ad

ad

Singidani (A Story From My Heart) - 20



 

Waliendelea kupungiana mikono mpaka gari lilipofika mbali. Chris akaenda kwenye maegesho, akaingia kwenye gari lake, akaondoka. Ilikuwa safari ya kuelekea kazini kwake. Saa 3:00 asubuhi hiyo alikuwa na kazi ngumu sana ya kumfanyia mtu upasuaji mkubwa!
SASA ENDELEA...
USO wa mzee huyu ulionyesha dhahiri kuwa hauna masihara; alitaka kujua jambo moja tu tena lenye hakika kutoka kwa mwanaye. Alitaka kujua kuhusu ndoa. Chris alitulia akimwangalia baba yake, kichwani akitafakari ni jibu gani lingemfaa baba yake.
“Chris niambie ukweli, umefikia wapi?” baba yake akamwuliza.
“Baba nilishakuambia kuwa lazima nitaoa mwaka huu kwa sababu tayari nimeshapata mchumba.”
“Sasa mbona unachelewesha mambo?”
“Si kuchelewesha baba, ni suala la mipango tu. Nipe muda.”
“Muda gani?”
“Miezi miwili inatosha kabisa, nipatie muda huo baba nitakamilisha hili suala.”
“Nataka iwe hivyo.”
Mzee Shila, baada ya kuzungumza hayo, alitoka haraka na kuelekea chumbani kwake, sebuleni alibaki Chris na mama yake tu. Waliangaliana kwa muda, kisha kila mmoja akajikuta akiinamisha uso wake chini.
“Lakini mwanangu, kwa nini usioe ili kuachana na haya manenomaneno ya baba yako?”
“Mama kwani nimekataa kuoa? Si tayari nimeshasema nimepata mchumba mama, kikubwa hapo ni muda tu.”
“Sawa.”
“Mama ngoja mimi niondoke, nina ratiba nyingi sana kesho asubuhi. Acha tu niende sasa,” akasema Chris akimtulizia macho mama yake.
“Sawa baba, usiku mwema.”
“Nanyi pia.”
***
Kichwa kilitaka kupasuka. Alitulia kitandani mwake akiwaza sana, dalili za kumpoteza mrembo Laura zilianza kuonekana waziwazi. Alitamani sana kumuoa Laura, hakuwa mwanamke wa kucheza naye kwa usiku mmoja tu!
Laura alikuwa mke!
“Lakini itawezekanaje wakati mzee naye analazimisha mke atokee kijijini?” akawaza Chris.
“Kuna kitu natakiwa kufanya hapa, lazima nimpate Laura maishani mwangu, siwezi kukubali akaolewa na mwanaume mwingine, haitawezekana hata kidogo,” akazidi kuwaza Chris.
Akiwa mawazoni, simu yake iliita. Haraka akaichukua na kuangalia kwenye kioo; akakutana na jina la Laura lilitokea. Akapokea haraka sana...
“Haloo mpenzi wangu...” sauti tulivu ya Chris ilitoka.
“Yes darling, za huko?”
“Nzuri tu mama. Unaendeleaje huko?”
“Nipo vizuri tu, nimekukumbuka mpenzi, hata usingizi umekata kabisa.”
“Kweli mpenzi?”
“Kweli kabisa.”
“Nataka kuuliza kitu dear maana naona dalili mbaya.”
“Dalili mbaya za vipi mpenzi?”
“Kuhusu mapenzi yetu.”
“Mh! Mbona sikuelewi? Hebu niulize.”
“Unanipenda kweli mama?”
“Nakupenda sana.”
“Unakumbuka nilikuambia nini kuhusu mzee wangu?”
“Nakumbuka.”
“Sasa hapo ndipo kwenye tatizo. Baba ameendelea kushikilia msimamo kuwa nioe mwanamke kutoka kijijini kwetu. Kuna kitu tunatakiwa kufanya mpenzi wangu ili tuweze kufanikisha jambo hili.”
“Mh! Kweli kuna kazi, kwa hiyo hutanioa Chris kwa sababu hiyo? Kumbuka mimi nakupenda na nimekuwa tayari kufanya kila kitu kwa ajili yako. Sipo tayari kukupoteza.”
“Najua, ndiyo maana nimekuambia, kuna jambo inabidi lifanyike ili tufanikishe.”
“Ni jambo gani mpenzi wangu?”
“Nimeshamwambia baba kuwa nimepata mchumba kijijini, sasa unachotakiwa kufanya.
Itabidi nikazungumze na baba mdogo kuhusu jambo hili ili wewe uende kijijini, ukakae kwa muda, mzee ajue unatokea kule. Lengo langu ili mambo yaweze kwenda bila matatizo, itawezekana kweli mpenzi wangu?” akasema Chris.
“Kwa nini ishindikane wakati nakupenda baba?”
“Sasa itakuwa lini?”
“Panga wewe. Wiki mbili zijazo tunamalizia muhula, tunafunga chuo kabla ya kurudi tena kumalizia chuo kabisa.”
“Safi kabisa, ngoja nijipange ndani ya muda huo mama. Vipi, nyumbani hakutakuwa na tatizo?”
“Hapana, nitajua cha kufanya. Niamini mimi.”
“Sawa mpenzi wangu, angalau sasa nina amani. Naweza kupata usingizi wangu vizuri nashukuru sana mama, usiku mwema.”
“Nawe pia.”
Mwanga wa ndoa yake na Laura ulionekana wazi kabisa. Moyo wake ukagubikwa na furaha ya ajabu. Haikuwa kazi ngumu tena kupata usingizi. Kilichobaki ilikuwa ni utekelezaji tu!
Itaendelea
Powered by Blogger.