YANGA VIZURI MKISEMA…AHSANTE PLUIJM, KARIBU SANA LWANDAMINA

LWANDAMINA |
Na Saleh Ally
HAKUNA ambaye anaweza kusema hakushituka
au kushangazwa na kuona Kocha Hans van der Pluijm akiondoka, tena
katika kipindi Yanga imeamka na kuanza kufanya vizuri.
Uongozi wa Yanga, umeamua kumleta Kocha
George Lwandamina na kufanya naye mazungumzo. Mzambia huyo kutoka Zesco
ya Zambia, alitua nchini na baada ya kumalizana na Yanga akaondoka.
Kuondoka kwa Pluijm, hakuwezi kushangaza
sana kama utaangalia mambo mengi yanayohusu mpira na makocha
walioondoka katika timu mbalimbali iwe Ulaya au hapa.
Mfano mzuri unaweza kuwa ni ule wa Yanga
wakati makocha kadhaa walioondoka walionekana wanaweza au wanafanya
vizuri lakini wakaondoshwa. Wako waliofanya vizuri zaidi walipokwenda na
wako waliofeli, hayo ndiyo maisha ya mpira.
Sam Timbe raia wa Uganda aliondoka
Yanga, Oktoba 2011, akiwa anafanya vizuri tena baada ya kuipa timu hiyo
ubingwa wa Kombe la Kagame, kumbuka aliifunga Simba chini ya Mganda
mwingine, Moses Basena.
Alifuatia Mbelgiji, Tom Saintfiet naye
akaipa ubingwa wa Kagame, hakudumu hata kwa siku 100 naye akaondoka na
nafasi yake kuchukuliwa na Mholanzi Ernie Brandts ambaye alikuwa na
mafanikio kwa kuipa Yanga ubingwa mara mbili.
Kama unakumbuka, kipigo cha mabao 3-1
katika mechi ya Bonanza la Nani Mtani Jembe. Brandts naye akatupiwa
virago, hakuna aliyeamini. Tangu Timbe, Saintfiet, Brands lilikuwa ni
suala la kutoamini kinachotokea.
PLUIJM |
Kocha ambaye alichukuliwa baada ya
Brandts, Marcio Maximo ndiye pekee alifeli katika mfumo huo wa makocha
kuondolewa Yanga kwa kushitukizwa. Waliobaki kila aliyeingia alifanya
kazi yake vizuri.
Mimi nilijua Maximo atafeli na nilieleza
mapema, sikuwa ninamaanisha ni kocha mbaya lakini Yanga imebadilika na
inataka mafanikio kwa kasi ya juu na si kujiandaa taratibu kama ambavyo
alifanya Maximo kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Yanga ina haraka, inataka mambo fasta na
kocha anayekuja anatakiwa kuanza kuleta matokeo, hakuna haja ya
kujipanga. Hilo pia linawezekana kwa Yanga kwa kuwa mara nyingi, kila
kocha anayejiunga nayo anakuta ina wachezaji wa ushindani na wanaoweza
kusaidia kupatikana kwa matokeo.
Kama Yanga itamalizana na Lwandamina,
basi hakuna shaka ukijumlisha rekodi zake kikazi na Yanga ilivyo sasa,
ataendelea kufanya vizuri lakini ni lazima aungwe mkono na Wanayanga
wenyewe.
Yanga wanachopaswa kwa sasa ni kufanya
mambo mawili makubwa ambayo yataifanya timu yao iendelee kufanya vizuri
katika mwendo ambao amewaachia Pluijm.
Kwanza, kumuonyesha Pluijm mapenzi,
wamalizane naye vizuri na kumpa heshima yake kutokana na kazi yake nzuri
ambayo amewafanyia na upendo alioonyesha. Mseme: “Ahsante Pluijm”.
Jambo la pili kubwa ni kumkubali,
kumpokea na kumuunga mkono kocha ajaye kama atakuwa ni Lwandamina au
mwingine. Maana ndiye atakuwa kocha wao, kocha wa timu yao ambaye
anakiongoza kikosi chao.
Kama Yanga watataka kufeli, basi
waendelee kulia na kupiga kelele kuhusiana na Pluijm ambaye ameamua
kujiuzulu na kuendelea na maisha yake mengine. Halafu wasubiri kumlaumu
au watamani Lwandamina au kocha mwingine atakayekuja afeli, hapo itakuwa
ni kujifelisha wenyewe.
Yanga walimshukuru Timbe, wakamuunga
mkono Saintfiet, wakamshukuru Saintfiet wakamuunga mkono Brandts.
Ulipofika muda, naye wakamshukuru pia na kumuunga mkono Pluijm.
Huu ni wakati kwao kumuunga mkono kocha
ajaye kwa ajili ya Yanga kwa kuwa ndiye atakuwa anaongozana nao na
kupambana kwa ajili ya kuwaleta mafanikio. Wakimfanya adui au
wasiyemtaka, basi ni sawa na mwanadamu kukataa moja ya kiungo cha mwili
wake wakati kinamsaidia kusimama, kuzungumza, kuona au kupumua.
Maisha ya soka ni mzunguko, hauwezi
kujua lini Pluijm ataisaidia tena Yanga, huwezi kujua kocha ajaye
atakuwa na faida na Yanga kwa kiasi gani. Hivyo maneno ya lawama,
yasipewe nafasi ili tuendelee kujifunza.
Kama kocha mpya atapewa ushirikiano,
halafu akafeli mwenyewe. Kila kitu kitaonekana kwa kuwa mpira hauchezwi
chumbani. Basi hapo, haki ya wanachama kusema kwa nia ya kujenga,
isiminywe, ili mradi mjadala uwe unaosaidia kujenga pia.
Post a Comment