HADITHI: Msafara wa Mamba - 13

MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’
ILIPOISHIA:
Kauli ile ilinishtua na kunifanya nikae vizuri kwenye kochi kutaka kujua niangamie kwa sababu gani.
"Mai una maanisha nini?"
"Hivi wewe na Joel mmejuana muda gani?"
"Mbona unaniuliza hivyo?"
"Herena jibu swali sio kuuliza swali juu ya swali."
"Muda mrefu."
"Unamjua vizuri?"
SASA ENDELEA…
"Kivipi?"
"Maisha yake kwa ujumla."
"Ndiyo," nilimjibu kwa mkato.
"Si kweli humjui vizuri Mr Joel," Mai alinikatalia bila kumwelewa.
Maneno ya Mai yalizidi kuniweka njia panda na kushindwa kumwelewa alikuwa akimaanisha nini.
"Mai mbona kama sikuelewi?"
"Ni vigumu kunielewa ila utanielewa muda si mrefu."
"Ehe una maana gani?"
"Herena mimi namfahamu vizuri Mr Joel kwani ile ndiyo hospital yake na siri zake naweza kusema nazijua mimi kati ya wafanyakazi wote."
"Unataka kuniambia ulikuwa mwanamke wake?" niliona Mai alitaka kunirusha roho.
"Sivyo ufikiliavyo, unajua Mr Joel ni rafiki mkubwa wa mchumba wangu hivyo ana siri zake nyingi ambazo aliniambia kama mchumba wake pale Mr Joel alipokuwa akija na wasichana kupima afya zao."
"Sasa Mai umekuja kunirusha roho ili niachane na mpenzi wangu, Mai unajua japo ni rafiki yangu naweza kukubadilikia sasa hivi naomba uzungumze mengine yaliyokuleta kuhusu mpenzi wangu hakuna cha kututenganisha.
“Walianza ooh ameathirika yote ili kunitilia mchanga chakula changu. Lakini leo umewaumbua watu , hilo halijaisha nawe unakuja na yako kujuana imekuwa nongwa au nawe ni mmoja wa wake wenzangu?"
"Herena kila unalofikiria sivyo la muhimu ni kuwa msikivu, mimi simtamani Mr Joel ila kilicho nileta hapa ni umuhimu wa ukaribu wangu na wewe. Sipo tayari kukuona ukiangamia nikikuona wakati bado una nafasi ya kuokoka."
"Mai kuwa muwazi ulikuwa ukitaka kusema nini juu ya Mr Joel?"
"Japo hili ni siri kati mume wangu na Mr Joel lakini kisu kimegusa mfupa. Herena ndio maana mwanzo nilisema wenye pesa wanatumaliza, kubali usikubali Mr Joel ni muuaji mkubwa."
Kauli ile ilifanya nihisi kama kuna kitu kimechoma katikati ya moyo wangu.
"Mungu wangu Mai una maana gani kumwita mpenzi wangu muuaji mkubwa?"
"Herena ndugu yangu yule mzee ni hatari anatumia pesa zake kueneza virusi vya ukimwi kwa wasichana na mwanamke yoyote mzuri. Ni wasichana wengi amewaumiza ambao ninaowafahamu ni zaidi ya wane."
"Mai ni maneno gani hayo ya uongo unayoyaleta nilikuona tokea mwanzo ukimtolea macho mpenzi wangu tangu nilipokutambulisha. Kwa hiyo naomba utoke taratibu kabla sijakasirika," nilimbadilikia.
"Herena hebu punguza munkali ninacho kizungumza ni kwa faida yako leo na kesho tusije nyoosheana vidole au kulaumiana kwa kujua jambo na kukaa kimya."
"Nimesema tokaaa...kama hutaki nitakumwagia maji ya moto unajifanya rafiki kumbe mnafiki...tokaaa."
Nilijikuta nimepandisha jazba na kumfukuza Maimuna kwa sauti ya juu kitu kilichomfanya mama atoke chumbani baada ya kutuacha tuzungumze. Alipotoka alinikuta nikimnyanyua Mai kwa nguvu ili nimtoe nje japo Mai aling'ang'ania kama shetani wa kutumwa.
"Herena vipi tena mbona hivyo?"
"Mama huyu ni mmoja wa maadui zangu."
"Maadui zako kwani tatizo nini? Hebu muache kwanza."
"Kila kukicha maadui wanaongezeka juu ya penzi langu na Anko wananiona nafaidi naye huyu kaja na mapya. Mama leo mwenyewe umeamini kuwa Anko afya yake ni salama yeye analeta umbea kuwa Anko ni mmuaji kamuua nani kama alikataliwa si yeye."
"Hebu punguza jazba eti mwanangu tatizo nini?" mama alimuuliza Mai.
"Mama sikiliza mimi na Herena ni marafiki wa muda mrefu sana sema tulipoteana. Kwa kweli leo nilipomuona nilifurahi sana ila furaha yangu ilitumbukia nyongo baada ya kujua rafiki ya shoga yangu ni yule muuaji mkubwa."
"Una maana gani kusema ni muuaji?" mama alimuuliza.
"Mama Mr Joel ni muathirika wa kipindi kirefu zaidi ya miaka saba sasa ila amekuwa akitumia madawa ya kuongeza nguvu. Hata mkewe mama Jose ni muathirika ila mkewe amekuwa akifuata ushauri wa daktari. Ila mumewe amekuwa kiwembe kwa kuusambaza ugonjwa kwa wasichana wadogo hasa wanafunzi na wanawake wazuri.
“Kwa vile hammjui vizuri ule sasa hivi si mwili wake alikuwa ana mwili mkubwa sana ila kutofuata ushauri kila kukicha akija hospital anapungua uzito."
Yalikuwa maneno mapya yaliyonifanya nirudi hadi kwenye kochi na kukaa nikifikilia kauli ya Maimuna ilikuwa na ukweli gani.
"Kwa nini unasema hivyo wakati leo tu tumetoka kupima na kukutwa wote wapo sawa?" Mama alimuuliza.
"Ni kweli majibu yameonyesha sawa ila ukweli unabakia palepale kuwa Herena yupo sawa ila Mr Joel ameathirika."
"Mbona hapo sikuelewi mwanangu aathirike kivipi majibu yameonyesha yupo sawa?" mama alishangaa.
"Mama ile ni siri nzito ambayo ameibeba mchumba wangu na baadhi ya madaktari wa ile hospitali ambao hupewa pesa kupindisha ukweli."
"Unasema?" Nilijikuta nimeropoka na kukaa kitako.
"Ukweli ndio huo kila siku anapobanwa na wasichana kupima hawezi kupima sehemu nyingine zaidi ya hospital yetu. Kama mnaona mimi muongo mwambie mwende hospitali nyingine kama atakubali."
Tulijikuta tukitazamana na mama kila mmoja alikosa jibu Mai aliendelea kuzungumza:
"Kwa kweli nimekuwa nikiumia kitendo cha Mr Joel kuwadanganya wasichana. Lakini leo kisu kimegusa mfupa sikuwa radhi kukuona ndugu yangu mtu niliyemuona kama taa yangu ukiumia nakuona lakini ukweli ndio huo."
"Mmh! Kweli naamini maneno yako mwanangu lazima nami niseme ukweli mimi mama yako nimeathirika na mtu aliyeniambukiza nilijua ni yeye lakini mwanangu alikuwa mbishi nina imani ukweli umeujua."
Nilikuwa kama nipo ndotoni nisipate jibu juu ya kuathirika kwa Anko iweje aathirike mimi niwe mzima. Japo niliamini kwa upande mmoja lakini kwa upande wa pili bado moyo ulikuwa mzito.
Kwa ushahidi Maimuna alitotolea vyeti vya Anko vilivyoonyesha ameathirika na jinsi maendeleo yake ya chembe za CD4 mwili. Baada ya wote kuvitazama nilijikuta nikitokwa na machozi na kunyanyuka hadi kwa Mai na kumpigia magoti kumuomba msamaha.
******************
Siku ya pili nilikwenda hadi kwenye kituo cha kupima na kutoa ushauri juu ya ugonjwa wa ukimwi. Baada ya kufika nilikutana na mshauri ambaye sikuwa mgeni kwake. Aliponiona alinikaribisha pamoja na kunikumbuka lakini jina langu hakulikumbuka.
"Karibu mdogo wangu."
"Asante dada yangu."
"Kama sikosei ni jana tu ulikuwa hapa?"
"Ni kweli dada yangu."
"Mm’hu ulikuwa na tatizo gani?"
"Nilikuwa na swali moja juu ya maambukizi ya ukimwi."
"Uliza tu."
"Hivi kuna uwezekano mtu mwenye ukimwi kutembea na mtu asiye na ukimwi na asipate?"
Nini Kitaendelea? Tukutane toleo lijalo.
Post a Comment