ad

ad

HADITHI: Msafara wa Mamba - 12


MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’

ILIPOISHIA:
"Jamani majibu yetu ni haya sasa mnataka nimpe kila mmoja au niyatoe mbele yenu?"
"Hapa hakuna siri ndiyo maana tumekuja pamoja," nilijibu kwa niaba ya wote.
"Majibu yapo kama hivi nitaanzia kwa mama, wewe majibu yako yanaonyesha damu yako ni.." aliposita moyo ulinipasuka na kujua nimekwisha labda vipimo nilivyopima asubuhi ni vya uongo.
SASA ENDELEA…
"Damu yako inaonyesha ni safi.." sikusubiri maneno mengine nilijikuta nimemvamia mama na kuanguka naye chini kwa furaha, baada ya kunyanyuka na kukaa kitini huku nikifuta machozi kwa kitambaa. Daktari aliendelea kutusomea majibu.
"Inaonyesha jinsi gani moyo wako ulivyo na furaha, sasa ningependa nitoe majibu ya upande wa pili ili baadaye tuweze kuzungumza kwa urefu nini cha kufanya baada ya majibu yote."
Alitulia akisoma majibu ya Anko na kutufanya wote kuwa kimya kumsikliza Anko ana majibu gani?
"Majini ya Mr Joel yanaonyesha damu yako ni.." alitulia kidogo na kuendelea
"Damu yako ni safi."
Ha! sikujua jinsi nilivyomrukia Anko kwa furaha kwa kukutwa na yeye damu yake ni safi. Nilijikuta nikijawa na furaha kuondoa ule utata wa mama juu ya kujua Anko ni muathirika.
Anko yeye alicheka wala hakuonyesha kushangazwa na majibu yale ile ilionyesha jinsi gani alivyokuwa na uhakika tofauti na mimi. Baada ya kupata majibu tulikumbatiana wote kwa furaha na kutoka ofisini ili kurudi nyumbani.
Kabla ya kuondoka nilikumbuka kumuaga shoga yangu Maimuna, nilikwenda hadi kwa Mai kumuaga kuwa narudi nyumbani na kutaka kupeana maelekezo ya kupatana.
Mai iliponiona kabla ya kuingia ofisini mwao alitoka na kunifuata nje. Cha kwanza kabla ya yote aliniuliza:
"Vipi majibu yenu?"
"Mungu ametusaidia wote mambo yamekwenda vizuri."
"Hata Mr Joel?"
"Ndiyo kwani vipi?"
"Aaah ni kitu cha kujivunia maana nimeshuhudia zaidi ya watu wanne waliofika kupima na wapenzi wao kukutwa mmoja ameathirika kwa upande wako imekuwa jambo la heri hongera sana mpenzi," Mai alinikumbatia kisha aliniuliza:
"M’hu shoga hebu nipe maelekezo ya kukupata."
Nilimpa namba yangu ya simu na kumwelekeza ninapoishi.
"Usiniambie yaani una nyumba na gari?"
"Mbona hayo madogo kuna duka kubwa la nguo nitalifungua wakati wowote katikati ya jiji."
"Mmh, hongera sana, nikuache umuwahi shemu ila jioni nitafika kwako nina mazungumzo muhimu sana si una kaa na shemu?"
"Hapana nakaa na mama yeye huja na kuondoka na hivi karibuni tulikuwa tumetengana baada ya wafitini kumzulia mpenzi wangu ameathirika."
"Kina nani hao?"
"Si mama yangu mzazi na mke wa Joel mama Jose waliompakazia ni wivu tu nashangaa hata mama yangu kunionea wivu lakini leo limemshuka."
Niliagana na Mai na kuwawahi mama na Anko ambao walikuwa wameisha ingia kwenye gari. Anko aliponiona aliniuliza:
"Vipi mbona umechelewa?"
"Nilipitia msalani mara moja," nilimdanganya sikupenda ajue nimechelewa kwa sababu gani.
"Tuliingia kwenye gari na kuturudisha nyumbani huku akipanga siku ya pili kufanya sherehe ya kunivisha pete ya uchumba. Kabla ya kuondoka alinijulisha kuwa siku ya kesho yake tungekwenda kufungua duka langu kubwa la nguo Kariakoo.
Mmh! Niliona jinsi gani Mungu alivyo niwashia taa ya mafanikio japo mama yangu alionekana kutofurahishwa na mafanikio yale.
******
Ajabu baada ya kutoka hospitali mama alionekana kutokuwa na furaha kitu kilichonitia wasiwasi, nilijiuliza mama yangu alipenda Anko akutwe na ugonjwa kwa nini asifurahie mwanaye nipo na mwanaume ambaye yupo salama.
Majira ya saa moja za usiku simu yangu iliita nilipoangalia ilikuwa ya Maimuna, niliipokea na kuzungumza.
"Haloo shosti lete habari."
"Herena nimefika nipo karibu na kwako lakini barabara imenichanganya."
"Okay nakuja mara moja kukuchukua upo wapi?"
"Nipo njia panda."
Nilitoka nje na kwenda hadi njia panda na kumkuta Mai ambaye nilimchukua na kwenda naye hadi nyumbani. Nilimtambulisha kwa mama ambaye alimfurahia.
"Ooh, karibu mwanangu."
"Asante mama."
"M’hu shoga karibu sana," nilimkarisha huku nikienda kwenye jokofu kumletea kinywaji.
Baada ya kumletea kinywaji nilikaa pembeni yake nikiwa na shauku la kumsikiliza shoga yangu niliyepotezana naye kipindi kirefu.
"Lete stori mmh, ni muda mrefu," niliyaanzisha mazungumzo.
"Ni kweli Herena vipi hukuendelea nilijua sasa upo chuo kikuu?"
"Mmh, we acha mambo yaliingiliana na kunifanya niyaache njiani."
"Kwa sasa unajishughulisha na nini?"
"Kwa kweli sina kufanya zaidi ya kulelewa na shemeji yako na kila ukionacho hapa ni yeye."
"Hongera."
"Asante vipi wewe umeisha olewa?"
"Bado ila shemeji yako ni yule daktari wa hospitali ninayofanya kazi tupo mbioni kukamilisha."
"Nina imani kila jema Mungu atalipa wepesi."
"Nitashukuru...Samahani Herena ..si.si.jui," Mai kidogo aliingiwa na kigugumizi kitu kilichonifanya niwe na wasiwasi na swali lake.
"Vipi Mai mbona hivyo?"
"Sijui nitakacho zungumza hakitakuchukiza kwani Herena wewe ni rafiki yangu wa siku nyingi na shuleni ulikuwa mtu wangu wa karibu nakumbuka mara nyingi ulikuwa mstari wa mbele kutuasa wasichana tujiepushe na ngono."
"Ni kweli kabisa."
"Amini usiamini maneno yako ndiyo yaliyonifikisha hapa nilipo, napenda kutoa shukurani zangu asante sana."
"Nashukuru kuwa ni mmoja wa viumbe vinavyokumbuka fadhira nami nashukuru kwa hilo."
"Herena siku zote nilikuamini wewe kama kioo changu popote nilipokwenda, hivyo basi nilitegemea kukuta upo kwenye taasisi ya ushauri nasaha kwa ajili ya kuwasaidia wasichana ambao wamekuwa wakipotea siku hadi siku kwa kugeuzwa asusa kwa wanaume wakwale.
“Wanaume wamekuwa wakieneza magojwa kwa wasichana wadogo ambao wengi wao umaskini ndiyo unaowaponza. Herena umaskini ni ugonjwa mbaya sana kuliko hata ukimwi. Umaskini unaua umaskini unapumbaza umasikini unafilisi umaskini unapoteza utu wa mtu umaskini unakunyima maamuzi na kukubali kila kitu ili tu mkono uende kinywani."
Mai alizungumza mpaka machozi yakamtoka na sauti yake kubadilika kuwa na majonzi, baada ya kutulia kidogo aliendelea kuzungumza:
"Herena wenye pesa wamekuwa wakituua kwa kutumia uwezo wao wa kipesa na umaskini wetu uliotutambaa mpaka kwenye mboni ya macho."
Nilijikuta nikishindwa kumwelewa Mai maneno yote yale alikuwa na maana gani ilibidi nimuulize:
"Shoga mbona leo umekuja na mada hiyo una maana gani?"
"Herena wewe ni shoga yangu sipendi nikuone ukiangamia nikikuona."
Kauli ile ilinishtua na kunifanya nikae vizuri kwenye kochi kutaka kujua niangamie kwa sababu gani.
"Mai una maanisha nini?"
"Hivi wewe na Joel mmejuana muda gani?"
"Mbona unaniuliza hivyo?"
"Herena jibu swali sio kuuliza swali juu ya swali."
"Muda mrefu."
"Unamjua vizuri?"
Nini Kitaendelea? Tukutane toleo lijalo.
Powered by Blogger.