ad

ad

SINGIDANI (A Story From My Heart) - 32



 

 “Potelea mbali fedha nilizopoteza, lakini safari hii nitaongozana na wewe hadi kijijini na nitahakikisha unaoa mwanamke kutoka kijijini!” Akasema mzee Shila kwa hasira.
SASA ENDELEA...
CHRIS alichanganyikiwa sana, alimwangalia baba yake akiwa haamini kabisa kama tayari alikuwa ameshajua kila kinachoendelea. Alihisi kichwa kumuuma sana.
Alibaki amesimama palepale akimwangalia baba yake. Ndoa yake na Laura ilikuwa inayeyuka, jambo ambalo hakutaka kabisa litokee.
“Una jipya la kuniambia?” Mzee Shila akauliza kwa hasira.
“Baba tuliza hasira kwanza. Nahitaji kuzungumza na wewe.”
“Sitaki mazungumzo na wewe, naomba uondoke haraka sana mbele ya macho yangu. Toka tafadhali,” akasema mzee Shila kwa hasira.
Chris hakuwa na cha kufanya zaidi ya kuondoka. Baba yake alikuwa amekasirika katika kiwango cha mwisho kabisa. Aliingia garini kisha akapiga gia hadi nyumbani kwake Kijitonyama.
Alifikia sebuleni na kujitupa kwenye sofa kubwa, akijaribu kutafakari. Macho yake tayari yalishaanza kulengwalengwa na machozi. Bila hiyari yake akajikuta akianza kulia.
Hakuwa na msaada wowote kwa wakati ule. Alisimama ghafla na kuelekea kwenye jokofu kisha akatoa bia moja na kuifungua, akiwa palepale mbele ya jokofu lake, aliimimina kinywani mwake yote ikaishia humo!
Aliposhusha chupa, ilikuwa tupu kabisa. Akachukua bia nyingine, akafanya vilevile kisha akachukua tena ya tatu, safari hii akatembea hadi kwenye sofa na kuketi.
Akaendelea kunywa!
Ni kama alikuwa amechanganyikiwa kabisa. Jambo lile lilimuumiza sana na aliona kama dunia yote ilikuwa ikimuangukia yeye.
Amkose Laura?
Ni jambo ambalo hakutaka kabisa kuliruhusu litokee. Alihisi mwili wote ukitetemeka. Akiwa katika hali ile, akapata wazo la ghafla. Aliona usalama wake ulikuwa kwa mzee Ngeleja.
Lilikuwa wazo alilolipitisha moja kwa moja. Haraka akachukua simu kisha akabonyeza jina la mzee Ngeleja na kumpigia! Simu haikuita muda mrefu, tayari mzee Ngeleja alikuwa hewani!
“Shikamoo baba,” Chris akasalimia kwa heshima.
“Marahaba mwanangu, vipi mnaendeleaje na maandalizi huko?”
“Mambo yameharibika.”
“Kuna nini? Hebu niambie mwanangu, acha kuniweka roho juu mimi na huu utu uzima.”
“Baba amegundua kila kitu. Amejua mchezo wote. Amefahamu kuwa Laura siyo Mnyiramba. Hataki kusikia ndoa tena, amesema ataongozana na mimi hadi kijijini akanitafutie mke yeye mwenyewe!” Akasema Chris huku akilia.
Kimya cha sekunde kadhaa kilipita. Mzee Ngeleja alibaki kimya huku sauti ya kilio cha Chris ikisikika kwenye simu. Baadaye mzee Ngeleja akaanza tena kuzungumza...
“Mwanangu kwanza nataka kukuambia, ni afadhali jambo hilo limetokea!”
“Afadhali? Kwa nini baba?”
“Ingewasumbua sana baadaye!”
“Kwa hiyo mzee uko tayari kuona ndoa yangu na Laura inayeyuka?”
“Kwanza nataka kukutia moyo mwanangu. Hakuna ndoa inayoyeyuka hapo. Kwanza tayari ninyi ni wanandoa halali, maana mmefunga ya kimila. Hilo ondoa shaka kabisa.
“Jingine ni kwamba, hilo ni jambo dogo sana ambalo lipo ndani ya uwezo wangu. Najua naweza kulishughulikia.”
“Kivipi baba? Utafanyaje wakati wewe uko huko mbali?”
“Kesho nakuja Dar, naomba uwe na amani. Kwa sasa jambo hili lifanye siri kabisa. Usimwambie hata Laura kama kuna kitu kama hicho kimetokea.”
“Sawa baba.”
“Ok! Siku njema, naomba uwe na amani.”
“Ahsante.”
Wakakata simu zao.
Angalau sasa Chris alihisi amani moyoni mwake. Aliendea kunywa akiwa na matumaini ya ndoa yake kufungwa baada ya mzee Ngeleja kuahidi kumsaidia.
***
Saa 10:00 alasiri, mzee Ngeleja akiwa ameongozana na mchungaji wa kanisa lililotarajiwa ndoa ya Laura na Chris kufungwa na mwenyeji wao Chris, walikuwa mbele ya geti la mzee Shila, Mbezi Beach.
Kwa bahati nzuri, mzee Shila mwenyewe alikuwepo ndani. Chris aliwakaribisha na wote wakaingia hadi ndani. Sebuleni walimkuta mzee Shila amekaa na mkewe.
Aliwakaribisha kwa hofu akiwa hajui ni akina nani na walichofuata nyumbani kwake. Kwa utulivu mkubwa, mzee Ngeleja aliketi, kisha mchungaji.
“Karibuni jamani,” akasema mzee Shila akionesha wasiwasi kidogo.
“Ahsante, nafurahi tumewakuta, tena wote kwa pamoja. Labda tujitambulishe, mimi naitwa mzee Ngeleja natokea Mwanza, ni baba mzazi wa Laura ambaye kwa wewe unamfahamu pia kwa jina la Njile, mchumba wake na Chris,” mzee Ngeleja akasema kisha akatulia kidogo.
Mzee Shila akatoa macho, hakuweza kuzuia hasira yake.
“Nimeongozana na mchungaji Samatta, huyu tumempitia mimi na Chris kanisani wakati tunakuja hapa nyumbani,” akasema kwa hekima sana mzee Ngeleja.
“Karibuni sana.”
“Ahsante. Kikubwa ni kuhusu vijana wetu, nimetoka Mwanza kwa ajili ya jambo hilo. Nahitaji tuweke haya mambo sawa!” Akasema mzee Ngeleja.
“Mchungaji nakuheshimu sana, mzee mwenzangu nakuheshimu pia, lakini sijaona mtu wa kubadilisha maamuzi yangu. Nilichoamua nimeamua,” akasema mzee Shila.
“Lakini mume wangu...” akadakia mama Chris.
“Kaa kimya! Wakati wanaume wanazungumza unatakiwa kufunga bakuli lako!” akasema mzee Shila kwa ukali.

Itaendelea kesho.

Powered by Blogger.