Lowassa kufumua mikataba ya gesi, mafuta
Mgombea
urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa,
amesema akichaguliwa na kuingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu Oktoba
25, atahakikisha kuwa mikataba yote ya gesi na mafuta inapitiwa upya
ili kuhakikisha kuwa kweli inawanufaisha Watanzania na siyo wawekezaji
wa kigeni peke yao.
Lowassa anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha
Wananchi (CUF), aliyasema hayo jana mbele ya maelfu ya wananchi
waliojitokeza kusikiliza kampeni zake kwenye viwanja vya Mashujaa mjini
hapa jana.
Alisema kwa kuanzia, ataunda tume ya kuchunguza upya mikataba ya gesi na mafuta.
Lowassa aliongeza kuwa anafahamu kiu ya wananchi wa Mtwara
kuhusiana na namna wanavyokerwa juu ya kunufaika na rasilimali hizo
ambazo ni chachu kubwa ya maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla na
pia ndoto yao ya kutaka wanufaike na rasilimali hizo.
Alisema wakazi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla, hawapaswi kuwa
maskini kutokana na kuwa na rasilimali nyingi kama gesi na mafuta na
kwamba akiingia madarakani atahakikisha maisha ya kila mwananchi
yanapiga hatua za kimaendeleo katika kila nyanja.
“Kama mkinichagua, kila Mtanzania atanufaika... kama alikuwa
anakula milo miwili basi iongezeke na kuwa mitatu. Na kama anamiliki
gari moja basi awe na magari mawili. Nataka kuwa Rais wa nchi hii kwa
sababu nimechoshwa na umaskini wa taifa na wananchi wake,” alisema
Lowassa.
Kadhalika, Lowassa alirudia pia ahadi yake ya kuwaboreshea
mazingira mazuri ya kazi madereva wa bodaboda na wafanyabiashara ndogo
ndogo maarufu kama machinga na kina mamalishe.
Wote hao aliwatambulisha kuwa ni marafiki zake na kwamba iwapo
atachaguliwa kuwa Rais, atahakikisha hawabughudhiwi katika kazi zao bali
wanasaidiwa ili nao wainuke kiuchumi.
Alisema anafahamu ugumu na changamoto wanazokumbana nazo ambazo kwa
kiasi kikubwa zinachangiwa na serikali iliyopo madarakani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), akisisitiza kuwa wahifadhi vizuri shahada zao za
kupigia kura na kujitokeza kwa wingi kumchagua ili awatumikie.
SUMAYE AMVAA MAGUFULI
Awali, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye alimtaka mgombea urais
wa CCM, Dk. John Magufuli, ahamie Ukawa na kuendelea na kampeni za
kuing’oa CCM madarakani kwani yaelekea ananogewa na kampeni zao na ndiyo
maana hutumia misemo yao, ikiwamo kubadili “Movement for Change’ (M4C)
ya Chadema kuwa ‘Magufuli for Change’.
SHUGHULI ZASIMAMA
Katika hatua nyingine, shughuli mbalimbali za biashara katika Soko
Kuu la Manispaa ya Mtwara Mikindani na maeneo mengine zilisimama kwa
muda jana baada ya wafanyabiashara kuamua kwenda kwenye viwanja vya
Mashujaa kusikiliza sera za Lowassa na Ukawa.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti kabla ya kufanyika kwa
mkutano huo, baadhi ya wafanyabiashara hao walisema kutokana na wanunuzi
wengi kuwa katika mkutano huo, wao hawana sababu ya kukaa katika
biashara zao ila ni kuungana na wananchi wengine kwenda kumsikiliza
Lowassa.
Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu,
alisema kwa kuwa ni maamuzi ya wafanyabiashara wenyewe kusitisha
shughuli zao, hakukuwa na sababu ya kuwazuia.
Dendegu alikaririwa akisema katika kituo kimoja cha redio mjini
hapa kuwa mtu akisitisha biashara kwa hiari yake hakuna tatizo, bali
kama kuna shinikizo lolote kutoka miongoni mwao, sheria huchukuliwa
dhidi ya wahusika.
Kabla ya kutua Mtwara mjini jana, Lowassa alifanya mikutano ya kampeni pia kwenye maeneo ya Newala na Tandahimba.
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment