NILIUA KUMLINDA MAMA YANGU- 11

Huo ndiyo ulikuwa mpango wake, alitaka kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa yaani kwani kwa kuanza kufanya umafia, angeanzia na kukata umeme, hivyo kama asingefanikisha kuriharibu jenereta basi wakati anazima umeme, jenereta lingejiwasha.
Alipohakikisha kila kitu kipo sawa, akarudi chumbani kwake. Baada ya kukaa huko kwa saa moja, akasikia mlango ukigongwa na mtu aliyeugonga alikuwa mfanyakazi wa ndani, Amina.
“Samahani wifi.”
“Bila samahani.”
“Kaka Salmin aliniambia kaka Joshua akija nikushtue...”
“Mimi?”
“Ndiyo! Sasa kaka amefika yupo sebuleni...”
“Sawa. Mwambie nakuja.”
Japokuwa Cynthia hakuwa amemaanisha alipomwambia mlinzi kuhusu uhuni wa bwana Kambani lakini hakuwa na jinsi, kwa sababu mlinzi alimwambia huyo kijana kwamba ndani alikuwepo yeye, akaona lingekuwa jambo jema kuonana na huyo kijana aliyekuwa karibu na bwana Kambani ili kuzungumza naye.
Alipomaliza kujiweka sawa chumbani, akaanza kupiga hatua kuelekea sebuleni. Alipofika, huko uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana, macho yake yakatua kwa mwanaume ambaye hakuwa mgeni machoni mwake, alimfahamu vilivyo, alikuwa mpenzi wake, Joshua, yule mwanaume aliyekutana naye kwenye ndege.
“Cynthia....” alijikuta akiita Joshua huku akiwa aamini kama yule shemeji yake aliyeambiwa na mlinzi angekuwa msichana wake aliyekuwa na ndoto nyingi za kuishi naye pamoja.
Kile alichokiona, wakati mwingine alihisi kwamba alikuwa ndotoni ambapo baada ya muda angeshtuka na kujikuta akiwa kitandani.
****
Joshua hakuamini kabisa, kila alipomwangalia mpenzi wake, Cynthia alibaki akiwa na mshangao mkubwa. Kichwa chake kikaanza kujiuliza maswali kwamba iliwezekanaje msichana aliyekuwa akimwamini kwa asilimia mia moja kuchukuliwa na bosi wake, kila alipojiuliza, akakosa jibu.
“Cynthia...” aliita Joshua huku akisimama.
“Cynthia?” aliuliza Cynthia huku akijifanya kushangaa.
“Unafanya nini hapa?”
“Nipo kwa mpenzi wangu!”
“Yaani Kambani ni mpenzi wako?”
“Ndiyo! Wewe ni nani?” aliuliza Cynthia huku akijifanya kumshangaa Joshua.
“Unasemaje?”
“Nimeuliza wewe nani, sikufahamu halafu unaniita jina la nani sijui...” alisema Cynthia.
“Wewe si Cynthia?”
“Mimi Cynthia...tangu lini?” aliuliza Cynthia, kwa kumwangalia tu, alionyesha kumaanisha kwamba hakuwa Cynthia.
Joshua akapigwa na mshangao, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea. Moyo wake ulimwambia kwamba msichana aliyesimama mbele yake alikuwa Cynthia, yaani kuanzia sura, umbo mpaka urefu, vyote hivyo alifanana na Cynthia.
“Hapana! Wewe ni Cynthia...”
“Cynthia ndiye nani?”
“Mpenzi wangu! Umefanana naye kweli.”
“Mmmh! Basi duniani wawiliwawili kaka! Naitwa Amina, ila unaweza kuniita Aminatha...” alijitambulisha Cynthia kwa jina la uongo.
Japokuwa Cynthia alimwambia kwamba hakuwa msichana huyo aliyemtaja lakini bado Joshua alikuwa na uhakika hivyo kitu kilichofuata kilikuwa ni kumchunguza tu.
Akaanza kuuangalia mwendo wake, kusikiliza vizuri sauti yake na vitu vingine. Mpaka kuweka uamuzi wa kufanya hivyo, tayari Cynthia alivishtukia hivyo hata sauti alibadilisha, mwendo wake ulibadilika kabisa na hata tabia alizokuwa akizionyesha mahali hapo, tabia za msichana asiyetulia zikampumbaza.
“Mmh! Nitakuwa nimemfananisha, Cynthia hana machepele haya, kwanza Cynthia yupo Madagaska” alijisemea Joshua.
Muda ulizidi kwenda, Cynthia hakuzungumza tena na Joshua, hivyo akamwambia kwamba angekuwa chumbani kwake hivyo asingeweza kutoka.
Ilipofika saa kumi jioni, Cynthia akaaga na kuondoka zake huku akiahidi kwamba angerudi usiku. Safari yake ilikuwa ni kwenda katika duka la vifaa vya umeme na kununua plaizi kwa kuona kwamba ingekuwa na kazi kubwa sana hapo baadaye.
Hakuishia hiyo, akanunua na glovu na vifaa vyote ambavyo hutumika na matanesco wanapokata umeme kwenye nguzo kisha kuondoka zake. Siku hiyo ndiyo ilikuwa ya kufanya mauaji aliyokuwa ameambiwa na ilikuwa ni lazima aue kama alivyoambiwa na baba yake kwamba ili mama yake aendelee kuishi kwa amani basi hakuna budi watu hao kufa.
Ilipofika saa tatu usiku, simu ya bwana Kambani ikaanza kuingia katika simu yake, aliliangalia jina lakini hakutaka kuipokea, aliiacha ikiendelea kuita mpaka kukata. Siku hiyo hakutaka kuzungumza na mwanaume huyo, alitaka kumuua usiku wa siku hiyohiyo hivyo kuzungumza naye lingekuwa kosa kubwa.
Hakulala, ilipofika saa saba na nusu, akatoka katika chumba cha gesti alichopanga na begi mgongoni na kuondoka zake, hata dada wa mapokezi alimshangaa, kwani alikuwa mwanamke, kwa nini aliondoka hapo gesti pasipo kuwa na hofu yoyote ile na wakati ilikuwa usiku.
Alipofika barabarani, akachukua bodaboda na kuondoka zake kuelekea alipokuwa akiishi bwana Kambani. Kutokana na kutokuwa na magari mengi, hawakuchukua muda mrefuwakafika katika mtaa alipokuwa akiishi bwana Kambani, nyumba mbili kabla ya kuifikia nyumba hiyo, Cynthia akahitaji kushuka, akashuka na kumlipa dereva kiasi cha fedha alichokitaka na yeye kuondoka.
Alitembea kwa kujifichaficha sana, mtaa mzima ulikuwa kimya, hakukuwa na mtu aliyekuwa akizurura hapa na pale, ni sauti za mbwa tu ndizo zilizokuwa zikisikika. Alitembea mpaka alipofika katika nyumba ya bwana Kambani na kuifuata nguzo iliyokuwa ikiingiza umeme ndani.
“Ni lazima nipande nikazime umeme,” alisema Cynthia.
Hicho ndicho alichokifikiria, hakutaka kupoteza muda, alichokifanya ni kupanda nguzo ile kwa lengo la kukata umeme na kupitia kwa kuruka ukuta kwani nyaya za umeme zilizokuwa juu ya ukuta uliozunguka nyumba ile, zilikuwa na umeme.
Mpaka anafika juu ya nguzo huku akiwa na glavu mikononi mwake na mavazi maalumu, hakukuwa na mtu yeyote aliyemuona. Hakuwa na tatizo katika suala zima la umeme, alifahamu waya upi uliokuwa ukipeleka umeme ndani ya nyumba, alifahamu kila kitu, kazi ikawa ni kuukata tu.
“Taap...” aliukata waya huo, hapohapo umeme ukakatika.
Hakutaka kuchelewa kule juu, alichokifanya ni kuteremka na harakaharaka kuuparamia ukuta. Nyaya za juu ya ukuta hazikuwa na umeme, alizishika na kuzikata kwa kutumia plaizi aliyokuwa nayo kisha kurukia ndani.
Alisikia vishindo vya mtu, akajificha kwa kuamini kwamba huyo alikuwa mlinzi. Alipoona vishindo hivyo vimepotea, akaanza kuufuata mlango wa kuingilia jikoni na kutekenya kitasa.
“Safi sana...” alisema Cynthia mara baada ya kukuta mlango ukiwa wazi.
Akaingia ndani na moja kwa moja kuelekea koridoni, hakukuwa na mtu aliyeamka, na muda wote aliokuwa akipiga hatua kuufuata mlnago wa kuingia chumbani kwa bwana Kambani, alikuwa makini mno.
Alipoufikia mlango, akakishika kitasa, haukuwa umefungwa hivyo kuingia ndani moja kwa moja. Mzee huyo alikuwa amelala, alichokifanya ni kuchukua kisu chake kilichokuwa kiunoni, hakutaka kumuamsha, hivyohivyo akiwa amelala, akamfuata na kumchoma kisu mara sita kifuani mwake.
“Aagghh...” alisikika akilalamika bwana Kambani.
Shuka alilokuwa amejifunika, likatapakaa damu, Hakutaka kuacha hivyohivyo, alichokifanya ni kuufumbua mdomo wa bwana Kambani kisha kuukata ulimi na kuuweka mfukoni, kilichofuata ni kutaka kuondoka mahali hapo.
“Ngoja niwachanganye polisi na mabilionea wenzake...” alisema na hapohapo kuchovya kidole chake katika kifua cha bwana Kambani ambacho kilitobolewa kwa kisu kisha kuandika ukutani maneno yaliyosomeka ‘Mwaka 231 KK’, kisha akaondoka zake huku akiwa amefanikiwa kumuua mtu wa kwanza.
*****
Taarifa zilisambaa kila kona ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwamba mtu aliyekuwa tajiri mkubwa nchini Tanzania, bwana Edson Kambani alikuwa ameuawa ndani ya nyumba yake iliyokuwa maeneo ya Mikocheni B jijini Dar es Salaam.
Kila aliyezisikia taarifa zile, alishtuka, hawakuziamini kwani miongoni mwa watu waliokuwa wakipendwa sana nchini Tanzania alikuwa mmojawapo. Utajiri wake mkubwa uliwafanya watu wengi kumuheshimu, wengi walimlilia shida, hakuwaacha, aliwasaidia kila pale alipoweza kufanya hivyo.
Leo hii, yuleyule mzee aliyeheshimika sana, aliyeonekana kuwa msafi kama malaika, zilisikika tetesi kuwa alikutwa akiwa ameuawa ndani ya nyumba yake huku ulimi ukiwa umekatwa.
Kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo taarifa zile zilivyozidi kuzagaa kila kona, kila mtu aliyezisikia, hakuamini kama zilikuwa kweli, wengi walihisi kwamba ulikuwa uzushi kwani kwa maisha aliyokuwa akiishi mzee huyo, hakukuwa na mtu aliyeamini kama alikuwa na maadui.
“Eti mzee Kambani ameuawa....ni kweli?” aliuliza jamaa mmoja.
“Acha masihara...ameuawa au amekufa?” aliuliza jamaa huyo.
“Ameuawa. Kuna mtu aliingia nyumbani kwake na kumuua!” alijibu mwanaume huyo.
“Mmh! Sidhani kama ni kweli! Ninachojua mzee huyo hakuwa na maadui, kama kufa, sawa, kila mtu atakufa, ila kuuawa, si kweli, hakuwa na maadui yule” alisema mwanaume huyo.
Hakukuwa na mtu aliyekubaliana na taarifa zilizokuwa zikizidi kusambaa kwa kasi kama moto wa kifuu. Watu kutoka sehemu mbalimbali wakawapigia simu ndugu na jamaa zao na kuwauliza juu ya zile tetesi zilizokuwa zikisikika, walitaka kufahamu kama zilikuwa kweli au uzushi, kila aliyeulizwa, hakuwa na jibu.
“Unasemaje?”
“Nasikia ameuawa usiku huu!”
“Hivi nyie Wabongo vipi? Yule muimbaji wa Kundi la Makoma mlisema amekufa, yule muigizaji wa kule Thailand mlisema amekufa, yaani kila mtu mnamuua nyie tu, leo, mnamuua mpaka Mtanzania mwenzenu, nyie kweli nuksi” alisikika jamaa mmoja akizungumza na rafiki yake kwenye simu mara baada ya kuulizwa kuhusu kifo cha bwana Kambani.
“Sasa si nimeuliza bob!”
“Ndiyo! Ila nyie mnaua sana,” alisema jamaa huyo na kukata simu.
Kazi kubwa ya watu ikawa ni kuwasiliana kwa njia ya simu tu. Kila mmoja alitaka kufahamu kile kilichokuwa kimetokea, kama kweli mwanaume huyo bilionea alikuwa ameuawa kama ilivyosikika au zilikuwa tetesi tu.
Hakukuwa na aliyepata ukweli, hata polisi ambao walipigiwa simu na mfanyakazi wa ndani nyumbani kwa bwana Kambani, walipoambiwa kwamba bwana Kambani alikuwa ameuawa, walishtuka, hawakuamini, waliuliza mara mbilimbili kama ilikuwa kweli, wakaambiwa ni kweli na hivyo kuanza kwenda huko.
Garini, polisi hao walikuwa wakiulizana, ilikuwaje mzee huyo auawe na wakati alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakipendwa mno? Ilikuwaje mzee huyo auawe na wakati alikuwa miongoni mwa watu walioheshima, yeye alikuwa namba moja, tena aliheshimika zaidi ya rais? Kila aliyejaribu kujishawishi kwamba mzee huyo alikuwa ameuawa, alishindwa kuamini hilo.
“Ila kuna ukweli jamani?” aliuliza polisi mmoja.
“Kwani nani alipiga simu?”
“Mfanyakazi wa ndani.”
“Akasemaje?”
“Kwamba bwana Kambani ameuawa.”
“Haiwezekani, huwezi kumuua mtu mwenye moyo safi kama mzee Kambani, hizo zitakuwa tetesi tu, si unajua Wabongo tunavyopenda kuua watu kwa mdomo,” alisema polisi mmoja na kuwafanya wenzake kukubaliana naye kwamba hizo zilikuwa tetesi za uongo tu.
Taarifa hizo hazikutulia, ziliendelea kuvuma kila kona, watu walizidi kuambia kwamba bwana Kambani alikutwa akiwa ameuawa nyumbani kwake jambo lililowafanya watu ambao walikuwa na ndugu zao polisi kuwapigia simu kwa ajili ya kusikia ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea, huko, wakapewa taarifa kwamba hata nao walisikia hivyohivyo ila polisi wa Kituo cha Polisi cha Osterbay walikwenda nyumbani kwake Osterbay kuhakikisha.
“Kwa hiyo hamna uhakika?”
“Sijajua, ila kuna polisi wamekwenda nyumbani, kwake, chochote kitakachojiri, nitakutaarifu, ila kuuawa, sidhani,” alisema polisi huyo.
Mara baada ya polisi hao kufika nyumbani kwake, wakateremka na kuanza kulifuata geti la kuingilia ndani ya eneo la jumba kubwa la kifahari. Mlinzi ambaye hakuonekana kufahamu chochote kile akaufungua mlango na kushangaa.
“Kuna nini afande?” aliuliza mlinzi huyo huku akionekana kushangaa.
“Mzee yupo?” “Ndiyo! Yupo chumbani kwake amelala!”
Polisi wale hawakutaka kuzungumza kitu chochote zaidi ya kuingia. Wakaufuata mlango wa kuingilia sebuleni ambapo wakawakuta wafanyakazi wa ndani wakiwa mahali hapo huku wakilia. Wakawauliza juu ya ile simu waliyokuwa wamepigiwa.
“Ni kweli!” alisema mfanyakazi mmoja.
“Chumba chake kipo wapi?”
“Ghorofani!”
Polisi wale wakaanza kuondoka na wafanyakazi hao kuelekea chumbani kwa mzee huyo, walipofika, kitu cha kwanza walichokutana nacho mlangoni ni damu zilizokuwa zikitoka ndani, wakaufungua mlango na kuingia ndani ambapo kulikuwa na mwanga hafifu, mbele ya macho yao kulikuwepo mwili wa bwana Kambani uliokuwa umechomwa kisu shingoni.
Kile walichokuwa wameambiwa, ndicho walichokutana nacho, hazikuwa tetesi kama nao walivyohisi bali ndicho ambacho walikutana nacho ndani ya chumba kile.
Polisi wale wakaufuata mwili ule kitandani, hakukutakiwa kuguswa kitu chochote kile, kwa sababu kulikuwa na mwanga hafifu, wakawasha taa ili kuona vizuri.
Ulikuwa mwili wa bwana Kambani, damu zilizokuwa zikitoka shingoni mwake zilionekana kuanza kukauka. Polisi walibaki wakiuangalia mwili ule huku damu zile zikimsisimua kila mtu aliyeziangalia.
“Mmh!” aliguna polisi mmoja.
“Nini?” “Angalia yale maneno ukutani,” alisema polisi huyo na wote kutupa macho ukutani.
‘Mwaka 231 KK’ yalikuwa maneno yaliyosomeka vizuri ukutani hapo yakiwa yameandikwa kwa kutumia damu iliyoyafanya kusomeka vizuri kabisa.
Kila mmoja akashangaa, walishtuka, hawakuelewa maneno hayo yalimaanisha nini, walijaribu kuvisumbua vichwa vyao ili wapate jibu juu ya maneno yale au kupata picha yoyote ile lakini hawakuelewa kitu chochote kile.
“Hii ni nini? Maneno haya yanamaanisha nini?” aliuliza polisi mmoja.
“Mmh! Mwaka 231 Kabla ya Kristo! Ndiyo nini hii?’ aliuliza polisi mmoja lakini alikosa jibu.
Walichokifanya ni kuwapigia simu polisi wengine wa kitengo cha upelelezi na kufika nyumbani hapo ambapo wakapiga picha na kuchukua vitu vyote walivyotaka kuwa navyo na kisha kuwapigia simu waandishi wa habari ambao walifika hapo na kufanya vile walivyotaka kufanya, walipomaliza, wakaondoka zao huku wafanyakazi na mlinzi wakichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi.
*****
Asubuhi ilipofika, magazeti mengi yakawa yameripoti tukio lile lililokuwa limetokea usiku uliopita ambapo bwana Kambani aliuawa kikatili chumbani kwake huku maneno yaliyoomeka ‘Mwaka 231 KK’ yakiwa yameandikwa ukutani.
Kila mtu aliyezisikia taarifa zile hakuamini, walishtuka, walihuzunika mioyoni mwao kwani mtu huyo aliyekuwa ameuawa alikuwa miongoni mwa watu wenye pesa ambao walikuwa radhi kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuwafanya watu wengine wapate vichache walivyokuwa wakivihitaji.
Ingawa taarifa zilitolewa magazetini lakini bado kulikuwa na watu wengi ambao hawakuamini kile kilichoendelea kwamba mtu aliyependwa kutokana na kuwasaidia watu, leo hii alikuwa ameuawa chumbani kwake.
Watu hao wakaelekea nyumbani kwake, walitaka kuhakikisha kile walichoambiwa kwamba mzee huyo alikuwa ameuawa kweli au zilikuwa stori za mitaani tu.
Walipofika huko, kile walichokiona kwenye magazeti na sehemu nyingine hasahasa kwenye mitandao ya kijamii ndicho walichokutana nacho nyumbani huko. Idadi kubwa ya watu ilifika nyumbani hapo, katika kila kona sauti za watu wakilia zilikuwa zikisikika.
Kila mmoja aliumia, walitamani mzee huyo afufuke na arudi katika uhai kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma ila sala zao hazikuweza kujibiwa, walitakiwa kukubaliana na ukweli kwamba bilionea huyo aliuawa chumbani kwake.
“Siamini...” alisema jamaa mmoja.
“Hata mimi siamini, ni wiki moja nyuma alisema angeanzisha siku maalumu kwa ajili ya kufurahia maisha na watu wenye ulemavu, leo hii, hata kabla dhamira yake hiyo haijatimia, watu wamemuua,” alisema jamaa mmoja aliyevalia fulana yenye maneno makubwa yaliyoandikwa ‘Jesus 100%’.
Kadiri muda ulivyozidi kusogea ndivyo watu walivyoendelea kuongezeka nyumbani hapo. Kila mtu aliyekusanyika mahali hapo, alionekana kuwa na majonzi, kifo cha bwana Kambani hakukuwa na mtu aliyekitegemea kabisa, wengi walihisi kwamba kulikuwa na mchezo nyuma ya pazia na taarifa hizo hazikuwa na ukweli wowote ule.
Wakati hayo yakiendelea nyumbani kwake, wafanyakazi wake wa ndani na mlinzi walikuwa katika kituo cha polisi huku wakiwa watuhumiwa namba moja katika kifo cha bwana Kambani.
Muda wote wafanyakazi hao walikuwa wakilia, hawakumini kile kilichotokea, hawakujua kama kulikuwa na mtu aliyeingia ndani ya nyumba hiyo ambaye hawakumuona. Kifo cha mzee huyo kiliwashangaza sana.
Baada ya kukaa sero kwa zaidi ya saa saba, mwanaume mmoja aliyekuwa na mwili wenye misuli mikubwa akaingia humo ndani na kumuita mfanyakazi mmoja na kumwambia kwamba alitakiwa kumfuata.
Kwa haraka sana mfanyakazi mmoja akasimama na kuanza kumfuata mwanaume huyo mpaka kwenye chumba kimoja ambapo huko kulikuwa na wanaume wengine wawili waliovalia nguo za kipolisi, wakamwambia akae kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza kubwa.
“Unaitwa nani?” aliuliza polisi huyo.
“Amina Rajabu!”
“Ulikuwa ukifanya nini katika nyumba ya bwana Kambani?”
“Mimi ni mfanyakazi wake wa ndani!”
“Sawasawa! Kwa nini uliamua kushiriki kumuua marehemu?”
“Sikumuua marehemu...sikumuua mzee Kam...” alisema Amina, hata kabla hajamalizia sentensi yake akaanza kulia.
Polisi wale wakaanza kumtaka anyamaze kwani bado walikuwa na maswali mengi waliyotaka kumuuliza. Amina alilia kwa kilio cha kwikwi na kunyamaza kisha maswali kuendelea.
Kila alichoulizwa mahali hapo ilikuwa kama mahakamani, aliulizwa maswali yenye mitego ambayo yalionyesha kwamba kama yeye naye alihusika katika mauaji ya bwana Kambani. Walichukua dakika ishirini kumhoji, walipomaliza wakamtaka kurudi sero kisha kuitwa msichana mwingine wa kazi, huyo aliitwa Rehema. Kama ilivyokuwa kwa mwenzake, hata naye aliulizwa maswali magumu na yenye mitego.
Muda wote macho ya msichana huyo yalikusanya machozi, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu mno.
“Kwa nini ulishiriki kumuua bwana Kambani?”
“Sikushiriki afande.” “Kumbe nani alishiriki?”
“Sijui! Mimi nilimwandalia maji kwa ajili ya kwenda kuoga!”
“Ikawaje?”
“Wakati nachemsha maji, umeme ukakatika! Sikujali kwa kuwa nilidhani kwamba jenereta lingejiwasha, hivyo nikasubiri,” alisema Rehema.
“Ikawaje?” “Halikuwaka kwa wakati mpaka baada ya dakika kumi ndipo jenereta liliwaka,” alijibu Rehema.
“Na siku nyingine umeme unapokatika, huchukua muda gani mpaka jenereta kuwaka?”
“Ni ndani ya sekunde mbili mpaka tatu.” “Sasa kwa nini jana halikuwaka kwa wakati?”
“Sijui chochote kwani hicho ni kitengo cha mlinzi,” alijibu Rehema.
“Asante! Tunashukuru!”
Rehema akachukuliwa na kurudishwa sero. Kule, akaungana na Amina na kuendelea kulia kama kawaida. Hawakunyamaza, mioyo yao iliwauma mno, hawakuamini kama mwisho wa siku maisha yao yangekuwa humo sero.
Polisi yule alipotoka hapo akaelekea katika sero ya wanaume na kumchukua mlinzi kisha kumpeleka katika chumba kilekile kwa ajili ya maswali kadhaa. Aliponmfikisha mule, akamuweka katika kiti kilichokuwa mbele ya meza na kuanza kumuhoji.
“Nini maana ya ‘Mwaka 2134 KK’?” aliuliza polisi.
“Ndiyo nini hiyo afande?”
“Hujui hiyo ni nini?”
“Sijui afande! Sijui kabisa.”
“Sawa! Kwa nini jenereta halikuwaka kwa wakati umeme ulipokatika?” aliuliza polisi yule.
“Hata mimi nilishangaa! Haikuwa kawaida. Nilipoona limekaa kwa sekunde thelathini bila kuwaka, hapo ndipo nilipokwenda kutazama tatizo lilikuwa nini,” alisema mlinzi huyo aliyeitwa Suedi.
“Tupe majibu tatizo lilikuwa nini!”
“Nilibaini kwamba kitufe cha kuifanya jenereta iwake kilikuwa kimetolewa,” alijibu Sued.
“Nani aliitoa?’
“Sijui ni nani!”
“Hujui na wakati wewe ndiye mlinzi?”
Post a Comment