NILIUA KUMLINDA MAMA YANGU- 14

“Unasema kwamba alikuwa msichana?” aliuliza Dismas huku kwa mbali akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndiyo!”
“Hajaja na mizigo mingine?”
“Hajaja nayo! Alikuwa na hiki kibegi tu.”
“Mhh!”
“Ndiyo hivyo!”
Hakutaka kukaa ndani ya chumba hicho, akili yake ilimwambia kwamba piga ua ilikuwa ni lazima mwanamke huyo apatikane. Wakatoka ndani ya chumba hicho na kuelekea katika choo cha nje kwa kuamini kwamba inawezekana alikuwa huko, walipofika, hakukuwa na mtu.
Wakarudi chumbani mule harakaharaka. Dismas akaanza kukiangalia kile chumba kwa umakini mkubwa, alijichukulia yeye kuwa mtuhumiwa halafu polisi walikuja kwa lengo la kumkamata, je angejificha wapi? Jibu lililokuja harakaharaka kichwani mwake ni juu ya dari tu.
“Atakuwa juu ya dari...kalete ngazi...” alisema Dismas na kuwafanya watu wote washangae.
“Juu ya dari?”
“Ndiyo! Kaleteni ngazi...” alisema Dismas, hapohapo dada wa mapokezi akatoka na kuelekea uani na baada ya dakika moja, akaingia huku akiwa na ngazi mkononi. Dismas akaichukua, akaiweka sawa, akaanza kupanda na kuufungua mfuniko wa dari kwa lengo la kuchungulia ndani.
“Nishaanza kusikia harufu ya pafyumu, nilijua yupo humu ndani,” alisema Dismas, akachukua simu yake, akawasha tochi, mkono wa kulia, akaupeleka kiunoni na kuchukua bastola yake tayari kwa mapambano.
*****
Cynthia alibaki akitetemeka, hakuwa na amani kule juu na alijua piga ua ilikuwa ni lazima kwa Cosmas au mtu yeyote kupanda kule juu na kuchungulia kilichokuwa kikiendelea. Hakutaka kujiuliza sana, alichokifanya ni kuanza kutambaa kwa umakini pasipo kusikika sauti yoyote ile, lengo lake likiwa ni kwenda kwenye chumba kingine kabisa kilichokuwa na mlango wa kutokea.
Kulikuwa na mabomba mengi yaliyopitishwa nyaya nyingi za umeme, hakujali, kulikuwa na panya lakini hakuwaogopa, kitu pekee alichokuwa akikihofia ni kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
“Hawawezi kunikamata...” alisema Cynthia na hapohapo akamsikia Cosmas akisema kwamba apande juu ya dari kuangalia kama kulikuwa na mtu.
Hapo ndipo akapata nguvu ya kutambaa zaidi, alitambaa kwa harakaharaka, mpaka mhudumu kwenda kuchukua ngazi na kuisimamisha, tayari aliufikia mlango wa dari, akaufungua, akatumbukia chumbani na harakahataka kuufunga.
Alichokifanya ni kuufuata mlango wa kutokea ndani ya chumba hicho, kilichomshtua zaidi, mlango ule haukuwa na mteja yeyote hivyo bado ulikuwa umefungwa kwa ufunguo. Hapo ndipo akili yake ilipoanza kucheza ni kitu gani alitakiwa kukifanya.
Hakutaka kuchelewa, harakaharaka akakimbilia chooni ambapo huko akakutana na kidirisha kidogo, kilikuwa na mbao zilizoonekana kuchoka, hakikuwa na nondo kama vilivyokuwa vidirisha vingine vya gesti nyingine, alichokifanya ni kusimamisha ndoo kisha kuanza kupanda.
Kutokana na kuwa mtu wa mazoezi, hilo wala halikuonekana kuwa tatizo kwake, aliweza kupanda harakaharaka kisha kuzipiga zile mbao ambazo zikavunjika na kudondokea nje, kilichofuata ni kupanda na kujipenyeza katika kidirisha kile, alipofanikiwa, akatua upande wa pili ambao ulikuwa na uchochoro na kisha kutokomea zake huku akiacha pasipoti ndani ya chumba kile.
*****
“Vipi mkuu! Yupo?”
“Hakuna mtu aiseee...”
“Ila si umesema umekutana na harufu ya pafyumu?”
“Harufu ipo ila mwenyewe hayupo,” alijibu Cosmas huku akichungulia ndani ya dari lile.
Cosmas akatoka harakaharaka, alikuwa na wasiwasi kwamba inawezekana mtu aliyekuwa akimtafuta alishukia upande wa pili. Akamuuliza dada wa mapokezi kama kulikuwa na mlango mwingine wa dari, dada yule akamwambia kwamba kulikuwa na mlango mwingine chumba cha jirani, wakaelekea huko, hakukuwa na mtu yeyote yule na walipokwenda chooni kuhakiki, wakakuta kidirisha kikiwa kimevunjwa.
“Daah! Tushamkosa...” alisema Cosmas huku akionekana kukata tamaa.
*****
Ilikuwa ni Jumapili ambayo idadi kubwa ya watu walikusanyika katika Kanisa la Praise And Worship kwa ajili ya kumuabudu Mungu kama zilivyokuwa Jumapili nyingine. Idadi ya watu siku hiyo ilikuwa kubwa mno kwani ndiyo siku iliyokuwa ikitangazwa kwamba Mungu angefanya miujiza mikubwa, viwete wangetembea, vipofu wangeona na hata wale ambao walikuwa kwenye vifungo vya shetani kufunguliwa na kuwa watu wapya.
Watu kutoka katika mikoa mbalimbali walifika kanisani hapo, walitaka kumsikia mtumishi wa Mungu, mpaka mafuta wa Bwana, mchungaji Yekonia ambaye alijulikana kuwa na upako mkubwa kutoka kwa Mungu. Kila alipokuwa akihubiri, alichukua kitambaa chake, akawapuliza watu, wakaanguka huku wakipiga kelele, watu wakashangilia pasipo kujua kama watu wote hao walikuwa wamepangwa.
“Leo ni siku ya kufunguliwa...” alisema mchungaji Yekonia, aliongea mpaka jasho likamtoka, aliwaangalia watu huku akionekana kuwa na hamu ya kuongea maneno mengi zaidi, tena yenye tumaini ambayo yangewafanya watu kumuamini zaidi.
Kila aliyekuwa akiyasikia maneno hayo, alipiga kelele za shangwe, kwao, mchungaji Yekonia alionekana kuwa na nguvu za Mungu, uchafu wake aliokuwa akiufanya ulikuwa siri kubwa, hakutaka mtu yeyote yule afahamu kilichokuwa kikiendelea.
Alihubiri kwa nguvu zote, ibada ilichukua saa sita mpaka kumaliza ndipo alipohitaji watu wenye matatizo mbalimbali kuombewa wafike mbele, kama kawaida ya watu waliopangwa ambao walijifanya vipofu, viziwi wakasogea mbele na kuanza kuombewa.
“Mungu atawaponya, leo ni siku yenu...” alisema mchungaji Yekonia.
“Amen....”
Alianza kuomba, alikemea sana na baada ya dakika kumi, kila mtu aliyejifanya kuwa na matatizo, akajifanya kufunguliwa na hivyo kuibua shangwe ndani ya kanisa hilo.
“Mungu wangu si muongo...” alisema kwa sauti kubwa.
Baada ya watu hao kufanyiwa maombezi, akahitaji watu waliotaka kuokoka wasogee mbele, watu kumi na sita wakasogea akiwemo Cynthia ambaye alijifanya kuwa changudoa ambaye alitaka kukombolewa kutoka katika kifungo cha shetani kilichomtesa miaka mingi.
“Unaitwa nani dada?” alimuuliza Cynthia.
“Naitwa Marry John...”
“Unataka nini binti yangu?”
“Nataka kuokoka...nimechoka kuishi maisha ya kidunia...”
“Leo Mungu atakuokoa, nuru yake itaangaza katika maisha yako....” alisema na kanisa zima kuitikia kwa kusema ‘Amen’.
Akaanza kuwaongoza watu hao sara ya toba. Alipomaliza akaanza kuwaombea kisha kuwaambia waende kukaa. Muda wote huo, Cynthia alikuwa akimwangalia mchungaji Yekonia, lengo lake kubwa lilikuwa ni kumuua na hapo alipokuwa alikuwa akiangalia ni kwa jinsi gani angeweza kumshawishi amuombee maombi binafsi.
“Mchungaji...” aliita Cynthia mara baada ya ibada kuisha.
“Ndiyo binti yangu!”
“Nahitaji maombi bonafsi...”
“Hakuna tatizo....”
“Nataka nije ofisini kwako, Shetani amenitesa sana maishani mwangu, ninataka kuishi maisha mapya, maisha ya kumtumikia Mungu milele...” alisema Cynthia huku akijifanya kulia.
“Nyamaza binti! Mungu atakufungua...” alisema mchungaji Yekonia.
Akamwambia Cynthia kuonana naye jioni ya siku hiyo! Msichana huyo akakubaliana naye.
****
Watu waliendelea kusubiri nje ya ofisi ya mchungaji kwa ajili ya kufanyiwa maombezi binafsi. Muda ulizidi kwenda mbele, japokuwa msichana aliyetoka ndani ya chumba kile alisema kwamba mchungaji Yekonia alihitaji dakika thelathini kwa ajili ya kufanya maombezi yake binafsi, kitu cha kushangaza ni kwamba muda huo ulikuwa umepita kitu kilichowafanya kuchoka kusubiri.
Kila mmoja akaanza kuangalia saa yake, walichoka kusubiri hivyo mmojawapo kusimama na kujaribu kutegesha sikio mlangoni kwa ajili ya kusikiliza kile kilichokuwa kikiendelea ndani, ukimya mkubwa ulikuwa umetawala.
Hilo likawatia wasiwasi mno na kudhani kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, ila kupiga hodi, walishindwa kwa kuwa hawakuona kama ingekuwa heshima kutokana na mchungaji huyo kuagiza kwamba angechukua dakika thelathini tu kwa kufanya maombi binafsi.
“Saa moja limekata...” alisema mwanamke mmoja.
“Mmh! Ila hii si kawaida yake....mara nyingi hutembea na wakati...” alisema mwanaume mmoja.
“Au kuna tatizo?”
“Sidhani kwa kweli...”
Waliendelea kusubiri kwa nusu saa nyingine ndipo walipoamua mmojawapo agonge mlango kwani tayari watu walizidi kuongezeka. Mlango ukagongwa lakini hakukuwa na sauti yoyote kutoka ndani kitu kilichoibua maswali mengi, kwa nini iwe hivyo?
Wakapiga mioyo konda, liwalo na liwe lakini ilikuwa ni lazima kuufungua mlango, wakafanya hivyo. Walichokutana nacho, wanawake wakabaki wakipiga kelele, mwili wa mchungaji Yekonia ulikuwa juu ya meza, damu zilizoonekana kuganda zilitapakaa kwenye meza hiyo na nyingine sakafuni.
Picha iliyokuwa ikionekana, ilimtisha kila mtu, wakabaki wakiiangalia maiti ile huku wakionekana kutokuamini kile walichokuwa wakikiangalia. Harakaharaka simu zikapigwa polisi na ndani ya dakika mbili, tayari watu wakaanza kujazana katika eneo la ofisi hiyo.
“Unasemaje?”
“Nasikia mchungaji amejiua kwa kujichoma kisu...”
“Acha utani, mchungaji ajiue?”
“Ndiyo! Huamini sasa?”
“Siwezi kuamini bwana...mchungaji kujiua, sidhani...”
Kutokana na tukio hilo kutokea, kila mtu alikuwa akiongea lake. Wapo waliosema kwamba mchungaji alikuwa amejiua kwa kujichoma kisu lakini pia walikuwepo wale waliosema kwamba mchungaji huyo alikuwa ameuliwa na mtu fulani.
“Atakuwa nani sasa?” aliuliza jamaa mmoja.
“Mmh! Hapa inawezekana akawa yule msichana...”
“Kuna msichana alikuwa humu?”
“Ndiyo! Tena alituambia kwamba mchungaji alihitaji nusu saa za kufanya maombi binafsi...”
Hapo ndipo wakapata jibu kwamba inawezekana yule msichana aliyekuwa ametoka ndani ndiye ambaye alimuua mchungaji ndani ya ofisi yake. Walichanganyikiwa, hata polisi walipofika, waliwaambia kwamba kabla ya kugundua kwamba mchungaji alikuwa ameuawa, ndani kulikuwa na msichana ambaye aliyafanyiwa maombezi binafsi kabla ya kutoka na kusema kwamba mchungaji alihitaji dakika thelathini za kufanya maombi binafsi.
“Huyo msichana mnamfahamu?”
“Hapana afande...”
“Ila mkimuona?”
“Tutamfahamu...”
ITAENDELEA...
Post a Comment