HADITHI: Msafara wa Mamba - 11

MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’
ILIPOISHIA:
Tuliteremka wote na kuingia kwenye gari la Anko ambalo aliendesha mpaka moja ya hospital kubwa jijini. Kabla ya kuteremka alituomba tumsubili na yeye kuingia ndani ya hospitali. Alirudi baada ya robo saa kisha alituomba tuteremke na kuongozana naye hadi ndani ya hospitali.
SASA ENDELEA…
Tulikwenda moja kwa moja hadi kwenye chumba cha daktari mkuu, aligonga mlango na kukaribishwa. Tuliingia wote hadi ndani na kupokelewa na mwanaume mmoja mtanashati aliyependeza kwenye vazi lake la udaktari.
Alipotuona alitukaribisha huku akimchangamkia Anko kuonyesha wanafahamiana.
"Ooh, Mr Joel za siku?"
"Nzuri doctor Ambe" walikumbatiana kisha alitugeukia na sisi.
"Ooh, karibuni sana."
"Asante" tulijibu kwa pamoja, baada ya kutukaribisha alimgeukia Anko
"Mhu mzee una tatizo gani?"
"Bwana kwanza kabla ya yote ningependa kukutambulisha nilioongozana nao. Huyu hapo ni mchumba wangu na anayefuata ni mama mkwe."
"Ooh! Karibuni sana shemeji karibu sana..Mama karibu sana."
"Asante" tulijibu kwa pamoja.
"M’hu mna tatizo gani?"
"Mimi na mchumba wangu tumekuja kupima afya zetu ili kujua tupo sehemu gani."
"Mmh, vizuri ni jambo zuri sana na la ujasiri, lakini naomba niwaulize swali."
"Uliza tu dakta," Anko alimruhusu.
"Ni nini kilichowapelekea kuja kupima afya zenu?"
"Ni hali ya kawaida kwa watu walio makini kujua afya zao ili waishi kwa matumaini."
"Urafiki wenu una miaka mingapi?"
"Miwili sasa."
"Mr Joel mbona mmekaa muda mrefu sana mpaka kuchukua jukumu la kupima au mliisha pima kabla?"
"Kila mmoja ameisha pima kivyake zaidi ya mara mbili na kila mmoja alikuwa na majibu mazuri."
"Mnataka kuniambia nini kilicho wapelekea leo wote mje mpime kwa pamoja?"
"Ni kutoana shaka kwetu sote si unajua siku hizi kuna vyeti vya kununua, unafikili mwenzio mzima kumbe unakuchimbia kaburi."
Maneno ya Anko yalinitoa hofu moyoni mwangu kutokana na kuonyesha jinsi gani anavyo jiamini na afya yake.
"Mnataka kuniambia kipindi chote mlitumia kinga katika kukutana kimwili?"
"Mmh mara chache na kwa vile tuna mpango wa kuoana na kupata watoto tumeamua kujua hali zetu kabisa."
"Je, kama kuna mmoja atakutwa ameathirika hapo mtachukua uamuzi gani?"
"Kwani bado nitaendelea kuwa naye kutokana na mapenzi yangu ya kweli kwake kwa kutumia kinga wakati wa tendo vilevile kuwa karibu yake ili usijione mpweke na kumhimiza yote tutakayo elezwa na washauri," Anko majibu yake yalinipa moyo kuonyesha jinsi gani alivyo na utu moyoni.
"Na wewe?" alinigeukia mimi
"Hata mimi nitakuwa naye karibu kama alivyojibu Anko."
"Shemu nikikuangalia bado msichana mdogo una mtoto?"
"Hata."
"Nina imani unatamani kuwa na mtoto kama ilivyo dhamira ya kiumbe chochote kupata mtoto ili kujenga familia. Swali kama imetokea mwenzako ameathirika nawe kuendelea kuwa naye kwa kukutana kwa kutumia kinga, vipi kuhusu suala la mtoto?"
" Ni vigumu kulisema kwa sasa lakini kama itatokea tutajua vinsi gani ya kulitatua kupitia wataalamu kama nyinyi."
"Na kwako mzee?" alimtupia swali Anko.
"Kwangu bado haitakuwa vibaya kwa vile tayari nina watoto."
"Kwa mfano usingekuwa nao?"
"Kwa kweli naungana na mwenzangu kwa kutulia na kupanga kwa kuwashirikisha wataalamu kama nyinyi nina imani ufumbuzi lazima utapatikana."
"Japo nina maswali mengi sitapenda kuwapotezeeni muda kutokana na mambo ya msingi kuyajibu. Sasa mpo tayari kuchukua vipimo?"
"Ndiyo," tulijibu kwa pamoja.
Baada ya kujibu daktari alichukua kitabu cha kalatasi za vipimo na kutuandika majina kila mmoja na kutuelekeza chumba cha kuchukulia vipimo (Maabara).
Tuliongozana na kumuacha mama ofisini kwa mganga mkuu na sisi kuelekea chumba kuchukua vipimo.
Tulipofika tulikuwakuta wauguzi ambao walichukua vipimo vyetu na kutoka chumba cha vipimo na kurudi ofisini kwa daktari kusubiri majibu ya vipimo vyetu ambavyo kwa upande wangu nilikuwa na uhakikia wa asilimia mia nipo safi wasiwasi wangu kwa Anko.
Tulipotoka nje ya chumba ili tuelekee ofisini nilisikia jina langu likiitwa kwa nyuma.
"Herena."
Sikuiitikia moja kwa moja kutokana na majina ya watu kunafanana, nilijua naweza kuitikia kumbe kuna mtu mwingine anaitwa. Niligeuka ili kupata ukweli kujua ni nani anaye niita. Nilipokutana na shoga yangu ambaye tulipotezana tokea darasa la saba.
"Ha! Maimuna ni wewe?"
"Ni mimi Herena, mmh, umekuwa mama mzima."
Shoga yangu alikuwa amevalia mavazi uuguzi wa hospitali ile, tulikumbatiana kwa furaha.
"Mm’ hu shoga za siku?"
"Mungu anajalia."
"Vipi mbona hapa una matatizo gani?"
"Haa! Shoga si unajua tunaunga mkono kampeni ya Rais kuwa Tanzania bila ukimwi inawezakana."
"Kwa hiyo unataka kuniambia umekuja kupima?"
"Ndiyo maana yake?"
"Mbona unaonyesha furaha majibu tayari nini?"
"Bado ila lazima ujipe moyo."
"Na yule iliyefuatana naye ndiye baba yako nini?"
"Yule ndiye usingizi wangu."
"Utani huo yaani mzee Joel ni mpenzi wako?"
"Kwani vipi mbona umeshtuka?"
"Mmh hata, lakini si ana mkewe yule?"
"Sasa ndugu yangu ukitaka kuyajua yote hayo utakufa na njaa si wajinga waliosema tutabanana hapahapa kama yeye kamuoa na mimi nyumba ndogo."
"Mmh hata mambo yako yanaonekana."
"Kwanini unasema hivyo?"
"Si unaona sisi tuona tegemea mshahara tuna tofauti kubwa na ninyi mtoto shavu shavu. Kwahiyo umekuja kupima na mzee?"
"Shoga siku hizi majibu ya upande mmoja yana ualakini, hivyo tumekuja wote ili tujue nani anachoma nyumba."
"Mmh vizuri, sasa shoga ukitaka kutoka unipitie ili tuelekezane pa kupatana baada ya kazi."
"Hilo halina taabu, huwezi kuamini Mai jinsi nilivyofurahi lazima ufike ninapoishi mpenzi."
Niliagana na Maimuna na kwenda moja kwa moja hadi ofisini kwa daktari. Nilimkuta mama na Anko wakinisubiri, baada ya kuketi daktari alinyanyuka na kutoka nje ya ofisi na kutuacha peke yetu wakati huo kulikuwa kumeletwa vinywaji kwa ajili yetu.
Baada ya dakika kama saba daktari alirejea na kuketi sehemu yake na kuendelea kunywa juisi iliyokuwa nusu glasi. Baada ya dakika tano majibu ya vipimo yaliletwa. Japo sikuwa na wasiwasi sana lakini mapigo ya moyo yalienda mbio kiasi.
Nilipomuangalia Anko yeye alionyesha hana wasiwasi, alikuwa ni mtu mwenye tabasamu muda wote huku akiendelea kunywa kinywaji chake. Daktari baada ya kupitia kalatasi zote za majibu yetu alipumua kidogo kabla ya kunyanyua macho na kututazama wote kisha alisema:
"Jamani majibu yetu ni haya sasa mnataka nimpe kila mmoja au niyatoe mbele yenu?"
"Hapa hakuna siri ndiyo maana tumekuja pamoja," nilijibu kwa niaba ya wote.
"Majibu yapo kama hivi nitaanzia kwa mama, wewe majibu yako yanaonyesha damu yako ni.." aliposita moyo ulinipasuka na kujua nimekwisha labda vipimo nilivyopima asubuhi ni vya uongo.
Nini Kitaendelea?
Post a Comment