YANGA KUWENI MAKINI NA MWAMUZI HUYU DHIDI YA TB MAZEMBE
Na Saleh Ally
SHIRIKISHO
la Soka la Afrika (Caf), limempa nafasi mwamuzi Janny Sikazwe kuamua
mchezo kati ya mabingwa wa Tanzania, Yanga dhidi ya TP Mazembe, hii ni
mechi ya Kombe la Shirikisho hatua ya makundi.
Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumanne na inasubiriwa kwa hamu kubwa.
Caf
imewatangaza waamuzi wasaidizi kuwa hivi; washika vibendera ni Berhe
O’Michael wa Eritrea na Wellington Kaoma wa Zambia pia atakuwa line 2.
Kamishna ni Celestin Ntangungira anayetokea Rwanda. Pia kutakuwa na
Mratibu Mkuu Maalum wa mchezo huo kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza.
Vizuri
kabisa Yanga ikamjua Sikazwe ni mtu wa aina gani. Huyu ni mwamuzi
aliyeingia kwenye fainali ya waamuzi bora wa Afrika katika tuzo za
Glo-Caf zilizofanyika nchini Nigeria, mwaka jana akichuana na waamuzi
wengine wa juu barani Afrika kama Alioum Neant wa Cameroon, Eric Arnaud
Otogo-Castane (Gabon), Ghead Zaglol Grisha (Misri) na Bakary Papa
Gassama wa Gambia aliyekuwa anashikilia tuzo hiyo.
Sikazwe ni mwamuzi mzuri bila shaka, mwenye mkwara kwa wachezaji na amekuwa akiutumia urefu wake kuonyesha hana hofu na hajali.
Lakini
rekodi zinaonyesha marefa bora wamekuwa wakitumiwa na timu kubwa na
wakati mwingine wadau wa karibu wa Caf kuziangamiza timu ndogo na
kuzitetea kubwa barani Afrika.
Timu
kubwa kama Al Ahly, TP Mazembe, Esperance na nyingine kubwa zimekuwa
zikibebwa mara nyingi hasa zinapoonekana zimezidiwa. Inaonekana ni siri,
lakini hakuna anayeweza kukataa kwamba kwenye soka kuna rushwa na timu
zenye fedha nyingi hutumia nguvu zao kifedha.
Hakuna
anayeweza kukataa, pia Yanga itaingia kwenye dimbwi la dharau inayopewa
ukanda wa Afrika Mashariki kuonekana hauna kitu. Vizuri timu za
Kaskazini na zile za Magharibi au Afrika ya Kati kama TP Mazembe zifanye
vizuri zaidi.
Timu
za ukanda wa Magharibi, Kaskazini na hata Kati, kweli ni bora, lakini
pia zinafanikiwa kutokana na uwezo mkubwa wa kuzibeba figisu za nje ya
uwanja. Waamuzi ni kati ya “Watumwa wa wafalme” ambao wamekuwa
wakisaidia.
Hatuwezi
kutanguliza lawama kwa Sikazwe lakini akikanyaga ardhi ya Tanzania,
wamfikishie salamu kwamba kinachotakiwa ni haki bin haki ili Yanga
ikifungwa kwa haki, Watanzania wajue kweli iliteleza na uwezo wake
ulipungua sehemu fulani.
Katika
mechi nyingi za TP Mazembe alizocheza Sikazwe zinaonyesha timu hiyo
ilipoteza moja tu kwa kufungwa bao 1-0 na Al Hilal mjini Khartoum,
Sudan. Hiyo ilikuwa Mei 16, 2014.
Ukiachana
na hivyo, mechi zote zilizobaki TP Mazembe ilishinda na nyingi kumekuwa
na lawama kubwa, kwamba alionekana kuwabeba wakubwa hao kama ambavyo
nimeelezwa.
Katika
soka, suala la lawama limekuwa kama ada. Waamuzi wengi wamekuwa
wakilitumia kama nafasi ya kuangamiza wengine kwa kuwa wanaamini lazima
watu watalaumu, hivyo wanataka kuonyesha ni lawama tu, wakati wao
wanakuwa wametekeleza malengo mengi.
Kumekuwa
na taarifa hata kitengo cha upangaji waamuzi kimekuwa kikizidiwa nguvu
na klabu kubwa, kwamba mwamuzi fulani achezeshe mechi zao.
Mfano
msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa, Sikazwe alichezesha mechi tatu za
TP Mazembe, ikashinda mbili dhidi ya Stade Malien (2-1) na Moghreb
(5-0), zote ikiwa nyumbani Lubumbashi kabla ya kufungwa 1-0 na Al Hilal,
Sudan.
Sikazwe
anaonyesha ni ‘mbaya’ kwa kadi za njano. Ni anayeonya kwa maneno sana,
halafu ukizidi njano inafuatia. Wakati mwingine ni mbabe na mgumu wa
kutoa kadi nyekundu.
Msimu
uliopita kwa ligi ya kwao Zambia na mechi zote za kimataifa kuanzia
zile chini ya Caf na Fifa, alitoa kadi za njano 214, nyekundu 6.
Alichezesha jumla ya mechi 63 za kimataifa.
Msimu
huo, Sikazwe alitoa jumla ya penalti 9. Hii inaonyesha mtu akifanya
ujinga katika eneo la 18, basi ajue ‘ameiharibia’ timu yake.
Kwa
Wazambia, DR Congo ni kama nyumbani, ninaamini Sikazwe ataonyesha
umahiri wake na kuchezesha kwa haki kwa kuwa Yanga inaweza kuwa na
nafasi ya kufanya vema kama uamuzi hautakuwa sehemu ya kuivuruga.
Vizuri
watakaofika Uwanja wa Taifa siku ya mchezo, washuhudie kwamba kama
Yanga imefanya vizuri bila ya kubebwa na mwamuzi. Ikifanya vibaya, basi
isiwe kwa kuonewa na Sikazwe kwa vile vigezo nilivyovitaja pale juu.
TAKWIMU:
Penalti: 9
Kadi nyekundu: 6
Kadi njano: 214
*MECHI ZA KIMATAIFA 63



Post a Comment