NILIUA KUMLINDA MAMA YANGU - 10

Hiyo ndiyo ilikuwa njia yake ya kupata fedha. Kila Jumapili, kwake ilikuwa ni siku ya muujiza, watu waliambiana, wakaenda mpaka kanisani humo na kuona miujiza ya bandia iliyokuwa ikifanyika.
Watu walimwamini, walimpongeza pasipo kujua kile kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia. Siku zikakatika na ndipo alipokutana na bwana Kambani ambaye alimwambia dhahiri kile alichotaka kufanya naye.
“Mimi nisafirishe madawa?” aliuliza mchungaji Yekonia huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo! Ni biashara nzuri na amini kwamba utafanikiwa.”
“Hapana! Ninamuabudu Mungu aliye hai, siwezi kufanya hivyo,” alijitetea.
“Mchungaji, jua kwamba unazungumza na mtu anayefahamu kila kitu, tangu lini ukawa na upako wa Kimungu? Umeanza lini? Au unahisi sijui madili unayopiga? Sikiliza, Mungu amekuacha, fanya ninachokwambia,” alisema bwana Kambani.
Mchungaji Yekonia alishtuka, hakuamini kusikia kile alichoambiwa, kila siku katika maisha yake alilifanya jambo hilo kuwa siri kubwa lakini kitu cha ajabu ni kwamba mbali na yeye na wale waliokuwa wakihusika, kulikuwa na watu wengine waliojua.
Kwake, ilikuwa aibu kubwa, swali kubwa lililokuwa kwake ni kwamba kama bwana Kambani alifahamu kila kitu, vipi kuhusu watu wengine? Kila alichojiuliza, akakosa jibu.
“Kwa hiyo?”
“Unataka kuniambia nini?”
“Tushirikiane!”
“Na nini?”
“Usafirishaji wa madawa ya kulevya,” alijibu bwana Kambani.
Mchungaji Yekonia akanyamaza, akabaki akimwangalia bwana Kambani, alimfahamu vizuri kwamba alikuwa bilionea mkubwa aliyejijengea heshima kubwa katika jamii, kitendo cha kumwambia kwamba alitaka kushirikiana naye katika kusafirisha madawa ya kulevya.
“Kwa nini mimi?”
“Wewe ni mtumishi wa Mungu, mizigo yenu huwa haichunguzwi bandarini na hata kuilipia kodi hamfanyi hivyo, naomba tushirikiane, kuna fungu kubwa sana kwa ajili yako,” alisema bwana Kambani.
“Nitakuamini vipi?”
“Tunza maneno yangu.”
Ilikuwa ni biashara kubwa na yenye fedha hivyo lingekuwa jambo la kitoto sana kuacha dili kubwa ama hilo limpite, hakutaka kubisha, hakutaka kukataa kwani aliamini kwamba angeingiza kiasi kikubwa cha fedha.
Hakutaka kujifanya sana mtumishi wa Mungu kwani mbali na kuwa na kanisa, nyuma ya pazia kulikuwa na dili la uponyaji wa uongo aliokuwa akiufanya, alichoona kuwa sahihi ni kukubaliana na bwana Kambani kwa ajili ya kutengeneza pesa.
“Hakuna noma.”
“Sawa.”
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki wao, biashara ikachangamka, madawa yakaendelea kuingizwa nchini kupitia mizigo ya kanisa kutoka sehemu mbalimbali. Bandarini, hawakuichunguza wala kuitoza kodi kwani ilionekana kama misaada ya kijamii.
Mchungaji Yekonia alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka miwili ndipo alipopata dili jingine ambalo aliamini kwamba lingemuingizia fedha. Alichokifikiria ni kuwasafirisha wasichana kwenda nje ya nchi, anawapa kiasi kikubwa cha fedha lakini kule Ulaya au China wanakwenda kwa kazi moja ya kujiuza tu huku pasipoti zao zikiwa zimechukuliwa.
Hiyo ilikuwa siri kubwa iliyoendelea kwa kipindi kirefu, hakukuwa mtu aliyekuwa akifahamu dhambi hiyo kubwa iliyokuwa ikiendelea kwa mchungaji huyo. Siku zikakatika, ili kuwafanya Watanzania waone kwamba alikuwa miongoni mwa watu wazuri, naye akaanza kutoa misaada.
Miujiza ya uongo iliyokuwa ikifanyika kanisani kwake, ikawafanya watu kumwamini kwa asilimia mia moja. Bwana Kambani na mabilionea wenzake hawakutaka kumuacha, waliendelea kuwa naye kwani alikuwa moja ya mlango salama wa kuingiza madawa ya kulevya nchini Tanzania.
*****
Bwana Kambani alichanganyikiwa, penzi la Cynthia lilimchanganya kiasi kwamba hata familia yake iliyokwenda Mbeya akaisahau. Huku nyuma, hakutaka kusikia la mtu yeyote yule, moyo wake ulitekwa katika penzi la msichana huyo mdogo ambaye kwa kumwangalia tu ilikuwa ni rahisi kusema kwamba alikuwa mtu hatari kitandani.
Kesho yake, akampigia simu Cynthia na kuomba kuonana naye nyumbani kwake kwani kulikuwa na sehemu alitaka kwenda naye, Cynthia hakukataa, alikubaliana naye na hatimaye kwenda nyumbani kwa bwana Kambani.
Mpaka kipindi hicho, bado mipango yake iliendelea kama kawaida, alikuwa na kazi kubwa mbele yake ya kuhakikisha kwamba anafanikiwa kumuua mzee huyo bila usumbufu wowote ule.
Alipofika nyumbani hapo, akamchukua na kuondoka naye, lengo la bwana Kambani lilikuwa ni kumpeleka Cynthia kwa marafiki zake wa dhati kwa ajili ya kuwatambia tu.
Walipofika huko na kutambulishwa, ilikuwa rahisi kwa msichana huyo kugundua kwamba watu waliokuwa mbele yake nao walikuwa kwenye ratiba kubwa ya kuwaua kama alivyokuwa ameagizwa isipokuwa mchungaji Yekonia ambaye hakuambiwa chochote kile kuhusu yeye.
“Huyu ni bilionea Nkone, na huyu ni bilionea Marimba, mwanzoni alikuwa mpokea rushwa mashuhuri katika mahakama moja hapa Tanzania,” alisema bwana Kambani kwa sauti ya utani na wote kuanza kucheka.
“Na huyu ni nani?” aliuliza Cynthia huku akiwa kwenye tabasamu pana.
“Huyu anaitwa mchungaji, pasta mwenye upako, mwenye kukemea mapepo, anaitwa mchungaji Yekonia, ukiwa na tatizo lolote hasa ugonjwa, mfuate na atakuombea, Mungu wake ana nguvu sana,” alisema bwana Kambani na wote kuanza kucheka tena.
“Ni shemeji huyu?” aliuliza Marimba.
“Ndiyo! Mtoto mbichi sana nimemtoa mbali, mwangalie alivyoumbika, angalia kiuno chake, huyu ndiye Cleopatra wangu,” alisema bwana Kambani huku akimshikashika Cynthia kiuno, japokuwa hakupenda, akaona bora atulie kwani alikuwa na kazi kuba mbele yake.
Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kula maisha, bwana Kambani alionekana kuwa na furaha zaidi na kila wakati alikuwa pembeni ya Cynthia akimshika huku na kule kama mtu aliyekuwa na lengo la kumpandisha mzuka ili alale naye.
Bwana Nkone hakuyatuliza macho yake, kila wakati alikuwa akimwangalia Cynthia kwa matamanio makubwa. Ni kweli aliwahi kukutana na wanawake wengi, wenye mvuto, ambao walikuwa na uzuri wa ajabu lakini macho yake yalipotua kwa Cynthia, akashindwa kuvumilia, alimuona kuwa na uzuri kama malaika.
Kila wakati alikuwa akimkonyeza kisiri na kwa sababu hata yeye alikuwa kwenye ratiba ya kuuawa, Cynthia akarudisha mkonyezo kitu kilichompa uhakika bwana Nkone kwamba piga ua ilikuwa ni lazima amchukue Cynthia kisiri.
“Tuondoke mpenzi!” alisema bwana Kambani, ilikuwa saa tisa alfajiri.
“Twende wapi?”
“Nyumbani kwangu.”
“Mkeo je?”
“Si nilikwambia kwamba yupo Mbeya na wale nguchiro wake, wala usijali,” alisema bwana Kambani.
“Sawa.”
Wakati wanaondoka, bwana Nkone alikuwa bize kumwangalia Cynthia kiasi kwamba alishindwa kuvumilia, akasimama na kumshika mkono msichana huyo na kumuaga. Bwana Kambani hakuhisi kitu chochote kile, kwake, marafiki hao walikuwa ni watu wa karibu sana kwake na kuamini kwamba wasingeweza kufanya kitu chochote hasa kwa wanawake aliokuwa akiwatambulisha kwao.
Wakaondoka. Garini, bwana Kambani alibaki akizungumza na Cynthia kwa maneno ya mahaba ambayo aliamini kwamba piga ua ilikuwa ni lazima watakapofika wafanye mapenzi kama alivyokuwa akitamani.
Gari lilipofika, wakateremka na kuanza kuelekea ndani. Bwana Kambani alimshika Cynthia vilivyo, mkono wake ulikuwa ukibinya kiuno chake. Walielekea chumbani ambapo mzee huyo akamlaza Cynthia kitandani.
“Nadhani leo ndiyo siku yenyewe....” alisema bwana Kambani huku akionekana kuwa na furaha ya ajabu.
“Leo?”
“Ndiyo!”
“Kwa leo hapana mpenzi...labda kesho!”
“Kesho tena? Kwa nini?” aliuliza bwana Kambani huku akionekana kuhamaki. Alichokifanya Cynthia ni kumsogelea bwana Kambani, akashusha kidogo suruali yake ya jinzi mpaka mapajani na kubaki na nguo ya ndani tu, kisha akamwambia aangalie.
“Sijakuelewa unamaanisha nini!”
“Leo ndiyo namaliza.”
“Unamaliza nini?”
“Jamani baby huoni?”
Bwana Kambani akaangalia vizuri, kile alichokiona ndiyo akakielewa kwamba siku hiyo haikuwa sahihi kufanya mapenzi na Cynthia kwani alikuwa katika kipindi hatari, hivyo alitakiwa kusubiri.
“Daah! Inaisha lini?”
“Nafikiri kesho! Usiku nitakuja, sasa hapo nitakuachia mwili wangu wote...” alisema Cynthia.
“Sawa. Nitashukuru sana.”
Alichokifanya bwana Kambani ni kulala tu huku mkono wake ukiwa kifuani mwa Cynthia ambaye kichwa chake kilifikiria jinsi ya kukamilisha mauaji ya huyo mzee, kwani piga ua ilikuwa ni lazima aue kama alivyoambiwa na baba yake.
Asubuhi ilipofika, bwana Kambani akatoka kitandani na kisha kuelekea bafuni kuoga. Alimwamini sana Cynthia kiasi kwamba hata alipomaliza kujiandaa, alimwaga na kuondoka zake huku mezani akimwachia kiasi cha hilingi milioni moja kwa ajili ya matumizi yake ya siku hiyo kabla ya usiku kuonana na kufanya mapenzi.
Alipohakikisha kwamba bwana Kambani ameondoka, Cynthia akainuka na kuchungulia dirishani, kitu cha kwanza kabia kilikuwa ni kuyazoea mazingira ya nyumba hiyo kwani ilikuwa ni lazima usiku wa siku hiyo amuue bwana Kambani.
Akatoka chumbani na kuelekea nje. Alitaka kuonana na mlinzi, kuzungumza naye kwani kulikuwa na kitu kikubwa alichotaka kukifanya. Kwa sababu mlinzi alikuwa akimfahamu kutokana na siku mbili mfululizo kutambulishwa kwamba huyo alikuwa shemeji yake, akamchangamkia sana.
“Za asubuhi shemeji...” alisalimia mlinzi.
“Salama. Hivi unaitwa nani vile?”
“Naitwa Salmin.”
“Sawasawa. Hivi huyu mzee siyo mtu wa vimwana kwa sana?” aliuliza Cynthia japokuwa alijua kwamba bwana Kambani alikuwa mtu wa wanawake.
“Huyu?”
“Ndiyo!”
“Hapana! Si mtu wa vimwana.”
“Unanidanganya Salmin...”
“Kweli tena.”
“Sikiliza, mimi kujua ukweli haimaanishi kwamba nitamwambia,” alisema Cynthia.
“Hilo swali wala siwezi kujibu labda umuulize kijana wake.”
“Kijana gani?”
Salmin akaanza kumwambia kwamba kulikuwa na kijana ambaye ndiye alikuwa rafiki mkubwa wa bwana Kambani ambaye ndiye aliyekuwa akifahamu mambo mengi kuhusu mzee huyo.
Hakutaka kumwambia kwamba kijana huyo ndiye aliyekuwa akimsaidia kusafirisha madawa ya kulevya nchi za mbali, alimfichaficha huku akimwambia mambo mengi kwamba kijana huyo ndiye aliyekuwa akijua mengi kuhusu huyo mzee.
“Yupo wapi?”
“Anaishi Manzese, ila si muda mrefu anaweza kuja.”
“Sawa. Akija nishtue, ngoja niendelee kuyazoea mazingira ya nyumba hii.”
“Haina noma.”
Cynthia akaondoka getini kwa mlinzi na kuanza kuzunguka huku na kule, mlinzi hakutaka kujali sana, aliuona uzuri wa Cynthia lakini hakutaka kuonekana kwamba ana tamaa kwani endapo angefanya hivyo na Cynthia kumwambia mpenzi wake basi ingekuwa balaa.
Hakutaka kumfuatilia hata kule alipokwenda. Cynthia alitembea kwa kujiamini mpaka alipofika katika kijumba kidogo kilichokuwa na jenereta, alichokifanya ni kukishika kitufe cha kuwashia jenereta na kisha kukiharibu, hakuridhika, kwa kuwa jenereta lilikuwa kwenye kijumba chake, akachukua kipande cha nondo na kisha kuukwangua ukuta, mchanga uliotoka, akauchukua kisha kuutumbukiza katika sehemu ya mafuta kisha kuondoka.
Huo ndiyo ulikuwa mpango wake, alitaka kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa yaani kwani kwa kuanza kufanya umafia, angeanzia na kukata umeme, hivyo kama asingefanikisha kuriharibu jenereta basi wakati anazima umeme, jenereta lingejiwasha.
Alipohakikisha kila kitu kipo sawa, akarudi chumbani kwake. Baada ya kukaa huko kwa saa moja, akasikia mlango ukigongwa na mtu aliyeugonga alikuwa mfanyakazi wa ndani, Amina.
“Samahani wifi.”
“Bila samahani.”
“Kaka Salmin aliniambia kaka Joshua akija nikushtue...”
“Mimi?”
“Ndiyo! Sasa kaka amefika yupo sebuleni...”
“Sawa. Mwambie nakuja.”
INAENDELEA...
Post a Comment