ad

ad

Tambwe, Ngoma waivuruga APR


 
Nicodemus Jonas, Kigali
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, Yanga, wapo jijini hapa tayari kabisa kwa kazi moja tu, kuipa kichapo Armée Patriotique Rwandaise FC maarufu kwa jina la APR ya nchini hapa katika mtanange wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo kuna matukio mengi yameshatokea lakini kikubwa ni Yanga kuonekana kuwa makini kuelekea mchezo huo.
Yanga imetua jijini hapa lakini kuanzia kwa mashabiki hadi benchi la ufundi la wenyeji wao, mazungumzo ni kuhusu uwezo wa Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Thaban Kamusoko na Simon Msuva.
Kutua Rwanda
Yanga iliondoka Dar es Saalam, Tanzania, jana alfajiri kisha ikawasiri majira ya asubuhi ndani ya Jiji la Kigali huku wachezaji wakionekana kutokuwa na hofu, muda mwingi wakicheka na kupiga stori za hapa na pale.
 

Mara baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali, msafara wa Yanga ulipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Balozi Ally Iddi Siwa.
Wagomea basi la APR
 

Mara baada ya kutua uwanjani hapo, APR walikuwa wamewaandalia Yanga basi ambalo Wanajangwani walilikataa kwa kuwa tayari kulikuwa na mipango ya kukodisha basi lingine ambalo ndilo wachezaji walilopanda na kuelekea kwenye Hoteli ya Mirror.
Wachezaji wafunguka
 

Baada ya kuwasili jijini hapa, Championi Ijumaa lilipata nafasi ya kuzungumza na wachezaji kadhaa wa Yanga, beki Juma Abdul na kiungo mchezeshaji, Thaban Kamusoko ambao walisema hali ya hewa siyo tatizo kwao na kila kitu kinaenda vizuri.
 

“Hali ya hewa siyo tatizo, binafsi nipo vizuri na hata wenzangu naona wapo vizuri pia, tunasubiri muda wa mechi tu,” alisema Kamusoko.
Kazi yaanza
 

Jana jioni, Yanga ilikuwa ikitarajiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Ferwafa ambao unamilikiwa na Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa). Mchezo wenyewe utapigwa kwenye Uwanja wa Amahoro.
Kocha APR achachawa
 

Kabla ya kupanda ndege kwenda Rwanda, Yanga iliichapa African Sports mabao 5-0 katika Ligi Kuu Bara, Jumanne ya wiki hii, matokeo ambayo yamemfanya Kocha Msaidizi wa APR, Emmanuel Rubona kukiri kuwa Yanga ni timu ngumu.
 

“Tumejiandaa vizuri kwa sababu tunafahamu kuwa tunacheza na timu kubwa Afrika Mashariki ambayo ina wachezaji wengi wenye uzoefu wa kucheza katika mazingira yoyote na kuweza kupata matokeo mazuri.
 

“Hofu ambayo tunayo kutoka kwao ni safu yao ya ushambuliaji ambayo ina yule mchezaji anayetokea Burundi (Amissi Tambwe) na yule Mzimbabwe (Donald Ngoma), hao watu ni hatari sana wanapokuwa wanasaka ushindi, muda wowote na wakati wowote wanaweza kubadili sura ya mchezo.
 

“Lakini kwa hilo hatuwezi kukata tamaa kiasi cha kutufanya tushindwe kupambana, tumesikia walipata ushindi wa mabao tano katika mchezo wa ligi ila hata sisi tulishinda pia, tumepanga ndani ya dakika 15 za kwanza tuweze kupata mabao ya haraka ili kupunguza kasi yao na ikiwezekana kuwazuia kabisa,” alisema Rubona.
Ngoma afunguka
 

Akizungumzia mchezo huo, Ngoma alisema: “Nia yetu ni ushindi,  naamini hilo litawezekana, maana tumejiandaa vizuri na tuna ari kubwa. APR ni timu nzuri na sisi tunahitaji kuongeza juhudi mara mbili ya hapa.”
 

Niyonzima afichua mbinu za APR Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima amesema kuna mambo mengi anayoyajua ya APR ambayo ni timu yake ya zamani na atawapa mbinu wenzake.
 

“APR ni timu nzuri na ina wachezaji wengi wazuri vijana, soka la Afrika Mashariki huwa linafanana hivyo wanaijua vizuri Yanga na tunatakiwa kujiandaa ili kuweza kufanya vema kwani mchezo wa kimataifa siku zote unakuwa mgumu.
“Nitakaa na wenzangu kuweza kuwaeleza yale machache ambayo nayajua mimi kuhusu APR ili yaweze kutusaidia japokuwa APR ya sasa ni tofauti na ile niliyokuwa nikiichezea,” alisema.


CHANZO: IJUMAA GAZETI

No comments

Powered by Blogger.