NILIUA KUMLINDA MAMA YANGU- 12

“Tupe majibu tatizo lilikuwa nini!”
“Nilibaini kwamba kitufe cha kuifanya jenereta iwake kilikuwa kimetolewa,” alijibu Sued.
“Nani aliitoa?’
“Sijui ni nani!”
“Hujui na wakati wewe ndiye mlinzi?”
“Sijui chochote afande, na hakukuwa na mtu aliyekwenda kule kwenye banda la jenereta.” “Kwa hiyo kitakuwa kilijitoa chenyewe?”
“Sifikirii hilo mkuu!”
Bado mlinzi alikuwa akiulizwa maswali mfululizo, majibu aliyokuwa akiyatoa yakawafanya polisi kuona kwamba walitakiwa kuendelea kumshikilia kwa kuamini kwamba wangekuwa na uhitaji naye mkubwa.
Bado kifo cha bwana Kambani kiliendelea kuwa gumzo kila kona, kila mtu alijaribu kujiuliza juu ya maneno yale yaliyokuwa yamekutwa yameandikwa ukutani lakini hakukuwa na aliyegundua kitu chochote kile.
Simanzi iliendelea kuigubika Tanzania, kila aliyezisikia taarifa hizo alihuzunika sana kwa kuona kwamba kipenzi cha watu hakuwa tena duniani, aliuawa katika kipindi ambacho kila mtu alikuwa akimhitaji kwa hali na mali.
****
“Hebu niambie mmefikia wapi!”
“Bado tunashughulika mkuu, tupo chumbani tunajaribu kuumiza vichwa vyetu,” ilisikika sauti kutoka kwenye simu.
“Chumba kipi?”
“Mawasiliano.”
Hapohapo simu ikakatwa.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Samsoni Kumbila alikuwa akizungumza na polisi wake ambao walikuwa katika kitengo cha upelelezi ambao aliwapa kazi kubwa ya kuhakikisha wanapata maana ya yale maandishi yaliyosomeka ukutani ambayo yaliandikwa ‘Mwaka 213 KK’.
Kazi haikuwa ndogo, ilikuwa kubwa mno. Wapelelezi hao walikusanyika ndani ya chumba hicho, walijiuliza huku wakiwa na kompyuta yao wakiangalia vitu vilivyotokea mwaka huo kwa kuhisi labda kungekuwa na tukio ambalo wangeweza kulihusisha lakini hawakufanikiwa kupata chochote kile.
“Vipi?” “Hapa Google inanionyeshea kwamba mwaka 213 Kabla ya Kristo kulikuwa na tukio kubwa moja lililotokea,” alisema mpelelezi.
“Lipi?”
“Misri ilijigawa sehemu mbili, yaani Kaskazini ikaitwa na Memphis na Kusini ikaitwa na Thebes,” alijibu mpelelezi huyo.
“Kingine?”
“Daah! Kwenye matukio makubwa yaliyotikisa dunia, lipo hili tu. Hakuna jingine mkuu,” alisema mpelelezi yule.
“Kwa hiyo tukio la kugawanyika kwa Misri na hili la mauaji, mbona ni vitu visivyoendana!”
“Hata mimi nashangaa, labda kuna kitu.”
Kiukweli walichanganyikiwa, maneno yale yaliyoandikwa ukutani yaliwafanya polisi na wapelelezi wote kutokuelewa maana halisi ya maneno hayo. Maneno yale hayakuwa siri tena, kila mtu alijua, wengi wakadiriki kuyaandika katika makaratasi yao ili kujua yalimaanisha nini lakini hakukuwa na mtu aliyejua kitu chochote kile.
Nyumbani kwake, vilio vilisikika kila kona, mke wake alizimia mara tatu, watoto wake walijifungia chumbani huku wakilia tu. Hakukuwa na aliyeamini kwamba ule ndiyo ungekuwa mwisho wa kumuona mzee huyo aliyeonekana kuwa na roho nzuri ya kusaidia watu zaidi ya Watanzania wote.
Msibani hapo, kulikuwa na marafiki zake watatu, mchungaji Yekonia, bwana Marimba na Nkone, hawa walikuwa watu wenye heshima kubwa ambao mpaka katika kipindi hicho, hata nao walijiuliza juu ya mtu aliyeamua kumuua rafiki yao kipenzi.
Siku hiyo, katika msiba huko mkubwa, rafiki yao kipenzi alikuwa amewatoka, walimpenda, alikuwa mmoja wa watu waliopendwa sana nchini Tanzania kama walivyokuwa wao.
Kundi lao la watu wanne likawa limepungua, mtu mmoja akawa amewatoka na hivyo kubaki watu watatu. Walishindwa kujua ni nani alikuwa nyuma ya tukio lile, mioyo yao ilijawa na maswali mengi yasiyokuwa na majibu.
Kila walipomfikiria rafiki yao huyo, waliumia mioyoni mwao lakini hawakuwa na jinsi, hawakuwa na nguvu ya kuweza kubadilisha kile kilichokuwa kimetokea.
“Siamini,” alisema mchungaji Yekonia.
“Hivi ni nani aliyefanya mauaji haya?” aliuliza Nkone.
“Hata mimi sifahamu na sikumbuki kama alikuwa na ugomvi na mtu yeyote yule,” alisema bwana James.
“Nahisi kuna kitu.” “Kweli?”
“Ndiyo! Hapa kuna kitu.”
“Sidhani! Kichwa kinaniuma sana, hakuna kitu ambacho marehemu aliwahi kukifanya tusijue, sasa ni nani aliyefanya hivi?”
“Hapa ni lazima tuwashinikize sana polisi wafanye upelelezi mpaka muuaji apatikane, haiwezekani suala hili tulifumbie macho,” alisema Nkone.
Walibaki wakizungumza mambo mengi kuhusu mauaji yaliyokuwa yametokea, vichwa vyao vilikuwa na maswali yasiyokuwa na majibu. Walimfahamu mzee mwenzao, alikuwa mtu aliyependwa na watu wengi kiasi kwamba hata nao wenyewe hawakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angeweza kufanya mauaji kwa mzee huyo ambaye alikuwa kipenzi cha watu wengi.
“Ni lazima muuaji apatikane,” alisisitiza bwana Nkone na wote kukubaliana kuwahamasisha polisi wafanye kile walichotaka wakifanye.
****
Kifo cha bwana Kambani kiliwahuzunisha lakini kwa upande wa bwana Nkone, wakati mwingine alijisikia furaha ya ajabu. Kitu alichokuwa akikifikiria kwa wakati huo ni mapenzi tu, alijua fika kwamba bwana Kambani alikuwa na msichana mrembo wa sura ambaye alimvutia sana na katika kipindi chote hicho alihitaji sana kuwa naye.
Muda huo, kwake ikaonekana kuwa nafasi, hakutakiwa kumuacha msichana huyo, alimpenda na hivyo akawa tayari kwa kitu chochote kile.
Kitu cha kwanza alichokifanya ni kuzungumza na ndugu wa marehemu na kuwaambia kwamba kuna kitu alikuwa akikihitaji kama mwanzo wa upelelezi kutoka kwa polisi, kitu hicho kilikuwa ni simu.
Hakukuwa na ndugu aliyekuwa na maswali yoyote yale, walimwamini kwa kila kitu kwani alikuwa miongoni mwa marafiki wa karibu wa bwana Kambani, hivyo wakampa.
Bwana Nkone akaichukua simu ile na kwenda nayo ndani ya gari, huko, akajifungia na kuanza kuipekua. Kitu alichokuwa akikitafuta hakikuwa kingine bali namba ya Cynthia tu.
Kulikuwa na majina ya wanawake wengi, tena walioandikwa kwa majina asiyoyaelewa, kwa hiyo alichokifanya ni kuzichukua namba zote tayari kwa kuzijaribu, zilikuwa namba kumi na nane.
Akaanza kujaribu moja baada ya nyingine, ilikuwa kazi kubwa lakini hakutaka kuacha kwa kuamini kwamba nyuma ya kazi hiyo ngumu kulikuwa na mafanikio makubwa.
Alijaribu na kujaribu, namba ya kumi na tano ndiyo ilikuwa ya mtu aliyekuwa akimhitaji, kwenye simu iliseviwa kwa jina la Wa Ukweli. Sauti nyembamba ya Cynthia ikasikika kwenye simu, mwili wake ukasisimka, hakuamini kama kweli msichana huyo angepokea simu kutokana na msiba uliokuwa ukiendelea.
“Unajua unazungumza na nani?”aliuliza bwana Nkone.
“Hapana.”
“Bilionea Nkone hapa.”
“Waoo...kumbe ni wewe shem?”
“Ndiyo! Upo wapi?”
“Nipo nyumbani!”
“Ulikwenda msibani?”
“Ndiyo! Ila nimerudi muda si mrefu,” ilisikika sauti ya Cynthia kwenye simu.
Kitendo cha kusikia sauti ya Cynthia tu, tayari mapigo yake ya moyo yakazidi kudunda kwa nguvu, hakuamini kama hatimaye baada ya msichana huyo kugundua kwamba alikuwa yeye, angeendelea kuzungumza kwa uchangamfu namna ile.
“Nahitaji kuonana nawe...”
“Mimi?” aliuliza Cynthia huku akijifanya kushtuka.
“Ndiyo!”
“Mmh! Kuna nini tena jamani?”
“Hakuna kitu kibaya...usiogope bwana...”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Ila mbona harakaharaka?”
“Nimeamua tu mpenzi...”
“Basi tufanye keshokutwa...”
“Mmmh! Mbona mbali?”
“Nivumilie tu...”
“Sawa hakuna tatizo.”
Huo haukuwa mwisho wa kuzungumza, mara kwa mara walikuwa wakiongea kwenye simu, bwana Nkone alichanganyikiwa, bado ndoto zake zilikuwa kummiliki Cynthia kwa gharama yoyote ile.
Alikuwa bilionea hivyo alichokifanya ni kumuonyeshea Cynthia kwamba alikuwa bilionea mkubwa, hivyo suala la kumtumia fedha wala halikuwa tatizo hata kidogo.
Cynthia hakutaka kujirahisisha kwa bwana Nkonekitu kilichomfanya mzee huyo kuona kwamba msichana huyo alikuwa mgumu. Siku ambayo aliambiwa kwamba wangeonana, hawakuonana kwani Cynthia akajifanya kuwa bize.
Kila siku akawa mtu wa kuzungushwa tu mpaka ikaonekana kama kero. Baada ya wiki nne kupita, ndipo bwana Nkone alimwambia ukweli kama alikuwa akitaka kuonana naye au la.
Kwa kuwa kipindi cha mwezi mzima ulikuwa umepita, Cynthia akakubali kuonana naye na sehemu waliyopanga ilikuwa katika Baa ya Casanova iliyokuwa Masaki jijini Dar es Salaam. Mara macho ya bwana Nkone yalipotua kwa Cynthia, hakuamini kama angeweza kukutana na msichana huyo aliyekuwa akimpenda kwa moyo wake wote.
Ili kuonyesha furaha kubwa aliyokuwa nayo, akamsogelea na kumkumbatia huku akimshushia mabusu mfululizo pasipo kumuogopa mtu yeyote yule. Usiku huo katika baa hiyo ilikuwa ni kumwambia Cynthia ukweli juu ya alivyokuwa akijisikia moyoni mwake.
“Kweli unanipenda?” aliuliza Cynthia.
“Kwa moyo wangu wote, ninakupenda sana,” alijibu bwana Nkone.
Cynthia hakutaka kuzungumza kitu, alibaki kimya kwa muda huku akimwangalia mzee huyo machoni. Ni kweli alikuwa na dalili zote za kumpenda lakini hakutaka kuwa naye kwa sababu moja kubwa hata huyo mzee mwenyewe naye alikuwa kwenye ratiba yake ya kuuawa.
Siku hiyo akamzingua tena, alitaka kupewa muda zaidi wa kujifikiria, kwa bwana Nkone halikuwa tatizo, kwani hiyo kwake ilionekana kuwa nafasi kubwa ya kumuonyeshea msichana huyo jinsi alivyompenda.
Wakati akiendelea kumfikiria mzee huyo, huku upande wa pili alikuwa akipanga mashambulizi yake. Kama alivyoambiwa kwamba watu hao kipindi cha nyuma walikuwa na mpango kabambe wa kumuua yeye na mama yake, hivyo aliona kulikuwa na umuhimu wa kumuua mzee huyo kama kisasi cha kutaka kumuua yeye na mama yake.
Siku zikakatika, kitu alichokuwa amekifikiria ilikuwa ni lazima kumuua mzee huyo sehemu nyingine yoyote lakini si nyumbani kwake kama ilivyokuwa kwa bwana Kambani, kwani mzee huyo alikuwa akiishi na familia yake, tena ilikuwa nyumbani kwake.
Sehemu ambayo aliifikiria mara moja ilikuwa ni ndani ya gari la huyo mzee. Alichokifanya ni kununua dawa ya usingizi iitwayo Morphonium ambayo ilikuwa ikitumia kumlevya mtu kupitia kinywaji, alipoinunua, akampigia simu bwana Nkone na kuomba kuonana naye.
“Unataka tuonane wapi?” aliuliza mzee huyo.
“Popote, nataka twende kwenye hoteli yoyote ile tukakae, tena tulale hukohuko,” alisema Cynthia.
“Kweli?”
“Ndiyo! Utafika muda gani hapa?”
“Nipe dakika ishirini, si uliniambia unaishi Sinza Makaburini?”
“Ndiyo!”
“Nakuja.”
Usiku wa siku hiyo ulikuwa ni wa mwisho kwa mzee huyo kuvuta pumzi ya dunia hii, Cynthia alitaka kummaliza kabisa hivyo akaomba kuonana naye sehemu na kuzungumza.
Lengo lake kubwa lilikuwa ni kumlevya kwanza kabla ya kumuua, hivyo kwa usiku wa siku hiyo ilikuwa ni lazima akamilishe kila kitu.
Kwa upande wa pili, bwana Nkone alikuwa na furaha tele, kila alipokaa, alizisifia fedha zake tu, aliziona kumrahisishia kila kitu alichokihitaji katika maisha yake hasa kuwa na msichana huyo ambae kwa kipindi kirefu alimtamani sana.
Alijiandaa harakaharaka, hata mkewe alipomuuliza juu ya mahali alipotaka kwenda muda huyo, hakumwambia zaidi ya kumdanganya kwamba alitaka kwenda kuonana na marafiki zake waishio Kimara, mwanamke huko hakujali sana.
Dakika zilikwenda mbele, ndani ya dakika kumi tu, akawa amekwishajiandaa na kilichofuata ni safari ya kuelekea huko kwa Cynthia ambaye tayari aliisuka mipango yake na kila kitu kilikuwa tayari, ni marehemu mtarajiwa tu ndiye aliyekuwa akisubiriwa.
*****
Alichukua dakika kadhaa mpaka kufika sehemu alipoelekezwa na Cynthia ambapo alimkuta msichana huyo na kumchukua na safari ya kuelekea hotelini kuanza. Njiani, kila mmoja alionekana kuwa na furaha tele, kwa bwana Nkone, kila kitu kilichokuwa kikiendelea hakukiamini na wakati mwingine kujiona kuwa miongoni mwa watu waliokuwa na bahati mno.
Cynthia akamwambia mzee huyo kwamba hakuwa amekula, hivyo alihitaji kula kwanza kabla ya mambo yoyote kuendelea. Kwa sababu walikuwa wakipita katika Barabara ya Sam Nujoma, wakapanga kupitia katika Mgahawa wa Samaki Samaki kwa ajili ya kununua juisi na chakula.
“Kwanza mpaka nile,” alisema Cynthia.
“Siyo tatizo! Twende kununua chakula.”
“Na hoteli gani umepanga twende?”
“Queen Elizabeth...”
“Ila baada ya kutoka katika Baa ya Casanova au?” aliuliza Cynthia.
“Baa sidhani kama kuna haja ya kwenda huko kwani si tayari chakula na vinywaji tutakuwa navyo?”
“Sawa, hakuna tatizo mahabuba...” alisema Cynthia hapohapo kumsogelea bwana Nkone na kumbusu, yote hayo ilikuwa ni kumchanganya tu.
Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamekwishafika katika maduka ya Mlimani City ambapo bwana Nkone akateremka na kwenda kununua chakula na vinywaji. Muda wote huyo Cynthia alikuwa akimwangalia tu, moyo wake ulimuomba Mungu mzee huyo ajisahau kwa hatua yoyote ile ili afanye kile alichopanga kukifanya.
Mzee huyo aliponunua vitu vilivyohitajika, akarudi ndani ya gari, Cynthia akachukua juisi yake, akaifungua na kuanza kunywa hapohapo, naye bwana Nkone akachukua na kuanza kunywa.
“Sant Anna ipo wapi?’ aliuliza Cynthia.
“Kwani uliniagiza na hiyo?”
“Ndiyo! Sasa jamani tutakunywa juisi tu kama watoto?”
“Aya subiri nifuate, chupa ngapi?”
“Mimi nataka moja, au kama wewe unahitaji pia,” alisema Cynthia.
“Hapana! Juisi inatosha.”
“Sawa, nenda kanunue mpenzi, lete hii nikushikie...” alisema Cynthia.
Kutokana na mahaba aliyoonyeshewa, bwana Nkone hakuwa na sababu ya kumkatalia Cynthia amshikie kinywaji kile, akampaka na kisha kuteremka na kwenda kununua mvinyo huo.
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi kwa Cynthia kufanya kile alichotaka kukifanya, hakutaka kuchelewa, hapohapo akachukua madawa yake ya usingizi kisha kumuwekea kwenye juisi yake kisha kumsubiria ambapo baada ya dakika chache, akarudi.
“Ushindwe wewe sasa....” alisema bwana Nkone huku akimkabidhi chupa ya pombe aliyokuwa akiitaka.
“Asante mpenzi...”
Wakaendelea kunywa vinywaji vyao kama kawaida. Bwana Nkone hakugundua kama ndani ya juisi ile aliwekewa madawa ya usingizi, akainywa juisi ile kama kipindi cha nyuma, baada ya hapo, wakaanza safari ya kuelekea huko hotelini.
Stori hazikuisha, waliendelea kuzungumza zaidi. Kama dakika tano baadaye, bwana Nkone akaanza kujihisi tofauti, macho yake yakaanza kuwa mazito. Cynthia alikuwa akifuatilia taratibu, alipoona hivyo, akamwambia mzee huyo asogee pembeni na yeye ashikilie usukani, akafanya hivyo.
Kiti alichowekwa bwana Nkone, hakuendelea kuwa na nguvu, hapohapo akajikuta akilala usingizi mzito, kilichoendelea, hakukijua.
Cynthia aliendesha gari kwa mwendo wa kawaida, mpaka kufikia hatua hiyo, tayari alijiona kuwa mshindi mkubwa. Hakukuwa na sehemu nyingine ambayo angeweza kumuua mzee huyo zaidi ya humohumo ndani ya gari lake.
Alichokifanya ni kuchukua Barabara ya Ali Hassani Mwinyi na kuanza kuelekea upande wa Kusini huku lengo lake likiwa ni kutaka kuelekea katika Ufukwe wa Coco. Hakuchukua muda mrefu, akaanza kukaribia eneo hilo ambapo akalipeleka gari hilo mpaka sehemu iliyokuwa na miamba na kuliegesha hapo.
“Ni lazima nifanye harakaharaka...” alisema Cynthia na kuchukua kisu chake.
Hakutaka kupoteza muda, ilikuwa ni lazima amuue bwana Nkone humohumo ndani ya gari, akachukua kisu chake, hakutaka kujiuliza nini cha kufanya, hapohapo akaanza kuuchoma kisu mwili ule, tena mfululizo, kifuani na tumboni, unyama wote huo, aliufanya pasipo huruma yoyote ile.
Gari likatapakaa damu, moyo wake ukaridhika, kitendo cha kumuua bwana Nkone, alijisikia amani moyoni mwake. Wakati akiwa humo huku akijifikiria nini cha kufanya, ndipo alipokumbuka kwamba ilikuwa ni lazima kuandika namba ambazo kwake zilikuwa na maana kubwa.
Akateremka kutoka garini na kuangalia huku na kule ambapo macho yake yakatua katika kibao kimoja, akakifuata, akakichukua na kuandika ‘Mwaka 213 Kabla ya Kristo’ kisha kukiweka mule ndani ya gari.
Hakutaka kuuacha mwili huo humo, akafungua mlango na kuubeba mwili ule na kuupeleka katika miamba na kuuacha huko huku akiivua blauzi yake na kuilowanisha maji na kufuta alama zote za mikono zilizokuwa katika mwili wa bwana Nkone.
“Pumzika kwa amani....bado wenzako wanakuja....” alisema Cynthia, alipomaliza, akaondoka zake na kuacha gari na vitu vingine mahali hapo.
****
“Habari yako!”
“Salama tu! Nazungumza na nani?”
“Unazungumza na msamaria mwema, Joseph.”
“Upo wapi?”
“Huku Coco Beach.”
“Ok! Nikusaidie nini?”
“Mimi na mke wangu tumeukuta mwili hapa ukiwa umetupwa huku kwenye miamba,” ilisikika sauti.
“Unasemaje?”
“Tumekuta huku mwili. Ni wa mtu ambaye ninamfahamu sana. Ni bwana Nkone...”
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo mkuu.”
Hiyo ilikuwa simu iliyopigwa katika kituo cha polisi cha Osterbay, mtu mmoja alipiga katika namba za usalama na kutoa taarifa iliyomshtua kila mmoja aliyeisikia.
Polisi wakashtuka, hawakuamini kile walichokisikia kwamba bwana Nkone aliuawa na mwili wakekutupwa katika miamba ndani ya ufukwe wa Coco. Polisi hao hawakutaka kubaki kituoni hapo, zaidi ya polisi kumi wakaingia ndani ya gari lao, bunduki mikononi na kuanza kuelekea huko.
Gari liliendeshwa kwa kasi, wananchi wakashangaa, hawakujua kulikuwa na nini mpaka gari lile kuendeshwa kwa mwendo wa kasi namna ile. Kwa kuwa kutoka katika kituo hicho mpaka katika ufukwe wa Coco hakukuwa mbali sana, walitumia dakika tano tu, wakaingia.
Kwa mbwembwe za kikomandoo wakajirusha kutoka ndani ya gari, kwa mbali mbele, kule kulipokuwa na miamba, idadi kubwa ya watu ilikuwa imekusanyika, wakajua kwamba huko ndipo kulipokuwa na hilo tukio, hivyo wakaanza kuelekea huko.
Walipofika, wananchi wakawaachia njia na kupenya mpaka mbele kabisa, mwili wa bwana Nkone ulitupwa pembezoni mwa bahari katika miamba hiyo, kila mtu aliyeuona, alijua wazi kwamba huo ulikuwa mwili wa mzee huyo bilionea.
Kila mtu aliyekuwa mahali hapo alikuwa bize na kamera yake, alikuwa akipiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Polisi hao wakawaamuru watu wasogee kwani walitaka kufanya kazi yao kama kawaida.
Wakaufuata mwili ule, walipouangalia, walikuwa na uhakika kwamba ulikuwa wa bwana Nkone, yule bilionea ambaye naye alisifika na watu wengi kwamba alikuwa na roho nzuri.
Pembeni ya mwili ule, kulikuwa na ubao uliokuwa na maneno yaliyosomeka ‘Mwaka 213 Kabla ya Kristo’. Maneno hayo yaliwachanganya polisi hao, wakashindwa kufahamu yalikuwa na maana gani, walichanganyikiwa.
Walikumbuka kwamba mwezi mmoja kulikuwa na mauaji yaliyotokea kwa bwana Kambani nyumbani kwake, ndani ya chumba chake, kulikuwa na maneno ambayo hayakutofautiana sana na yale ambayo waliyakuta yakiwa yameandikwa ubaoni.
Hali hiyo ilimaanisha kwamba muuaji alikuwa mmoja, alikuwa nani na kwa nini aliua? Kila aliyeuliza, alishindwa kujibu chochote kile.
Ndani ya nusu saa, tayari taarifa zilisambazwa katika mitandao ya kijamii, kila mtu aliyeziona, alipigwa na butwaa, hakuamini kile kilichokuwa kikionekana katika simu na kompyuta zao, mwanaume wa pili, mwenye roho nzuri ambaye hakuangalia maisha yake aliuawa kikatili na mwili wake kutupwa pembezoni mwa bahari katika ufukwe wa Coco.
“Jamani! Hivi ni macho yangu au?’ aliuliza dada mmoja, alishika simu yake, alikuwa na marafiki zake.
“Kuna nini shosti?”
“Eti bwana Nkone ameuawa!”
“Acha masihara wewe.” “Kweli tena! Hebu angalia jamani!” aliwaambia wenzake huku akiwaonyeshea taarifa hiyo kwenye simu.
“Mmmh! Taarifa ya uongo hiyo.” “Ila imeandikwa na ukurasa wa Global Publishers! Kweli wanaweza kudanganya? Haiwezekani, hawakuwahi kudanganya kwenye maisha ya watu,” alisema msichana huyo.
Huo ulikuwa ukweli, mtu mwingine aliyekuwa akipendwa sana aliuawa kikatili, hakukuwa na aliyeamini kwamba mzee huyo alikuwa ameuawa na mwili wake kutupwa baharini.
Polisi wale waliokuwa katika eneo la tukio wakauchukua mwili ule na kuondoka nao kuelekea hospitalini. Walipofika huko, hata madaktari walioupokea hawakuamini macho yao, waliangalia mara mbilimbili kuona kama walikuwa wamemfananisha au alikuwa mwenyewe.
“Si bwana Nkone huyu?” aliuliza nesi mmoja huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndiyo! Mpelekeni ndani!”
Mwili ule ambao tayari uliwekwa kwenye machela ukaanza kusukumwa kuelekea ndani ya hospitali hiyo. Waandishi wa habari ambao tayari walipewa taarifa kitambo, walikuwa mahali hapo huku wakipiga picha kila hatua iliyokuwa ikiendelea.
Shati lake jeupe alilokuwa amelivaa ilikuwa vigumu kujua kama shati hilo lilikuwa jeupe kutokana na damu zilizokuwa zimetapakaa baada ya kuchomwa visu mfululizo vya tumbo kiasi kwamba mpaka utumbo wake kutoka nje.
ITAENDELEA KESHO
Post a Comment