NILIUA KUMLINDA MAMA YANGU- 08

“Una uhakika sijakwambia ninapokwenda?”
“Ndiyo! Hukuniambia.”
“Mmh! Aya! Mimi nakwenda Mexico.”
“Kuna nini huko?”
“Mambo yangu binafsi tu, wewe unakwenda Cuba kufanya nini?”
“Kusoma.”
“Vizuri sana.”
Safari iliendelea, ndege ilipofika Uholanzi, wakatakiwa kuteremka na kusubiri ndege nyingine tayari kwa kwenda nchini Canada, Cuba, Mexico na Brazil.
Kwa kuwa abiria wote walipewa saa mbili kusubiri, wakachukua muda huo kutoka nje ya jengo la uwanja huo na kuanza kuzungukazunguka katika sehemu mbalimbali za Jiji la Amsterdam, ila si mbali kutoka katika uwanja huo.
Huko, walishikana mikono kama wapendanao, kila mmoja alionekana kuwa na furaha huku kichwa cha kila mmoja kikifikiria mapenzi tu.
“Nimefurahia kampani yako,” alisema Joshua.
“Hata mimi pia, nadhani tutaendelea kuwasiliana baada ya hapa.
“Ndiyo! Hilo usijali, ila unajua kwamba kutoka hapa Uholanzi tunachukua ndege tofauti?” aliuliza Joshua.
“Kivipi?”
“Ni mara yako ya kwanza kwenda Cuba?”
“Ndiyo!”
“Utaratibu upo hivi, kuna ndege nyingi zinakuja na kufanya safari ya kuelekea Marekani Kusini na Kaskazini. Watu wanakwenda Washington na Ottario watachukua ndege moja ila kwa sisi wa Mexico na nchi nyingine za Amerika Kusini na Kati tutaingia kwenye ndege tofauti,” alisema Joshua maneno yaliyoonekana kuwa kama somo kwa Cynthia.
“Kumbe ipo hivyo?”
“Ndiyo!”
Moyo wa Cynthia ukanyong’onyea, hakuamini kile alichokisikia kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa wao wawili kuwa pamoja. Alitokea kumzoea mwanaume huyo, hakutaka kabisa kutengana naye, alitamani aendelee kuwa naye zaidi na zaidi.
Hakuwa na jinsi, alitakiwa kukubaliana na ukweli kwamba huo ulikuwa muda wa kutengana, hivyo wakabadilishana mawasiliano na saa mbili baadaye kila mmoja alikuwa ndani ya ndege yake kuelekea alipokuwa akielekea.
Baada ya saa kumi, ndege ikaanza kushuka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jose Marti uliokuwa katika Jiji la Havana. Cynthia akabaki akiliangalia jiji hilo kwa juu, lilikuwa jiji kubwa lililojengwa kwa majengo makubwa ambayo yaliushangaza sana moyo wake.
Baada ya ndege kusimama, abiria wote wakaanza kuteremka. Cynthia na wenzake wakapitia katika njia zote walizotakiwa kupita na alipotoka nje, akakutana na wasichana wawili waliokuwa wameshika karatasi kubwa lililokuwa na jina lake. Akawafuata.
Kilichoendelea ni kwenda ndani ya gari iliyoandikwa St. George University na safari ya kuelekea huko chuoni kuanza. Njiani, Cynthia hakutaka kuzungumza neno lolote, alikuwa kimya huku akiangalia mazingira la jiji zuri la Havana.
Safari hiyo ilichukua dakika ishirini, gari likaanza kuingia ndani ya geti moja ambalo ndani yake kulikuwa na jengo kubwa. Hicho ndicho kilikuwa chuo cha St. George lakini ndani yake kulikuwa na wanajeshi wengi, na hata walinzi wa getini na sehemu nyingine walikuwa wanajeshi.
Cynthia alitulia, mlango ulipofunguliwa, wakaelekea katika chumba ambacho aliambiwa huko angekutana na wahusika, hivyo alitakiwa kusubiri kitini.
Baada ya kukamilisha kila kitu, akachukuliwa na kupelekwa katika chumba alichotakiwa kuanza maisha, humo ndani kulikuwa na vitanda viwili ambapo baadaye msichana mmoja ambaye kwa kumwangalia ingekuwa rahisi kugundua kwamba alikuwa na miaka thelathini akaingia na kusalimiana.
“Naitwa Emmaculatha.”
“Mimi naitwa Cynthia.”
“Karibu sana. Nipo mwaka wa pili chuoni hapa,” alisema Emmaculatha.
Huyo ndiye akawa mwenyeji wake, alianza kumpeleka huku na kule na kumuonyesha mazingira ya chuo hicho huku akimweleza mengi kuhusu wanachuo waliokuwepo chuoni hapo. Baada ya siku mbili masomo yakaanza rasmi.
****
Kambani na wenzake waliendelea na maisha yao, kila siku ilikuwa ni lazima kumzungumzia Anita ambaye bado alionekana kuwa tishio katika maisha yake hapo baadaye.
Alijaribu kutuma watu kwenda kumuua mwanamke huyo lakini hawakufanikiwa. Alichanganyikiwa mno hasa baada ya watu kujitokeza na kuanza kumsaidia mwanamke huyo.
Hakujua watu hao walikuwa wakina nani na kwa nini waliamua kumsaidia mwanamke huyo. Hilo, lilikiumiza kichwa chake mpaka siku ambayo naye aliwekwa chini ya ulinzi wa watu hao na kuwaomba wasimumuue na mwanaume mmoja kumwambia kwamba mtu aliyetakiwa kumuua alikuwa binti wa Anita.
Hakuelewa watu hao wana maana gani, alipuuzia japokuwa kwa kipindi kirefu kichwa chake kiliendelea kujiuliza juu ya watu wale ambao alikuwa na uhakika kwamba hawakuwa Watanzania.
Aliwaambia mabilionea wenzake kuhusu watyu hao, wote wakashangaa, hata wao walikuwa kama yeye kwamba hawakuwafahamu watu hao na wala hawakujua walikuwa chini ya nani.
Kambani hakutaka kukubali, kumuua Anita ilikuwa ni njia mojawapo ya kumfanya kuishi kwa amani, alichokifanya ni kuendelea kumtafuta ikiwezekana kumuua yeye na mtoto wake ambaye aliambiwa kwamba ndiye ambaye angekuja kumuua hapo baadaye.
Watu aliowatuma kwa ajili ya kumtafuta Anita na mtoto wake walirudi mikono mitupu. Walihangaika katika kila kona lakini hawakufanikiwa kabisa kuwaona watu hao.
Kambani alichanganyikiwa, kwa kutumia utajiri wake mkubwa, alijitahidi lakini mwisho wa siku vijana hao walirudi mbele yake na kumwambia kwamba walitafuta na kutafuta lakini hawakuambulia chochote mpaka pale alipoamua kumuoa mwanamke aliyeitwa kwa jina la Edith.
Siku zikakatika, miezi ikaenda mbele na miaka kukatika. Kwa kipindi cha miaka yote kumi aliyojitahidi kumtafuta Anita na binti yake hakuwa amefanikiwa kabisa, hivyo aliamua kupuuzia na akili yake kumwambia kwamba mwanamke huyo alikuwa amekufa.
“Ni kipindi kirefu sana, atakuwa amekufa tu,” alijisemea.
Jina lake liliendelea kuwa kubwa nchini Tanzania, alikuwa bilionea mkubwa ambaye kila siku alionekana kuogelea katika bwawa la fedha. Hakuacha kuwasaidia masikini kwa kuficha biashara haramu ya madawa ya kulevya aliyokuwa akifanya na wenzake.
Kila siku vijana ambao waliambiwa kwamba wao ndiyo taifa la kesho walikuwa wakiathiriwa na madawa hao kiasi kwamba kila kona ya nchi ya Tanzania, watu walikuwa wakilalamika tu.
Serikali ilipewa malalamiko yote lakini kitu cha siri kabisa ambacho watu wengi hawakukifahamu ni kwamba watu waliokuwa wakihusika na uingizaji wa madaya ya kulevya nchini Tanzania ndiyo ambao kila siku watu waliwapa sifa kwamba waliwasaidia masikini na kuwatukuza.
Ndani ya kipindi chote ambacho aliamua kumtapeli Anita mali zake, tayari Kambani alikuwa na utajiri wa shilingi trilioni tatu, kiasi kikubwa kabisa cha fedha ambacho kilimfanya kuishi maisha yoyote aliyokuwa akiyataka.
“Tufanye Anita amekwishakufa...kuna anayebisha?” aliuliza Kambani huku glasi ya mvinyo ikiwa mkononi mwake, alikuwa akiwaambia mabilionea wenzake.
“Kwa hiyo leo tunasherehekea kifo chake, si ndiyo?” aliuliza bwana Nkone.
“Ndiyo! SI chake peke yake bali hadi mtoto wake,” alisema Kambani na kuwafanya wote wagongesheane glasi kama ishara ya furaha waliyokuwa nayo mioyoni mwao.
*****
“Halo Cynthia...”
“Halo Joshua.”
“Unaendeleaje?”
“Naendelea salama tu! Wewe?”
“Nipo poa kabisa. Nilitaka kukwambia kwamba nakuja,” ilisikika sauti ya Joshua.
“Wapi? Cuba?”
“Ndiyo! Nimekumisi sana, naomba nije nikusalimie,” alisema Joshua.
“Usijali! Karibu sana. Nitafurahi kukuona,” alisema Cynthia.
Ilipita miezi sita pasipo wawili hao kuonana zaidi ya kuendelea kuwasiliana kwenye simu tu. Kwa Cynthia, maisha yalikuwa ni mateso makubwa, aliujua moyo wake, kwa kipindi hicho aliuhisi ukiwa kwenye hali ya tofauti kwa Joshua.
Kila siku alimfikiria, alilikumbuka tabasamu lake, mguso wake na kila kitu alichokuwa akikifanya pamoja naye. Alitamani sana kumuona na kitendo cha kumwambia kwamba alikuwa akielekea nchini Cuba kwa ajili ya kumuoana tu, kwake ilikuwa faraja kubwa.
Akajikuta akipata nguvu upya, hakutaka kumuona Joshua akija na kuondoka pasipo kumwambia ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake, alimpenda, alitamani sana kuona akiwa mpenzi wake, hivyo akamsubiri kwa hamu.
Baada ya wiki moja, Joshua akafika nchini Cuba, akampokea, wakaelekea hotelini na kukaa kitandani. Hiyo ilikuwa ni mara yake ya kwanza Cynthia kukaa chumba kimoja na mwanaume, kila alipomwangalia Joshua, mapigo ya moyo wake yalimdunda kwa nguvu, hakuamini kwamba hatimaye baada ya kipindi kirefu angekuwa na mwanaume huyo chumbani.
Alimpenda sana lakini hakujua ni kwa namna gani angeweza kumwambia ukweli, alibaki kimya kwa muda huku akimwangalia tu. Jicho lake tu lilionyesha ni jinsi gani alimtamani sana mwanaume huyo mwilini mwake.
“Cynthia....” aliita Joshua.
“Abeee....”
“Mbona hauzungumzi kitu mwenyeji wangu?”
“Kwani si hata mgeni anatakiwa kuzungumzia kitu?”
“Mmmh! Aya!”
Alichokifanya Joshua ni kumsogelea Cynthia pale alipokaa na kuhakikisha kwamba uso wake unakuwa karibu na mwili wa msichana huyo. Kwa kumwangalia tu, ilikuwa rafhisi sana kuona jinsi Cynthia alivyokuwa akikitetemeka.
Mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa kasi, alikuwa kama mtu aliyekuwa akiogopa kitu fulani. Joshua hakutaka kuishia hapo, alichokifanya ni kuupitisha mkono wake wa kulia begani mwa Cynthia na kumvutia kwake.
“U msichana mzuri sana Cynthia...” alisema Joshua huku hata sauti yake ikiwa imebadilika.’
“Mmh!”
“Niamini! Nimekutana na wasichana wengi sana, ila wewe umekuwa wa tofauti sana, u mcheshi, unajitambua na msichana mwenye msimamo wa aina yake, hakika unastahili kuwa mke wangu,” alisema Joshua kwa sauti ndogo iliyomchanganya Cynthia.
“Mmmh!”
Hakuwa na cha kuongea, alibaki akiguna tu. Moyo wake ulikuwa ulikuwa kwenye hali mbaya, siku hiyo ambayo Joshua aliamua kumwambia ukweli kwamba alikuwa akimpenda, hata naye pia alipanga kumwambia hivyohivyo kama tu asingemwambia.
Hakutaka kuonekana kuwa msichana mwepesi, japokuwa naye moyo wake ulipagawa kwa Joshua lakini kwenye suala hilo la mapenzi alitaka kuonyesha msimamo japokuwa naye moyo wake ulipagawa kwa Joshua lakini kwenye suala hilo la mapenzi alitaka kuonyesha msimamo wake.
“Joshua, hapana, siwezi kuwa na mpenzi kwa sasa,” alisema Cynthia.
“Kwa nini? Haunipendi? Unahisi mimi si mwanaume sahihi kwako?” aliuliza Joshua huku akionekana kuchanganyikiwa, alichokisikia, hakukiamini.
“Simaanishi hivyo!”
“Kumbe unamaanisha nini?”
“Nahitaji kuwa peke yangu!”
“Mpaka lini?”
Kila swali alilouliza Joshua lilikuwa gumu kwa Cynthia na mbaya zaidi lilijaa mitego mingi. Alibaki akimwangalia kijana huyo na mwisho wa siku kumwambia kwamba wangewasiliana, hivyo hakutaka kuwa na presha yoyote ile.
Joshua hakutaka kubaki nchini Cuba kwa kipindi kirefu, alichokifanya ni kuondoka kurudi nchini Tanzania huku akiahidiwa kwamba angepewa jibu la uhitaji wake siku za usoni.
Hawakuacha kuwasiliana, kila siku ilikuwa ni lazima kuzungumza kwenye simu, kutumiana jumbe mbalimbali za mapenzi. Siku ziliendelea kukatika mpaka kufika kipindi ambacho Cynthia alibakiza miezi sita kabla ya kumaliza masomo yake na ndipo aliposafiri kuelekea nchini Tanzania.
Uwanja wa ndege alipokelewa na Joshua, mwanaume mtaratibu hata kwa kumwangalia, akachukuliwa na kupelekwa mahali alipokuwa akiishi mwanaume huyo huko Manzese.
Walipofika huko, Cynthia hakuamini kile alichokiona, Joshua alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiishi katika nyumba ya gharama sana ambayo kwa kifupi ingeweza kukaliwa na mtu aliyekuwa na fedha nyingi.
Cynthia akabaki akiliangalia jumba lile, kila alipojiuliza kama hapo ndipo mahali alipokuwa akiishi mpenzi wake au la, alikosa jibu la moja kwa moja. Akakaribishwa na kuingia ndani, bado aliendelea kulishangaa jumba hilo ambalo ndani lilionekana kuwa na kila kitu.
Katika sehemu ya maegesho ya magari, kulikuwa na magari tofautitofauti, tena ya bei mbaya ambayo kwa hesabu ya harakaharaka, kila gari moja liligharimu zaidi ya shilingi milioni mia moja kwenda juu.
Kushangaa kwake kukabaki moyoni mwake, hakutaka kuuliza chochote kile, akakaribishwa mpaka sebuleni ambapo huko napo kulionesha ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alikuwa na fedha.
“Joshua...hapa ndipo unapoishi?” aliuliza Cynthia huku akionekana kushangaa.
“Ndiyo mpenzi! Kupo vipi kwani?”
“Pazuri, nimepapenda,” alijibu Cynthia.
Wakakaa kochini na kutulia, macho ya Cynthia yalikuwa yakitembea sebuleni hapo kisiri. Walizungumza mambo mengi pamoja na namna watakavyoweza kuyaboresha mapenzi yao mpaka siku watakapofunga ndoa.
“Nikuulize kitu?” aliuliza Cynthia.
“Uliza tu.”
“Unafanya biashara gani?”
“Haha! Nimejua tu! Ninauza magari kutoka Japan na kuyaleta hapa Bongo,” alisema Joshua.
Siku hiyo walizungumza mambo mengi, Cynthia hakutaka kwenda kulala hotelini, alichokifanya ni kulala kitanda kimoja na Joshua ndani ya nyumba hiyo.
Asubuhi ilipofika, wakatoka wote na kwenda kutembea, huko, Joshua aliendelea kumsisitizia Cynthia kwamba uhusiano wao wa kimapenzi usingeishia hapo bali ungeendelea mpaka pale watakapoona.
Maneno hayo yalimfurahisha sana Cynthia kwani naye hicho ndicho kitu alichokihitaji sana kwa wakati huo. Alikaa Tanzania kwa siku tatu, baada ya hapo akaondoka na kuelekea Madagaska kwa ajili ya likizo kisha kurudi nchini Cuba kuendelea na masomo.
*****
Bwana Phillip alisubiri kwa kipindi kirefu, kitu alichokitaka ni kuona bwana Kambani na kampani yake wote wakiuawa na hivyo kuzirudisha mali zote mikononi mwake na mtu pekee ambaye alikuwa akimtegemea katika kufanya mauaji hayo alikuwa binti yake, Cynthia.
Kitendo cha kumuona msichana huyo nyumbani kwake, kilimpa faraja kubwa kwani hata jinsi alivyokuwa akimwangalia, alivyojengeka kimwili aliamini kwamba Cynthia angeweza kufanya kile alichotakiwa kufanya.
Alimpongeza kwa masomo yake pia hakutaka akae sana nyumbani, alichokifanya ni kumpa nafasi ya kujifunza zaidi mambo ya kijeshi katika kambi moja hapo Antananarivo nchini Madagaska.
Cythia alifanya mazoezi ya nguvu, alijipa mazoezi ya kupambana na watu hata watatu, alikuwa mzuri katika kutumia bunduki na alipewa mazoezi yote ya shabaha.
Mbali na hiyo, pia alikuwa mtaalamu wa kutengeneza sumu mbalimbali kwa kutumia vitu tofautitofauti na kuweka kwenye chakula au kinywaji. Uwezo wake mkubwa ndiyo uliomfanya kila mwanachuo kumhuheshimu nchini Cuba alivyokuwa chuoni.
Alikaa Cuba kwa mwezi mmoja na nusu na ndipo aliporudi nchini Cuba kuendelea na masomo. Kwa jinsi sura yake ilivyokuwa nzuri, ilikuwa ngumu sana kugundua kwamba binti huyo mrembo alikuwa mwanajeshi mwenye nguvu ambaye alikuwa akiandaliwa kuwa usalama wa taifa nchini Madagaska.
“Ukifanikiwa, kazi itaanza,” alisema baba yake.
“Hakuna tatizo. Ulisema wapo wangapi vile?”
“Watatu!”
“Nitawajuaje? Yaani sehemu wanapoishi?”
“Ni watu maarufu sana, tena wanashughulika na uuzaji wa madawa ya kulevya Afrika ila serikali haiwafanyi chochote,” alisema bwana Phillip.
“Sawa, nitahakikisha nafanikiwa kwa kila kitu.”
Baada ya miezi sita kumaliza masomo yake na ndipo akarudi nchini Tanzania, kazi kubwa iliyokuwa mbele yake ni kuwaua watu ambao aliamini kwamba ndiyo ambao walitaka kumuua mama yake na tena inawezekana mpaka kipindi hicho bado walikuwa wakimtafuta ili wamuue.
Hakutaka kumwambia Joshua kwamba alikuwa nchini Tanzania, ilikuwa siri yake kwani alijua kwamba endapo angemwambia mwanaume huyo kwamba alikuwa nchini Tanzania basi inawezekana angemfanya kutokukamilisha kile anachotaka kukifanya.
Akachukua chumba katika hoteli ya Vila Park iliyokuwa Magomeni jijini Dar, humo hotelini ndipo alipokuwa akiwafuatilia watu hao kupitia kwa wahudumu ambao alihakikisha anawazoea huku kwa kuwadanganya kwamba alikuwa Mtanzania aliyeishi nchini Marekani sasa alikuwa amerudi nyumbani.
“Unamfahamu bwana Kambani?” alimuuliza mhudumu mmoja ambaye alizoeana naye sana tu.
“Kuna mtu asiyemfahamu Kambani? Tanzania nzima inamfahamu, miongoni mwa watu wazuri sana Tanzania, ana utajiri mkubwa ambao kila siku anatamani atumie na watu wengine,” alijibu mhudumu huyo huku akimmwagia sifa kemkem.
“Mmmh!”
“Kwani wewe humjui?”
“Hapana! Simjui. Na vipi kuhusu Marimba na Nkone?”
“Hahah! Mbona unawataja sana?”
“Ni kwa sababu nina kazi nao, nataka kujua nani anajua kuhonga,” alisema Cynthia.
“Anayejua kuhonga wala sijui, ila ukienda kwa Kambani, ni rahisi kumtega, anapenda sana vitoto,” alisema mhudumu.
“Na hajaoa?”
“Ameoa, ila ameachana na mkewe ambaye aliondoka na watoto wake, yupo alone tu, unamtaka?” aliuliza mhudumu.
“Kama inawezekana! Nimetoka Uganda baada ya kusikia kuhusu wao, na mimi nataka kuwa tajiri shoga yangu,” alisema Cynthia maneno yaliyomfanya kuaminika kwa asilimia mia moja.
Kuanzia siku hiyo hata mavazi yake yakabadilika, akawa mtu wa kutoka hotelini hapo usiku na kwenda klabu. Hakuwa akipenda kwenda huko ila kutokana na kazi kubwa iliyokuwa mbele yake, hakuwa na jinsi.
Alivyokuwa akijiweka, wahudumu wote wakajua kwamba mwanamke huyo alikuwa changudoa tu. Uzuri wake uliwadatisha wahudumu wengine huku yule mhudumu aliyeongea naye aitwaye Asha akijitahidi kujiweka katribu na Cynthia ili aweze kumshawishi zaidi achukue wanaume na mwisho wa siku wagawane fedha atakazozipata.
“Ukifanikiwa usinisahau basi,” alisema Asha.
“Usijali, ila ulisema anapendelea kwenda wapi vile?”
“White Pearl Cassino,” alijibu Asha.
White Pearl Cassino ilikuwa kasino kubwa iliyokuwa maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam. Watu wengi wenye fedha zao walipenda kwenda huko kwa kuwa ndani yake kulikuwa na matajiri wakubwa ambao kazi yao kubwa kwenda ndani ya kasino hiyo ilikuwa ni kucheza kamari tu.
Kasino hiyo ikawa maarufu, watu wengi wenye fedha zao na hata wale ambao walijulikana kwa kiasi fulani nchini Tanzania ndiyo kilikuwa kiwanja chao cha kujidai.
Mbali na starehe zilizokuwa ndani ya kasino hiyo maarufu, kilichowavutia watu wengi zaidi ni wanawake warembo waliokuwa wakifika ndani ya kasino hiyo kila siku.
Hakukuwa na wanawake wa Kiafrika tu, kulikuwa na Wachina, Wazungu, Wahindi ambao wengi wao kazi yao kubwa ilikuwa ni kujiuza tu. Machangudoa waliokuwa ndani ya kasino hiyo walikuwa wazuri na wa kimataifa ambao hawakulipwa kwa fedha za Kitanzania, wote walilipwa kwa dola na paundi.
Bwana Kambani ambaye mara kwa mara alikuwa akifika ndani ya klabu hiyo alipendelea kwenda na kampani yake ya watu wawili, vijana ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kutumwa na bwana Kambani kumuitia wanawake aliokuwa akiwaona na kuwapenda.
Alipofika humo, kazi yake kubwa ilikuwa ni kuitawala michezo ya kamari na mara nyingine kucheza kwa salio kubwa lililowashangaza watu wengine, kitu cha ajabu, kwenye kila kamari aliyokuwa akicheza kuanzia Pokker, Slots mpaka Roulette, bwana Kambani alionekana kuwa na kismati kwani kote huko alikuwa akila.
Aliweka rekodi ya kuwa miongoni mwa watu waliofanikiwa kula fedha nyingi sana katika kamari, watu walimfagilia na hata siku ambazo alikuwa akienda huko, watu waliokuwa wakiwekeana dau, wengi walimuwekea kwamba angeshinda kwenye kila mchezo.
Cynthia hakumkumbuka Kambani, mara ya mwisho kumuona alikuwa mdogo sana. Akaingia ndani ya kasino hiyo, alivalia sketi fupi iliyoyaacha mapaja yake wazi kwa asilimia kubwa, ukiachana na hiyo, kwa juu alikuwa na nguo fulani iliyoonyesha mpaka ndani kabisa na kukifanya kifua chake kilichosimama kuonekana dhahiri.
“Wewe ni mgeni maeneo haya?” alisikika mwanaume mmoja akimuuliza Cynthia.
“Kwa nini unauliza hivyo?”
“Nakuona tu, kama mgeni sema nikupe kampani.”
“Utaweza?”
“Kwa nini nisiweze? Unanichukuliaje?”
“Hahaha! Aya! Karibu.”
ITAENDELEA
Good story!
ReplyDelete