Mgogoro CUF Kuwaweka Rehani Wabunge wake 9
Licha
ya Chama cha Wananchi (CUF) kujivunia uzoefu wa migogoro, huu wa sasa
umeweka rehani majimbo yake tisa ya ubunge yaliyopo Bara na hatari ya
kupoteza mvuto na wafuasi kama ilivyotokea kwa vyama vingine huko nyuma.
Vyama
ambavyo vimewahi kupita kwenye kipindi kigumu kama inavyopita CUF sasa
ni NCCR-Mageuzi, UDP na TLP. Lakini zaidi mgogoro wa NCCR-Mageuzi ndiyo
unaotaka kufanana na CUF japo kwa mazingira tofauti.
Chama
cha UDP kilichopata umaarufu kwa kauli yake ya ‘kuwajaza mapesa watu’
kwenye Uchaguzi Mkuu wa 1995 kilipata wabunge wanne ambao ni wengi
kulingana na mvuto wa chama kwa wakati huo.
Lakini,
chama hicho kilikumbwa na mgogoro wa uongozi baada ya mwenyekiti wake,
John Cheyo kupinduliwa mkutanoni na nafasi yake kuchukuliwa na Nzugule
Amani Jidulamabambasi, ambaye hata hivyo hakudumu kwenye nafasi hiyo
kutokana na Msajili wa Vyama vya Siasa kutomtambua.
Pamoja
na msajili kulipinga kundi lililofanya mapinduzi, chama hicho kilianza
kudhoofu na kupoteza mvuto hasa Kanda ya Ziwa ambapo kwenye Uchaguzi
Mkuu wa 2005 kilipata mbunge mmoja- John Cheyo- aliyedumu hadi 2010, kwa
sasa chama hicho hakina mbunge na kimepoteza ule mvuto wake wa
‘kuwajaza mapesa watu’.
Augustine
Mrema mwanzoni mwa miaka ya tisini alipojiunga na NCCR-Mageuzi baada ya
kutoka CCM alikwenda na wafuasi wengi na kukiimarisha chama hicho
kilichokuwa hakina nguvu ikilinganishwa na vyama vingine.
Nguvu
ya NCCR-Mageuzi ilionekana kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama
vingi mwaka 1995, ambapo Mrema aliyegombea urais kwa chama hicho
alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,808,616 na kupata wabunge
katika majimbo 19 Tanzania Bara.
Matokeo
hayo yalimuonyesha Mrema kuwa tishio kwa chama tawala cha CCM, lakini,
baada ya uchaguzi huo mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho ulianza.
Aliyekuwa
mwenyekiti wa chama Mrema alianza kupambana na katibu mkuu wake Mabere
Marando, hadi chama kuwa na ofisi mbili tofauti, kugawana wajumbe wa
baraza la wadhamini, wajumbe wa sekretarieti na kamati kuu.
Mazingira
hayo yanataka kufanana na mgogoro wa CUF uliopo sasa kati ya Profesa
Ibrahim Lipumba kwa upande mmoja na katibu mkuu, Maalim Seif Sharif
Hamad.
Katika
mgogoro wa NCCR wakati huo, Msajili wa Vyama vya Siasa wa wakati huo,
Jaji George Liundi (sasa marehemu), aliutambua upande wa Marando
kiutendaji kwa kuwapa ruzuku bila kutamka hadharani kwamba anaunga mkono
kundi lipi.
Nguvu
ya msajili ilimdhoofisha Mrema na kundi lake kwa kuwa hawakuwa na fedha
za kuendesha shughuli za chama, ndipo akaamua yeye na wafuasi wake
kuhamia Tanzania Labour Party (TLP), huku aki tamka ofisi zote mikoani
zilizokuwa za NCCR-Mageuzi zibadilike kuwa za TLP.
Licha
ya waliobaki NCCR-Mageuzi kuonyesha kufurahishwa na uamuzi wa Mrema wa
kuondoka, chama hicho kilichokuwa kikijivunia majimbo 19 ya ubunge,
kilianza kudhoofika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, kwanza
hakikusimamisha mgombea urais, pili kilipoteza majimbo 18 ya ubunge na
kubaki na jimbo moja tu la Kifu Gulamhussein Kifu (Kigoma Kusini) ambalo
nalo lilipotea kwa njia ya mahakama.
NCCR-Mageuzi,
mbali na kupoteza wabunge, pia chama hicho kilipoteza wafuasi na
umaarufu iliyokuwa nao, hali ambayo CUF inaonekana kuwa nayo kwa kuwa
inapita kwenye njia zile zile.
Hata
hivyo, Mrema aliyekuwa akijivunia mtaji wa kura milioni 1.8 alijikuta
akipiga mwereka kwenye uchaguzi mkuu wa 2000 alipogombea urais kupitia
TLP alikoambulia kura 637,115 na wabunge watano.
Kuonyesha
kwamba CUF inapita njia ya NCCR-Mageuzi katika kudhoofika, sasa chama
hicho kimegawanyika lakini mbali na hivyo Msajili wa Vyama vya Siasa
ameibuka hadharani kuunga mkono kundi moja na sasa ameonyesha dalili za
kuwapa nguvu ya fedha.
Hata
hivyo, kundi la Profesa Ibrahim Lipumba linaloungwa mkono na msajili
likifanikiwa kupata ruzuku litakuwa na nguvu, lakini kwa wananchi chama
hicho kitapoteza mvuto na kuweka rehani wabunge wa majimbo tisa wa Bara
na madiwani.
Huu
ni mgogoro wa tano wa kiuongozi ndani ya CUF baada ya kupitia katika
kipindi kigumu wakati wa James Mapalala, aliyekuwa mwenyekiti wake wa
kwanza, Naila Jidawi, Michael Nyaluba, aliyeanzisha chama hicho upande
wa Bara na Hamad Rashid Mohamed.
Uzoefu
wa migogo kwa CUF siyo kigezo kwamba chama hicho hakiwezi kuwa kama
vyama vingine vilivyopoteza mvuto na kupoteza wabunge na madiwani
waliowapata katika uchaguzi uliopita.
Kesi ya wadhamini
Katika
hatua nyingine, mchakato wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wananchi
(CUF), kupata kibali cha kufungua kesi dhidi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa na wenzake unaanza rasmi leo wakati maombi yaliyofunguliwa na bodi
hiyo yatakapotajwa.
Bodi
hiyo ya wadhamini CUF imefungua maombi hayo Mahakama Kuu Masjala Kuu
dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwenyekiti wa chama hicho
anayetambuliwa na Msajili, Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na wanachama
wengine wa chama hicho waliosimamishwa uanachama wao.
Katika
maombi hayo namba 75 ya mwaka 2016, bodi hiyo inaomba kibali cha
kufungua kesi dhidi ya Msajili, Profesa Lipumba na wenzake kadhaa,
pamoja na mambo mengine, kupinga uamuzi wa Msajili kumtambua Profesa
Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho.
Post a Comment