HATA MALINZI WA BMT NAYE NI JIBU TU, KABISA ANASTAHILI KUTUMBULIWA
Na Saleh Ally
SIKU
chache zilizopita, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nnape
Nnauye alitangaza kutengua utezi wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza
la Michezo Tanzania (BMT), Henry Lihaya.
Nnape
alieleza kutofurahishwa na utendaji wa kiongozi huyo ambaye amekaa BMT
kwa miaka saba. Maana yake hakuwa mtendaji mzuri au hakufanya vizuri
majukumu yake.
Wakati
Lihaya anaondoka, naona Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi anaendelea
kubaki na amepewa kazi ya kuteua katibu mtendaji mwingine ambaye
anaamini ni mchapakazi.
Kwanza nianze hivi, ninauunga mkono kabisa uamuzi huo wa Waziri Nape kwa kuwa sasa tunatakiwa mabadiliko makubwa katika michezo.
Tukubali
waungwana, mwendo na mwenendo katika michezo umekuwa ni wa kusuasua
sana kwa kuwa watu hawako makini na bado wana yale mawazo ya kizamani
kabisa kwamba michezo ni kitu cha ziada.
Miaka
10 nyuma, hata serikali iliamini michezo ni kitu cha kujifurahisha tu.
Hakukuwa na maana ya kukitilia maanani lakini leo utaona mambo ni
tofauti.
Hata
kama serikali ingekuwa haitaki, inalazimika kufanya hivyo. Leo
inachukua kodi kutoka michezoni, inasaidiwa upatikanaji wa ajira,
inasaidiwa katika suala la kupunguza vijana kuvuta unga na mambo mengine
ya uhalifu. Michezo inaliwakilisha taifa na wakati mwingine kulipa
sifa.
Kama
ni sekta muhimu, tukubali ikitiliwa maanani na kuongozwa kwa jicho la
wanaotaka mafanikio, nchi yetu itafaidika na kufaidisha wananchi wengi
kwa furaha na hata kipato.
![]() |
| NAPE (KUSHOTO) AKIWA NA MALINZI... |
Sasa
watu wanaotakiwa mfano kuongoza baraza la michezo kama BMT, hawapaswi
kuwa wale wanaofanya kama vile sehemu ya burudani. Mfano Mwenyekiti wa
BMT, Dionis Malinzi ambaye ni mfanyabiashara mkubwa.
Sijawahi
kuona ubunifu wake, sijawahi kuona anasimama na kusema jambo akasimamia
utakelezaji. Kama kweli Nape aliona Lihaya alilala, basi bosi wake
alilala zaidi yake.
Utaona
hadi waziri anakwenda kumuondoa Lihaya kwa kuonekana hakuwa mtendaji
sahihi lakini Malinzi hakuwahi kueleza kutoridhishwa kwake na
wanamichezo wakajua. Kama alisema labda hawezi kumng’oa, mbona
hatujawahi kusikia hata amefanya jambo lililoleta mabadiliko katika
vyama vya michezo.
Yanayofanyika
ni yaleyale ya enzi zile. Ninaamini ana kazi nyingi sana za kibiashara
na BMT huenda ni kama sehemu ya kuburudika tu kwake. Huu ndiyo wakati
mwafaka akae kando.
BMT
inatakiwa kuingia kuleta mabadiliko. Inatakiwa BMT ya wabunifu na wenye
nia ya kusaidia michezo ya Tanzania na si hii ya sasa chini yake.
Mara
kadhaa nimehoji mara nyingi kuhusiana na BMT, hata yale makato kutoka
katika mechi za soka, yanakwenda BMT kwa sababu ipi na yenyewe
inaifanyia nini michezo.
Kama
ilivyo kwa ule mfuko wa maendeleo ya michezo. Ambao umekuwa ukichota tu
fedha na hatujui unafanya nini au kwa msimu uliingiza kiasi gani.
Nilikuwa
nikilia na wale watendaji wa wizarani, mfano aliyekuwa Mkurugenzi wa
Michezo, Leonard Thadeo. Nilikuwa nikiwaona wakati timu inakabidhiwa
bendera, au kuna hafla watakuwa wamealikwa kama wageni rasmi au wameenda
pale kwa kuwa waziri yuko pale.
Nape
ameamua kuwasimamisha, yeye amekuwa shujaa ambaye hajakata kona wala
kuingia woga. Ninaamini alipoanzia ni njia nzuri na huenda ikawa ni
sehemu ya mabadiliko ya michezo lakini kama wengi mtamuunga mkono.
Kuanza
upya si ujinga, ikiwezekana Malinzi naye atumbuliwe, apumzike na
kupisha wengine ikiwezekana atakapokuja mtendaji mpya, basi akutane na
mwenyekiti mpya ili waanze pamoja.


Post a Comment