Ray, Aunt msiyumbishwe, kila mtu ana uhuru wake
KWENU wakali wa filamu Bongo, Vincent Kigosi ‘Ray’ na Aunt Ezekiel. Mambo vipi? Vuguvugu la uchaguzi mnalionaje?
Binafsi namshukuru Mungu. Mambo yanakwenda vizuri katika ubora wake na leo imekuwa siku njema kwangu kuzungumza nanyi kupitia barua maana siku nyingi kidogo hatujaonana kutokana na ubize wa majukumu.
Dhumuni la barua hii ni kutaka kwanza kuwasalimu lakini baada ya salamu nataka nizungumze nanyi kuhusu suala zima la uchaguzi mkuuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu. Kutokana na imani ya wengi kwamba ninyi mnawaunga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), watu wamezua maneno.
Nimefuatilia katika mitandao ya kijamii, baadhi ya watu wameonesha kwamba hamkuwa sahihi kuonesha mmehamia CCM. Wengi walipenda mbaki katika umoja huo ambako wanaamini ndiko kwenye mabadiliko.
Ndugu zangu, msiwaamini maana bahati mbaya zaidi tunaona watu wengi wanataka mabadiliko ukiwauliza kwa nini wanataka mabadiliko wanakosa jibu la moja kwa moja. Wanafikiri hayo mabadiliko yatakuja kama vile kushushwa kutoka mbinguni pasipo kujua mabadiliko yanaanza na wewe mwenyewe.
Kujituma katika ndoto yako, kuwa na malengo na kufanya kazi kwa bidii. Ray na Aunt ninyi ni watu wazima, sitaki kuamini kwamba hamna upeo wa kupima sera za wagombea hivyo kama kweli mlikuwa Ukawa lakini mkaona uelekeo si mzuri basi pia ni jambo la heri kwenda kule mnakoona kunafaa.
Msikubali kuyumbishwa. Maana kipindi hiki huwa kila mtu anasema lake. Kuna ambao wanadai mmetumika, lakini kwangu haiingii akilini maana si ninyi tu bali wasanii wenzenu wengi walishafanya chaguo la kuwa CCM na hakuna aliyewalaumu.
Mbona wamehama viongozi wengi tu vyama na kwenda katika vyama vingine na hawakulalamikiwa?
Edward Ngoyai Lowassa aliyekuwa Chama cha Mapinduzi (CCM), amehamia Chadema na kugombea urais, achilia mbali viongozi wengine walioachia ngazi katika Ukawa na kubaki bila chama. Uzuri katika kipindi hiki cha kampeni, mtu unaweza kuguswa na sera za kiongozi fulani na kuona yule uliyekuwa unamuamini hafai hivyo unahama. Ndiyo maana kukawa na kipindi hiki cha kampeni, wagombea wanapata nafasi ya kutoa sera zao, kunadi ilani za vyama na mikakati yao pindi watakapokuwa viongozi.
Yawezekana kabisa ninyi mliangalia suala hilo kwa makini. Mkapambanua mambo kwa hoja na kuona hamko katika njia salama, mkaamua kurudi CCM mkiamini kuna mwanga mzuri kisera, ilani na hata mikakati kwa nini tusiheshimu maamuzi yenu?
Hata watu wakiponda kwamba mmetumika, acha waseme, fanyeni kazi zenu huku mkisimamia sera za upande ambao mnauamini. Ni matumaini yangu mtakuwa mmenielewa, niwatakie kazi njema!

Post a Comment