HADITHI: Msafara wa Mamba - 08
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’ILIPOISHIA:
Hilo sikuhofia kwa kujua hata mama aliipata nafasi kama ile na alijimwaga bila woga. Naikumbuka siku moja ambayo itakuwa vigumu kunitoka akilini na ndio mwanzo wa kuelewa nini nilichokuwa nikikifanya na kunipelekea kuandika walaka huu.
SASA ENDELEA…
Nina imani kila anaye soma asichukulie kama haditi tamu au kisa cha kusikitisha bali ni somo tosha maishani. Tatizo langu sipendi mtu mwingine limkute nitajisikia vibaya na kuona ujumbe wangu hukuwafikia walengwa. Elimu si darasani tu, la hasha elimu ni chochote kikutokeacho mbele yako chenye mafunzo kwa kuona au kusikia.
Ilikuwa siku ambayo iliniingiza dunia nyingine ambayo sikuitegemea kuuingia hata siku moja japo ndipo nilipokuwa nikielekea.
Ilikuwa ni siku ya jumamosi majira ya saa tatu usiku nakumbuka nilikuwa na wiki sijarudi nyumbani baada ya kuwekwa kwenye hoteli ya kifahari na Anko. Niliwasiliana na mama kwa njia ya simu na kunipa moyo kuwa hali yake ni mzima wa afya nje hofu kubwa ilikuwa kwangu.
Nilimtoa hofu kuwa yangu hali ilikuwa salama salimini, hakutaka kujua nipo wapi zaidi ya kuniombea dua niendelee kuwa salama. Siku hiyo baada ya kukaa upande wa baa na kunywa pombe ambazo nilimuona kama Anko zimemzidia. Nilimnyanyua ili nimrudishe chumbani.
Kwa kweli nilipata shida kumnyanyua na kuweza kumtembeza kwa shida, tulikwenda kwa shida sana huku tukiyumba kama gari umetatika senta bolti. Nilimtoa kwenye baa na kumpeleka kwenye vyumba vya kulala. Kutokana uzito nilimfikisha kwa shida hadi mlangoni na kuanza kufungua mlango kwa funguo.
Nilimzuia kwa mguu ili asiende chini na kujitahidi kufungua mlango.
Sauti ambaye haikuwa ngeni masikioni yangu lakini akili yangu haikukubali kama ni yenyewe iliniita nyuma yangu:
"Helena ni wewe?"
Niligeuka akili yangu asiamini ni kweli ile sauti ni ya mama yangu mzazi, haikuwa tofauti na mapokeo yangu kuwa ni kweli ni mama yangu mzazi mama Herana. Nilishindwa kumjibu haraka nilikuwa kama mwanga aliyeshikwa akiwanga mchana kweupe.
"Huyu nani?" aliniuliza ikionesha haamini macho yake.
"Anko."
"Imeanza lini? Helena mwanangu siamini nimekubali duniani hakuna kitu cha bure."
Mama alionekana amepagawa nina imani hakupenda nichangie mume mmoja na yeye. Wakati huo Anko alikuwa bado amelala chini sakafuni.
"Herena mwanangu kwa nini usiulize kabla ya kuingia kwenye msafara huu, mmh, kweli msafara wa Mamba haukosi kenge na mijusi. Siamini na sitaamini mpaka naingia kaburini kama mwanangu umeingia kwenye msafara wa Mamba usiokuhusu.
“Wasiwasi wangu umekuwa kweli, Herena kwa nini lakini umeingia kwenye msafara wa mamba?"
"Kwani mama tatizo nini, huyu si baba yangu mzazi pia mliisha achana na mwisho nilifanya hivi kuokoa maisha yako," nilimjibu mama huku nikijikaza kutokana na hali aliyoonesha mama yangu aliyekuwa akizungumza huku machozi yakimtoka.
"Herena huwezi kuniokoa huku akijiangamiza, nilikueleza mara ya mwisho kuwa sipendi uishi maisha yangu. Kwa nini mwanangu umechukua kila kitu kwangu, kwa nini hukutaka kuendelea na tabia yako ya awali ya msimamo leo hii umeingia kwenye msafara wa mamba.
“ Oooh! Mwanangu yaani leo nimesikia uchungu kama siku iliyokuleta duniani, uchungu huu ni wasiwasi kukupoteza duniani."
Maneno ya mama niliyaona kama uchuro, nilimweleza sehemu ile si muhimu muhimu ya kuyazungumza kwa kina ni nyumbani. Mama hata yule bwana aliyekuwa naye alimuacha na kuondoka huku akilia. Mwanaume aliyeongozana naye alibakia njia panda asijue nini kinaendelea. Nami nilitumia nafasi ile kumwingiza ndani Anko aliyekuwa hajitambui kwa pombe.
****
Siku ya pili niliporudi nyumbani nilimkuta mama macho yamemuiva na kuvimba kuonesha amelia kwa muda mrefu. Hali ile ilinitisha na kujiuliza kuna kingine kilichomliza mama yangu au ni kilekile cha kunikuta na Anko. Niliamini kikubwa kilichomuumiza ni kuchangia mwanaume mmoja na mwanaye.
Lakini kwa upande wangu sikuona kosa kwa vile Anko hakuwa baba yangu wa kunizaa pia alikuwa ameachana na mama. Kingine nilichokiamini kuwa nipo sawa kilitokana na msaada mkubwa wa Anko uliosababisha hali ya mama kurudi katika hali yake ya kawaida.
“Mama kuna nini?” nilimuuliza mama.
“Ina maana hujui?”
“La kunikuta na Anko?”
“Mwanangu kwa nini unajiua ukiwa bado maisha hujayajua.”
“Kivipi mama?”
“Umeingia kwenye msafara ya mamba bila kujijua wakati wewe ni mjusi.”
“Kivipi?”
“Leo mwanaume ni muuaji asikuue kama mimi mama yako.”
“Lakini mama Anko ndiye aliyeshikilia maisha yetu baada ya wewe kuugua.”
“Kivipi?” mama alitaka kujua.
Ilibidi nimweleze sababu ya kuwa na Anko na sababu kubwa alikuwa yeye baada ya kumtukana mbele ya mkewe na kuamua kukata misaada.
“Mama kuwa na Anko sikupenda bali ilibidi nikubali ili kuokoa maisha yako bila hivyo ningekupoteza. Pia Anko amekuwa na malengo makubwa kwangu kwa vile hakutaka kunichezea ameninunulia gari na sasa hivi na muda si mrefu nitaingia katika jumba la kifahari.”
“Mmh!” mama hakuwa na la kusema aliinama wakati huo nilikuwa nimemsogelea kwa vile kitendo cha kutoa machozi kiliniumiza sana.
“Mama najua kiasi gani nimekukosea adabu ya kutembea na mwanaume uliyewahi kuwa naye ambaye sawa na baba yangu. Lakini mama sikuwa na jinsi kuuvua utu wangu kwa ajili ya maisha yako mama yangu. Mama wewe ni kila kitu kwangu kama nitakupoteza nitakuwa mgeni wa nani.
“Hivyo basi mama naomba unisamehe nipo chini ya miguu yako, sikuwa na nia mbaya zaidi ya kutafuta njia ya kukomboa hali yetu ya maisha kibaya zaidi hali yako mama ilikuwa mbaya sana ya kutishia amani ya moyo wangu.”
“Herena mwanangu nakujua vizuri jinsi ulivyokuwa na msimamo, najua Mr Joel ametumia mwanya huo kunichanganya na mwanangu. Kwa vile mna malengo siwezi kuingilia. Vipi mkikutana mnatumia mpira?”
“Mpira kivipi?”
“Kondomu.”
“Ndiyo mama si unajua siwezi kumuamini mpaka tupime kwa vile anataka mtoto,” nilimdanganya mama kwa kujua lazima angenilaumu sana kama ningemwambia ukweli.
“Kama hivyo afadhali,” mama alishusha pumzi ndefu kitu kilichonishtua na kuuliza.
“Mbona hivyo mama?”
“A’aa kawaida, ila usikubali kufanya naye mapenzi mpaka mwenye mkapime.”
“Sawa mama.”
Maneno yangu kidogo yalimfanya mama arudi kwenye hali yake ya kawaida, japokuwa jioni ya siku ile nilitakiwa kukutana na Anko nimuomba radhi ili niwe karibu na mama. Siku ya pili mama aliamka katika hali nzuri kitu kilichonipa nafasi ya kuweza kutoka.
Mchana Anko alinipigia simu kuwa ana safari ya nje ya mkoa hivyo alinitaka mapema kwa ajili ya mipango ya safari. Nilimuaga mama ambaye muda huo alionesha hana kinyongo tena.
Nini kitaendelea? Endelea kufuatilia.
Post a Comment