Eric Shigongo: Novemba 19, 2016 Jumamosi ya Machozi Kwangu
Kumbukumbu za Kweli za Maisha Yangu Eric Shigongo.
Nawaomba radhi sana wananchi wa Singida, sikuweza kuwepo Namfua baada ya waandaaji kuahirisha tamasha, ipo siku tutakutana.
Nimekwishasema mara
nyingi kwamba, hata mimi, kama ilivyo binadamu wengine huwa nina siku
mbaya na nzuri katika maisha yangu, kwa sababu kwa watu wengi tafsiri ya
maisha bora ni kuwa na gari, nyumba, kazi, fedha nk. Ni rahisi kudhani
kwamba ninaishi maisha ya furaha kila siku, si kweli, kuna siku natokwa
na machozi kama binadamu mwingine, naomba nikushirikishe sasa siku yangu
ya Novemba 19, 2016, siku ya Jumamosi iliyopita, ili upate uhalisia wa
maisha.
Usingizi ulikata saa tisa na nusu usiku,
nikaanza kuyapitia maisha yangu na changamoto ninazokutana nazo, mambo
ninayoyafanya lakini pia kufanyiwa na watu. Mawazo yangu haya
yananifikisha kwenye uhusiano wangu na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho
kwa muda mrefu sana nimekuwa kada wake, mara kadhaa nikijitoa mhanga
mimi mwenyewe kukitetea na kukipigania nikiamini ndiyo chama pekee
kinachoweza kuwaletea Watanzania mabadiliko ya kweli.
Naipenda CCM, nakiamini chama hiki hata
kama kuna baadhi ya watendaji ndani yake natofautiana na jinsi
wanavyofanya mambo kiasi cha kuathiri hatma ya chama hiki kama taasisi,
wapenzi, mashabiki na wanachama wake.
Pamoja na kuwa mfanyabiashara nimewahi
kuacha kazi zangu na kuzunguka karibu nusu ya nchi yetu nikipiga kampeni
na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, lakini kwa sababu mtu yeyote anayeonesha
mapenzi kwa CCM hasa akiwa mfanyabiashara hutafsiriwa anajipendekeza au
mwoga, pengine hivyo ndivyo ninavyoitwa, lakini kwangu mimi ambacho
hunisukuma kufanya mambo haya ni mapenzi na imani niliyonayo kwa CCM
kama taasisi na zilivyo sera zake.
Kama nilivyosema hapo awali, tatizo
langu kubwa huwa ni watendaji wa CCM, ambao wakati mwingine hufanya
mambo ambayo huathiri mapenzi yangu kwa taasisi yenyewe, hali hii
imewavunja moyo watu wengi sana waliokuwa na mapenzi pamoja na imani
kubwa kwa CCM.
Yesu ni mwokozi wangu, daima
nitazungumza ukweli, hata kama utanigharimu! Nakumbuka huko nyuma
nimewahi kuzungumza ukweli kuhusu CCM kwenye ukurasa huu, baadhi ya
viongozi wa juu hawakufurahishwa na nilichokiandika, Katibu Mkuu Kinana
nikiongea naye ofisi kwake aliniambia “Eric wewe ni kijana wa hapa, siku
nyingine ukiwa na suala la kuzungumza tueleze sisi moja kwa moja,
usilipeleke barabarani!”
Nilikubaliana naye na sikuwa tayari
kabisa kusema maneno yaliyotokana na mawazo yangu ya usiku gazetini
tena, kwani nilimuahidi nisingefanya hivyo, lakini nifanye nini, nisemee
wapi? Kama katibu mkuu wangu nampigia simu kila siku hapokei?
Namuandikia ujumbe kwa njia ya WhatsApp na unaonekana umesomwa lakini
hanijibu, tafsiri yangu ni ya haraka ni kwamba ananidharau ingawa mimi
namuheshimu kama baba na kiongozi wangu, angalau angekuwa anapokea simu
hata kunipa tu matumaini, nisingefikia hatua ya kuzungumza hapa.
Kuanzia usingizi ulipokata saa tisa na
nusu usiku, nilifikiria mambo mengi sana juu ya namna ambavyo baadhi ya
watendaji wa CCM wamekuwa wakinifanyia pamoja na kujitoa kwangu kote kwa
chama hicho, moyo unaniuma mno kwani sistahili hata kidogo kufanyiwa
mambo ambayo leo natendewa na chama ambacho mimi binafsi naamini
nimejitoa kiasi kikubwa mno kukitumikia kwa akili, muda na mwili wangu.
Inahitaji usiwe mtu mwenye hofu au
uliyekata tamaa kufungua mdomo na kuzungumza nitakayoyasema leo, ndugu
zangu, Watanzania wenzangu, moyoni mwangu pamejaa uchungu mwingi mno,
acha niseme labda nitakuwa mwepesi! Sijui kitakachonipata, Mungu anajua,
mimi ni msema kweli, nionavyo mimi ni bora kuzungumza ukweli ukapata
matatizo kuliko ubaki hai ukiendeleza unafiki, NASHINDWA.
Mawazo haya juu ya CCM yananitoa
machozi mke wangu akiwa usingizini kando yangu, sitaki kumuamsha,
sitaki kumshirikisha kinachoendelea, mimi ni mtoto wa kiume mambo
mengine natakiwa kukabiliana nayo mwenyewe, kwa muda mrefu naendelea
kuwaza nikiwapitia viongozi mbalimbali wa CCM kuanzia mwenyekiti
mstaafu, mwenyekiti aliyeko madarakani, katibu mkuu na mweka hazina.
“Mama!” saa kumi na mbili na dakika kumi namuamsha mke wangu.
“Bee!”
“Tulikubaliana kwenda hospitali Muhimbili kusalimia mgonjwa.”
“Kweli.”
“Mzima lakini?”
“Naendelea vizuri, wewe?”
“Mimi mzima, nina mafua tu kidogo!” nilimjibu hivyo kwa sababu sikutaka agundue kilichokuwa kimetokea.
Kawaida ya wanawake ni kujiandaa
taratibu sana, mpaka tunaondoka kwenda Muhimbili tayari ilikuwa ni saa
moja asubuhi, tumechelewa muda wa kuona wagonjwa. Mbele ya Jengo la
Mwaisela, alipolazwa mgonjwa ambaye ni mkamwana wa mama mmoja aitwaye
Mama Swai, ambaye tulikuwa tukiabudu naye Kanisa la Word Alive kabla
hatujahamia Victory Christian Center, tunakutana na mlinzi mkali kama
pilipili.
“Muda wa kuona wagonjwa umekwisha.”
“Tusaidie kaka” nambembeleza kwa muda,
hatimaye akionekana kunionea huruma, anasema “basi aende mmoja tu, tena
mwanamke, maana hii wodi ni ya wanawake.”
“Mama nenda basi wewe!”
Mke wangu anaondoka na kuniacha
nimesimama peke yangu nje ya wodi, mawazo yananirejesha tena kwa CCM
baada ya kubaki peke yangu, najiuliza ni kitu gani nimekikosea chama
hicho mpaka kunitendea mambo wanayonitendea! Roho inaniuma, nasikia
huzuni kubwa moyoni mwangu, niko chini kabisa kiroho leo, sina furaha
hata kidogo, mawazo ya CCM na mambo wanayonitendea, wakati mimi
nilishafanya mema mengi kwao yamenivuruga.
Dakika ishirini baadaye mke wangu
anatokeza kutoka wodini, alikuwa amepewa muda mfupi sana, pamoja
tunaongozana mpaka kwenye gari, namfungulia mlango, anaketi nami nakaa
kwenye usukani na kuanza kuendesha kuelekea ofisini, anawahi kazini
kwake kwa sababu leo ana sherehe ya watu waliokodisha hoteli.
Njiani nasikia wimbo wa vijana kutoka
Kenya waitwao Sauti Sol, uitwao ‘Kuliko Jana’ nilishawahi kuusikia wimbo
huo kabla, lakini leo unaonekana kuwa wimbo mpya kabisa kwangu, maneno
yake yananigusa sana moyo, namshikirisha Vene kwenye wimbo huo,
anaonekana kama hanielewi au ninachokiongea hakimgusi, bila shaka
anawaza sherehe inayofanyika hotelini kwake.
“Hawa vijana wanaimba sana, natamani
siku moja niwaalike hapa Dar es Salaam, nifanye tamasha kubwa la vijana
kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu, bure! Nifundishe vijana wa taifa hili
uzalendo na kupenda nchi yao.” Natamka maneno hayo ingawa moyoni mwangu
kuna uchungu mwingi;
Bwana ni mwokozi wangu,
Tena ni kiongozi wangu,
Ananipenda leo kuliko jana!
Baraka zake hazikwishi si kama binadamu habadiliki,
Ananipenda leo kuliko jana,
Kuliko jana, kuliko jana,
Yesu nipende leo kuliko jana,
Kuliko jana, kuliko jana,
Yesu nipende leo kuliko jana,
Nakuomba Mungu uwasamehe
Wangalijua jinsi unavyonipenda
Mimi wasingenisema
Na maadui wangu nawaombea
Maisha marefu wazidi kuniona ukinibariki
Ujue binadamu ni watu wa ajabu sana
Walimkana Yesu mara tatu kabla jogoo kuwika…
Safari inaendelea, wimbo uliokuwa
ukipigwa redioni umefika mwisho, kwa kutumia simu yangu nilitafuta ‘You
tube’ kisha kuuchagua wimbo huo ambao unaendelea kupiga mpaka namfikisha
mke wangu ofisini kwake, kila unapokwisha naurudia tena, unanizidishia
uchungu moyoni, namshusha mke wangu na kuendesha tena kuelekea ofisini
kwangu.
Mawazo ni mengi, kichwa kimevurugika,
Mariam, msaidizi wangu anaingia na kunitayarishia chai, nakunywa lakini
haipandi. Baadaye anaondoa vyombo na kuniacha peke yangu, muda mfupi
baadaye aliingia mzee Mbizo, sijui kama alinielewa kwa hali aliyonikuta
nayo, nilikuwa kwenye siku yangu mbaya, niko chini sakafuni nawaza,
baada ya salamu tu tofauti na siku nyingine zote ambazo mimi na yeye
huongea mambo machache, anaaga na kuondoka.
Nabaki peke yangu nikiendelea kufikiria,
naikumbuka siku ya mwisho nilipofika ofisi ndogo ya CCM pale Lumumba,
ambako nilikwenda nikitarajia kulipwa fedha zangu ninazodai kwa kazi
niliyoifanya (kwa leo sitataja ni kiasi gani) kama nilivyokuwa
nimeahidiwa baada ya kuwa nimesubiri mwaka mmoja na miezi sita, hapo
katikati nikiwa nimelipwa fedha kidogokidogo sana.
Tofauti na matarajio kwamba siku hiyo
ningelipwa fedha zote, nikalipwa kiduchu tena! Nikiwa ndani ya ofisi ya
mweka hazina wa chama, mama Zakia Meghji, yeye ni shahidi, kama nasema
uongo au ukweli anajua, machozi yalinitoka! Hali yangu kibiashara ni
mbaya, fedha nyingi ziko mikononi mwa CCM na nina madeni makubwa
ninayodaiwa, baadhi ya wadai wanataka kupiga mnada mali zangu! Chama Cha
Mapinduzi kimeniingiza kwenye matatizo makubwa.
Nakumbuka alichokifanya mama huyu ni
kunipa chupa ndogo ya maji ya Kilimanjaro na kuniambia “Kunywa maji
mwanangu, upunguze uchungu!” nikayapokea na kuyanywa, niliondoka ofisini
hapo nikiahidiwa kwamba ningelipwa muda si mrefu, lakini haikuwa hivyo,
siku zinazidi kusonga na hali inazidi kuwa mbaya na hakuna anayeonekana
kujali.
Kwenye saa 5: 00 asubuhi hivi, naamua
kuachana na mawazo hayo kwani maisha bado yanaendelea na kuamua kwenda
kuungana na wenzangu kwenye kikao cha asubuhi kujadili maendeleo ya
Gazeti la Ijumaa Wikienda ili nifute kilichokuwa kikiendelea kichwani,
nafanikiwa kufanya kikao hicho bila mtu yeyote kugundua kilichokuwa
kikiendelea akilini mwangu na baadaye narejea ofisini ambako naendelea
kuusikiliza Wimbo wa Sauti Sol huku nikizidi kuhuzunika.
Muda mfupi baadaye anaingia Davina Lema,
msimamizi wa kampuni yetu ya Blue Mark Real Estate ambayo
inajishughulisha na upangishaji wa nyumba, tunaongea naye kuhusu
biashara na namna ya kufanya biashara katika kipindi hiki kigumu,
nampenda Davina, alianza kazi hii akiwa hajui chochote lakini sasa
amemudu kazi, baada ya mazungumzo hayo ndiyo naanza kumweleza kidogo
kuhusu maisha na namna ambavyo mtu unaweza ukatenda wema lakini ukalipwa
ubaya.
Sikuweza kuzungumza hadi mwisho, machozi
yananitoka mbele ya mfanyakazi wangu, si jambo jema lakini sikuwa na
jinsi, siandiki haya ili nionewe huruma la hasha! Nawaeleza muone baadhi
ya siku zangu ambavyo huwa zinakuwa, mtu asinione napita barabarani
akadhani maisha yangu ni keki kila siku, kuna mateso na maumivu makubwa
nyuma yake!
Alichofanya Davina ni kunitafutia tishu
za kufutia machozi kisha kuondoka baada ya meneja wetu mkuu, Abdallah
Mrisho kuingia na kunikuta katika hali mbaya niliyokuwa nayo, akaketi
chini na kuanza kunidadisi ni kwa nini nilikuwa nalia! Kwikwi ilikuwa
imenishika sikuweza kuongea, kuna jitu lilikuwa kooni ambalo nahisi ni
hasira.
“Braza inaniuma sana,
nimejitahidi maishani mwangu kuwa mtu mwema, nikikusanya senti tanotano
kwa njia halali mpaka kufika hapa nilipo, mimi ni tofauti sana na
wanasiasa ambao wanaweza kutia saini mkataba mmoja tu wa kifisadi
wakaingiza bilioni ishirini au watoto wa viongozi wanaoweza kutumia
majina ya wazazi wao kujipatia mikataba minono ya kuwatajirisha, kaka
unajua mimi nadunduliza kila siku nikijinyima na kuishi maisha ya
kawaida ili niwaachie watoto wangu urithi, leo hii nahisi kabisa nataka
kunyang’anywa haki yangu niliyoitesekea kwa muda mrefu, inaniuma!
Kwa mwili huu nilikuwa na uwezo
wa kushika bunduki na kuingia benki kuchukua fedha au kwenda Brazil
kupakia mzigo mkubwa wa heroin au Cocaine na kuleta hapa nyumbani kuja
kuharibu watoto wa watu akili, sikutaka kufanya hayo yote kwa sababu
sitaki kufanya dhambi au kupata fedha ambazo baadaye nitajilaumu,
nimechagua kufanya biashara halali kuanzia gazeti la shilingi mia moja
mpaka leo shilingi elfu moja, kwa nini sasa kikundi fulani cha watu
kininyime haki yangu? Sitakubali, ni bora nife kuliko kubaki hai wakati
haki yangu inataka kuchukuliwa na wanaoona kwamba wana nguvu na hawawezi
kufanywa chochote.”
Wakati nayasema maneno hayo yote
nilikuwa nikilia kwa uchungu mno, meneja mkuu alijaribu kunituliza
lakini alishindwa, roho ilikuwa ikiniuma sana, mimi mtoto wa maskini,
niliyetoka chini kimaisha nikapambana mpaka hapa nilipo, unidhulumu
kiasi kikubwa cha fedha namna hiyo? (nitakitaja hivi karibuni). Hapana,
ni bora kufa au kupigania haki mpaka tone la mwisho, huko ndiko kunaitwa
kuwa mwanaume.
Baadaye nilitulia, tukazungumza na braza
Mrisho kwa muda mrefu akinisihi nitulie wala nisichukue hatua yeyote,
yeye akiamini haikuwa rahisi kudhulumiwa wakati tulikuwa na mikataba!
Jambo moja ambalo hakulifahamu ni kwamba dhamana tulizoweka kwa
waliotukopesha fedha zingeweza kuuzwa, hata kama baadaye tungelipwa na
CCM ingekuwa haina maana kubwa, wazungu wana msemo usemao “Justice delayed is justice denied”
yaani haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki ambayo haikutolewa, wakati
wa kulipwa na CCM ni sasa ili tuepuke kuuziwa dhamana zetu.
Alipoondoka meneja mkuu ofisini kwangu,
aliingia Nyemo Chilongani, mmoja wa vijana wachapakazi ofisini kwangu
ambaye husimamia ukurasa wangu wa Facebook, aliongozana na wasichana
wawili ambao aliwatambulisha kwangu kama mashabiki wa ukurasa wangu
ambao walikuja ofisini kununua vitabu na walitaka niwasainie vitabu vyao
na pia tupige picha pamoja.
Wasichana hawa walikuwa ni Zainabu na
Dina kutokea Kigamboni, mara moja nilibadilisha muonekano wangu kama
vile kilikuwa hakijatokea kitu, tukaanza kuongea mambo mbalimbali kuhusu
maisha, nikiwaeleza umuhimu wa kuthamini vipaji maishani, ambavyo kila
mmoja wetu anavyo, “Mtu anaweza kufeli darasani kama nilivyokuwa
nikifeli mimi, lakini kipaji kikamuinua na kumfanya awe mtu mwenye
mafanikio!”
Mwisho wa mazungumzo yetu nilipiga nao
picha na kwa kweli walifurahi kukutana nami ambaye ujio wao na
mazungumzo tuliyoyafanya ulisaidia sana kubadilisha akili yangu na
kunipa uwezo wa kuketi chini na kuandika haya unayoyasoma leo.
Hivyo ndivyo siku yangu ya Novemba 19,
2016, ilivyoanza, nifuatilie wiki ijayo nipate kukueleza kwa undani
kilichotokea mpaka nikajikuta katika haya niliyoyaandika leo.
Tukutane wiki ijayo…

Post a Comment