HADITHI: Msafara wa Mamba - 09
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’Maneno yangu kidogo yalimfanya mama arudi kwenye hali yake ya kawaida, japokuwa jioni ya siku ile nilitakiwa kukutana na Anko nimuomba radhi ili niwe karibu na mama. Siku ya pili mama aliamka katika hali nzuri kitu kilichonipa nafasi ya kuweza kutoka.
Mchana Anko alinipigia simu kuwa ana safari ya nje ya mkoa hivyo alinitaka mapema kwa ajili ya mipango ya safari. Nilimuaga mama ambaye muda huo alionesha hana kinyongo tena.
“Herena mwanangu naomba kabla hamjaondoka mkapime afya zenu kwanza.”
“Sawa mama.”
Niliagana na mama na kwenda sehemu Anko aliyosema anikute, wakati namsubiri nilikuwa na mawazo mengi juu mama kung’ang’ania kupima na kushusha pumzi ndefu baada ya kumwambia natumia kinga. Nilijikuta nikipata wazo la kijinga la kutafuta cheti cha kununua ili kumpelekea mama aondoe wasiwasi kwa Anko.
Baada ya ziara ya kikazi tulitotumia siku nne nje ya mkoa, nilibahatika kununua vyeti viwili vyenye majibu mazuri kuwa wote tupo sawa. Niliporudi nilimpa mama, baada ya kuvipokea mama alivisoma na kusema kwa mshtuko.
“Unataka kuniambia Anko wako naye yupo salama?”
“Ndiyo mama, mbona umeshtuka?”
“Walaa! Kawaida tu,” kauli ya mama ilinitisha na kutaka kujua mbona hakufurahia zaidi ya kuyashangaa majibu ya Anko.
“Mama mbona sikuelewi?”
“Nipo sawa, kwani hospitali aameambiwa nini?”
“Wametupongeza na kutuomba turudi baada ya miezi mitatu ili kupata uhakika wa majibu.”
“Kama hivyo hakuna tatizo.”
Siku zilizidi kukatika huku nikiendelea kula raha na mzee mzima, nakumbuka siku moja tukiwa hotelini na Anko, mkewe alilengeshwa na wapambe aje afumanie. Siku hiyo nilitamani ardhi ipasuke inimeze kwa kujua mkewe anaweza hata kuniua.
Lakini ilikuwa tofauti baada ya mkewe kuingia ndani aliangua kilio huku akimlaumu mumewe. Maneno aliyoyasema yalikuwa kama msumeno ulioupasua moyo wangu bila ganzi.
“Mume wangu hii tabia ya kuendelea kuua wasichana bila kosa utaisha lini, hebu mwangalie huyo binti alivyo mdogo sana na mwanao wa mwisho. Hivi wanao wakifanyiwa hivi utafurahi? We binti mlipokutana mmetumia kondomu?”
Nilikataa kwa kichwa kwani uoga ulikuwa umenitawala.
“Si kweli hiyo kondomu ipo wapi? Ona sasa, umeniumiza mimi mkeo hukuridhika sasa unaisambaza tu, binti inawezekana hunijui mimi ndiye mkewe mzee Joel. Mume wangu ni muathirika anayesambaza virusi kwa kuwahonga wasichana wadogo na kufa nya nao ngono zembe. Ukitoka hapa kapime ili ujue hali yako lakini muongope mwanaume kama ukoma”
Kauli ilinishtua na kunifanya ninyanyuke kitandani na kupitia nguo zangu zingine nilimalizia kuvaa kwenye korido. Nilipofika nje nilikodi gari hadi nyumbani, bahatu nzuri nilimkuta mama. Nilipomuona niliangua kilio kama nimefiwa.
Mama alinishangaa na kutaka kujua kulikoni kuwa katika hali ile.
“Vipi tena kulikoni?”
“Kumbe kweli Anko muathirika.”
“Una maana gani kusema hivyo?”
“Mkewe kanihakikishia kuna nini hapo.”
“Kakuhakikishia nini?”
“Kuwa Anko ni muathirika.”
“Sasa wewe unamuamini nani mkewe na vipimo?”
“Mama nilikudanganya kuwa nimepima kumbe uongo.”
“Eti!?”
“Kweli mama nilinunua cheti ili kukudanganya?”
“Mungu wangu, Helena mwanangu kwa nini ulifanya hivyo?”
“Mama ni akili za kitoto.”
“Sasa una uhakika gani kama umeathirika?”
“Sikutumia kinga mara nyingi nilipokutana naye.”
“Lakini bado huwezi kujua kama umeathirika bila kupima.”
“Hapana mama, nasikia kawaambukiza wengi.”
“Si nilikuambia ukapindisha maneno, lakini bado usijihukumu, unatakiwa kwenda kupima ili kujua ukweli.”
Nilikubaliana na mama kwenda kupima muda ule ule, baada ya kuoga na kubadili nguo. Tuliongozana wote hadi kutuo cha ushauri nasaha ili kujua afya yangu, tulivyo fika kituo cha ushauri na kupima virusi vya ukimwi. Katika kuchukua namba ya kuingia nilikutana na shoga yangu niliyekuwa nasoma naye shule moja.
Aliponiona alishtuka na kuniuliza.
“Helena kulikoni huku?”
“Hidaya mambo ya kucheki afya si unajua tumecheza sana rafu.”
“Ni kweli, hata mimi ndicho kilichonileta, una taarifa?”
“Zipi hizo?”
“Za mwalimu Zakayo,” mimi kiroho pa!
“Taarifa zipi?”
“Helena upo wapi wewe?”
”Hidaya sikuwemo muda mwingi jijini.”
“Kwa taarifa yako, mwalimu Zakayo amejinyonga baada ya kugundulika ameathirika.”
“Mungu wangu tumekwisha.”
“Kweli tumekwisha, wanafunzi kibao na walimu waliotembea naye wote wameumia na mimi nimeona nije nipate ukweli sijui wewe shoga yangu.”
Mmh, kweli nilikuwa katikati ya balaa nyuma mwalimu mbele Anko, sikuamini kama ningetoka salama. Wazo la haraka lilikuwa kama nikikutwa nimeathirika ninywe sumu ili kuikimbia aibu ya kuvishwa nepi.
Kwa vile Hidaya alikuwa ameisha chukua kadi, nami nilikwenda kuchukua kadi kusubiri zamu yangu kuitwa kwenye vipimo. Baada ya kuchukua kadi nilirudi kusubiri kuitwa, Hidaya alitangulia kuitwa baada ya muda alitoka. Zamu yangu nami ilifika niliitwa na kuingia ndani.
Nilipokelewa na dada mmoja mpole ambaye alivyo hukufanya mtu uondoe wasiwasi wa moyo.
“Karibu mdogo wangu.”
“Asante.”
“Mm’hu,” alionesha kuuliza nini kilichinipeleka pale.
“Kama hivyo dada nimekuja kujua afya yangu.”
“Ooh, vizuri kipi kilichokushawishi kupima.”
“Nafikili kuunga mkono kauli mbiu ya Muheshimuwa Rais Tanzania bila ukimwi inawezekana.”
“Vizuri sana, je ukijikuta umeathirika utafanyaje?”
“Sina la kufanya kwa vile nimeisha athirika kinachotakiwa ni kufuata masharti yanayotakiwa ili niishi muda mrefu.”
“Vizuri, na ukijikuta upo salama?”
“Vile vile sitakubali kufanya ngono zembe huku nikimuhimiza mwenzangu naye kupima afya yake ili tufanya ngono salama.”
“Vizuri sana binti kwa uelewa wako, sasa hivi utaelekea chumba cha kutolea damu.”
Nilinyanyuka hadi chumba cha kutolea damu kisha nilirudi nje kusubiri vipimo. Baada ya muda Hidaya alitangulia kuchukua majibu yake, muda kidogo alitoka akionesha kuchanganyikiwa hata kujigonga mlangoni wakati wa kutoka. Niliamini hata mimi nilikuwa nimekwisha, mapigo ya moyo yalinienda kwa kasi, nilimuomba Mungu aniepushe na balaa lile lililokuwa mbele yangu. Jasho lilinitoka kwa hofu la majibu, mama aliliona lile na kunipoza.
“Najua upo katika wakati mgumu, lakini kila kitu kipo katika mpango wa Mungu zuri au baya yatakiwa tulipokee ili tukabiliane nalo. Jibu baya lisikutishe tupo pamoja kuambikizwa si kufa,” mama alinitia moyo.
Nini kitaendelea? Endelea kufuatilia.
Post a Comment