A-Z Ya Dada wa Msuya Kuchinjwa… Mchezo ni Huu
Jeneza lenye mwili wa marehemu.
Na Waandishi Wetu, UWAZI
DAR ES SALAAM: Bado habari ni
moto! Majonzi yanaendelea kutawala kwenye familia ya Bilionea Erasto
Msuya (43) aliyeuawa kwa kupigwa risasi Agosti 8, 2013, Uwanja wa
Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia) kufuatia safari hii, mdogo wake
wa kike, Aneth Simon Msuya (30) naye kuuawa kwa kuchinjwa shingo na watu
wasiojulikana, Uwazi limebaini mchezo mzima.
Aneth (pichani) alifanyiwa ukatili huo,
Mei 26, mwaka huu chumbani, nyumbani kwake, Block 16, Kibada- Kigamboni
jijini Dar es Salaam akiwa na mtoto wake, Allan Kimario.
Mauaji hayo yaligunduliwa na jirani
asubuhi baada ya mtoto wa marehemu, Allan kwenda kusema mama yake haamki
na yeye anataka kwenda shule huku basi la shule likiwa limemwacha. Pia
alisema anahisi njaa.
Jirani huyo aliongozana na mtoto huyo
hadi ndani na kuubaini mwili huo ukiwa umalala sakafuni kwenye dimbwi la
damu na kisu kilichotumika kumchinjia kikiwa pembeni yake na hivyo
kutoa taarifa polisi.
Tangu kutokea kwa tukio hilo, vyombo
mbalimbali vya habari nchini vimekuwa vikiripoti tukio hilo katika njia
za kusikitisha sana kutokana na unyama aliofanyiwa Aneth na ndipo, Uwazi
nalo likazama mitaani kuchimba kwa kina ili kuwapa wasomaji wake mambo
mapya zaidi.
Madai yaliyosambaa ni kwamba, kuna kundi
la watu limepanga mkakati mzito wa kuhakikisha familia ya Msuya
inafutika kwenye uso wa dunia kutokana na kisasi cha kibiashara (bila
kufafanuliwa).
“Ilivyo ni kwamba, baada ya kaka yao
(Erasto) kuuawa, kwa kupigwa risasi, kuna kundi la watu limeamua kuifuta
familia hiyo kwenye uso wa dunia. Ndiyo maana mbali na Aneth kuchinjwa,
kuna akina Msuya wengine wameshakumbana na vitendo vya kuashiria
kwamba, roho zao zinasakwa
Kwa mujibu wa chanzo kimoja toka ndani
ya Jeshi la Polisi Tanzania, msichana anayedaiwa kufanya kazi za ndani
‘hausigeli’ nyumbani kwa marehemu Aneth na kuondoka siku ya mauaji hayo,
anapewa nafasi ya kwanza katika kuchunguzwa akisemekena kuujua mchezo
mzima wa kifo cha bosi wake huyo na sasa jeshi hilo linamsaka kwa udi na
uvumba.
“Kwanza nataka kusema kuwa, hausigeli
ndiye mshukiwa wetu wa kwanza ndani ya jeshi la polisi. Huyu msichana wa
kazi aliondoka mchana, usiku yakatokea yaliyotokea, akipigiwa simu
hapatikani.
“Huyu tunamtuhumu kuujua mchezo wote.
Kwa hiyo pa kuanzia kwetu tunafanya juu chini kumpata ili aisaidie
polisi,” kilisema chanzo hicho huku kikiomba hifadhi ya jina kwa vile,
si msemaji sahihi wa jeshi hilo.
ALIPANDIKIZWA?
Pia, chanzo hicho kiliendelea kusema
kuwa, utafiti wa awali wa jeshi hilo unataka kukubaliana kwamba,
kutokana na mlolongo unaotokea wa mauaji au kujeruhiwa kwa watu
mbalimbali wa familia ya Msuya, kuna uwezekano msichana huyo wa kazi
alipandikizwa na watu hao kufanya kazi kwa Aneth.
“Kuna wasiwasi yule dada wa kazi
alipandikizwa. Kuna uwezekano alifika pale katika njia za mtego ili
kumsoma Aneth na mazingira yake pamoja na mwenendo, sasa baada ya
kukamilisha ndiyo akaamua kuondoka na usiku wauaji wakafika. Kwa hiyo
hayo yote sisi polisi tunayachunguza,” kilisema chanzo.
WAUAJI WALIINGIAJE NDANI?
Kwa mujibu wa chanzo hicho, inaaminika
kwamba, wauaji hao walifanikiwa kuzipata funguo halisi za geti kubwa la
mlango wa kuingilia sebuleni kwa Aneth, wakaenda kuchongea nyingine
ambazo siku walipofika, waliweza kufungua geti na kuingia kama kwao.
“Lile geti kubwa linafunga kwa nje na
funguo, kwa ndani unavuta loki tu. Kwa hiyo wao waliingia ndani kwa
kufungua. Walipomaliza kutenda ukatili wao, inaonekana walifunga geti
kubwa kwa kuloki ambapo kwa mtu mwingine wa nje asingeweza kuingia ila
yule mtoto (Allan) aliweza kutoka nje kwa sababu loki yake ni ya kubetua
tu.”
KWA NINI WAUAJI WALIIBA TIVII TU?
Chanzo hicho kikasema kuwa, watuhumiwa
hao hawakuiba kitu zaidi ya tivii (flat) lakini inaonekana kwamba
waliamua kuichukua runinga hiyo kwa vile waliamini ni skrini kwa ajili
ya kamera za ulinzi (Closed-Circuit Television au CCTV) ambapo walijua
picha zao zilichukuliwa. Hata hivyo, tivii hiyo waliitupa mbele ya
safari.
HAIKUWA RAHISI KUMCHINJA ANETH
Chanzo hicho kilisema kuwa, mazingira ya
chumba yalionesha kuwa, kabla ya kuchinjwa, kulikuwa na purukushani
kubwa kwani neti ilikutwa imechanwa, baadhi ya vitu vimepinduliwa,
vingine vimezagaa kila mahali hali ambayo iliashiria kuwa, marehemu
hakukubali kuchinjwa kirahisi.
MAISHA YA ANETH
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti
hili wakidai kumjua dada huyo, walisema kuwa, baada ya kifo hicho
wamebadili mawazo kuhusu yeye kuwa huenda alijua anawindwa.
“Awali tulijua ni dada anayeringa, kwani
alikuwa akifika dukani, anaegesha gari jirani kabisa na mlango wa duka
kisha anaagiza kitu anachokitaka, anapelekewa, analipa pesa anaondoka.
“Hata siku tatu kabla ya kifo, alifika
kwenye kibanda cha chipsi, akaagiza na kufungiwa akiwa ndani ya gari.
Alikuwa hana kawaida ya kushuka, huenda alijua anawindwa,” alisema mkazi
mmoja wa maeneo ya Kibada huku akiomba hifadhi ya jina lake.
SIMU ZA KUULIZWA ALIPO
Mmoja wa watu waliodai kufanya kazi na
marehemu wizara ya fedha, alisema kuwa, wiki chache nyuma, Aneth aliwahi
kusema kuwa, kuna wanaume wamekuwa wakimpigia simu na kumuuliza; Aneth
uko wapi?’ lakini akiuliza we nani? Simu inakatwa!
“Huenda wale watu nao si sehemu ya
watuhumiwa hawa. Maana hali hiyo alisema hakuwahi kukumbana nayo siku za
nyuma. Baada ya kusikia amechinjwa sasa nahisi huenda Aneth
alifuatiliwa kwa siku nyingi nyuma lakini yeye alikuwa hajui,” mtu mmoja
aliliambia Uwazi kwa kumkariri mfanyakazi mmoja wa wizara hiyo.
MAISHA YAKE NA MAJIRANI
Baadhi ya majirani na nyumba ya marehemu
walisema kuwa, haikuwa rahisi kubaini mienendo ya watu wasioeleweka
nyumbani kwa Aneth kwa vile maisha yake yalikuwa hayasomeki kwa mwanga
wa kawaida.
“Alikuwa akikuona anakusalimia akiwa
ndani ya gari, akiingia kwake ameingia. Sasa isingekuwa rahisi kumjua
kwa undani yeye na wageni wanaofika kwake. Lakini mimi nimewahi kusikia
kwamba, Aneth aliolewa ila kwa bahati mbaya ndoa yake ilivunjika mwaka
mmoja na baba wa mtoto wake,” alisema jirani mmoja kauli ambayo pia
ilithibitishwa na dada mmoja wa Aneth.
NDUGU WASHTUKA, WAWEKA MLINZI
Gazeti la Uwazi pia lilifanikiwa kufika
nyumbani kwa marehemu ambapo lilikuta nyumba inalindwa na mlinzi ambaye
alisema aliwekwa hapo baada ya mauaji hayo.
UWAZI OFISINI KWA RPC TEMEKE
Hayo yote yalikuwa maneno mbalimbali ya
vyanzo vyetu, hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Uwazi lilifika ofisini
kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Gilles Mroto ili kumsikia kama
ana mtiririko huo, lakini kwa upande wake, alisema kuwa, wapo katika
msako mkali kuwasaka wauaji hao.
“Hata huyo hausigeli pia tunamsaka sana
ili kulisaidia jeshi la polisi kwa vile uondokaji wake na mauaji kuna
utata,” alisema Kamanda Mroto.
MATUKIO YA KUIANDAMA FAMILIA
Tangu kutokea kwa mauaji ya Erasto, kumekuwa na matukio mengi ya kuiandama familia hiyo kwa kutaka kuwatoa roho wahusika.
KUNA ALIYEMWAGIWA SUMU
Dada wa Aneth aliyetajwa kwa jina la
Antuja aliwahi kumwagiwa kitu kinachosadikiwa kuwa ni sumu wakati akiwa
amelala chumbani na mtoto wa Aneth, Allan hivyo kuathirika na sumu hiyo.
TUKIO LA HONGERA BAR
Desemba mwaka jana, dada mwingine
aitwaye Ester na muwewe walipigwa risasi mgongoni na kifuani wakiwa
katika Baa ya Hongera, Kijitonyama, Dar.
Mwili wa Aneth alisafirishwa jana kwenda Kijiji cha Kairo, Mererani, Simanjiro, Manyara kwa mazishi. Mungu aiweke pema peponi, roho yake. Amina.
CHANZO: UWAZI/GPL
Post a Comment