NILIUA KUMLINDA MAMA YANGU- 07

“Sikiliza Abrah! Ni vigumu kupata utajiri ukiwa chini ya mtu. Huwezi kufanikiwa zaidi ukiwa umeajiriwa, ni lazima akili yako ichaji, ujue ni kwa namna gani unaweza kuingiza fedha. Anzisha biashara zako, usiwe na mlango mmoja wa kuingiza fedha, hakikisha unakuwa na milango hata mitatu, hapo ndipo utakapoona mafanikio yako,” alisema Phillip.
“Ebwana! Unajua wewe kuwa muokotaji wa chupa za maji siyo haki kabisa,” alisema mlinzi.
“Kwa nini?”
“Ungekuwa profesa sasa hivi! Una maneno mazito sana ambayo ni faida kwa kila mtu,” alisema mlinzi.
Kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele na ndivyo walivyoendelea kuzoeana zaidi. Usiri mkubwa ulikuwepo baina ya Phillip na Emmanuel, mwanaume huyo hakutaka kumwambia mtu yeyote kwamba Phillip alikuwa hai, kila kitu kilichokuwa kimetokea kwake kilikuwa siri nzito.
Baada ya kuzoeana kwa kipindi cha miezi sita ndipo alipoanza kumdadisi mlinzi juu ya maisha ya mkewe na Edson ndani ya nyumba hiyo. Kwa kuwa mlinzi ilifika kipindi alimwamini sana Phillip, akaamua kumwambia mengi tu.
“Mwanaume anazingua sana, kutwa kuingiza wanawake, anakula bata sana, nafikiri kwa sababu mali hakuzitafuta kwa nguvu zake,” alisema mlinzi.
“Kwani mali si zake?”
“Thubutuuuu...mali za marehemu mume wa Anita. Alikufa baharini, baada ya hapo Anita akawa na huyu mwanaume mpaka ndugu zake wakashangaa....” alisema mlinzi.
“Kwa nini washangae?”
“Ilikuwa mapema mno, ila yeye hakujali.”
“Ila kuna vijitetesi nimevisikia kwa jirani nilipokwenda kuokota chupa.”
“Vipi?”
“Kwamba huyu jamaa anataka kumtapeli mali hizi mwanamke!”
“Hizo si tetesi. Kesho wateja wanakuja kwa ajili ya kununua nyumba hii.”
“Acha masihara.”
“Sasa nikutanie ili iweje Kizota. Yaani kila ninapomwangalia shemeji, siamini, ananyanyasika sana, hana mbele wala nyuma, badala ya mapenzi sasa imekuwa ni maumivu usiku na mchana,” alisema mlinzi.
Mlinzi hakuishia hapo, aliendelea kumwaga umbeya, katika mazungumzo yake akawataja mabilionea ambao walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Phillip anapata mali hizo.
“Wakina nani?”
“Kuna mmoja alikuwa hakimu, huyu anaitwa James Marimba na mwingine mfanyabiashara anaitwa Andrew Nkone,” alisema mlinzi.
“Mmh! Kweli kazi ipo. Pole yake.”
Phillip hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka kuelekea nyumbani kwake. Njiani, hasira zilimkamata kooni, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea.
Alimkumbuka mkewe, mtoto wake ambao kwake walikuwa kila kitu, hakuamini kama Edson, yuleyule mwanaume mchafu aliyeonekana kupigwa na maisha ndiye ambaye alitaka kujimilikishia kila kitu ambacho alikitafuta kwa jasho lake.
Japokuwa utapeli ulitaka kufanyika lakini kwake halikuwa tatizo kubwa, alijua kwamba hati alizokuwa nazo mkewe hazikuwa zenyewe bali zilikuwa za kugushi ambazo kwa kuziangalia zilionekana kuwa zenyewe.
Kesho yake alipoingia, akaambiwa na mlinzi kwamba watu hao walikuwa ndani tayari kwa kukamilisha kila kitu kuhusu kuuzwa kwa nyumba hiyo. Wakati wanazungumza hayo, hawakukaa sana, Anita akafika nyumbani hapo, alionekana kuwa na haraka huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa.
Hakuzungumza kitu chochote kile, akaingia ndani. Phillip na mlinzi hawakutaka kubaki mahali pale, walisogea mpaka karibu na dirisha na kuanza kusikiliza huko ndani ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea.
Walimsikia Anita akimlalamikia Edson kwamba alitaka kuuza nyumba hiyo huku kiasi kikubwa cha fedha kikiwa kimetolewa katika akaunti yake na kuachiwa milioni tano tu.
Phillip alinyong’onyea, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, wakati mwingine alitamani kuingia ndani na kuwaambia watu hao kwamba alikuwa Phillip na hakuwa radhi kuona mali zake zikiuzwa.
“Unasikia, kimeshanuka humo ndani, nyumba inauzwa,” alisema mlinzi huku wakitegesha masikio kusikia vizuri.
*****
Alichokitaka Phillip ni kuanza kufanya upelelezi wake, alitaka kuwafahamu watu ambao walitajwa na mlinzi kwamba ndiyo waliokuwa wakishirikiana na Edson Kambani kwa ajili ya kumtapeli mke wake mali zile.
Akaanza kufanya uchunguzi, mtu wa kwanza aliyetaka kumfahamu kwa undani alikuwa James Marimba. Alikumbuka kwamba aliambiwa kuwa mtu huyo alikuwa hakimu hapo mwanzo, hivyo akataka kufuatilia alikuwa hakimu wa wapi na kwa namna gani alizipata fedha zake na kuwa bilionea mkubwa.
Alichokifanya ni kuanza kumfuatilia kupitia Google, humo, akagundua kwamba alikuwa hakimu mkazi wa mahakama moja jijini Dar es Salaam. Hakuridhika, alitaka kufuatilia zaidi, akagundua mpaka sehemu alipokuwa akiishi kwa wakati huo, katika jumba moja lililokuwa Msasani.
Ufuatiliaji wake haukuishia katika mitandao tu bali kwenda mpaka alipokuwa akiishi mzee huyo. Ilikuwa nyumba kubwa, ndani kulikuwa na mfanyakazi mmoja na pia familia yake ya mke mmoja na watoto wawili.
Aliendelea na uchunguzi wake, akagundua kwamba watoto wa mzee huyo walikuwa wakisoma St. Anne Marie iliyokuwa Kipawa na mke wake alikuwa mkurugenzi wa kampuni yao changa iitwayo Wood Forest Marimba Company iliyokuwa ikijishughulisha na usambazaji mbao baada ya kukata miti porini.
Alipomaliza kumfuatilia bwana Marimba, akaanza kumfuatilia na Andrew Nkone. Akagundua kwamba mzee huyo alikuwa tajiri mkubwa aliyevuna fedha kupitia kampuni zake mbili, moja ikiwa ni ya kutengeza mabati na nyingine juisi.
Nyumbani, alikuwa na mke mmoja na watoto wanne. Mbali na fedha zake, mke wake mzuri lakini bwana Nkone alikuwa mtu wa kutoka sana nje ya ndoa. Alikuwa na vimada viwili, wa kwanza alikuwa Upendo, msichana aliyempangia nyumba maeneo ya Magomeni na mwingine aliitwa Sikitu ambaye pia alimpangia nyumba maeneo ya Kimara Suka.
Upelekezi wake ulipokamilika, akaanza kuwa na jukumu la kuilinda familia yake kwani alijua kwamba ilikuwa ni lazima mkewe afukuzwe nyumbani na baada ya hapo kuanza kutafutwa kwa lengo la kuuawa.
Alichokuwa amekifikiria ndicho kilichotokea, baada ya siku kadhaa, Anita akafukuzwa nyumbani kwake na hivyo kuelekea kwa wazazi wake. Binti yake aliyekuwa akisoma katika shule za kitajiri, akafukuzwa na kuanza kusoma shule za uswahilini.
Aligundua kwamba huo usingekuwa mwisho, hivyo alichokifanya ni kurudi Madagaska kisha kuwatuma vijana ambao wangefuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea na baada ya miaka kadhaa ndipo alipoanza kuagiza kufanywa baadhi ya matukio ambayo yalikuwa na lengo la kuilinda familia yake.
*****
Kilichotokea, vijana hao waliotumwa nchini Tanzania waliweza kufanya majukumu yao yote, walifanikiwa kumlinda Anita na mtoto wake kwa kuwaua vijana wote waliotumwa na mabilionea wale kisha kumchukua mtoto Cynthia na kuondoka naye kuelekea Madagaska.
Katika kipindi ambacho Cynthia alifikishwa nchini humo, Phillip hakuamini, kila alipomwangalia mtoto wake, machozi yalikuwa yakimtoka tu. Kilipita kipindi kirefu hakuwa amemuona, kitendo cha kumuona kwa mara nyingine kilimpa furaha kubwa.
Cynthia hakujua kama yule ni baba yake, aliondoka nchini Tanzania akiwa mtoto mdogo kabisa, miaka miwili. Alimwangalia mtu aliyesimama mbele yake, kwa mbali alihisi kufanana naye lakini kila alipojaribu kuvuta kumbukumbu kama aliwahi kumuona sehemu fulani, hakukumbuka chochote kile.
Phillip akamchukua Cynthia, akampakiza ndani ya gari na kuanza kuondoka naye. Muda wote huo Cynthia hakuzungumza kitu, alimshangaa mtu aliyekuwa naye, alikuwa akitokwa na machozi lakini hakujua sababu haswa ilikuwa nini.
Kichwa cha Cynthia kilikuwa na maswali mengi, hakutaka kuuliza, alibaki kimya huku akimwangalia baba yake tu. Safari ile iliishia nje ya jengo moja kubwa na la kifahari, kwa jinsi alivyoliangalia jumba lile hakuamini kama na yeye angeweza kuingia humo.
Geti likajifungua na kuingia ndani. Watu zaidi ya watano waliokuwa na bunduki walikuwa wakizunguka huku na kule. Ulionekana kuwa ulinzi mkubwa kitu kilichomfanya kujiuliza juu ya mtu huyo aliyekuwa amemchukua.
Gari lilipopakiwa sehemu ya maegesho, wote wawili wakateremka na kuelekea ndani. Cynthia alionekana kuwa huru, alimwamini mtu huyo kwani watu ambao walimchukua nchini Tanzania alizungumza nao na kumwambia kwamba angekuwa salama.
“Unahitaji nini?” aliuliza Phillip huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
“Nataka chakula.”
Hapohapo Phillip akamuita mfanyakazi wa ndani na kumwambia amletee chakula, kwa haraka, chakula kikaletwa na kuanza kula, alipomalizwa, akachukuliwa na kupelekwa katika chumba kimoja kilichoonekana kuwa na mvuto mkubwa.
“Unajua mimi ni nani?” aliuliza Phillip.
“Hapana!”
“Hujawahi kuniona?”
“Hapana!”
Alichokifanya Phillip ni kusimama na kisha kuifuata kompyuta yake, akaifungua, akaunganisha na internet kisha kuingia katika akaunti yake ya Yahoo. Huko, kulikuwa na picha nyingi ambazo alizihifadhi, picha alizopiga na Cynthia kipindi cha nyuma hata kabla hajaondoka nchini Tanzania.
Akamuita Cynthia na kumuonyeshea zile picha. Cynthia aliziangalia, alipojiona, alijitambua kwamba alikuwa nani na hata alipomwangalia mwanaume alyiyepiga naye picha alimtambua kwani mara kwa mara mama yake alimuonyeshea picha zile na kumwambia kwamba alikuwa baba yake.
“Baba...” alisema Cynthia.
“Ndiyo binti yangu,” alisema Phillip huku akimwangalia Cynthia usoni.
“Mom told me you died...” (Mama aliniambia ulikufa...)
“I did’nt die, God saved me,” (Sikufa, Mungu aliniokoa) alisema Phillip.
Kilichofuata ni kukumbatiana wote wawili. Ikawa zamu ya Cynthia kulia, hakuamini kama yule aliyesimama mbele yake alikuwa baba yake. Kwa kipindi kirefu mama yake alimwambia kwamba alikufa baharini, moyo wake ulimuuma sana lakini mwisho wa siku, leo hii alikutana naye nchini Madagaska.
Kilichoendelea ni Phillip kumpa mahitaji yote muhimu binti yake. Akampeleka katika shule nzuri waliyosoma watoto wa matajiri, alitaka apate elimu bora kwa ajili ya kumsaidia baadaye.
Kila siku Phillip alikuwa na jukumu la kumpeleka shule na kumrudisha, upendo baina yao wawili ukawa mkubwa, Cynthia alijisikia amani moyoni mwake, kuwa na baba yake kulimpa furaha na kujiona kuwa mtu wa kipekee katika dunia hii.
Siku zikaendelea kukatika, uwezo wa Cynthia darasani ulikuwa mkubwa kiasi kwamba walimu walimshangaa sana kwani japokuwa aliwakuta wenzake wamekwishaanza masomo lakini aliweza kufanya vizuri kabisa.
Mwaka huo ukapita, mwaka mwingine ukaingia huku Phillip akiendelea na jukumu lake la kila siku la kumpeka shule na kumrudisha nyumbani.
“Baba!” aliita Cynthia.
“Unasemaje binti yangu.”
“Nataka kumuona mama! Atakuja lini huku?” aliuliza Cynthia.
“Atakuja tu, wala usijali.”
“Nataka nimuone mama, sina furaha mpaka nitakapowaona nyie wawili mkiishi pamoja,” alisema Cynthia.
“Usijali! Nakuahidi utamuona.”
“Kwani mmeachana?”
“Hapana!”
“Kwa nini hamtaki kuishi pamoja?”
“Bado muda haujafika binti yangu, ukifika, tutarudi na kuwa kama zamani,” alisema Phillip.
Shauku ya Cynthia kila siku ilikuwa ni kuwaona wazazi wake wakiishi kama zamaini. Hakuonekana kuwa na furaha, kitendo cha mama yake kuwa nchini Tanzania kilimuondolea amani kabisa mpaka wakati mwingine kuhisi kwamba inawezekana wawili hao walikuwa wameachana pasipo kumwambia.
Mwaka ukaisha na kuingia mwaka mwingine, shuleni bado aliendelea kuonekana mwiba kwa wanafunzi wengine. Walimu walijivunia kuwa na mwanafunzi kama yeye, mara kwa mara walimuita ofisini na kumpa zawadi kitu kilichomhamasisha kufanya vizuri kila siku.
Baada ya miaka saba, Cynthia akakamilisha masomo yake ya elimu ya sekondari na hivyo kutakiwa kujiunga na Chuo Kikuu hapo Antananarivo na kuanza kusomea masomo yake ya udaktari.
“Upo tayari kuwa daktari?” aliuliza Phillip huku akimwangalia binti yake usoni.
“Nipo tayari.”
“Sawa. Nataka nikupe zawadi.”
“Zawadi gani?” aliuliza Cynthia.
“Unauona ule mlango?” alimuonyeshea mlango wa chumbani kwake.
“Ndiyo!”
“Nenda kaufungue, zawadi yako utaikuta humo,” alimwambia binti yake.
Cynthia akawa na presha kubwa, hakujua ni zawadi gani ilikuwa mule ndani, akaanza kupiga hatua kuufuata mlango wa kuingilia chumbani kwake, alipoufikia, akakishika kitasa na kisha kukitekenya.
Alichokikuta ndani, hakuamini, mama yake alisimama mbele yake, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, pasipo kutarajia, hapohapo akamrukia na kumkumbatia mpaka wote wawili kuanguka chini.
“Nimekukumbuka mama...” alisema Cynthia huku machozi yakimtoka.
“Nimekukumbuka pia binti yangu...”
Ilikuwa furaha moyoni mwake, hakuamini kama kweli mama yake alifika nchini Madagaska, kila alipomwangalia, alitamani kuwa karibu yake kila wakati. Alimpenda mno, kilio chake cha kila siku kilikuwa ni kumwambia baba yake kwamba alitaka kuwaona wawili hao wakiishi pamoja, hatimaye leo hii maombi yake yalikubaliwa.
Ikawa familia yenye furaha, ikaungana tena na hatimaye Cynthia kutakiwa kuanza masomo yake katika chuo kimoja kilichokuwa nchini Cuba. Japokuwa alikuwa na lengo la kusoma chuo cha kawaida, akapelekwa katika chuo cha jeshi nchini humo.
“Nataka uwe na nguvu, ujue jinsi ya kutumia silaha na mambo mengine, kuna kazi kubwa itakuja mbele yako,” alisema Phillip.
“Kazi gani?”
“Kumlinda mama yako!”
“Kumlinda mama yangu? Na nini?”
“NA watu wabaya! Unawakumbuka waliokuteka kipindi kile?”
“Wale wanaume siwakumbuki.”
“Achana na wale, kuna ambao waliwatuma wale watu kuja kumuua mama yako, mmoja aliamua kumtapeli mali zote nilizomwachia,” alisema Phillip.
“Ni wakina nani hao?”
“Nitakupa majina yao, kwanza nenda chuoni kasome,” alisema Phillip.
“Sawa. Hakuna tatizo.”
Hakukuwa na cha kupoteza, kwa kuwa alikwishakamilisha kila kitu ilikuwa ni lazima kuondoka na kuelekea nchini Cuba kwa ajili ya kuanza masomo hayo ambayo yangemweka nchini humo kwa miaka mitatu.
Baada ya siku mbili, alikuwa ndani ya ndege akielekea nchini humo. Pembeni yake alikaa na mvulana mmoja, kwa kumwangalia tu, alikuwa mzuri wa sura, alimvutia lakini hakutaka kuzungumza jambo lolote lile kuhusu mapenzi.
Hakutaka kabisa kusikia kitu chochote kile kuhusu mapenzi, aliyafahamu, hakuwahi kuwa na mpenzi lakini kwa jinsi alivyokuwa akiwaona marafiki zake wakilia, wakijiua, hakuwa na hamu nayo japokuwa hakuwahi kabisa kuonja ladha yake.
Wakajikuta wakianza kupiga stori, wakachangamkiana na kuifanya safari yao kuchangamka kabisa. Ndege ilitua nchini Misri katika Jiji la Cairo, hapo, abiria wengine wakaingia na hivyo safari ya kuelekea Dubai kuanza.
Walichukua saa kadhaa, wakafika nchini humo ambapo walitakiwa kubadilisha ndege na kuchukua ndege nyingine yenye hadhi kubwa kuzunguka katika anga la Ulaya.
Katika kipindi chote hicho walikuwa wote, kila walipokwenda kupumzika, walikuwa pamoja huku wakiwa karibukaribu kama wapenzi.
“Ila sikukuuliza swali moja Joshua.”
“Swali gani?”
“Unakwenda wapi?”
“Una uhakika sijakwambia ninapokwenda?”
“Ndiyo! Hukuniambia.”
“Mmh! Aya! Mimi nakwenda Mexico.”
“Kuna nini huko?”
“Mambo yangu binafsi tu, wewe unakwenda Cuba kufanya nini?”
“Kusoma.”
“Vizuri sana.”
ITAENDELEA KESHO
Post a Comment