ad

ad

INAWEZEKANA KABISA, KILIMANJARO STARS ISITUMIE JEZI ZA TAIFA STARS



Na Saleh Ally
KILA siku binadamu anajifunza jambo jipya, huenda jana halikuwepo au kusikika. Lakini leo mambo yanabadilika na linakuwa gumzo au linalotakiwa kufanyiwa kazi.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo ulizaa Tanzania yenye Bara na Visiwani. Hili ni jambo ambalo Watanzania wengi wamekuwa wakilipigania kuhakikisha linadumu.
Lakini kuna kitu ambacho nilikifikiria, lakini pia nikapata changamoto kutoka kwa mdau mmoja wa soka. Linahusu jezi ambazo timu zetu tatu kubwa za taifa zimekuwa zikitumia.
Tuna Taifa Stars ambayo inajumuisha Tanzania Bara na Visiwani na hii ndiyo inayobeba picha ya muungano hasa.
Taifa Stars inatuwakilisha kila tunapokwenda kushiriki mashindano yoyote chini ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na lile la Afrika (Caf).
Lakini tuna timu nyingine mbili ambazo zinakuwa wawakilishi wa Watanzania wakati wa michuano ua Ukanda wa Afrika Mashariki. Hiyo ni michuano ya Chalenji ambayo Bara wanawakilishwa na Kilimanjaro Stars huku Visiwani wakiwakilishwa na Zanzibar Heroes.
Hizi timu zinakuwa zinajitegemea kwa maana ya ukanda na Tanzania inakuwa na wawakilishi kutoka pande mbili. Jambo ambalo ni zuri kwa kuwa linatanua wigo zaidi.
Sitaki kuingia kwenye ile vita ya Zanzibar nao wamekuwa wakitaka uwakilishi upande wa Caf na Fifa. Mimi zaidi nitalenga kwa upande wa jezi, bora zikiwa za aina tatu tofauti na sasa ni aina mbili.
Wachezaji wa Zanzibar wanapokuwa pamoja wale wa Tanzania Bara, wanaunda Taifa Stars na kutumia jezi moja. Wakienda kwenye michuano ya Chalenji, Zanzibar Heroes wanakuwa na jezi zao lakini Kilimanjaro Stars wanabaki na jezi za Taifa Stars.
Hii kidogo ndiyo inanipa mkanganyiko, ndiyo maana nikaamua kuifikisha hapa kama sehemu ya mjadala. Simlaumu mtu, badala yake natamani nanyi mlifikirie hili ana kuona nini kifanyike.

Binafsi ninaona itakuwa sahihi kama kutakuwa na jezi za aina tatu tofauti. Kwa kuwa tayari zipo za Taifa Stars na Zanzibar Heroes, basi Kilimanjaro Stars ingekuwa na jezi zake zinazojitegemea kabisa.

Kwangu naona hii, kwanza italeta usawa sahihi na maana sahihi ya kuwa Tanzania ina timu tatu tofauti zenye hadhi ya kuitwa timu ya taifa. Lakini itatengeneza taswira inayoeleweka kwa kila kikosi kati ya hivyo vitatu.
Kwa sasa taswira ya kikosi cha Kilimanjaro Stars, imejificha ndani ya kivuli cha Taifa Stars, jambo ambalo ninaona si sahihi hata kidogo, kwa nia nzuri tu.

Tuaiacha Taifa Stars iendelee kujitegemea kuliko kuifanya Kilimanjaro Stars ni sawa na Taifa Stars wakati inakuwa haina wachezaji kutoka Zanzibar.

Tuwafanye wachezaji wapate hisia ya tofauti kati ya Taifa Stars na Kilimanjaro Stars kama ambavyo wanavyoipata wale wanaokwenda Zanzibar Heroes, kwa kuwa jezi pekee zinaweza kuwapa hisia hiyo, sasa wako upande upi.
Hili si kosa, huenda watu hawakuwahi kuliona kama ni muhimu sana lakini kwangu naona lina umuhimu mkubwa kuanzia kwa maana, kwenda kwa wachezaji wenyewe kwa hisia lakini pia hata thamani pia hisia za mashabiki.
Ninaamini bado wachezaji wanapaswa kujua heshima ya jezi hizo tatu. Pia bado wana kila sababu ya kujua, kufanya vizuri katika klabu, kufanya vizuri zaidi katika Zanzibar Heroes na Kilimanjaro Stars ni uhakika wa kuitumikia Taifa Stars ambayo inatubeba Watanzania wote.
Jezi haliwezi kuwa jambo gumu sana kama TFF itaamua kulifanyia kazi mara moja na kulimaliza hilo. Baada ya hapo, utambuzi na tofauti zitakuwa wazi.
Hakuna haja ya kuepuka au kuona si sahihi kwani hata majina tu ya timu zenyewe, yanaonyesha jezi zinatakiwa kuwa tatu tofauti.

Kila la kheri Kilimanjaro Stars katika michuano ya Chalenji dhidi ya Ethiopia, leo.
Powered by Blogger.