Snura amkabidhi jipu mama Samia

Makamu wa Rais, Samia Suluhu.
STAA wa muziki
Bongo, Snura Mushi ameibuka na kumkabidhi Makamu wa Rais, Samia Suluhu
jipu la wanaume wanaowakataa watoto wao na kuwaachia wanawake mzigo wa
kulea peke yao.
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko,
Snura alisema siku hizi wimbi la wanaume kuwakataa watoto wao ni kubwa
sana hivyo tatizo hilo ni sawa na majipu mengine, anamuomba mama Samia
alitumbue.
“Namuomba mama Samia kwa sababu ni
mwanamke mwenzetu atusaidie kulitumbua hili jipu maana ni kubwa sana
yaani tena ni tambazi kabisa, kama rais anavyowatumbua watu naye atumbue
hili maana wanawake tumechoka.
“Nina watoto wawili lakini baba zao
wamenisusia, wa kwanza alimkataa tangu nikiwa na mimba ya wiki mbili
mpaka sasa nalea mwenyewe, huyu mwingine hajawahi kutoa chochote tangu
mwanaye huyu azaliwe kitu ambacho kinaumiza sana,” alisema Snura.
Aliendelea kusema kuwa baada ya mama
Samia kutumbua hilo jipu anaomba serikali iweke sheria ya kwamba kila
kituo cha polisi kiwe kinapokea malalamiko ya wanawake wanaosusiwa
watoto au mimba ili shtaka linapokwenda waandikishane na baada ya mtoto
kuzaliwa ikigundulika mtoto ni wa mwanaume husika alipishwe fidia.
“Pia kipimo cha DNA kiwepo katika
hospitali mbalimbali ili iwe rahisi kupima kwa wale wanaume wanaokataa
kwamba watoto siyo wao, sheria hizi zikiwekwa zitasaidia kutokomeza
tatizo hilo la watoto kukataliwa na baba zao,” alisema Snura.
Jitihada za kuzungumza na Waziri wa Afya
, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kujua
ameipokeaje changamoto hiyo, hazikuzaa matunda kufuatia simu yake
kutopatikana hewani.
Snura ni mama wa watoto wawili kila
mmoja na baba yake ambapo anawalea mwenyewe huku akikiri kwamba huwa
anawaeleza wanaye hao jinsi baba zao walivyowakataa ili baadaye kusije
kutokea mvutano wa kimasilahi pindi watakapofanikiwa.
CHANZO: GPL
Post a Comment