HADITHI: Msafara wa Mamba - 10
ILIPOISHIA:
Niliamini hata mimi nilikuwa nimekwisha, mapigo ya moyo yalinienda kwa kasi, nilimuomba Mungu aniepushe na balaa lile lililokuwa mbele yangu. Jasho lilinitoka kwa hofu la majibu, mama aliliona lile na kunipoza.
“Najua upo katika wakati mgumu, lakini kila kitu kipo katika mpango wa Mungu zuri au baya yatakiwa tulipokee ili tukabiliane nalo. Jibu baya lisikutishe tupo pamoja kuambikizwa si kufa,” mama alinitia moyo.
SASA ENDELEA...
Wakati huo jina langu liliitwa ndani kuchukua majibu, nilitulia kwa dakika moja bila kutikisikia kisha nilionyanyuka juu. Mama alinivutia kwake na kunikumbatia kisha alioniruhusu nikapokee majibu. Moyoni nilishindwa nimlaumu nani japo Anko alijijua na kunifanyia kitu kama kile.
Niliingia hadi chumba cha ushauri, nilipofika nilikaa kwenye kiti kusubiri majibu, palipita utulivu huku mshauri akipitia majibu yangu nami nilitulia tuli huku mapigo ya moyo yakienda mbio.
Baada ya kulitulia zaidi ya dakika nzima bila maelezo yoyote mtoa nasaha aliniita jina langu
"Helena"
"Abee," niliitikia kwa mkato.
"Umejiandaa vipi kupokea majibu?"
"Mpaka naamua kuja kupima nilijiandaa vilivyo na kuwa tayari kwa jibu lolote litakalo tokea mbele yangu kwa vile sina wa kumlaumu."
"Una uhakika gani kama mwenzako ameathirika?"
"Hilo halina mjadala mkewe ndiye aliyesema."
"Mmh! Si kweli, uhakika ni kupima kujua afya yake."
"Sawa lakini naomba jibu langu."
"Kwa hiyo majibu nikupe sasa hivi au nikupe kwa siri?"
"Dada yangu kuna siri gani wewe lipasue hilo jipu nivune nilichopanda."
"Bado majibu yako yanaonyesha...," aliposita kidogo nilihisi mwili kupandwa na joto la ajabu na kunifanya nitokwe na jasho jingi, nilimsikia akirudia.
"Majibu yako yanaonyesha damu yako ni safi," alinieleza huku akitabasamu.
Mmh! Kauli ile niliisikia lakini sikuamini niliona kama nipo ndotoni nilijikuta nikimuuliza
"Etiii! Unasema?"
"Ni kweli majibu yako ni safi ndiyo maana ulitakiwa umpime mwenzio ili ujue afya yake."
"Lakini dada kuna umuhimu gani wa kumpima mtu wakati mimi afya yangu ni nzuri lazima na mwenzangu atakuwa na afya nzuri. Ni wazi watu walipandikiza maneno ili tuachane."
"Hapana mdogo wangu bado si kumuamini kwa vile wewe umejikuta salama. Huwezi jua labda ni mgonjwa la muhimu ni kwenda naye kupima ili upate uhakika."
"Mmh! Sawa lakini hapa yeye alinihakikishia afya yake ni salama na kuwa tayari kwenda kupima wakati wowote."
"Itakuwa vizuri kabla ya kukutana naye kimwili mkapime ili mjue afya yake, vilevile hiyo haitoshi mtatakiwa kutumia kinga hadi miezi mitatu mtakaporudi kuhakikisha afya zenu wakati huo kila mmoja awe muaminifu kwa mwenzake."
"Sawa dada nashukuru yaani huwezi kuamini jinsi nilivyo furahi."
"Naomba furaha yako ikamilike kwa mwenzio naye kupima ili muishi kwa uhakika kufuta ule uvumi wa mwenzio kuwa na matatizo katika afya yake."
"Sawa nitafuata kila ulilo nieleza na kulifanyia kazi."
Nilikumbatiana na mshauri na kutoka nje nilimkuta mama akinisubiri kama kawaida yake aliniwahi kunikumbatia. Sikuacha kutokwa na machozi ambayo yalikuwa ya furaha kwa mara nyingine kukutwa nipo safi.
"Vipi mwanangu majibu yanasemaje?"
"Mama majibu yangu ni mazuri nipo salama."
"Ooh! Mungu mkubwa inatosha sasa," kauli ya mama ilinitisha kidogo.
"Inatosha nini mama?"
"Kuanzia leo nisikuone ya yule mwanaume nasema inatosha nimechoka kila siku kupatwa na ugonjwa wa moyo Mungu anakupenda lakini bado mapenzi yake unayapiga teke."
"Mama huwezi kumhukumu Anko bila kuwa na ushahidi wa kutosha. Nina uhakika kama mimi nipo salama na yeye yupo salama."
"Herena mwanangu naomba uwe muelewa kwa nini unakuwa mbishi?"
"Mama hata wewe ulinieleza kuwa usimhukumu mtu kwa macho bali kuwa kuijua afya yake tena kwa kupima."
"Ni kweli nakuomba kama unataka kuendelea na Anko wako basi tuondoke wote mguu kwa mguu kuja kupima ili nipate uhakika nami nijue ugonjwa sikuupata kwake na maneno ya mkewe ni ya uongo."
"Sawa mama ili kupata ukweli nitampigia simu ili tuje pamoja leo hii kupata ukweli na kung'oa mzizi wa fitina."
Baada ya kukubaliana na mama nilimpigia simu Anko aje pale kituo cha kupimia afya na kutoa ushauri kwa wagonjwa pamoja na vijana. Simu upande wa pili ilipokewa.
"Halo mpenzi unasemaje?"
"Ni hivi kutokana na kauli ya mkeo kuwa wewe ni muathirika naomba uje ili twende tukapime kwenye kituo cha afya kilichopo karibu na benki ya NMB."
"Herena mimi ni mtu mwenye hadi siwezi kwenda kwenye vituo vya uchochoroni."
"Kwa hiyo?" nilimuuliza.
"Njoo ofisini unipitie twende kwenye hospitali moja yenye hadhi yangu tukapime japo niliisha kueleza mimi ni salama ili kukuhakikishia njoo twende ili kuondoa ule wasiwasi wako."
"Hakuna tatizo nakuja sasa hivi"
"Okay nakusubiri"
Nilikata simu na kumgeukia mama ambaye aliniwahi kwa swali
"Vipi amekubali."
"Ndiyo lakini amesema twende kwenye hospitali kubwa yenye vifaa vya kisasa."
"Hakuna tatizo, lini?"
"Sasa hivi."
"Basi tusipoteze muda tuongozane pamoja."
Tuliingia kwenye gari na kuelekea kazini kwa Anko, tulipofika nilimjulisha nimeisha fika namsubili nje. Alinieleza anatoka baada ya dakika chache, baada ya dakika kama tano Anko alitoka na kuja hadi kwenye gari langu. Nilimuona akishtuka kidogo baada ya kumuona mama.
"Vipi upo na mama?"
"Ndiyo ingia garini twende."
"Hapana tutatumia gari langu, lako utaliacha hapo nitamtuma mtu alipeleke kwako kwani baada ya kutoka hospitali nitawarudisha moja kwa moja nyumbani kwenu."
Tuliteremka wote na kuingia kwenye gari la Anko ambalo aliendesha mpaka moja ya hospital kubwa jijini. Kabla ya kuteremka alituomba tumsubili na yeye kuingia ndani ya hospitali. Alirudi baada ya robo saa kisha alituomba tuteremke na kuongozana naye hadi ndani ya hospitali.
Post a Comment