ad

ad

Ukawa waibua mazito vituo vya kura

Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinachoungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Juma Duni Haji, ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuuruhusu umoja huo kufanya uhakiki wa vituo vya kupigia kura, akidai umebaini uwapo wa takriban  vituo  20,000 hewa vya kupigia kura.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mgombea Mwenza huyo wa Ukawa alidai umoja huo umebaini kuna  mbinu chafu ya kuongeza vituo hivyo ili Chama cha Mapinduzi (CCM) kiweze kupata ushindi wa goli la mkono.
Aliwaagiza wagombea ubunge na udiwani wa umoja huo kuhakiki vituo vya kupigia kura katika maeneo yao ili kujiridhisha kama vituo hivyo ni halali.
 
Alisema kilichoushtua umoja huo ni takwimu za Nec ambazo zinaeleza kuwa Watanzania watakaopiga kura ni  milioni 23.7 na kutakuwa na vituo vya kupigia kura 72,000 na kila kituo kitakuwa na  watu wasiopunguza 450.
 
Duni alisema katika hesabu ambazo wamezipitia kutokana na idadi ya wapigakura waliotajwa, kulitakiwa kuwe na  vituo takriban 53,000 na si 72,000 ambavyo tume imeeleza.
 
"Kwa hesabu hii, ukichukua idadi ya wapigakura hao milioni 23.7 ukagawanya na watu 450 ambao wanatakiwa kuwapo kwenye kila kituo, utaona vituo vilipaswa viwe 53,000. Hizi ni njama za goli la mkono, unaweza kudanganya vyovyote lakini  namba ukitaka kuidanganya haikubali," alisema na kuongeza:
 
“Kwa vituo 72,000 kulitakiwa kuwe na wapigakura milioni 32.4, ambapo katika sensa ya 2012 Watanzania walikuwa milioni  44.92 na kwasasa inakadiriwa kuwa na watu milioni 48, haiwezekani watu milioni 32 wakapiga kura.”
 
"Hapa unaona kabisa watu milioni tisa hawapo, hapo ndiyo goli ya mkono, wakati Lowassa anaanza na kura sifuri Magufuli anaanza na kura milioni 9 hilo ndiyo goli lenyewe, tunataka tume waturuhusu tufanye uhakiki tujiridhishe kabla ya kwenda kwenye uchaguzi."
 
Alisema umoja huo umeshtukia mchezo huo na hautakubali mchezo huo ujirudie  tena, akidai mwaka 2010 walijiandikisha watu milioni 20 lakini waliopiga kura ni milioni 8.6 ambapo Rais Jakaya Kikwete alishinda kwa kura milioni 5.7 sawa na 61.7.
 
“Haiwezekani watu milioni 12 wawe hawakupiga kura halafu Kikwete akapewa ushindi wa zaidi ya asilimia 50 ambayo hajafikia idadi ya wapigakura kura waliojiandikisha,” alisema.
 
"Ni vyema Jaji Lubuva akae na sisi atueleze kwanini iwepo namba hii na wagombea wetu nawaagiza mkafanye uchambuzi wa vituo 72,000 maana isije ikawa mkono wa kushoto unapewa halafu wa kulia unaminywa."
 
Duni alisema Ukawa watakuwa tayari kuueleza umma ambacho tume itakuwa haijakieleza kwani wao ni mawakala wa wananchi.
 
NEC YATOA UFAFANUZI
Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani Kailima, alisema idadi ya vituo vya kupigia kura iliyotolewa ilikuwa ya awali, kwani tume hiyo bado haijakamilisha mchakato wa ugawaji vituo ili kutoa idadi kamili.
 
Alisema mara baada ya mchakato huo kukamilika wiki ijalo, Nec itatoa idadi kamili ya vituo vyote vitakavyotumika kupigia kura na inaweza kupungua au kuzidi idadi iliyotolewa awali.
 
Alisema wingi wa vituo hivyo ni maalum kwa ajili ya kukabiliana na msongamano wa wapiga kura, ambapo tume imewagawa   katika vituo vidogo vidogo ndani ya kituo kikubwa kimoja, huku akitolea mfano kuwa endapo kituo kimoja kina idadi ya watu 4,000 basi watagawanywa katika makundi ya watu 450 kwa kila kituo.
 
Alisema wapiga kura watarajie uwapo wa vituo vingi vya kupigia kura kuliko vituo walivyojiandikishia ili kukabiliana na msongamano ambao unaweza kuzuilika kwa utaratibu huo.
 
Kailima aliwataka wagombea kuendelea kunadi sera zao na kuwaondoa hofu kuwa kila chama na kila mgombea atapatiwa idadi ya vituo na idadi ya wapigakura.
 
"Wasiingilie masuala ya kitaalamu maana wataumbuka, wasubiri tutawapatia orodha ya wapiga kura na vituo kwa kila chama, wagombea waendelee tu kunadi sera zao," alisema Kailima.
 
Akizungumzia kuhusu mikutano yake ya kampeni, Mgombea huyo mwenza wa Ukawa alisema mpaka sasa ametembea katika majimbo 130 na amekutana na wananchi wengi wanaohitaji mabadiliko kutokana na kuchoshwa na uongozi wa CCM.
 
"Naongea bila kificho wala kuonea aibu na si mambo ya kisiasa watu wanataka mabadiliko, kuna dhana kuwa wanaotaka mabadiliko ni watu wa mjini, kuna vijiji nimeenda huko hata viongozi hawajawahi kufika...wananchi wanataka mabadiliko viongozi wa serikali wasilazimishe mambo vinginevyo wanaweza kuleta machafuko," alisema.
 
Duni alisema amekutana na wananchi wakilalamika matatizo mbalimbali ikiwamo kero ya maji maeneo mengi mijini na vijijini, shule hazina madawati na vyoo,  zahanati  hazina dawa au vifaa au ipo mbali na makazi ya wananchi na barabara nyingi ni mbovu.
 
Alisema matatizo mengine ni manyanyaso kwa watu wanaoishi karibu na mbuga za wanyama wanachukuliwa kama wakimbizi, wanapigwa, wanateswa na kutolea mfano katika eneo Liwale, mkoani Lindi.
 
Hata hivyo, alisema pia kuna kodi nyingi na  michango mingi kwenye sekta ya elimu na mageti ya ushuru wa mazao.
 
AMPONDA MAGUFULI
Duni aliponda ahadi inayotolewa na mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, kuwa akichaguliwa kuwa Rais ataanzisha mahakama ya kushughulikia mafisadi,  hana nguvu za kikatiba kufanya hivyo.
 
KIGAILA
Kwa upande wake, Mgombea ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini (Chadema), Benson Kigaila, alisema wanafunzi wa vyuo vikuu wamepewa likizo ya wiki mbili waende nyumbani ili wasipige kura na kudai hizo ni dalili za goli la mkono.
 
CHANZO: NIPASHE
Powered by Blogger.