CCM yakanusha Zilizosambaa Kwamba Imekubali Kumkabidhi Maalim Seif Ikulu
Chama cha Mapinduzi CCM kimekanusha
Taarifa iliyozagaa katika Mitandao ya Kijamii kwamba Chama hicho
kimeridhia aliyekuwa Mgombea wa Urais wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad
akabidhie nchi kuiongoza kwa miaka mitano.
Akikanusha Taarifa hiyo mbele ya
Waandishi wa Habari Afisini kwake Kisiwandui Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Vuai Ali Vuai amesema taarifa hiyo ni uzushi uliotungwa ili kuwatia
taharuki WanaCCM na Wananchi kwa Ujumla.
Amesema toka kusambaa kwa Taarifa hiyo
Jana amekuwa akipigiwa simu na Watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi
kujua ukweli wa Taarifa hiyo hasa ikizingatiwa kuwa ilidaiwa kusainiwa
na Naibu huyo. “Huu ni Uzushi Mkubwa na kwamba unafaa kupuuzwa maana
hauna lengo jingine zaidi ya kuwagawa WanaCCM” Alismema Vuai.
Amesema kilichopo nikwamba CCM
inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa Marejeo kama ambavyo Tume ya
Uchaguzi ilitangaza kuufuta Uchaguzi na hivyo kurudiwa upya. Aidha Vuai
amesema kuwa tayari wamewasiliana na Wanasheria wao pamoja na wataalamu
mbalimbali ili kuwabaini waliohusika kusambaza Taarifa hizo na
kuwapeleka katika Vyombo vya Sheria.
“Tumeshafanya mawasiliano na Wataalam wetu na tukiwabaini Sheria ya Makosa ya mtandao itachukua nafasi yake” Alisema Vuai.
Katika taarifa hiyo iliyosambaa na kudai
kusainiwa na Vuai Ali Vuai ilisema kuwa Chama cha mapinduzi kimeridhia
na kukubali kumpa nchi Maalim Seif Sharif kupitia chama chake cha Cuf
kuwa ndio rais wa uchaguzi ulopita,na yeye ndio atakayeongoza serikali
ya umoja wa kitaifa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa CCM imekubali
kushirikiana na maalim Seif katika kuongoza nchi chini ya serikali ya
umoja wa kitaifa na kukubali kutoa makamo wa kwanza wa rais na nusu ya
mawaziri.
Vuai amerejea kauli yake kuwa mazungumzo
yanayofanywa na Viongozi wa Kitaifa kwa kushirikiana na Viongozi Rais
Wastaafu wa Zanzibar hayawezi kubatilisha maamuzi ya Tume ya kufuta
matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
Post a Comment