Yanga yakamata mchawi APR
Pluijm, raia wa Uholanzi, ambaye anainoa Yanga iliyofikia katika Hoteli ya The Mirror iliyopo Remera, Kigali, ameliambia Championi Jumamosi kuwa: “Nimekamata kila kitu cha APR kwa kuambiwa na kutazama, kwa ujumla tupo vizuri kwa mchezo huu.”
Kikosi cha timu ya APR kikifanya mazoezi Kigali siku ya jana.
APR inayonolewa na kocha mpya Nizar Khanfir raia wa Tunisia,
inawategemea zaidi nyota wake Jean-Claude Iranzi, Yannick Mukunzi na
Abdul Rwatubyaye.Hivi karibuni, Rwatubyaye aliifungia APR mabao matatu ‘hat trick’ dhidi ya Mbabane Swallows na kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 4-2. Awali APR ilifungwa bao 1-0 halafu ikashinda 4-1.

Wachezaji wa APR wakiendelea na mazoezi.
Yanga ilitua juzi jijini hapa na jioni yake ikafanya mazoezi kwenye
viwanja vya Shirikisho la Soka Rwanda (Ferwafa) na jana Ijumaa jioni
ilifanya mazoezi Uwanja wa Amahoro.Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa APR, Khanfir alisema: “Ni mechi yangu ya kwanza lakini nitapambana, nina furaha nimekuta kikosi bora APR, ni lazima tucheze vizuri nyumbani.”
ZIPO MOTO
Yanga iliyoitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani, Jumanne wiki hii iliifunga African Sports mabao 5-0 katika Ligi Kuu Bara.
Katika ligi kuu, Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 50 katika mechi 21 huku ikifunga mabao 51 na kufungwa 11 tu, APR yenyewe Jumatatu wiki hii ilishinda mabao 3-0 dhidi ya AS Muhanga.
Kama ilivyo kwa Yanga, APR nayo ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 30 ambazo ni mbili nyuma ya vinara Mukura Victory Sports huku ikiwa na michezo miwili mkononi wakati Yanga wanao mmoja.
MTN GUMZO
Ukiachana na Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite ambao wamewahi kuichezea APR kabla ya kutua Yanga, gumzo kubwa katika kikosi cha Yanga tangu kilipotua jijini hapa ni MTN, yaani washambuliaji Simon Msuva, Amissi Tambwe na Donald Ngoma.
Katika mazoezi ya kwanza, mashabiki walijazana kwenye viwanja vya Ferwafa kuwatazama nyota wa Yanga waliokuwa wakifanya mazoezi chini ya Pluijm. Hata basi la Yanga linapopita mitaani mashabiki wamekuwa wakilishangilia.
Katika mazoezini ya jana jioni ya Yanga kwenye Uwanja Amahoro ambayo yalianza huku mvua ikinyesha, Pluijm alizuia wapigapicha za video wakiwemo wa Azam TV akihakikisha hakuna kitu kinachorekodiwa.
Mchezo wa leo umekuwa gumzo Rwanda hasa jijini Kigali kiasi kuwagawa mashabiki kwani wapo wengi wanaoonekana kuishangilia Yanga.
Jezi za Yanga zimeonekana kuwa na soko kubwa ambapo mpakani zilikuwa zinauzwa hadi Sh 15,000 wakati awali zilikuwa zikiuzwa Sh 5,000. Mshindi kati ya Yanga na APR atacheza na Recreativo do Libolo ya Angola au Al-Ahly mwezi ujao. Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuwa; Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Vincent Bossou, Kelvin Yondani, Twite, Msuva, Thabani Kamusoko, Ngoma, Tambwe na Niyonzima.
CHANZO; GPL
Post a Comment