Yametimia: Magufuli apewa cheti cha urais
RAIS mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli na Makamu wa Rais mteule, Samia Suluhu Hassan, wamekabidhiwa kwa mujibu wa sheria hati za kuchaguliwa kuwa Rais na Makamu wa Rais.
Hatua hiyo ya kukabidhi hati kwa washindi ilifanywa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva jijini Dar es Salaam jana. Jaji Lubuva alisema hatua ya kukabidhi hati hizo, imehitimisha kazi za tume hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kabla ya kukabidhi hati hizo kwa Dk Magufuli na Samia, Jaji Lubuva alisema hati hiyo imeandikwa kuwa Dk John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi, kwa mujibu wa Ibara ya 38 (1) na Ibara ya 41 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1997 na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 Kifungu 35 (f) (8), unachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Pia, alisema kwa kuzingatia kanuni za sheria, Samia Suluhu Hassan amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais na sasa wanasubiri kuapishwa, baada ya Tume kumaliza kazi yake ya kuwatangaza na kuwapatia hati kisheria. Baada ya kukabidhiwa hati hizo, Dk Magufuli na Samia, walipita kuwaonesha viongozi wote waliohudhuria hafla hiyo kwa kuanza na Rais Jakaya Kikwete, viongozi wa dini, mabalozi, waangalizi na viongozi wengine.
Shukrani za NEC Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Lubuva aliwashukuru wapigakura kwani mwaka huu wamejitokeza kwa wingi na kufikia wapigakura milioni 15.3 kutoka wapigakura milioni 8.3 waliojitokeza mwaka 2010. Ufafanuzi wa Mkurugenzi NEC Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu, majimbo ya uchaguzi ambayo wananchi walitarajiwa kuchagua wabunge ni 264.
Lakini ni majimbo 256 tu, ambayo wagombea ubunge walipigiwa kura. Kwa mujibu wa Kailima, hakukuwa na uchaguzi wa wabunge katika majimbo manane, ambapo katika majimbo sita kulitokea vifo vya wagombea na majimbo mawili, kulitokea hitilafu za picha katika karatasi ya kura. Kailima alisema kata 3,957 nchini zilitarajiwa kufanya uchaguzi wa madiwani. Lakini, kata 34 hazikushiriki uchaguzi huo, ambapo nane ni kutokana na vifo vya wagombea udiwani na 26 kutokana na hitilafu mbalimbali.
Kwa upande wa uchaguzi wa urais, Kailima alisema wagombea wanane walishiriki, ambao ni Rais mteule, Dk Magufuli aliyegombea kwa tiketi ya CCM, mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, mgombea wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, mgombea urais wa ADC, Chifu Lutalosa Yemba na mgombea urais wa TLP, MacMillan Lyimo. Wengine ni mgombea urais wa UPDP, Fahmi Dovutwa, mgombea urais wa NRA, Janken Kasambala na mgombea urais wa Chaumma, Hashim Rungwe.
Kailima alisema kati ya hao, ni wagombea sita waliosaini hati ya kukubali matokeo na wawili hawakusaini, jambo ambalo kisheria halizuii kutangazwa kwa mshindi wa urais. Wagombea ambao hawakusaini hati hiyo ni Lowassa na Rungwe. Mwakilishi wa wagombea urais Akizungumza kwa niaba ya wagombea wenzake, mgombea wa ACT-Wazalendo, Mghwira alisema anakubaliana na matokeo ya uchaguzi na kuongeza kuwa hoja ya msingi ni mabadiliko, kwani lazima yaonekane na anaamini Dk Magufuli atasimamia mabadiliko hayo.
Alimtaka Dk Magufuli kuanza na suala la Katiba mpya, inayoendana na matakwa ya wananchi, kwani ndiyo chanzo cha mabadiliko katika sehemu nyingine, kama vile usawa, usimamizi wa serikali na mfumo wa uchumi ili Watanzania waache kujiita masikini. “Umoja wa kitaifa ni muhimu pamoja na kuungana kutetea fahari ya Watanzania. Nashukuru chama changu kwa kuniamini ili nisimamie ilani yetu hivyo namkabidhi Rais mteule ilani yetu ili nayo aisimamie,” alisisitiza.
Wageni Hafla hiyo ilihudhuriwa na Rais Kikwete, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda, Waziri Mkuu mstaafu Joseph Warioba, Spika mstaafu Pius Msekwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangulla. Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu John Malecela, mke wa Rais Kikwete Mama Salma na mke wa Rais mteule, Janeth Magufuli.
Pia walikuwepo viongozi wa dini, waangalizi wa uchaguzi wakiongozwa na Rais mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan, mabalozi, viongozi wa serikali wastaafu na waliopo sasa pamoja na baadhi ya wagombea urais. JK na umoja Akizungumza baadae katika hafla ya kusalimia wananchi, iliyofanyika katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba Dar es Salaam, jana, Rais Kikwete alisema Serikali sasa ina marais wawili, ambao ni yeye na Magufuli ambaye anasubiri kuapishwa Novemba 5 mwaka huu, siku ambayo yeye atastaafu.
Rais Kikwete alisema kuna watu ‘walichonga’ kuwa CCM imemeguka vipande vipande, kwamba CCM itakufa na itamfia Kikwete mikononi, badala yake haijafa. Ndipo Kikwete aliwahoji wananchi “Dua la kuku?” na wananchi wakamjibu “halimpati mwewe”. Rais Kikwete alisema katika kinyang’anyiro cha uchaguzi, walijitokeza wagombea mbalimbali ambao baada ya Dk Magufuli kushinda, wengine waliondoka kwenda kutafuta maslahi katika vyama vingine na huko wamekosa.
Aliwashukuru wana CCM kwa umoja wao, waliouonesha katika kipindi chote cha kampeni na baada ya uteuzi wa Dk Magufuli. Alisema ukitaka kujua wana CCM, ni pale inapotokea tishio kwa chama chao, vinginevyo kama hakuna tishio, wana tabia ya kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa Taifa. Rais Kikwete alisema amefurahi kwamba alipata nafasi kwa miaka 10 kutumikia Taifa.
Alisema ametumikia miaka hiyo 10 kwa kwa kadiri ya uwezo na karama zake na kuifikisha nchi ilipo sasa, anapokwenda kustaafu. “Baada ya siku chache nitakuwa Rais mstaafu, na mke wangu atakuwa mke wa Rais mstaafu na Rais atakuwa Dk Magufuli na ‘First Lady’ atakuwa Mama Magufuli,” alisema Rais Kikwete. Alimpongeza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa kuwa mbunifu wakati wote wakati akihakikisha mambo ya chama yanakwenda vizuri na kwa kufanya kazi wakati wote bila kuchoka.
“Namshukuru sana Kinana, msione vitu vinaelea, vimeundwa. Kinana ni jembe kweli kweli, ni raha kufanya kazi na Katibu Mkuu kama huyu…huo ndio ukomredi wakati wote ujue mambo yanaendaje,” alisema Rais Kikwete. Pia, alimpongeza Mbunge mteule wa Bumbuli, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kushughulikia wasanii na ujumbe ambao alikuwa akituma katika mitandao wakati wa kampeni, akishirikiana na vijana aliokuwa akiwaongoza.
Dk Magufuli Akizungumza Lumumba, Dk Magufuli alituma salamu kwa wale wote ambao waliondoka CCM wakati wa kampeni za uchaguzi, kwamba kampeni zimeisha, hivyo watubu na kurejea. “Sasa kwa sababu uchaguzi umekwisha, watubu, wajirekebishe, warudi kwenye mstari tufanye kazi pamoja tusonge mbele, ni mara kumi kuwa na mpinzani kutoka nje kuliko kuwa na mpinzani kutoka CCM,” alisema Dk Magufuli. Magufuli alitoa ahadi ya kuanza kazi mara tu baada ya kuapishwa kwa kuingia ofisini siku hiyo hiyo, kuanza kupambana na changamoto za wananchi.
Alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kumekuwa na changamoto nyingi na kwamba waliokiumiza chama hicho ni watu ambao walikuwa viongozi wa chama hicho, wakaamua kukihama. Aliwataka watendaji serikalini kufanya kazi kwa bidii na kwa wale ambao hawatatimiza wajibu wao, hatawaonea aibu. Alisema hatakuwa na msamaha na mtu yeyote ambaye atakuwa mzembe katika kuhudumia wananchi, ambao wamemuamini na kumpa nafasi ya kuwatumikia.
Dk Mafufuli alisema ameomba nafasi hiyo, sio kwa kujaribu, lakini kufanya kazi ile ambayo Watanzania wanatarajia katika kuifikisha nchi pale wanapopahitaji. Aliwashukuru wanachama wa CCM na wananchi wote waliomuamini na kumchagua na kusherehekea ushindi wake tangu juzi. Lakini, alisema kazi kubwa iliyopo mbele yake ni deni la kuwatumikia kwa moyo wote. Pia, Magufuli aliwashukuru viongozi wa kiroho ambao wamekuwa mstari wa mbele kuiombea amani nchi.
A aliwashukuru wasanii walioshiriki katika kampeni pamoja na vyombo mbalimbali vya habari. “Nataka wakafanye kazi... kwangu mimi ni Kazi Tu watanzania bila kujali vyama vyao, dini zao, makabila yao wanataka Kazi Tu … Tanzania ni Kazi Tu,” alisema Dk Magufuli. Magufuli alimwambia Rais Kikwete kuwa anaiacha nchi katika mikono yake ikiwa salama, lakini akamuomba kuwa ataendelea kumsumbua kila mara pale atakapohitaji msaada wa ushauri wake.
“Watanzania wote, kwa moyo wa dhati, nasema nina deni kubwa kwenu, la kuwafanyia kazi, ndio maana nasema muendelee kutuombea, tuendelee kutimiza na kufikia matumaini yenu,” alisema Dk Magufuli.
Magufuli alisema ni kweli walizunguka nchi nzima, kuinadi Ilani ya CCM lakini ushindi walioupata ni wa Watannzania wote, kwa sababu kuna baadhi ya maeneo, mbunge na diwani wa CCM walikosa kura za kuwawezesha kushinda, lakini walitoa kura nyingi kwa rais wa CCM. Alisema kuna kero nyingi ambazo zinawakabili Watanzania hivyo anaomba ushirikiano wa wananchi ili azitatue.
Post a Comment