ad

ad

Singidani (A Story From My Heart) - 21



ILIPOISHIA...
Mwanga wa ndoa yake na Laura ulionekana wazi kabisa. Moyo wake ukagubikwa na furaha ya ajabu. Haikuwa kazi ngumu tena kupata usingizi. Kilichobaki ilikuwa ni utekelezaji tu!
SASA ENDELEA...
DK. Chris aliandika maneno fulani kwenye kadi alilokuwa nalo mkononi kisha akayarudisha tena macho yake kwa mgonjwa aliyekuwa ameketi mbele yake. Alikuwa mwanamke anayeelekea kuwa na umri si zaidi ya miaka 30. Alikuwa mpole, mkimya na anayeonekana kuhitaji huduma ya haraka sana. Hiyo ilikuwa ni muda mfupi baada ya kwenda maabara kutoa vipimo
. Aliitwa Sandra.
“Kuna tatizo kwenye mkojo wako. Una maambukizi. Kitaalamu tunaita Urinary Tract Infection, kwa kifupi UTI. Pia una malaria kali. Kwa namna hali yako ilivyo, ni lazima tukulaze ili tukuanzishie drip za kwinini mara moja ambayo inaweza kutibu malaria vizuri na haraka zaidi. Nitakupa na Antibiotics kali kwa ajili ya UTI.
“Hata hivyo lazima uwe makini sana matumizi ya vyoo, ambavyo hasa ndiyo chanzo kikuu cha maambuzi ya UTI. Pole sana Sandra,” alisema kwa sauti tulivu sana Dk. Chris.
“Ahsante dokta.”
“Ngoja nimuite sista aje kukuchukua,” akasema Dk. Chris.
Akainua mkonga wa simu iliyokuwa mezani kisha akabonyeza namba fulani na kuanza kuzungumza na upande wa pili. Muda mfupi baadaye alifika na  kukabidhiwa kadi la Sandra, kisha akaongozana naye wodini. Mgonjwa mwingine akaingia.
Ndivyo siku ya Dk. Chris ilivyokuwa kazini kwake, Hospitali ya Kinondoni siku hiyo. Ilikuwa siku ambayo alidili na wagonjwa wa kawaida tu. Hakuwa na ratiba ya upasuaji siku hiyo.
***
Ilikuwa lazima apange safari ya Singida haraka iwezekavyo. Baba yake mzee Shila asingemwelewa hata kidogo kama angeendelea kuchelewa kuoa. Tayari alishatengeneza mazingira mazuri ofisini kwake.
Ni muda ambao hata Laura naye alikuwa ameshafunga chuo baada ya kumaliza mitihani. Ilikuwa ni kipindi cha likizo fupi ya wiki mbili. Hizo zilitosha kabisa kukamilisha mpango waliokubaliana.
Chris alisafiri hadi Singida ambapo alikutana na Laura na kuweka mipango yao sawa. Hakuwa na hofu tena, alishaamini kabisa kuwa Laura hakuwa mke wa mtu kama alivyojulishwa awali.
Hata hivyo kwa hofu ya usalama wake, hakuwa tayari kukutana naye katika hoteli ileile ya awali. Alifikia hoteli nyingine iliyokuwa nje kidogo ya mji.
“Laura unanipenda kweli? Kumbuka hapa nakwenda kufanya usaliti lakini ni kwa ajili ya penzi letu.”
“Najua baba, nakupenda, niamini.”
“Ahsante mama, sidhani kama tunatakiwa kutoka, maana kesho asubuhi tunakwenda kijijini. Mipango yote nitakuambia hukohuko, sawa mpenzi wangu?”
“Nimekuelewa baba.”
Walilala wakiwa na matumani makubwa ya kufanikisha mpango uliokuwa mbele yao; mpango wa ndoa. Safari haikuwa mbali sana.
Ni kesho tu!
***
Walishuka katika kituo cha Ibaga saa kumi jioni ikiwa ni safari ya takribani saa tano kutoka Singida Mjini hadi hapo katika mji mdogo wa Ibaga.
Kama miundombinu ingekuwa mizuri, ni safari ya saa mbili tu tena kwa mwendo wa kawaida. Walikuwa wachovu sana kwa safari hiyo. Walitafuta nyumba ya wageni na kulipia. Hapo ndipo filamu ilipotakiwa kuanza rasmi.
“Lazima mavazi yako yabadilike sasa, utavaa zile nilizokununulia mjini. Unapaswa kufanana na watu wa huku. Mchezo ulivyo ni kwamba, leo mimi nitakwenda nyumbani - Mkalama, wewe utalala hapa hadi kesho.
“Nitakwenda kuzungumza na baba mdogo ambaye anajua kila kitu kuhusu wewe, halafu yeye atazungumza na bibi kwamba, wewe utakuja kututembelea. Pale ndiyo sehemu ya kuchukua pointi, usilaze damu, ujitahidi kuendana na kila kitu cha pale nyumbani.
“Kwa bahati nzuri, hakuna shida sana, halafu kipindi hiki si cha kilimo kwa hiyo hawatakupeleka shamba. Kifupi uonyeshe heshima na mwonekano wa mtu wa kijijini usiyejua mambo ya mjini sana.
“Lakini itabidi tudanganye kuwa, hufahamu vizuri lugha yetu kwa sababu wazazi wako walihamia Mwanza tangu ukiwa mdogo lakini sasa wameamua kurudi tena kijijini. Mambo mengine utaniachia mimi.
Umenipata?” akasema Chris.
“Nimekuelewa vizuri sana.”
Mpango mzima ukawa umekamilika, ilibaki utekelezaji tu!
***
Chris alikodi baiskeli kutokea Ibaga hadi Mkalama, kijijini kwao. Alifika baada ya nusu saa tu. Alipokelewa vizuri na baba yake mdogo ambaye alimpa mpango mzima ulivyokuwa.
“Wazo zuri sana Chris, acha nizungumze na bibi. Naamini naye atafurahi. Hatajua mchezo wetu na inabidi iwe siri yetu tu,” akasema Shamakala.
“Sawa baba mdogo.”
“Zoezi linafanyika lini?”
“Hakuna kusubiri, ni kesho tu baba mdogo.”
“Sawa.” Itaendelea
Powered by Blogger.