinda alimpeleka Prosper hospitali na kuishughulikia afya yake, katika muda wa miezi miwili tayari afya yake ilisharejea na Prosper alipendeza na kuvutia, uzuri wa sura yake ulianza kurudi.
Kwa pesa kidogo iliyobaki Belinda aliendelea na biashara ya kwenda Zanzibar kununua bidhaa na kuzikopesha maofisini, pesa iliyopatikana kama faida iliwasaidia kuendesha maisha na kutunza akiba kidogo.
****************
Miaka mitatu baadaye:
“Acha mimi niende Zanzibar wewe baki na mtoto si unamwona hali yake ilivyo?” Prosper alimwambia mkewe.
“Kwa kweli inabidi nibaki maana hali yake inazidi kuwa mbaya siku hadi siku, haya majipu ndiyo yanayomsumbua zaidi!”
“Itabidi kesho umpeleke tena kwa daktari ili wambadilishie dawa anazotumia!”
“Sawa mume wangu! Ila nunua mikoba ya kutosha maana mahitaji ni mengi hasa kwenye duka la Kariakoo”
Biashara yao ilishakuwa na maisha yao yalikuwa bora, walipata kila walichokitaka!Kasoro pekee waliyokuwa nayo ni afya ya mtoto wao Alicia, mtoto huyo aliugua karibu kila siku na alibadilisha magonjwa kama nguo.
Prosper alijisikia wajibu kwa ugonjwa wa mtoto wake, alijua bila yeye kujihusisha na ushoga gerezani na Savimbi, Alicia asingekuwa mgonjwa! Jambo hilo lilimuumiza sana moyo wake hasa alipoona jinsi mtoto wake alivyozidi kukonda.
Kila siku alipokwenda shule alirudishwa nyumbani akiwa hoi, ilikuwa akisoma wiki moja wiki ya pili anakuwa hoi kitandani! Belinda na mume wake walijua kilichokuwa kikimsumbua mtoto wao lakini hata siku moja hawakudiriki kumwambia ukweli ingawa mara kwa mara Alicia aliuliza juu ya ugonjwa uliokuwa ukimsumbua.
“Mama mimi naumwa nini mbona siponi? Kila siku naumwa! Mbona mimi siko kama watoto wenzangu?”
“Utapona tu mwanangu!”
“Ona haya majipu kila siku yanaota na kupona mpaka lini itakuwa hivi?”
Maswali ya Alicia kwa mama yake yalikuwa mengi kupita kiasi na yalimuumiza sana moyo Belinda!Alishindwa amjibu nini mtoto wake kwa maswali aliyoulizwa ingawa alijua siku moja ni lazima wamwambie ukweli na hakujua siku hiyo ingekuwa lini.
****************
Alicia shuleni:
St.Thomas ilikuwa ni shule maarufu ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam ni shule hiyo ndiyo Alicia alisoma, ilisifika kwa kutoa elimu bora kitu ambacho Belinda na mumewe wake walitaka kumpa mtoto wao ingawa walijua wazi alikuwa ni mgonjwa.
Siku hiyo ya Jumatatu Alicia alikuwa shuleni baada ya wiki nzima kupita bila kuingia darasani sababu ya majipu yaliyokuwa yamevimba mwilini mwake, alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo waliokuwa katika chumba cha mikutano wakimsikiliza mtaalam wa Afya akiongea na wanafunzi juu ya gonjwa hatari la Ukimwi lililotishia maisha ya Watanzania na lilimuogopesha Alicia kupita kiasi.
“Dalili zake ni nyingi lakini kubwa kabisa ni homa za mara kwa mara, kukohoa kwa muda mrefu, kuharisha, mwili kuwasha na majipu!” Alisema mtaalam huyo wanafunzi wote wakiwa kimya na kumsikiliza kwa makini.
Dalili zote ambazo mtalaam alizitaja zilikuwa mwilini mwa Alicia, mwili wake ulijaa upele, ukurutu na ulimwasha kupita kiasi, alikohoa na alikuwa na majipu mengi mwilini mwake!Homa hazikukatika, karibu kila siku alikuwa na homa na pia alipoteza uzito wa mwili na kukonda.
Dalili zilipotajwa wanafunzi wote ndani ya ukumbi waligeuka kumwangalia yeye! Kitendo hicho kilimuumiza moyo Alicia na kumfanya alie machozi.
“Kwanini mnaniangalia hivyo? Kwani mmeambiwa mimi nina Ukimwi?” Aliuliza Alicia na hakuna mtu aliyelijibu swali lake.
Hakutaka tena kubaki shuleni alitoka nje ya ukumbi na kutembea taratibu kwenda nyumbani kwao njia nzima akilia machozi! Hakuwa tayari kukubali kuwa alikuwa na Ukimwi, aliziona dalili alizokuwa nazo ni za ugonjwa mwingine wowote lakini si Ukimwi.
Alipofika nyumbani kwao aliingia ndani na kwenda moja kwa moja hadi chumbani kwa mama yake, alimkuta amejilaza kitandani, mama alishangazwa na hali aliyokuwa nayo mtoto wake.
“Vipi Alicia?”
“Mama niambie ukweli!”
“Ukweli gani mwanangu?”
“Mama kwanini mnanificha?”
“Tunakuficha nini Alicia?”
“Daktari ametufundisha kila kitu juu ya Ukimwi! Dalili zote za Ukimwi mimi ninazo, mama niambie ukweli je, mimi nina Ukimwi?”
Badala ya kujibu swali Belinda alianza kulia akiwa amemkumbatia mtoto wake Alicia mikononi, alitamani amwambie ukweli lakini aliogopa!Alijua ungemuumiza sana kwani siku zote alionekana kutishwa sana na ugonjwa huo.
“Mama usilie tafadhali niambie ukweli na kama ni Ukimwi mimi niliutoa wapi mbona bado mdogo? Nani aliniambukiza? Au ni wewe mama?” Alicia aliendelea kuuliza maswali mfululizo.
Belinda aliendelea kulia hakuwa na jibu la kumwambia mtoto wake, ilikuwa ni siku mbaya sana kwake, siku aliyotakiwa kueleza ukweli ambao aliuficha kwa muda mrefu.
Belinda aliendelea kutokwa na machozi mbele ya mtoto wake, hakuwa na kitu cha kumweleza Alicia aliyetaka kuufahamu ukweli kuhusu afya yake baada ya kuugua na kuteseka kwa muda mrefu.
Hakuwa tayari kuitoboa siri ya ugonjwa wa mwanae alijua wazi alikuwa mgonjwa na ugonjwa uliomsumbua ulikuwa ni Ukimwi uliompata yeye kutoka kwa mume wake naye akaufikisha kwa mtoto wao.
Alikuwa na uhakika asilimia mia moja hata yeye na mume wake walikuwa wagonjwa wa ugonjwa huo wakisubiri kifo! Lakini kwa upande wao aliona walistahili kwa sababu walishiriki tendo la ndoa! Alicia hakuwa na sababu yoyote ya kufa kwa kosa ambalo hakulifanya kifo chake kilikuwa cha damu isiyo na hatia.
“This is a death of an innocent blood!”(Hiki ni kifo cha damu isiyo na hatia!) Belinda alijikuta akitamka maneno hayo huku akilia machozi, Alicia alipoyasikia alishtuka.
“Mama unasemaje?”
“Nimesema hiki ni kifo cha damu isiyo na hatia, lakini si makosa yangu mwanangu ni makosa ya baba yako!”
“Nini mama mbona sikuelewi!?” Alicia aliuliza kwa mshangao, alishindwa kuvumilia kumwona mama yake akilia naye machozi yalianza kumtoka.
“Mama hakuna sababu ya kulia tafadhali niambie ni kosa gani baba alifanya?” Alicia aliendelea kudadisi.
Kabla Belinda hajafungua mdomo kujibu swali hilo mlango ulifunguliwa na Prosper akaingia, alishangazwa na hali aliyoikuta sebuleni! Mke wake na mtoto walikuwa wamekumbatiana wakilia na kwa jinsi mwili wa Alicia ulivyokuwa umekondeana uliishia katika mikono ya mama yake.
“Belinda vipi tena?” Aliuliza Prosper lakini hakuna jibu lililipatikana na aliendelea kuuliza tena na tena lakini bado Belinda hakujibu kitu chochote zaidi ya kumwaga machozi.
“Nini kimetokea mke wangu?”
“Alicia anataka kuufahamu ukweli!”
“Ukweli gani?” Prosper aliuliza.
“Juu ya afya yake, mimi nimeshindwa kumtobolea ukweli huo ni bora umweleze mwenyewe!” Alisema Belinda.
“Baba nielezeni ukweli nimeteseka sana na ugonjwa huu, ni miaka mingi naumwa lakini hamjawahi kunieleza naumwa nini lakini leo nataka kujua au ni Ukimwi nini? Nielezeni tu msiogope ili nikisubiri kifo changu vizuri!” Alicia aliongea kama mtu mzima, siku hiyo wazazi wake walimshangaa sana.
Prosper alitetemeshwa na swali la Alicia, alishindwa kuelewa ni jibu gani angempa mtoto wake, ingawa alielewa wazi ni kitu gani mtoto wake alitaka kufahamu! Ni yeye ndiye alikuwa na wajibu wa matatizo yote ndani ya familia yake na ni yeye ndiye aliyeuingiza Ukimwi ndani ya nyumba yake kwa sababu ya tabia ya kishoga aliyojifunza gerezani.
“Mwanangu Alicia!”
“Naam baba!”
“Ni mimi mwanangu ni mimi ninayekutesa!”
“Kwani ulifanya nini baba?”
Post a Comment