Kutoka mkimbizi, babantilie, BBC hadi Azam TV -2
MTANGAZAJI
wa kimataifa, Kassim Kayira ndiye anayetupambia ukurasa huu. Anasimulia
kila kitu kuhusu maisha yake, tangu kuzaliwa hadi alipo sasa.
Ni simulizi tamu, yenye kusisimua na iliyojaa mafunzo mengi kuhusu maisha na mafanikio.
Mitihani, misukosuko,
mihangaiko, mateso na mikikimikiki aliyokutana nayo, ndiyo imekuwa
chachu na ngazi muhimu ya kumfikisha hapo alipo sasa.
Hii ni sehemu ya pili ya
simulizi hii. Wiki jana, nilieleza hatua kwa hatua tangu wakati nampokea
kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar
ambapo mazungumzo yanaanzia kwenye gari, kuelekea yaliko makao makuu ya
kituo chake kipya cha kazi, Azam TV, Ilala jijini Dar.
SASA ENDELEA…
ELIMU
“Sawa, nimekuelewa sasa, nitakupigia
tena badaye, niko na mazungumzo muhimu hapa,” anasema Kayira kupitia
simu, akimpa maelekezo mtu aliyekuwa akizungumza naye.
“Basi, kwa hiyo mimi nilianza kusoma
mwaka 1979 katika Shule ya Msingi Mbarara, lakini sikufika hata darasa
la pili, kutokana na vita iliyokuwa ikiendelea kati ya Uganda na
Tanzania, kwenye harakati za kumuondoa Dikteta Nduli Idd Amin Dadaa,
sikuweza tena kuendelea na masomo,” anasema Kayira na kunitazama sana
usoni bila kupepesa macho.
“Mmh, ikawaje sasa?,” nami najikuta nikimtupia swali bila kujali jinsi alivyokuwa akinikazia macho.
“Dah! Nakumbuka mbali sana Brighton,
historia ya maisha yangu huwa siisimulii mara kwa mara, inauma sana,”
anasema Kayira na kuendelea;
“Wazazi wangu walilazimika kuhamia
nchini Rwanda, ingawa ni nyumbani kwao na mama kama nilivyokwishaeleza
kuwa ni Mnyarwanda, lakini tuliishi kama wakimbizi, hapakuwa na furaha
niliyoizoea Uganda,” anasema Kayira.
Kayira anasema, maisha yalibadilika sana
kwani baadhi ya jamii waliwaona ni wakimbizi, licha ya mama yao kuwa
raia wa nchi hiyo, anasema kilikuwa kipindi kigumu mno. Alipotezana na
baadhi ya rafiki zake kutoka nchini Uganda, kuna waliouawa kwenye vita
na kuna waliokimbilia sehemu mbalimbali kunusuru maisha yao.
“Zilikuwa ni siku mbaya sana,
tukalazimika kuishi kwenye kambi ya wakimbizi japo ilikuwa ni kwa siku
chache mno kabla ya kupata sehemu nzuri, namshukuru sana Mungu kwa
kuninusuru na janga hilo la vita,” anasema Kayira lakini hapohapo,
namuona akiinuka kidogo na kutumbukiza mkono wake wa kuume kwenye begi
dogo lililokuwa mapajani kwake, anachomoa kitu kama karatasi yenye
michoro na maelezo kadhaa.
Bila kusema chochote, ananisogelea na kuanza kuikunjua karatasi hiyo huku akichukua kalamu yake iliyokuwa kwenye mfuko wa shati.
“Hii ndiyo ramani ya Mbarara nchini
Uganda nilikozaliwa na kuanza kusoma kabla ya kukimbia kwa sababu ya
vita,” anasema Kayira huku akinionesha kwa kutumia kalamu hiyo.
“Ok,” najibu kwa sauti ya chini na kuendelea kuitazama ramani hiyo.
“Kwa hiyo nikapelekwa tena shule, ujue
baba yangu ni mtu anayependa sana elimu, ya dunia na haswa ya dini, kama
nilivyokueleza anaitwa Alhaji Ibrahim Kayira, huyu ni Sheikh, kwa hiyo
ni kwa namna gani unaweza kuona vile baba alikuwa amekolea kwenye mambo
ya dini,” anasema Kayira kwa lafudhi ya Kiganda na kwa msisitizo zaidi.
“Nikaanza kusoma tena kwenye Shule ya
Msingi Rwanda Islamic Center au Rwandan Centre Islamique kwa Kifaransa,
lakini hata mwaka haukuisha, na mwaka 1980 tukarejea tena nchini Uganda
baada ya hali kutulia, ilikuwa ni balaa tupu,” anasema Kayira.
“Kwa hiyo nikaendelea tena kusoma Shule
ya Msingi Mbarara hadi mwaka 1983, nikahamishiwa tena nchini Kenya na
kujiunga na Shule ya Msingi Machaakos Township hadi mwaka 1987.
AREJEA TENA UGANDA KWA MASOMO YA CHUO
“Nilipohitimu masomo ya msingi nchini
Kenya, nilirejea tena nyumbani Uganda na kujiunga na shule ya sekondari
iliyokuwa chini ya Taasisi ya Kiislamu (Bilal Islamic Institute), ambapo
nilisoma kidato cha kwanza hadi cha sita, kuanzia mwaka huo wa 1987
hadi 1992,” anasema Kayira na kukohoa kidogo.
“Nilipohitimu masomo ya sekondari,
nilifaulu vizuri, lakini nikawa nahisi kama naweza kuwa mwalimu, hivyo
nikaamua kusomea ualimu na kuchukua shahada ya elimu,” anasema Kayira.
Je, nini kitafuata? Usikose kufuatilia wiki ijayo kwa muendelezo wa simulizi hii tamu ya gwiji huyu katika tasnia ya habari.

Post a Comment