Ufafanuzi wa tuhuma za Freeman Mbowe Kwa wabunge wa CCM kupewa rushwa ya mil 10

Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe jana alisababisha taharuki
katika kikao cha Bunge baada ya kuzusha tuhuma za rushwa kwa wabunge wa
CCM katika kipindi cha maswali na majibu na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa.
Ingawa
swali lake hilo lenye tuhuma lilizuiwa kujibiwa na Naibu Spika, Dk
Tulia Akson kwa kuwa halikuwa swali la kisera, hoja iliibuliwa tena na
wabunge wengine wakati wa kuingia kipindi cha majadiliano, kama
miongozo.
Mbowe
katika swali lake kwa Waziri Mkuu alituhumu wabunge wa CCM, kupewa
rushwa ya Sh milioni 10 kila mmoja na serikali ya chama hicho ili
kuupitisha Muswada wa Huduma za Habari unaowasilishwa bungeni leo.
Aidha
alidai rushwa hiyo, pia imetolewa kupitisha Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa mwaka 2017/18. Pamoja na tuhuma hizo kutojibiwa na Waziri Mkuu
kutokana na muundo wa maswali ya papo kwa hapo kugusa sera, Mbunge wa
Momba, David Silinde (Chadema) aliomba mwongozo wa Spika huku akitaka
kuundwe Tume Huru ya Kimahakama ya Bunge, kuchunguza tuhuma hizo.
Naye
Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) alisimama na kuomba mwongozo, na
kumtaka Mbowe athibitishe tuhuma hizo au achukuliwe hatua.
Nkamia
alisema yeye akiwa Mbunge wa CCM, hajapata rushwa hiyo wala hakuiona na
kuhoji kwa nini Mbowe ahoji wakati yeye si Mdhibiti na Mkaguzi wa
Hesabu za Serikali (CAG), hivyo akitaka Mbowe athibitishe tuhuma hizo na
akishindwa, alitaka mwongozo ni hatua gani Bunge itamchukulia.
Akijibu
hoja zote hizo za wabunge, Naibu Spika alimtaka Mbowe kupeleka tuhuma
zake kwa vyombo husika ili vichukuliwe hatua stahiki.
Akifafanua
zaidi, Naibu Spika katika majibu yake ya miongozo hiyo alisema
:“Wabunge tuwe makini, ukisema kuna rushwa ujue kuna vyombo vyake
maalumu vya kushughulikia hilo, Bunge haliwezi kusikiliza kesi hizo,
Bunge na Waziri Mkuu hawana mamlaka kwa mambo yasiyohusiana nayo,
nashauri suala hilo lipelekwe kwenye vyombo husika.”
Kuhusu
mwongozo wa Nkamia, alisema kwamba hatomtaka Mbowe athibitishe kwani
alimzuia kuliongelea, lakini mwenye uthibitisho apeleke kwenye chombo
kinachohusika na rushwa ili kifanye kazi yake.
Mbowe aitisha mkutano
Baada
ya tafrani hiyo kuzuka bungeni na kumalizwa na Naibu Spika kwa
kutoruhusu mjadala wake, Mbowe aliitisha mkutano na waandishi wa habari
katika ukumbi wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Bunge mjini hapa,
akiwa na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu na viongozi
wengine wa Chama cha Wananchi (CUF).
Katika
mkutano huo, Mbowe alimtaka Rais Magufuli kumtumbua Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa kwa kile alichoeleza kuwa yeye (Majaliwa) pamoja na Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana walihusika kutoa kwa wabunge hao wa CCM
272 fedha hizo.
Alisema
pia kuwa, wanamuandikia barua Rais kutaka aunde Tume ya Kimahakama ya
Uchunguzi, kuchunguza suala hilo kwa kuwa linawahusu wabunge, na Bunge
haliwezi kujichunguza lenyewe.
Akifafanua
kuhusu fedha hizo, Mbowe alisema taarifa walizonazo, zinathibitisha
kuwa katika kikao cha wabunge wa CCM cha Oktoba 25, mwaka huu, Majaliwa
na Kinana waligawa fedha Sh milioni 10 kwa kila mbunge wa CCM ili
kuwapooza kuhusu hali ya mdororo wa uchumi.
Alisema
pia kuwa fedha hizo, zilizoanza kutolewa Oktoba 26, zililenga pia
kuwashawishi wabunge hao wa CCM, kupitisha Muswada wa Huduma za Habari
wa mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18, ambao
mapendekezo yake yamewasilishwa bungeni.
Mbowe
alisema tuhuma hizo ni nzito na Bunge haliwezi kujichunguza lenyewe,
hivyo ni lazima iundwe tume huru ya kimahakama kuchunguza jambo hilo.
Mbowe alisema ushahidi wa kutosha wanao na watautoa mbele ya tume hiyo.
Mbowe
alisema walimshangaa Naibu Spika, Dk Akson kwa kuwazuia kutoa ushahidi
ndani ya Bunge, kama walivyoombewa mwongozo na Nkamia. Alieleza kuwa
hiyo ni mara ya kwanza kwa upinzani, kuzuiwa kutoa ushahidi kwa jambo,
ambapo linaonekana kama ni uongo.
Lisu naye azungumza
Kwa
upande wake, Lissu alisema watamuandikia Rais Magufuli barua rasmi
kueleza kilichofanywa na viongozi wake, na kumtaka achukue hatua kuhusu
suala hilo.
“Magufuli
amejinadi yeye anapambana na ufisadi, mtihani wa pili aufanye na
aufaulu ni huu. Magufuli amtumbue Kassim Majaliwa kutoka kwenye nafasi
hiyo ya uwaziri mkuu,” alisema Lissu.
Lissu
alisema Sheria ya Tume za Uchunguzi, inampa Rais mamlaka ya kuunda tume
ya uchunguzi kwenye jambo kubwa na muhimu, linalohusu mambo ya umma.
“Katika
barua hiyo tunamgusia Tulia Ackson. Kwa maoni yangu kisheria, kiongozi
wa kuteuliwa anaondolewa na mamlaka ya uteuzi, Rais amuondoe huyu mama
bungeni, hafai,” alisema Lissu.
Viongozi wa CUF waliokuwa katika mkutano huo ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Mngwali.
Awali,
ndani ya Bunge baada ya Naibu Spika kuzuia swali hilo kwa kuwa si la
kisera, Mbowe akinukuu Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma ya mwaka
1995 na Sheria ya Rushwa ya mwaka 2007, alisema masuala ya rushwa ni ya
kisera.
Hata
hivyo, Dk Akson alimtaka Mbowe kuheshimu kiti na kanuni, na kusisitiza
kuwa, yeye (Naibu Spika) anaongozwa kwa kanuni na kanuni zinaeleza kuwa
swali hilo si la kisera.
Post a Comment