ad

ad

SINGIDANI (A Story From My Heart) - 34



ILIPOISHIA...
Mchungaji Massawe alianza kwa kumwuliza Chris: “Christopher Joseph Shila, upo tayari kuoana na huyu Laura John Ngeleja awe mke wako, ushirikiane naye katika shida na raha, hadi kifo kiwatenganishe? Kama ndivyo, sema ndiyo Mungu anisaidie.”
Chris hakujibu kitu!
SASA ENDELEA...
HISIA kali ilimshika Chris. Ni kama alikuwa kwenye ndoto ya kusisimua. Hakuamini kama ni yeye alikuwa mbele ya kanisa akiwa amevaa suti kali nyeusi na shati jeupe huku shingoni akiwa amevaa tai fupi nyekundu!
Laura alitingisha! Alivaa gauni jeupe na shela iliyoburuzika hadi chini. Furaha ikamfanya asahau kuwa yupo kanisani na alitakiwa kujibu swali la Mchungaji ili kukamilisha uhalali wa ndoa yao.
Kanisa zima lilikuwa kimya. Wengine walianza kuogopa, wakahisi  huenda Chris aliamua kubadilisha mawazo. Kwamba aliamua kuachana na suala la ndoa na Laura.
Haikuwa hivyo.
Chris alimpenda sana Laura, alichanganywa na tukio lililokuwa mbele yake ambalo lilikuwa kama sinema ya kusisimua.
“Christopher...” Mchungaji akaita.
“Naam!”
“Hujaona sehemu ya kusoma kijana wangu?” akauliza Mchungaji.
“Nimeona.”
“Sawa, nami nitakuuliza tena: “Christopher Joseph Shila, upo tayari kuoana na huyu Laura John Ngeleja awe mke wako, ushirikiane naye katika shida na raha, hadi kifo kiwatenganishe? Kama ndivyo, sema ndiyo Mungu anisaidie.”
“Ndiyo Mungu anisaidie,” akajibu Chris.
Ukumbi mzima ukalipuka kwa shangwe na nderemo. Matarumbeta nayo hayakuwa nyuma, yalisikika yakipulizwa na hivyo kuamsha shangwe ukumbini humo.
Mchungaji akamgeukia Laura kisha akamwuliza: “Laura John Ngeleja, upo tayari kuoana na huyu Christopher Joseph Shila awe mume wako, ushirikiane naye katika shida na raha, hadi kifo kiwatenganishe? Kama ndivyo, sema ndiyo Mungu anisaidie.”
“Ndiyo Mungu anisaidie,” akajibu Laura.
Kelele zikazidi kuwa kubwa, kanisa zima lilishangilia. Ilikuwa furaha kwa wote. Zoezi lililofuata baada ya hapo ilikuwa ni kuvalishana pete.
Ndoa ikawa imefungwa!
Chris na Laura wakawa mume na mke rasmi.
***
Sherehe ilikuwa katika Ukumbi wa Mlimani City. Hiyo ilikuwa ni baada ya maharusi na ndugu wengine kuzunguka sehemu mbalimbali za jiji na kupiga picha.
Waandishi wa habari walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanapata picha nzuri za kupamba magazeti yao. Chris kuoa ilikuwa habari kubwa sana kwa magazeti Pendwa Bongo.
Waandishi na wapigapicha maarufu, Issa Mnally, Richard Bukos na Shakoor Jongo walikuwa wanashindana kutafuta picha bora zaidi ambayo ingependekezwa kutokea kwenye ukurasa wa mbele wa Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.
Achana na hao, wapigapicha wa magazeti mengine ya kila siku na michezo walipigana vikumbo kupata picha nzuri. Msanii wa Bongo Muvi kuoa halikuwa jambo dogo!
Ndani ya Ukumbi wa Mlimani City, wasanii walikuwa wengi sana. Walialikwa watu maalum tu. Viongozi kadhaa wa kiserikali walikuwemo, wabunge, mawaziri, wakuu wa wilaya na madaktari.
Ilikuwa sherehe yenye heshima kubwa sana. Chris alijisikia mwanaume kamili kati ya wanaume. Wapambe wao walikuwa ni wasanii wa filamu, Jaybee na mkewe Vanessa.
MC wa shughuli hiyo alikuwa ni Chika, ambaye siku zote amekuwa akiongoza hafla mbalimbali za wasanii na watu wengine. Kwa Chris ilikuwa siku mpya ya kipekee ambayo ilikamilisha haja ya moyo wake.
Wenye kunywa walikunywa sana. Chakula kililiwa hadi kikabaki. Fungakazi ilikuwa zawadi, watu walitoa zawadi nyingi sana, achilia mbali wazazi wa pande zote ambao waliwazidi wote.
Alianza mzee Shila: “Umefanya kitu kikubwa sana mwanangu. Leo umenifanya nijisikie baba yako kamili. Nakupenda sana mwanangu. Kuhusu namna ya kuishi na mwenzako tumeshazungumza mengi, najua umeyashika.
“Kuna kitu ambacho nataka kukisema mbele ya watu wote hapa. Kwa tendo hili, nasema kwamba nimebadili fikra zangu. Nilichukia sana mwanangu kutokuoa mapema, lakini sikutaka kusikia anaoa mjini.
“Akilini mwangu niliamini wasanii wote ni wahuni, wana tabia mbaya na ni watu wasiofaa kwenye jamii. Kumbe nilikuwa nawaza tofauti. Nikadhani mke sahihi lazima atokee kijijini, kumbe siyo kweli.
“Leo hii mwanangu amepata mke mwema, sahihi na mzuri ambaye atamsaidia kama vitabu vinavyosema. Ninawabariki wanangu, mkaishi kwa amani na upendo. Kuanzia sasa, sina kinyongo na kazi ya mwanangu Chris. Pamoja na kwamba nilikulazimisha kusomea udaktari, nashukuru unaifanya kazi hiyo vizuri.
“Unasaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi kupitia taaluma yako. Wakati ukifanya yote hayo, bado pia unafanya sanaa kama sehemu ya kipato na fani uliyoichagua na kuipenda.
Kuhusu zawadi, najua una gari la kutembelea, lakini mimi nimekununulia jingine, litakalofanana na hadhi yako ya ubaba, maana sasa umekuwa baba. Nimekununulia Toyota Range Rover, iko hapo nje. Funguo zake hizi hapa,” akasema mzee Shila na kwenda kumkabidhi.
Shangwe zikaibuka upya!
Chris alipokea funguo za gari, kisha akanyanyua mkono juu na kuwaonyesha wageni ukumbini. Ghafla akagonganisha macho na mtu ambaye hakutarajia kabisa kumuona!
Chris alishtuka sana!

Powered by Blogger.