NILIUA KUMLINDA MAMA YANGU- 09

Cynthia hakumkumbuka Kambani, mara ya mwisho kumuona alikuwa mdogo sana. Akaingia ndani ya kasino hiyo, alivalia sketi fupi iliyoyaacha mapaja yake wazi kwa asilimia kubwa, ukiachana na hiyo, kwa juu alikuwa na nguo fulani iliyoonyesha mpaka ndani kabisa na kukifanya kifua chake kilichosimama kuonekana dhahiri.
“Wewe ni mgeni maeneo haya?” alisikika mwanaume mmoja akimuuliza Cynthia.
“Kwa nini unauliza hivyo?”
“Nakuona tu, kama mgeni sema nikupe kampani.”
“Utaweza?”
“Kwa nini nisiweze? Unanichukuliaje?”
“Hahaha! Aya! Karibu.”
Huyo alikuwa mwanaume wa kwanza kumuona Cynthia akiingia kwenye kasino hiyo, alishindwa kuvumilia, kumuacha msichana mrembo kama huyo kilikuwa kitu kisichowezekana, alijua kwamba endapo angeingia ndani ni lazima wanaume wangemuwahi kwani kwa jinsi alivyokuwa mrembo, wanaume rijali wasingeweza kujizuia.
Ndani, macho yake hayakutulia sehemu moja, alikuwa akiangalia huku na kule kama mtu aliyekuwa akimtafuta mtu fulani. Aliangalia kwenye kila meza, hakuridhika, aliendelea kuangalia zaidi na zaidi.
“Vipi tena? Kuna mtu unamtafuta?” aliuliza mwanaume yule.
“Ndiyo!”
“Nani?”
“Bwana wangu!” alijibu Cynthia.
“Bwana wako? Mbona nimekuona umekuja peke yako mrembo! Au ndo unataka kunibania?” aliuliza mwanaume huyo huku udenda ukiwa umemtoka.
“Hapana! Sijakubania bali nakwambia ukweli.”
“Bwana wako nani?”
“Kambani!”
“Daah! Ndiye bwana wako! Pole yako binti!”
“Kwa nini?”
Mwanaume yule hakusema kitu, aliposikia kwamba Cynthia alikuwa akimtafuta mwanaume huyo, alimpa pole kisha kuondoka zake.
Cynthia hakutaka kujali sana, alijua kwamba mwanaume huyo aliamua kumpa pole kwa kuwa alikuwa amemuulizia mwanaume aliyekuwa na wanawake wengi, hivyo hakutaka kujali sana.
Mkononi hakuwa na picha, lakini kitendo cha kumuona mzee huyo kwenye intaneti ilimpa uhakika kwamba asingeweza kumpoteza hata kidogo. Aliendelea kusubiri ndani ya kasino hiyo ambapo baada ya saa moja akaanza kusikia watu wakipiga makofi.
Hakujua ni nini kilikuwa kikiendelea, alichokifanya ni kuangalia kule mlangoni ambapo watu wengi mahali hapo walikuwa wakiangalia huku wakiendelea kupiga makofi na ndipo macho yake yakatua kwa mtu ambaye alikuwa na uhakika kwamba alikuwa bwana Kambani.
Akasogea karibu ili aweze kumuona vizuri kwani kule alipokuwa amesimama alikuwa mbali. Aliposogea na kumwangalia vizuri akagundua kwamba alikuwa bwana Kambani.
“Ndiye mwenyewe,” alijisemea Cynthia.
Kwa mbwembwe nyingi bwana Kambani akaanza kupiga hatua kuelekea mahali ambapo mara kwa mara alipendelea kukaa, katika sehemu zote alizokuwa akipita, watu walimpigapiga mgongoni kama kumkaribisha.
Alikuwa na fedha, maarufu ambaye kila alipoingia ndani ya kasino hiyo, alimwaga fedha na kucheza sana kamari. Utaalamu wake katika mchezo huyo uliwapa sana watu fedha kwa kumpigia chepuo katika kamari za nje.
“Karibu sana,” alisema mmoja wa wahudumu katika mchezo wa kamari wa karata, Pokker.
Alikaa kwenye kiti chake anachokaa kila siku, akawepa dau la milioni mbili kisha karata kuchangwa na kuanza kucheza na Wazungu waliokuja kasino kwa ajili ya kucheza kamari.
Moto wake ulikuwa mkubwa, akawala sana Wazungu. Cynthia alikuwa pembeni, macho yake yalikuwa kwa mzee huyo aliyeonekana kuwa bize kucheza kamari. Kadiri alivyomwangalia ndivyo alivyopata hasira zaidi, alikumbuka mbali sana wakati mzee huyo alipokuwa akimtesa mama yake na hata kuwatuma watu kwenda kumteka kwa lengo la kumuua.
Ilipofika saa kumi alfajiri, bwana Kambani akainuka, akapongezwa na kuondoka mahali hapo. Huo ulikuwa mwanzo tu, siku iliyofuatia, kama kawaida Cynthia alikuwa ndani ya kasino hiyohiyo kwa ajili ya kumsubiria mzee huyo, tajiri na mwenye umaarufu mkubwa.
****
“Mambo vipi mrembo....”
“Safi tu...”
“Unaitwa nani?”
“Cynthia....”
“Okey! Nimeagizwa na mzee nikuite...”
“Mzee yupi?”
“Yule pale...”
Cynthia alikuwa akizungumza na kijana mmoja, kama kawaida yake alivalia sketi fupi iliyoyafanya mapaja yake yaliyojaajaa kuonekana vilivyo. Mbele yake alisimama kijana ambaye kwa maneno yake alisema kwamba alikuwa ameagizwa na mzee ambaye baada ya kunyooshewa kidole, akagundua kwamba mzee huyo alikuwa bwana Kambani.
Kitu cha kwanza alichokifanya ni kujiweka katika muonekano wa kusikia aibu, hakuutaka kujiweka wazi, hakutaka kuonekana kawaida, alichokuwa akikihitaji ni kujifanya kuwa mgeni wa mambo ya mapenzi.
Hakutaka kugoma, alipoonyeshewa bwana Kambani, akasimama na kuanza kumfuata huku akiongozana na kijana yule. Walipomfikia, mzee huyo akatoa tabasamu pana na kumkaribisha kitini.
“Karibu mrembo...” alimkaribisha, akakaa.
Kitu cha kwanza alichokifanya mzee huyo ni kuagiza vinywaji, pombe kali. Cynthia hakuwa mlevi hivyo akamwambia mzee huyo kwamba asingeweza kunywa pombe yoyote ile bali kinywaji pekee ambacho angeweza kunywa ni soda au juisi.
“Hunywi bia?” aliuliza mzee Kambani huku akionekana kushtuka.
“Sinywi...huwa sijazoea kunywa bia..”
“Mbona unakosa burudani sana, yaani mrembo kama wewe usinywe bia, jamani, sasa hivyo viwanda vinatengeneza bia za kazi gani kama warembo kama nyie hamtaki kunywa?” aliuliza bwana Kambani.
Mzee Kambani alichanganyikiwa, kila alipokuwa akimwangalia Cynthia, msichana huyo alionekana kuwa mrembo mno, alipagawa na kujikuta akitetwa jasho huku mapigo yake ya moyo yakidunda katika kasi ambayo hakuwahi kuipata.
Siku hiyo walizungumza mengi, bwana Kambani hakutaka kumuacha Cynthia, alichokifanya ni kumwambia waondoke wote kwenda nyumbani kwake kwani mkewe hakuwepo.
Kama ingekuwa kwenye hali ya kawaida, Cynthia asingekubali lakini kwa sababu mzee huyo alikuwa kwenye mipango yake, akakubali kuondoka naye kwa kujifanya kuwa msichana mwepesi kabisa kama wengine ambao mara kwa mara walikuwa kasino.
Wakaondoka huku mzee huyo akionekana kuwa na furaha mno. Nyuma ya gari walipokuwepo, ilikuwa ni kuonyeshana mahaba ya njiwa, mara washikane hapa na pale, mara wabusiane na kufanya mambo mengine ambayo hayaandikiki.
“Subiri kwanza...” alisema Cynthia kwa sauti ya mahaba.
“Kuna nini baby wangu?” aliuliza bwana Kambani.
“Subiri tufike...”
“Nyumbani mbali sana...kwa nini tusianze hapahapa kwanza?” aliuliza mzee Kambani.
“Hapana! Subiri tufike...”
Mzee huyo hakuwa na la kusema, kwa kuwa aliambiwa kwanza wasubiri wafike, wala hakutaka kuwa na wasiwasi. Walichukua dakika kadhaa ndipo gari likawasili nyumbani na hivyo kuteremka na kuingia ndani.
Bwana Kambani alikuwa kwenye mhemko mkubwa, mwili wake ulichachamaa na kitu pekee alichokihitaji kwa wakati huo ni kufanya mapenzi na Cynthia tu. Hakumfahamu msichana huyo, kipindi alichoondoka kwake, alikuwa binti mdogo mno, kila alipomwangalia, hakuwa na kumbukumbu yoyote kama aliwahi kumuona binti huyo mahali popote pale.
Alipomfikisha chumbani, akamlaza kitandani, akamwangalia kwa macho yaliyojaa matamanio, kitu alichokuwa akikifikiria kwa wakati huo ni ngono tu. Cynthia hakusema kitu, alibaki akimwangalia huyo mzee.
Kitu kilichomjia kichwani ni kumuua mzee huyo. Alipolifikiria hilo, akaona kwamba huo usingekuwa wakati muafaka wa kufanya hivyo kwani kipindi ambacho aliingia ndani, mlinzi alimuona hivyo lingemuweka matatani.
“Vua nguo basi, au nikusaidie?” aliuliza bwana Kambani kwa sauti ya kilevi kwa mbali iliyoonyesha tamaa ya kufanya mapenzi.
“Unataka kufanya nini?” aliuliza Cynthia.
“Niingie katikati...”
“Hapana!”
“Kwa nini mpenzi? Mbona unataka kunitesa?” aliuliza bwana Kambani.
“Yaani siku ya kwanza tu! Jamani mpenzi, naogopa utaniona malaya na wakati mimi nimekuja kwako kwa lengo la kukaa nawe kipindi kirefu,” alisema Cynthia.
“Jamaniiiii...”
“Ndiyo! Nikikupa leo, utanichukulia mimi malaya, yaani mwanamke anayejiuza kwa lengo la kutafuta pesa,” alisema Cynthia.
Maneno hayo yakamuingia bwana Kambani, hakutegemea kama kuna siku angekutana na mwanamke mwenye akili kama alivyokuwa Cynthia. Mzuka wa kufanya ngono ukamtoka, mtu aliyekuwa mbele yake, alionekana kujitambua mno.
Akanywea, kilichofuata ni kulala mpaka asubuhi, tena bila kufanya chochote kile, akaagana naye, akampa milioni moja na kuomba kuonana naye usiku wa siku hiyo ili amtambulishe kwa marafiki zake, Cynthia akakubaliana naye, akamwambia hakuna noma, wangekutana.
*****
“Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu, Amen,” ilisikika sauti ya mchungaji mmoja katika Kanisa la Praise And Worship lililokuwa jijini Dar es Salaam.
Ndani ya kanisa hilo kulikuwa na washirika zaidi ya mia moja ambao wote walifika asubuhi na mapema kwa ajili ya kusali ibada ya asubuhi. Mchungaji huyo, Christopher Yekonia aliendelea kuwaombea baraka watu wote waliokuwa ndani ya kanisa lile kiasi kwamba watu wengi waliokuwa wagonjwa wakahisi kupokea uponyaji.
Japokuwa kulikuwa na idadi kubwa ya wachungaji waliokuwa wakifungua makanisa kwa lengo la kupata fedha lakini kwa mchungaji Yekonia ilikuwa tofauti kabisa, hakuangalia fedha, kwake, kitu alichokijali ni kuona watu wakimwabudu Mungu wa kweli na kuyabadilisha maisha yao.
Maisha yaliendelea, aliingiza kiasi kikubwa cha fedha, akawa tajiri mkubwa kiasi kwamba akawa mchungaji maarufu nchini Tanzania pasipo kujua kwamba nyuma ya pazia, mchungaji huyo alikuwa mtu wa tofauti kabisa.
Ilikuwa ngumu kuamini kwamba mambo mengi aliyokuwa akiyafanya yalikuwa maigizo, watu wazima waliojifanya viwete walikwenda kanisani kwake, tena kwa kulipwa kiasi kikubwa cha fedha na yeye kujifanya kuwaombea na kupona.
Hiyo ndiyo ilikuwa njia yake ya kupata fedha. Kila Jumapili, kwake ilikuwa ni siku ya muujiza, watu waliambiana, wakaenda mpaka kanisani humo na kuona miujiza ya bandia iliyokuwa ikifanyika.
Watu walimwamini, walimpongeza pasipo kujua kile kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia. Siku zikakatika na ndipo alipokutana na bwana Kambani ambaye alimwambia dhahiri kile alichotaka kufanya naye.
ITAENDELEA ...
Post a Comment