Mrembo asakwa Kisa utapeli na RB 20
Mrembo Brigita Vitalis.
Imelda Mtema
AIBU! Kisa
utapeli, mrembo Brigita Vitalis, mkazi wa Mtoni Kijichi anasakwa na
polisi kwa RB 20 baada ya kudaiwa kuwaingiza chaka watu 20 ambao
waliungana na kumfungulia mashtaka Kituo cha Polisi Magomeni na kupewa
hati ya mashtaka iliyosomeka; MAG/RB/9768/2015.
Mmoja wa watu waliotapeliwa na mrembo
huyo aliyejitambulisha kwa jina la Diana alimueleza kamanda wa Kikosi
cha Kufichua Maovu cha OFM kuwa aliingizwa kwenye utapeli na rafiki yake
aitwaye Anna ambaye alimwambia kuwa kuna rafiki yake anaitwa Brigita
anawatafutia watu kazi lakini ili upate ni lazima utoe pesa.
“Kwa sababu ya ugumu wa kupata kazi
tulikubaliana na Brigita hivyo tulitoa shilingi laki mbili kila mmoja na
kazi hiyo ilikuwa ya Supermarket ya Uchumi,” alisema Diana.
Aidha Diana alisema baada ya kukaa muda
mrefu bila kuitwa alifuatilia na ndipo yeye na rafiki yake Anna
waligundua kuwa wametapeliwa kwani waliambiwa kuwa Uchumi hawajawahi
kuhitaji wafanyakazi wala hawajatangaza, wakaamua kutupia mtandaoni
picha ya Brigita na kumtangaza kwa utapeli aliowafanyia kwani
alishakusanya pesa za wengi.
Baada ya tangazo hilo waliibuka watu
wapatao 18 kila mmoja akilalamikia kuibiwa kiasi kama hicho cha fedha na
mrembo huyo ndipo wakakubaliana kuunda kundi waliloliita
‘waliotapeliwa na Brigita’ kwa ajili ya kumsaka.
“Tulikubaliana kumfungulia mashtaka na
moja kwa moja tukaenda Kituo cha Polisi Magomeni ambapo tuliandikiwa
hati ya mashtaka iliyojumuisha malalamiko ya watu wote,” alisema Diana.
Baada ya OFM kupata taarifa hizo,
walimsaka Brigita kwa mbinu zao na kufanikiwa kumpata ambapo alisema
kuwa yeye hakuwa na nia ya kuwatapeli hao watu lakini kuna kijana
aliwaambia kuwa kuna kazi Uchumi ndipo alimtaarifu Anna rafiki yake ili
awaambie ambao hawana kazi kwani hata yeye alitoa hela yake.
“Hata mimi nilitapeliwa kama wao na
aliyefanya yote haya ni kaka mmoja Mkenya hivyo naona waliofikisha
habari hii hapa wananifanyia fitna tu,” alisema Brigita pasipo kuelekeza
aliko huyo aliyemuita Mkenya.
CHANZO: RISASI JUMAMOSI

Post a Comment