Huu mgogoro wa Wabunge na Naibu Spika utatuliwe haraka

Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.
Tumsifu Mungu
kwa kutupa uhai na afya tele leo. Baada ya kusema hayo niingie moja kwa
moja katika mada ya leo kuhusu mgogoro unaoendelea kufukuta ndani ya
bunge letu tukufu hivi sasa.
Mgogoro huo ni msuguano kati ya Naibu
Spika, Dk. Tulia Ackson na wawakilishi wa wananchi wa kambi ya upinzani.
Kiini cha mtafaruku huo kimeelezwa kuwa naibu spika amekuwa akitumia
vibaya kanuni ili kuwanyima haki, uhuru na demokrasia wabunge wa kambi
hiyo.
Msuguano huo umekuwa mkubwa na si wa
kuuangalia na badala yake nashauri vikao vya uongozi wa bunge vifanyike
au Spika Job Ndugai aingilie ili kuondoa tofauti za pande mbili hizo.
Vikao hivyo vikifanyika viangalie
malalamiko ya wabunge kama kweli wao wanaambiwa wanatumia lugha ya
kuudhi ama la na kama wana hoja kuhusu madai yao ya kung’ang’ania Bunge
kuoneshwa ‘laivu’, haya yalikuwa yafanyike haraka.
Nasikitika kusema kwamba mpaka naandika
maoni haya hayo hayajafanyika na matokeo yake wabunge wa upinzani sasa
wamekuwa wakitoka bungeni kila anapoingia Dk. Tulia kuendesha Bunge.
Mtindo huo umewafanya Wabunge wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kuomba mwongozo wa spika kwamba wabunge hao wa
upinzani wanaosusia vikao wawe wakikatwa posho yao ya siku, mwongozo
ambao awali ulijibiwa na Dk. Tulia kuwa haiwezekani mpaka sheria
zibadilishwe lakini mwishoni mwa wiki iliyopita alibadili msimamo huo,
akatoa uamuzi wa kukata posho za wanaosusia.
Sakata zima Dk.Tulia ndiye
anayelalamikiwa na wasusiaji vikao na ndiye aliyepokea hoja za wabunge
wa CCM namna ya kuwashughulikia wapinzani na ndiye aliyetoa hukumu ya
kukatwa posho wapinzani.
Kwa maoni yangu nadhani haki ya msingi (matural justice), haikuzingatiwa.
Haki ya msingi inataka walalamikaji
kupewa haki ya kusikilizwa malalamiko yao pili uamuzi kuhusu hoja zao
ufanywe na mtu huru ambaye hahusiki na tatizo, tatu uamuzi utolewe kwa
kuzingatia ushahidi uliotolewa na uwe wazi.
Nikirudisha nyuma mawazo yangu, nadiriki
kusema kwamba maspika waliopita, Samwel Sitta na Pius Msekwa katika
uongozi wao walikuwa wakijali sana haki na wamekuwa tochi na kielelezo
katika uendeshaji wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Kwa mfano, kuna wakati Spika Pius Msekwa
ilipokuwa ikifika zamu ya kujadili Wizara ya Afya, iliyokuwa ikiongozwa
na mkewe, Anna Abdallah, alikuwa anakaa kando na kiti kuongozwa na mtu
mwingine na hata Samwel Sitta alipokuwa Spika ilipokuwa inafika zamu ya
mjadala wa Wizara ya Elimu ambayo ilikuwa ikiongozwa na mkewe, Magreth
Sitta, alikuwa anakaa kando.
Wote kwa nyakati tofauti walikuwa
wakisema wanafanya hivyo ili kuwapa uhuru zaidi wabunge kuzijadili
wizara hizo kwa uwazi na bila woga kwa kuwa wanaoziongoza ni wake zao.
Kutokana na mifano hiyo, nashauri kiti
cha naibu spika kizingatie haki ya kusikilizwa wanaokilalamikia kwa
sababu yupo spika na hata kamati ya uongozi ambao wanaweza kusikiliza
shauri hili ili kuondoa tatizo hili ambalo naamini wananchi wamechoka
nalo.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Post a Comment