HUYU NI MESUT OZIL WA ARSENAL, ISHI KAMA ANAVYOISHI YEYE
Na Saleh Ally
MWAKA
2010 nilibahatika kumuona Mesut Ozil akiichezea Werder Bremen kwenye
uwanja wao wa nyumbani. Nikahoji kuhusiana na mchezaji huyo, kwamba vipi
hayuko klabu kubwa kama Bayern Munich?
Mwenyeji wetu uwanjani pale akasema, mjadala wa viongozi wa Werder Bremen
ni
kuwa Ozil ni kati ya wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kufika mbali
na anachukuliwa kama sehemu ya mradi katika klabu hiyo na wanaamini
baada ya muda atakwenda Bayern Munich au klabu kubwa za Hispania na
England.
Akanifafanulia
mimi na Mtanzania mwingine ambaye tulikuwa pale uwanjani mjini Bremen,
Ujerumani kwamba kinachoweza kumkwamisha Ozil ni misimamo, hasa ile ya
kidini kwa kuwa wakati mwingine anakataa kufanya mambo kadhaa kwa kuwa
Uislamu unakataza.
Mimi
ilinishangaza, sikuamini mtu anaweza kukwama kwa kufuata misingi ya
dini na hata nilipomueleza, mjadala ulikuwa mrefu bila sababu za msingi,
nikaamua kuacha.
Miezi
michache baadaye Ozil mwenye asili ya Uturuki, aliondoka Bremen na
kujiunga na Real Madrid. Nikapata nafasi ya kuwasiliana na rafiki yangu
huyo ambaye aliniambia kwa soka atafika mbali, bado anaamini hivyo ila
kwa ile misimamo yake atafeli. Bado Ozil akafanya vizuri na Real Madrid,
tena sana.
Ilipofikia
anaondoka kwenda Arsenal, rafiki yangu alikuwa wa kwanza kunipigia na
kuniambia anaondoka kwenda London kutoka jijini Madrid, kwake aliona
kama anafeli na kocha alikuwa hajafurahishwa na misimamo yake, kwa
kifupi alidai ni mtukutu wa chinichini.
Nikamueleza
alikuwa akienda Arsenal kwa bei kubwa ya pauni milioni 42.5 ambayo ni
rekodi kwa Arsenal, ukaanza tena mjadala mrefu usio na faida. Nikaamua
kuachana nao.
Tangu
ametua Arsenal, Ozil ni staa na tegemeo katika kikosi hicho cha Arsene
Wenger. Asipofunga anatoa pasi ya bao na amekuwa gumzo kwa pasi zake
ndani ya England.
Jicho
la Wenger linastahili pongezi kwa kuwa kamnunua mchezaji wake wa kwanza
kwa bei ghali licha ya kupewa sifa ya ubahili, kweli imeonekana
alilenga na alichofanya ni sahihi.
Baada
ya Kocha Jose Mourinho aliyewahi kumfananisha Ozil na Zinedine Zidane
kutokana na pasi zake kuonyesha nia yake ya kumsajili atue Man United,
nami nikampigia simu rafiki yangu wa Ujerumani na kumkumbusha namna
ambavyo Ozil anavyozidi kupaa akipitia misimamo yake. Ukaanza ule
mjadala mrefu ambao umejaa ubishi usio na msingi, nikauacha tena.
Pamoja
na kuuacha mjadala huo, kwangu nimejifunza kwamba ni vizuri binadamu
kuwa na misimamo yako, kuishi unavyotaka ilimradi unakuwa na nidhamu na
kazi yako, pia unawaheshimu watu waliokuzunguka na wengine wote
inapobidi.
Ozil
amekuwa akizungumza namna anavyofanya. Katika kila mechi husali mara
sita. Kipindi cha kwanza, kabla ya kuingia, akiwa na wenzake na wakati
akitoka na kipindi cha pili hivyohivyo.
Amewahi
kuzungumzia suala la kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kwamba kuna
wakati huwa hafungi kwa kuwa analazimika kula na kunywa maji mengi
kulingana na hali halisi, lakini bado kuna baadhi ya mechi hucheza akiwa
amefunga.
Ozil
ni kati ya wachezaji wanaoendesha magari makali ya bei ghali, kati ya
wachezaji wachache kabisa wenye nyumba kali na ghali. Zile anazoishi au
alizonunua, zote ni nyumba hasa.
Hata
mpenzi, amechagua mrembo hasa na ukimuona utasema naam! Huyu ni mtu
anayefanya mambo yake anavyotaka yeye, anaishi anavyotaka yeye lakini
kazi yake inaonekana ni bora kila anapokwenda.
Katika
sehemu alizopita hasa katika suala la utoaji pasi, Ozil alikuwa
mwanasoka bora kwa utoaji pasi zinazozaa mabao Ulaya yote, hii ilikuwa
ni msimu wa 2010-11. Jiulize watu kama Andres Iniesta na Xavi Hernandez
walikuwa wapi na aliwazidi vipi, jibu ni kwamba ana kipaji na anajituma
kwa sababu anaithamini kazi yake.
Msimu
wa 2011-12, Ozil alikuwa ndiye namba moja katika utoaji pasi hizo za
mabao maarufu kama asisti mbele ya Xavi ambaye aliaminika ni pass master
wa La Liga. Hiki si kitu kidogo.
Katika
Kombe la Dunia mwaka 2010 ambako Ujerumani ilishika nafasi ya tatu na
Hispania kulibeba ikiifunga Uholanzi kwa bao la Iniesta, yeye ndiye
alikuwa mtoa pasi bora na nyingi zilizozaa mabao.
Alipotua
Arsenal, hilo tena limejirejesha na ameonyesha hii kazi ya utoaji wa
pasi za mabao si kazi anayoibahatisha na Mourinho hakukosea kumfananisha
na Zidane.
Leo
anamhitaji, inaonyesha wazi kabisa kwamba Mourinho amegundua anakosa
mtoaji wa pasi za mabao kwa kuwa watu wa kumalizia anao wa uhakika
lakini hawana fundi nyuma yao.
Hauwezi tena ukakataa kuwa Ozil ndiye staa wa England kwa kipindi hiki kwa maana ya ubora wa kazi, wengine watamfuatia.
Licha
ya kuwa si mwenye mambo mengi nje ya uwanja, Machi mwaka huu alifikisha
mashabiki milioni 28 kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook na kushika
nafasi ya saba baada ya Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, David Beckham,
Neymar, Kaka na Ronaldinho, wengi wakiwa wamejichimbia mizizi tokea
awali.
Kupitia
Ozil unaweza kujifunza mengi, mfano kumuachia mtu aishi maisha yake na
kuikubali kazi yake. Pili kuishi unavyotaka lakini ukafanya kazi yako
kwa ubora wa juu. Ozil anaonekana anaipenda kazi yake na anajituma,
ndiyo maana hachuji.
Pia
si mtu wa kukata tamaa, hata baada ya kuondoka Madrid, alipotua Arsenal
‘hakufa’ ameendelea kufanya yake na huenda akang’ara zaidi. Ntaona kama
nina muda, nitampigia tena yule rafiki yangu wa Ujerumani, nikiona
mjadala mrefu bila sababu za msingi, nitaacha naye tena!
SOURCE: CHAMPIONI






Post a Comment