YANGA KUCHUKUA TUZO ZOTE ZA LIGI KUU TANZANIA BARA?
Bado
tuzo mbalimbali kwa wachezaji na makocha hazijatoka kwa ajili ya msimu
wa 2015/16 uliomalizika wikiendi iliyopita na Yanga kuibuka bingwa
lakini tayari wadau mbalimbali wa soka nchini wameonyesha wazi kuvutiwa
na tuzo ya kocha bora itue kwa Kocha wa Yanga, Mdachi, Hans van Der
Pluijm.
Kila
mmoja amekuwa akitaja sababu zake ikiwemo nani anastahili kuwa mchezaji
bora wa ligi hiyo ambapo kwa upande huo pia, mshambuliaji wa Yanga,
Mzimbabwe, Donald Ngoma naye ameonekana kuwakuna wengi kwa kazi
aliyoifanya.
Kocha
wa zamani wa Geita Gold ya Geita, Selemani Matola ambaye amewahi kuinoa
Simba miaka ya nyuma amefunguka kuhusiana na hilo: “Kwa upande wangu,
Pluijm anastahili kuchukua hiyo tuzo, ameifikisha Yanga fainali ya FA,
ameipa ubingwa na mwisho akaipeleka nane bora ya Kombe la Shirikisho.
“Amefanya
kazi nzuri kila mmoja ameiona. Ngoma naye amekuwa msaada mkubwa kwa
Yanga kwenye ushambuliaji, asipokuwepo unaiona Yanga siku hiyo inapata
shida kidogo, naye anastahili uchezaji bora ingawa ningependa kuona TFF
(Shirikisho la Soka Tanzania) iache masuala ya uzawa na kumpa mtu
anayestahili tuzo kutokana na kazi aliyofanya.”
Abeid
Kasabalala ambaye ni katibu msaidizi wa Chama cha Wachezaji wa Soka
Tanzania (Sputanza) naye alisema: “Kocha bora ni Pluijm, amefanya vizuri
kwa kweli msimu huu, ameisaidia Yanga kila sehemu waliyokuwa
wakishiriki na mwishowe wamepata mafanikio, ukiangalia Kombe la FA,
Kombe la Shirikisho na hata ubingwa ligi kuu.
“Kwa
uchezaji bora nafikiri Kamusoko (Thabani) anastahili sana katika hili,
ameisaidia Yanga kwa kiasi kikubwa katikati ya uwanja katika kukaba,
kuanzisha mashambulizi na hata pasi zenye madhara, amekuwa bora sana
msimu huu.”
Naye
kocha msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal ‘Bilo’ aliitupa karata
yake kwa Pluijm huku akitaja vigezo vinavyoshabihiana na Matola na
Kasabalala na kwa upande wa mchezaji bora akamtaja Ngoma, hasa
alivyohusika katika kuchangia mabao mengi aliyofunga Mrundi, Amissi
Tambwe aliyeibuka mfungaji bora kwa kutupia mara 21.
“Ngoma
anafaa kuwa mchezaji bora msimu huu, amekuwa tishio na msaada mkubwa
kwa Yanga tangu mwanzo wa ligi mpaka mwisho. Hata ukiangalia upande wa
mabao, yeye mwenyewe kafunga mengi lakini pia amesaidia mno kumpikia
mabao Tambwe msimu huu, msaada wake ulikuwa mkubwa mno,” alisema Bilo.
Pia
kumekuwa na minongono kuwa tuzo ya kipa bora inaweza kwenda kwa Ally
Mustapha ‘Barthez’ ambaye amefanya kazi kubwa msimu huu, huku tuzo ya
mfungaji bora ikienda kwa Tambwe aliyefunga mabao 21.
Post a Comment