Dk Mwaka Jeuri Kwisha...Serikali yazidi kumkaanga, biashara yake yadoda
DAR
ES SALAAM: Kufuatia tumbutumbua majipu inayoendelea katika sekta
mbalimbali nchini, imebainika kuwa kitendo hicho kimemsababishia mtabibu
wa Kliniki ya Fore Plan iliyopo Ilala-Bungoni jijini Dar, Mwaka Juma
Mwaka, ‘Dk Mwaka’ apoteze wateja (wagonjwa) kwa madai ya kupoteza imani
naye, Risasi Mchanganyiko linakupa stori kamili.
Jengo la Kliniki ya Fore Plan.
SAKATA LILIPOANZIA
Sakata
la Dk. Mwaka na serikali lilianza Desemba 14, mwaka jana baada ya
daktari huyo kudaiwa kumkimbia Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla mara baada ya kufanya
ziara ya kushtukiza kwenye kliniki yake.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala.
NINI KILIFUATA?
Katika
ziara hiyo, naibu waziri huyo aliagiza viongozi wa tiba asilia kukagua
taaluma ya daktari huyo na ya washirika wake sambamba na aina ya dawa
zinazotumika kituoni hapo.
Aidha,
Dk. Kigwangala aliongeza kuwa, Dk. Mwaka amekuwa akiuka sheria za tiba
asili kwa kujitangaza zaidi kupitia vyombo vya habari na kurusha vipindi
vinavyoonesha akiuchambua mwili wa binadamu kana kwamba ni daktari,
yote hayo yakiwa kinyume na taratibu za tiba asilia.
BIASHARA YADODA
Mara
baada ya kauli hiyo ya serikali kutolewa na kuonesha kuwa ni dhahiri
mtabibu huyo ana ‘figisufigisu’ kwenye huduma zake, taarifa kutoka kwa
chanzo chetu zilieleza kuwa wagonjwa wameanza kupungua katika kliniki
hiyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
TUJIUNGE NA CHANZO
“Serikali
ni kama iliwafungua wananchi maana kulikuwa na malalamiko ya chini kwa
chini juu ya kutokuwa na imani na hizi huduma za kina Mwaka lakini
ilikuwa ni za mtu mmojammoja sasa aliposema waziri, watu wameacha kwenda
kwa wingi.
“Yani
sasa hivi ukifika huduma zinaendelea lakini watu ni wachache sana.
Zamani ilikuwa si mchezo. Ukifika pale mapokezi hupati hata nafasi
lakini sasa nafasi ipo maana imani ya watu katika kliniki hiyo
imepungua,” kilisema chanzo chetu.
MABENCHI MEUPEE
Mwandishi
wetu alishuhudia mabenchi ya wagonjwa yakiwa ‘meupe’ tofauti na kipindi
cha nyuma huku wahudumu wa kituo hicho wakiwa wamejipanga getini na
kuonesha ukarimu wa hali ya juu kwa wagonjwa wachache waliojitokeza
kituoni hapo.
SERIKALI YAZIDI KUMKAANGA
Ukiachana
na kauli ya awali ya serikali, wiki iliyopita, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema vituo
vingi vya tiba asili ikiwemo cha Dk. Mwaka havina sifa za kutoa tiba
asili na mbadala.
Alisema
havina sifa kwa sababu vinajiendesha kinyume na taratibu za tiba asilia
ambapo alipiga marufuku dawa zote zisizosajiliwa na kutolewa katika
vituo vya tiba asilia na mbadala kwa sababu zina hatari kwa afya ya
binadamu.
KIGWANGALA TENA!
Kama
hiyo haitoshi, kwa mara nyingine Dk. Kigwangala alizidi kupigilia
msumari suala hilo kwa kusema Dk. Mwaka amekuwa akitoa tiba pasipokuwa
na dawa ya aina yoyote iliyosajiliwa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wala TFDA.
WANANCHI WANENA
Mkazi
mmoja wa Ilala Dar es Salaam aliyetimbulisha kwa jina moja la Juma,
alisema serikali imechelewa kubaini tatizo hilo kwani kama wamegundua
kuna matatizo katika tiba hizo, tayari watu wameshaathirika kwa muda
mrefu.
“Serikali
ilikuwa wapi siku zote. Haioni kwamba tayari kuna Watanzania wengi tu
wameshaathirika? Yani kwa kweli hili ni janga,” alisema Juma.
MWAKA ANASEMAJE?
Mwanahabari
wetu alipotaka kuonana na Dk. Mwaka ili aweze kuzungumzia sakata hilo
alikutana na mmoja wa manesi aliyejitambulisha kwa jina moja la Agnes na
kusema kuwa Dk. Mwaka hakuwepo kituoni hapo na kumtaka mwandishi wetu
kuacha mawasiliano na maswali ya kumuuliza pindi atakapofika.
“Siruhusiwi
kuzungumza chochote mpaka nitakapozungumza na mkuu wangu wa kazi. Wewe
acha namba zako na maswali yako, nitamfikishia,” alisema Agnes.
CHANZO: RISASI

Post a Comment