Chura ya Snura yazinduliwa
BAADA ya kufungiwa
na kutakiwa kurekebishwa kwa video ya Wimbo wa Chura ulioimbwa na mkali wa
Muziki wa Mduara, Snura Antony Mushi ’Snura’ ambao ulikosa maadili hatimaye
video hiyo leo imeruhusiwa kuchezwa.
Akizungumza na
wanahabari jijini Dar es Salaam, Snura ambaye pia ni muigizaji amesema kuwa Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya Waziri wake, Nape Nnauye imemuandikia
barua ya kumruhusu kuchezwa kwa video yake hiyo baada ya kuirudia na kuzingatia
vigezo vyote alivyokuwa amepewa awali ikiwemo kuzingatia maadili ya Kitanzania.
Snura aliviomba
radhi tena kwa mara nyingine vyombo vya serikali vinavyosimamia sekta ya sanaa
kwa kutokufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika uendeshaji wa sanaa
nchini.
Amefafanua kuwa anamshukuru,
Nape Nnauye kwa kuuruhusu Wimbo wa Chura na video yake kupigwa na kuonyeshwa
katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni baada ya kuona video hiyo
ikiwa na ujumbe na maadili ndani yake.
Alifafanua kuwa awali
alipewa masharti ya kuwa video yake na wimbo vingefunguliwa pale ambapo
angefanya video mpya iliyozingatia maadili ya Kitanzania.
Vilevile alieleza
kuwa video hiyo inaeleza maana halisi ya neno Chura kwa kumaanisha ni mwanamke
anayerukaruka katika uhusiano wa kimapenzi kwa kubadilisha wanaume mbalimbali
na matokeo yake kupata magonjwa hatarishi.
“Nimeona mara nyingi
watu waliokuwa kwenye uhusiano linapotokea tatizo baada ya kukaa na kutatua na mwenzake
au kutumia familia zao kuwasuluhisha anachukua maamuzi ya hasira kubadili
wanaume na kuona ndiyo maamuzi sahihi kwake kumbe anapotea,huyo ndiye Chura
niliyemzungumzia mimi kwenye muziki wangu huo.

Post a Comment