KIPINDI HIKI CHA USAJILI, KUWENI MAKINI NA MAMENEJA MAJALALA
Na Saleh Ally
HIKI
ndicho kile kipindi gumzo zaidi katika mchezo wa soka. Kipindi cha
usajili, kila timu inajaribu kujiimarisha ili kuwa na nguvu ya kutosha
msimu ujao.
Wakati
wa maandalizi kila timu inajiandaa kuwa bingwa, ingawa baada ya kuanza
kwa msimu, taratibu mafuta huanza kujitenga na maji.
Kipindi hiki kwa mashabiki ni kile ambacho wangependa kuona timu wanayoiunga mkono ikifanya usajili wa uhakika.
Upande
wa viongozi huwa na presha juu kwa kuwa wanataka kufanikisha usajili
sahihi ambao ni bora kwao na wangependa kuona wanafanikiwa kuwapata
wachezaji bora wanaowahitaji ili kukiimarisha kikosi chao.
Wakati
kila upande ukipambana, kuna kundi moja limegeuka kuwa tatizo kubwa
katika zoezi hilo la usajili. Hawa ni wale watu wanaojiita mameneja.
Wengi
wao naweza kuwabatiza jina mameneja majalala. Yaani watu wanaojulikana
kuwa ni mameneja, lakini ukweli wengi wao ni wajanja-wajanja tu na
wanaokuwa katika harakati hizo kwa ajili ya harakati za kutunisha
matumbo yao.
Kuna
mchezaji mmoja siku chache zilizopita, alikuwa amekubaliana na klabu
moja asajiliwe kwa kitita cha Sh milioni 20. Siku ya kwenda kuanguka
saini, akaibuka na kusema kwamba anataka kupata Sh milioni 40. Klabu
hiyo ikaachana naye na kumsajili mwingine.
Siku
chache alirejea na kusema alikuwa tayari kusajiliwa kwa kitita cha Sh
milioni 20 tena. Lakini alishachelewa na klabu hiyo ilishasaini mchezaji
mwingine, akakosa dili.
Baadaye
alieleza majuto yake kwa kuwa alilaghaiwa na mtu aliyejidai ni meneja
ambaye alimshawishi kuomba fedha nyingi zaidi akiamini kwamba lazima
zingepatikana ili mchezaji huyo afaidike zaidi na meneja aondoke na
chake.
Mwisho
mchezaji huyo amekosa, meneja hana hasara. Hiyo ndiyo hali halisi
ilivyo katika matukio mengi kwa kuwa kuna kundi la watu ambalo
limejitokeza na linataka kujenga utaratibu wa kufaidika na fedha
wanazolipwa wachezaji wakati wa usajili.
Lakini
wachezaji wenyewe wanaonekana bado wako usingizini kwa kuwa wanashindwa
kuelewa kwamba wananyonywa au wanatumika kuwafaidisha watu wengine na
ikiwezekana wao kutopata wanachostahili. Kuwa na meneja ni jambo zuri,
lakini vizuri awe ni yule mtu makini anayefanya kazi kweli kwa ajili ya
mchezaji husika.
Vizuri
meneja akawa na mchezaji katika kipindi chote ili kufuatilia maendeleo
yake, kujali kwa kupigania au kushawishi kuhusiana na maslahi yake
lakini si kusubiri wakati wa uingizaji fedha, basi ndiyo awe karibu.
Vichwa
vya hao mameneja majalala wanaoibuka kipindi cha usajili pekee
vinapaswa kukatiliwa mbali. Badala yake wachezaji wawe makini na
kujisimamia vizuri.
Lakini
inaweza kuwa vizuri zaidi kama watawatafuta mameneja mapema, hata kabla
ya kipindi cha usajili na kuanza kufanya nao kazi katika kipindi
ambacho wanajijenga ili kujua uwezo wao, msaada na faida ya kuwa nao na
si kipindi cha uingizaji fedha pekee, ndiyo wanainua vichwa vyao.
Kwa
kawaida, mchezaji ndiye anapaswa kuwa bosi wa meneja. Lakini meneja
anapaswa kuwa kiongozi wa mchezaji na msimamizi wa mambo yake mengi nje
ya uwanja, mshauri wa mengi uwanjani pia.
Longolongo
imekuwa juu na wachezaji wanaendelea kutumika, amkeni sasa. Mlio
wababaishaji, imetosha na muwe na imani na hao wachezaji. Mmewatumia
sana kujifaidisha, sasa ni kipindi cha kuwapa nafasi ili nao wazidi
kukua kimaisha kwa kuwa wamekuwa wakiyapigania kwa muda mrefu kwa kuwa
wana ndoto za kukua.
Pia
ni vizuri kwa mameneja wachache ambao wamejitokeza na kuwa makini. Basi
wanaweza kuongeza idadi ya wachezaji ili kuendelea kuwaelekeza,
kuwasaidia kwa lengo la kuwainua. Pamoja na msaada, pia hili
litawasaidia wachezaji hao kuingia kwenye mikono ya mameneja majalala.

Post a Comment