Tiba asili kumpigania Dk Mwaka mahakamani

Shirikisho la Vyama vya
Tiba Asili Tanzania (Shivyatiata) linakusudia kwenda mahakamani kufungua
kesi dhidi ya Baraza la Tiba za Asili likidai limewaadhibu kinyume cha
sheria kwa kuwafungia matabibu saba na vituo vya tiba hiyo.
Mwenyekiti
wa Shivyatiata, Abdulrahman Lutenga alisema jana kuwa Baraza hilo
limewahukumu wenzao hao bila kuzingatia vifungu vya sheria namba 23 ya
tiba za asili na tiba mbadala ya mwaka 2002, hivyo wameamua kwenda
mahakamani kuomba tafsiri sahihi.
Lutenga alisema Shivyatiata imepokea
barua za malalamiko kutoka kwa waganga walioadhibiwa na Baraza hilo, na
baada ya kufanya uchunguzi wamebaini kwamba uamuzi huo ulitolewa bila
kuzingatia taratibu na sera na uendelezaji wa viwanda katika eneo la
tiba asili.
“Shivyatiata tunatambua kuwa Baraza hilo ni chombo cha
kitaalamu kwa mujibu wa Sheria namba 23 ya tiba za asili na tiba mbadala
hivyo lina mamlaka ya kuwaadhibu wanaokwenda kinyume cha sheria hiyo
ikiwa ni pamoja na kutoa onyo au kumsimamisha mganga au mkunga na
muuzaji wa tiba za asili, lakini uamuzi uliochukuliwa na baraza hilo
hatukubaliani nao,” alisema Lutenga.
Alisema ingawa uamuzi unaweza
kutolewa bila kikao kwa kuwapelekea wajumbe nakala za shauri, mjumbe
yeyote anaweza kutaka uamuzi uahirishwe na suala hilo lijadiliwe katika
kikao cha Baraza, lakini cha kushangaza mwenyekiti wa Baraza
hakukizingatia kifungu hiki.
Alisema shirikisho hilo pia linamuomba
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutumia mamlaka aliyonayo kuwaondoa
watendaji wa Baraza hilo kwa madai kuwa wamekuwa wakiwadhalilisha na
kuwakatisha tamaa wanachama wake.
Katibu Mtendaji wa Shivyatiata
Othman Shem alisema wameshangazwa na uamuzi wa Baraza hilo kwa kuwa
waganga waliosimamishwa ni miongoni mwa waliokuwa wakiwategemea katika
kuanzisha viwanda vya tiba za asili kutokana na uwezo wa kifedha na
kitaalamu walionao.
“Baraza hili kweli linatakiwa kuajiri watu ambao
wanataaluma hii kwa sababu mazingira ya uamuzi yanaonyesha umetolewa kwa
lengo baya la kukandamiza taaluma yetu na kuturudisha nyuma kwa hatua
tulizoanza kupiga,” alisema.
Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba
Mbadala, Dk Edmund Kayombo alitangaza uamuzi kukifutia usajili kituo cha
Foreplan kinachomilikiwa na Juma Mwaka kwa kutokidhi masharti ya
usajili na kufanya kazi kinyume cha usajili wake.
Post a Comment