MPANGO MZIMA WA BABU PLUIJM NAMNA AMBAVYO YANGA ITABEBA KOMBE SHIRIKISHO AFRIKA
Kocha
wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amepania kulichukua Kombe la Shirikisho
Afrika, kwani amepanga kutokubali kufungwa kwenye mechi zote za ugenini
ikiwemo dhidi ya TP Mazembe.
Hiyo
ni baada ya juzi na jana kukaa na kuweka mikakati ya jinsi ya
kulichukua taji hilo baada ya kuingia hatua ya makundi ya Kombe la
Shirikisho waliyoingia kwa kuwatoa Sagrada Esperanca ya Angola.
Yanga
ipo kwenye Kundi A na timu za MO Bejaia ya Algeria, Medeama (Ghana) na
TP Mazembe ya DR Congo. Kundi B zipo Kawkab na FUS Rabat zote za
Morocco, Etoile du Sahel (Tunisia) na Ahly Tripoli ya Libya.
Pluijm
amesema ushindi wa ugenini unaifanya timu pinzani kucheza kwa presha
kubwa katika mchezo wa nyumbani, hivyo amepanga kutumia mbinu hiyo
akiamini itampa taji hilo.
Pluijm
alisema, amefikia hatua hiyo baada ya tathmini aliyoifanya kwenye mechi
za Ligi ya Mabingwa Afrika kwani walifungwa michezo miwili ya ugenini
dhidi ya Al Ahly mabao 2-1 na Esperanca bao 1-0.
“Timu
yetu ina rekodi mbaya ya kufungwa mechi za ugenini na hilo nimeliona
kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo sitaki kuliona hilo likijitokeza
kwenye Kombe la Shirikisho.
“Nitakachokifanya
ni kupambana kwenye mechi zote tutakazozicheza ugenini kwenye hatua hii
ya makundi Kombe la Shirikisho, kuhakikisha tunashinda ili kuwapa
mazingira magumu wapinzani wetu kwenye michezo ya nyumbani.
“Hiyo
tathmini nimeifanya kwenye Ligi ya Mabingwa kwani tulipata matokeo
mazuri nyumbani pekee na ugenini tukafungwa, hivyo sitaki kuona
tukiendelea hivi.
“Naendelea
kukiboresha kikosi changu kuhakikisha tunachukua ubingwa wa Kombe la
Shirikisho, lengo ni kuzima utawala wa Mazembe,” alisema Pluijm.
Katika
rekodi zake, TP Mazembe imetwaa mara tano ubingwa wa Ligi ya Mabingwa
Afrika katika miaka ya 1967, 1968, 2009, 2010 na 2015, pia imetwaa mara
moja Kombe la Washindi (sasa Kombe la Shirikisho) mwaka 1980. Yanga
haijawahi kutwaa ubingwa wowote wa Afrika.
Mtanzania Thomas Ulimwengu ni miongoni wa wachezaji tegemeo wa TP Mazembe hivi sasa.
Yanga
itaanza mechi zake za makundi ya Kombe la Shirikisho kati ya Juni 17
hadi 19, mwaka huu kwa kucheza na Mo Bejaia ya Algeria ugenini halafu
itaikaribisha TP Mazembe nyumbani kati ya Juni 28 na 29.
Post a Comment